Home Makala Kenya yaja na Tume mpya ya uchaguzi

Kenya yaja na Tume mpya ya uchaguzi

367
0
SHARE

Nairobi, Kenya

Kenya inafanya uchaguzi Mkuu Agosti 8, 2017. Huu utakuwa uchaguzi Mkuu wa pili tangu nchi hiyo kufanya mabadiliko makubwa ya Katiba yake.

Katiba hiyo ilitumika katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2012, lakini kukaibuka malalamiko kutoka kwa Muungano wa vyama vilivyounda Umoja maarufu kwa jina la CORD ulikuwa chini ya mgombea urais Raila Odinga (Waziri Mkuu Mstaafu wa nchi hiyo).

Muungano wa Cord, ulitoa malalamiko yao kwa Tume ya Uchaguzi ambayo awali ilipaswa kuendesha uchaguzi huo kielektroniki na wakati uchaguzi huo ukifanyika mfumo wake ukashindwa kufanya kazi.

Cord wakalalamika kuwa wenzao wa Muungano wa Jubilee ambao walitangazwa kushinda uchaguzi huo, chini ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, walicheza faulo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wapiga kura katika maeneo ambayo umoja huo ulikuwa unakubalika zaidi.

Baada ya uchaguzi huo kumekuwepo na harakati nyingi zenye lengo la kuhakikisha uchaguzi Mkuu ujao unafanyika katika mazingira ambayo yatakuwa ya wazi na yanayojenga haki kwa wshiriki wote.

Umoja wa Cord uliendesha maandamano makubwa yenye kuitaka Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo iliyo chini ya Mwenyekiti wake Ahmed Issack Hassan iachie ngazi.

Alhamisi ya wiki iliyopita, ikafika hatua tume hiyo kukubali kubwaga manyanga. Hili ni tukio kubwa sana katika historia ya siasa za Afrika Mashariki na zinaiweka Kenya katika hatua nyingine, kama nchi ambayo inaweza kuamua masuala yake na hasa kuzingatia kuboresha demokrasia nchini humo.

Bunge la nchi hiyo limepitisha sheria mpya ya uchaguzi na kupitia sheria hii, kunaundwa Jopo Maalum la Usaili, jopo litakalokuwa na majukumu ya kupitia orodha ya waombaji wa nafasi za kazi katika Tume ya Uchaguzi kwa nafasi za Makamishna.

Jopo hili lipo chini ya Kamati ya Huduma za Bunge na linashirikisha majina yanayopendekezwa kutoka katika Muungano wa Jubilee na ule wa Cord.

Sambamba na majina hayo pia yapo mengine yanayotoka katika vikundi mbalimbali vya Madhehebu ya Dini. Kwa pamoja majina haya yanapitia kwa Katibu wa Bunge anayesimamia Huduma  na kisha kuyawasilisha kwa Rais ili ayatangaze rasmi, na yakisha kutangazwa zoezi la kuapishwa linafanywa chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mara tu baada ya taarifa ya kuachia ngazi kwa makamishna wa Tume iliyopo kutangazwa, tayari vyama viundavyo mashirikisho ya Jubelee na Cord vyote kwa pamoja vikatangaza kuwa tayari vimeshateua majina mawili mawili kutoka kila upande.

Majina hayo ndiyo ambayo wanataka yawawakilishe katika Jopo la Usaili wa makamishina wapya wa tume hiyo ya uchaguzi.

Jubilee wamewateua wanasheria Evans Monari na Mary Karen Kigen-Sorobit  huku Cord ikitaja majina ya Jaji Mstaafu Tom Mbaluto na Bi. Olga Karani Chemweno.

Jopo la usaili baada ya taratibu zote kukamilika litakuwa na kazi ya kuhakikisha kuwa orodha ya walioomba nafasi inawekwa wazi pamoja na taaluma ya kila mwombaji. Kisha jopo hilo hilo, litafanya kazi ya kupunguza orodha hiyo na kutangaza wale watakaokuwa wamefanikiwa kuingia hatua ya usaili.

Kazi zote hizi kwa mujibu wa sharia hii mpya zitatakiwa kufanyika kwa uwazi mkubwa. Kwanza orodha nzima itapaswa kuchapwa katika Gazeti la Serikali na pia kwenye magazeti mengine mawili. Pili itabandikwa katika mtandao nwa Bunge ili kutoa fursa ya wananchi kuiona.

Waombaji watakaofanikiwa kwenda hatua ya pili nao watafanyiwa hivyo hivyo lakini sasa itaongezeka suala moja kubwa, ambalo ni kufanyika kwa usaili wa wazi ambao vyombo vya habari na wananchi wataruhusiwa kuutazama. Yote haya yanafanyika ikiwa ni muendelezo wa kutoa uwazi na kuongeza uwajibikaji kwa wananchi ambao Katiba mpya ya Kenya unatoa.

Baada ya kupata watu wanaofaa, Jopo la Usaili litapendekeza majina mawili kwa ajili ya nafasi ya Mwenyekiti na mengine tisa kwa ajili ya nafasi za makamishna wa tume.

Orodha hiyo ikishapatikana itapelkekwa kwa Rais ambaye atakuwa na Mamlaka ya kutangaza jina moja kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Tume pamoja na mengine sita kwa nafasi za kamishna wa tume.

