Home Makala Tujiandae tusijegeuka soko la ajira la wenzetu

Tujiandae tusijegeuka soko la ajira la wenzetu

388
0
SHARE

Tunaelekea katika uchumi wa viwanda. Ni ndoto njema sana na inayovutia hususan katika kipindi hiki ambacho serikali iliyopo madarakani imeamua kurejesha utawala wa sheria, kanuni na taratibu kote nchini.

Hatua zinazochukuliwa hivi sasa za kuhakikisha kwamba kila mtu anafanya kazi na kupata kipato halali zimeibua hisia mchanganyiko.

Wapo wanaoshukuru kwamba hatimaye tunarejea kwenye mstari kama taifa na wakati huo huo wapo wanaolalamika kwamba maisha yamekwazwa sana na kupotea kwa fedha za madili.

Uchumi wa kipigaji ulikuwa umepeperusha beramu yake kote nchini. Maisha yalikuwa ni dili na dili ni maisha ili mradi wajanja wachache walijihakikishia pepo hapa duniani wakati wengine walio wengi wakiumia.

Mabadiliko ambayo yalikuwa yanatarajiwa ni kurejesha mazingira ya utawala wa sheria. Hakuna jambo linalowavutia wananchi walio wengi kama jitihada zinazofanyika hivi sasa za kutaka kuirejesha nchi katika utawala wa sheria.

Matumaini ya wananchi ni kwamba itafika siku nchi yetu itapiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na jitihada zetu wenyewe bila ya kumtegemea mjomba ya shangazi ye yote yule huko ughaibuni.

Katika jitihada hizo za kutaka nchi ipige hatua ya kweli kimaendeleo kiongozi wetu Rais John Magufuli amelivalia njuga suala la viwanda. Ni hatua ya kishujaa inayohitaji ujasiri mkubwa.

Tanzania iliwa kuwa na viwanda. Idadi kubwa ya wafanyakazi wa nchi hii walikuwa ni watumishi katika viwanda mbalimbali vilivyokuwa vimesambaa nchini.

Viwanda hivyo kwa kiasi kikubwa vilitegemea katika mali ghafi inayolimwa hapa nchini. Kilichotokea kwa viwanda vyetu ni historia. Kwa nini vilikufa majibu ni mengi ingawa moja lililokuwa wazi ni kwamba kulikuwapo na ubadhirifu mkubwa uliotokana na kutokuwapo mtu mmoja ambaye angetambulika kama mmiliki wa viwanda.

Umiliki wa viwanda zama zile za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulikuwa mikononi mwa serikali. Hilo suala la umiliki kuwa wa serikali ulisababisha hujuma ambazo hazikuwa na mdhibiti kutokana na tabia iliyojitokeza na kujengeka kwamba hiyo si mali ya mtu bali ni mali yetu.

Katika jitihada za kutaka kufufua viwanda nchini ni lazima hili la ushiriki wa serikali liwekwe kwa namna ambayo haitasababisha historia kujirudia. Angalizo hilo ni muhimu katika majadiliano yote tunayofanya kwa ajili ya kuwa na viwanda nchini. Kama utakuwapo ushiriki wa serikali ni lazima ufanyike kwa namna ambayo viwanda hivyo havitakuwa havina mmiliki mwenye uchungu navyo.

Mbali na hilo la umiliki moja ya mambo ambayo ni muhimu katika kipindi hiki cha kuelekea katika Tanzania ya viwanda ni kufanya maandalizi ya kutosha ya nguvu kazi.

Viwanda vitakuwa na tija na maana kwa Watanzania kama wananchi watakuwa na fursa ya kuajiriwa na kuchangia katika ustawi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kupitia ajira.

Hata hivyo, ni lazima kutambua kwamba viwanda tunavyovizungumzia katika karne ya 21 ni tofauti sana na vile vya karne ya 20. Hivi ni viwanda vya kisasa zaidi ambavyo vinatumia teknolojia ya kisasa zaidi. Mitambo ya kuendesha viwanda vya karne ya 21 ni tofauti sana kwani ni vya teknolojia ya kisasa zaidi.

