Home Makala Kimataifa Kauli za Rais Buhari na mkewe ni mpambano wa kisiasa?

Kauli za Rais Buhari na mkewe ni mpambano wa kisiasa?

480
0
SHARE

ABUJA, NIGERIA

WAFUATILIAJI wa mambo ya siasa za Afrika wanajiuliza, je, kinachoikumba sasa familia ya Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ni mpambano wa kisiasa ndani ya nyumba au ukweli mchungu ambao unaweza kumaliza safari ya kisiasa ya familia hiyo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Buhari alionekana mwenye hasira  na ghadhabu, uso wake haukuwa na furaha hata kidogo.

Yote hayo yanatajwa kusababishwa kwa kiasi kikubwa na onyo na tishio la mkewe Aisha Buhari, ambaye ameonekana kutaka kuingilia masuala nyeti ya kiuteuzi.

Aisha amejibebesha mamlaka ya mumewe kwa kumpa maelekezo yaliyokwenda sambamba na tishio la kutomuunga mkono kwenye safari yake ya kisiasa ndani ya uchaguzi mkuu ujao.

Aisha alimuonya mumewe kuwa huenda asishirikiane nae kisiasa kwa kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao iwapo hatafanya mabadiliko kwenye serikali yake.

Kwenye mahojiano yake na BBC, Aisha alisema mumewe hawafahamu maafisa wakuu aliowateua serikalini, jambo ambalo ni hatari kwake kwani yeye anaona serikali imetekwa, na kwamba kuna watu wachache ambao huamua ni nani watateuliwa au kupewa kazi na rais.

Baada ya onyo hilo la mkewe, Rais Buhari nae aliamua kujibu mapigo, hata hivyo pamoja na uso wake kutawaliwa na jazba na hasira alijitahidi kuwa mtulivu katika kutolea ufafanuzi kauli ya mkewe.

Kwa kicheko cha dharau, Rais Buhari alibeba majibu yalioonesha kuwa mke wake haijui siasa na kusema kuwa anachokijua yeye stahiki ya mkewe ni jikoni, sebuleni na chumbani kwake.

“Sijui mke wangu yuko chama gani, lakini mahali pake pekee ni jikoni kwangu, sebuleni kwangu na chumbani kwangu.

“Natumai mke wangu atakumbuka kuwa nilikuwa kwenye harakati za uongozi kwa miaka 12, nimejaribu mara tatu kuwania urais na mara ya nne nikafanikiwa.

“Zile mara tatu za kwanza zote nilijikuta nikiishia kwenye   mahakama kuu ya Nigeria, kwa hiyo mimi  nina uelewa mkubwa wa masuala ya siasa kuliko wanasiasa wote wa upinzani kwa sababu nimefanikiwa,”alisema.

Jibu hilo linaelezwa na wachambuzi wa mambo ni kama kumfunga mdomo mke wake na kwamba hajui siasa hivyo anapaswa kukaa kimya.

Wanaoitazama hoja hiyo kwa mrengo wa ubaguzi wa kijinsia wanaweka wazi kuwa huenda mapambano hayo ya hadharani kati ya Rais Buhari na mkewe yakaendelea kwani Aisha anatazamwa kama mwanamke mwenye uwezo wa kujisimamia.

Buhari alichaguliwa mwaka jana baada yake kuahidi kukabiliana na ufisadi uliokuwa umekithiri serikalini pamoja na ubaguzi na upendeleo.

Ukweli ni kwmaba uamuzi wa mke wa kiongozi huyo kusema hayo hadharani umeshangaza wengi, lakini pia unatajwa kuwa ni ishara ya kiwango cha wananchi wengi  kutoridhishwa na uongozi wa Rais Buhari.

Rais Buhari alitangaza wakati wa kuapishwa kwake kwamba yeye hamilikiwi na mtu yeyote na anamilikiwa na watu wote na kwamba atahakikisha anawatumikia wote.

Aisha Buhari alipata jeuri ya kusema kuwa Rais hawafahamu watu 45 kati ya 50 aliowateua na kwamba hata yeye kama mke wa rais hawafahamu licha ya kuwa mke wake kwa miaka 27.

Alisema kinachoonekana ni kwamba watu walioteuliwa hawana maono sawa na ya chama tawala cha All Progressives Congress (APC) na kwamba wameteuliwa kwenye nyadhifa kubwa kubwa kwa sababu ya ushawishi wa watu wachache.

“Watu wengine wanaketi manyumbani mwao wakiwa wametulia kisha wanaitwa na kupewa kazi ya kuongoza idara au kuwa mawaziri.”

Aliopulizwa awataje watu waliokuwa wameteka serikali, alikataa na kusema: “Utawajua ukitazama televisheni”.

Kuhusu iwapo Rais bado anadhibiti serikali, alisema: “Hilo ni watu wataamua.”

Aisha alisema mumewe bado hajamwambia iwapo atawania urais uchaguzi wa mwaka 2019.

“Bado hajaniambia lakini nimeamua, kama mkewe, kwamba mambo yakiendelea hivi hadi 2019, sitatoka kwenda kumsaidia kwenye kampeni na kuomba wanawake wampigie kura kama nilivyofanya awali. Sitafanya hilo tena.”

Alipoulizwa ni jambo gani anachukulia kuwa ufanisi mkubwa wa serikali, alisema ni kuimarisha usalama kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ambapo serikali imekuwa ikikabiliana na wapiganaji wa Kiislamu wa Boko Haram ambao walianza maasi 2009.

“Hakuna anayelalamika kuhusu kushambuliwa nyumbani kwake. Tunashukuru kwamba sasa watu wanaweza kutembea bila kusumbuliwa, na kwenda maeneo ya ibada na kadhalika. Hata watoto wa Maiduguri wamerejea shuleni.