Safari ya kuipata tume mpya inakuwa haijaisha. Orodha itakayotoka kwa Rais itapelekwa tena kwa Katibu wa Bunge, ili wateuliwa wakathibitishwe au kukataliwa na Bunge. Ikitokea wakawa wamethibitishwa basi ndipo zoezi la kuapishwa litafanyika na wateuliwa kuchukua nafasi zao.

Kazi kubwa watakayokuwa nayo Mwenyekiti wa Tume pamoja na makamishna wapya ni kuandaa na kusimamia Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 8, 2017.

Mwanasheria Monari ambaye ni mwakilishi wa Jubelee, pia amewahi kuhudumu kama mwanasheria wa Mkuu wa Polisi wa zamani wa Kenya Hussein Ali, katika kesi yake dhidi ya mauaji yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2004, katika mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai iliyopo The Hague.

Bi. Kigen-Sorobit kwa sasa ni Mkurugenzi katika Mamlaka ya Barabara, ambapo ni Mwenyekiti wa idara Ukaguzi, Udhibiti na Utawala. Pia alikuwa Msaidizi katika jopo la kuchuja majaji na Mahakimu nchini humo.

Bw. Mbaluto alifukuzwa kazi na Mahakama baada ya kubainika kuwa hana sifa ya kuhudumu nafasi ya Ujaji  kufuatia kukutwa na hatia ya kuonesha utovu wa nidhamu mwaka 2003. Bi. Chemweno ni Mweka Hazina Msaidizi wa chama cha ODM.

Katika uchaguzi wa mwaka 2013, alikuwa miongoni mwa watu wa ndani kabisa wa chama cha URP, ambacho kiongozi wake alikuwa Makamu wa Rais  William Ruto.

Wanne hawa sasa wataungana na wawakilishi wengine waliochaguliwa kutoka kwa vyama vya madhehebu na dini mbalimbali na wataingia moja kwa moja katika Jopo la Usaili.

Japokuwa tume ya uchaguzi ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Ahmed Issack Hassan, ilikuwa imepeleka barua za kuomba kuachia ngazi kwa Rais wa Kenya, bado watatakiwa kuwepo katika nafasi zao mpaka pale Makamishna wapya watakapokuwa wamepatikana.

“Kitendo hiki cha kutoa barua za kuachia ngazi kwa makamishna wa tume inatoa fursa kwa rais kutangaza kuwa nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi iko wazi pamoja na nafasi zingine za tume hiyo ambazo zimewekwa kwa mujibu wa sheria,” anasema Joseph Kinyua, Mkuu wa Utumishi wa Umma Kenya, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti Mwenza wa Kamati iliyotoka na mapendekezo ya Kuitaka timu nzima ya Tume ya Uchaguzi chini ya mwenyekiti wake Hassan kuachia ngazi.

Mwenyekiti wa Tume pamoja na makamishna, Bi. Lilian Mahiri-Zaja (Makamu Mwenyekiti), Bw. Albert Bwire, Bi. Kule Godana, Dk. Yusuf Nzibo, Bw. Abdulahi Sharawe, Bw. Thomas Letangule, Bi. Muthoni Wangai na Bi. Mohammed Alawi, watatakiwa kulipwa kiasi cha fedha shilingi za Kenya milioni 200. Malipo haya yatatakiwa kufanyika baada ya Makamishna wapya kuwa wamechukua nafasi zao.

Bw. Kinyua, ambaye pia ni Mkuu wa Wasaidizi wa Rais, alisema Rais Uhuru Kenyatta alikwisha pokea taarifa kuhusu kujiuzulu kwa Makamishna hao mapema kabla hawajatangaza na kwamba ni siku hiyo hiyo, kwa mujibu wa taratibu walipaswa kuwa katika kukamilisha mpango wao wa kuachia nafasi hizo.

Kamisheni ya Tume ya uchaguzi ina jukumu la kuifanya sheria ianze kutekelezwa. Hii ndiyo sababu wajumbe wake watapaswa kubakia katika nafasi zao ili kanuni zitengenezwe. Bila makamishna hawa Sekretarieti haina mamlaka ya kutekeleza sheria hii mpya.

Bw. Kinyua aliishukuru Tume hiyo kwa kazi kubwa kwa nchi na kuongeza kuwa: “Utoaji wa taarifa zao za kuachia ngazi pia kunatoa fursa kwa nchi kuwa na muda wa kutosha kwa tume ya sasa kujipanga kuikabidhi tume mpya na hivyo kuwepo pia muda kwa serikali kuanza maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwakani,” anasema.

Dai la makamishna hao kuendelea kuwepo hadi tume mpya itakapotangazwa ni jambo ambalo vyama vya upinzani vinalipinga. Seneta wa Siaya, James Orengo, alionesha kushtushwa kwake na taarifa hiyo ambapo alielezea hatari ya kuwepo malengo ya wazi ya kuufanya uchaguzi wa mwakani usiwe huru na haki kufuatia kuonekana serikali ikipingana na sheria ambayo imepitishwa na bunge ambayo ilitokana na Seneta Orengo na Seneta Kiraitu Murungi kuweka muswada wa pamoja.

Anasema Cord, wangetaka na wataendelea kusisitiza kuhusu kuwataka makamishna walioachia ngazi kutoendelea na majukumu yoyote ya tume kwa sasa.