Tukitaka kujua ni aina gani ya viwanda tunavizungumzia hivi sasa tuangalie zana zinazotumika hivi sasa katika maandalizi ya vyakula majumbani. Nyenzo na vifaa vingi vya jikoni ni vya kisasa. Mitambo midogo iliyopo ndani ya majiko ya kisasa ni ushahidi wa ni aina gani ya viwanda vimezagaa sasa hivi duniani.

Viwanda vingi vinatumia teknolojia ya kisasa ambayo kwa namna moja au nyingine ina uhusiano wa karibu na teknolojia ya mawasiliano (ICT). Kwa mantiki hiyo ni muhimu sana kuliona hilo katika maandalizi ya kada ya kuja kufanya kazi kwenye viwanda hivyo.

Katika maandalizi ya vijana wetu kwa ajili ya kutumika katika viwanda vinavyotarajiwa kujengwa nchini ni muhimu kuangalia mitaala yetu ya elimu ili kuwaandaa ipasavyo kushiriki katika mchakato huo.

Hii ni dunia ya teknolojia ya kompyuta. Huko nje kwa wenzetu suala la matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ndiyo linaloongoza katika maisha ya kila siku. Dunia imegeuka kuwa ni ya kompyuta. Kila familia huko nje inaweza kutumia kompyuta kwani ni muhimu kiasi kwamba maisha yanakuwa magumu bila uelewa wa jinsi inavyotumika.

Kwa maana hiyo basi elimu yetu ni lazima itilie maanani umuhimu wa kompyuta na teknolojia ya mawasiliano kwa ujumla kama moja ya vitu muhimu sana.

Kiwanda cha nguo cha karne ya 21 ni tofauti na kiwanda cha nguo cha karne ya 20 kwa sababu ya matumizi ya teknolojia ya kisasa ya mawasiliano. Ili kupata ajira katika viwanda vya kisasa ni lazima uwe na uelewa wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kinyume chake ni shida.

Zama za matumizi ya nguvu na mitulinga katika viwanda zimepita. Hivi sasa wanahitajika watu wenye elimu ya teknolojia ya kisasa. Ili kuipata elimu hiyo ni lazima kuangalia upya mitaala yetu ya elimu na kuona ni kwa kiasi gani inalingana na mahitaji na matarajio yetu kama taifa linalotaka kuwa la viwanda.

Katika zama tulizo nazo matumizi ya nguvu katika utendaji kazi na uzalishaji mali umepungua kwa kiasi kikubwa. Ukitupa jicho katika bandari utagundua kwamba shughuli ya ukuli kama ulivyokuwa miaka kumi iliyopita imebadilika kwa kiasi kikubwa. Mizigo mikubwa inasogezwa na mitambo. Inapakiwa kwenye meli na mitambo. Inafunguliwa kwa mitambo na kadhalika ili mradi shughuli nyingi zinafanywa na mitambo.

Huko nje katika bandari kubwa kama ya Dar es Salaam asilimia zaidi ya 80 ya shughuli hufanywa na mitambo ambayo inaendeshwa na watu wenye ujuzi. Hali kadhalika huko tuendako kwenye uchumi wa viwanda mitambo itakuwa na nafasi kubwa zaidi katika uzalishaji jambo ambalo litatulazimisha kuwa na watu wenye kuendana na mapinduzi hayo.

Tusitegemee kuwa na nchi yenye viwanda vya kisasa na kufaidika kama hatutawaandaa vijana wetu kushiriki kikamilifu katika fursa hiyo. Tusipobadili mitaala ya elimu yetu na kuwaandaa vijana wetu kwa ajili ya Tanzania ya viwanda huenda tukajikuta ni soko la ajira kwa ajili ya wageni ambao nguvu watakayokuja nayo nchini ni kwamba wana elimu na ujuzi unaohitajika katika kusimamia na kuendesha mitambo itakayokuwapo katika viwanda vilivyojengwa kwa ridhaa yetu.