Home Makala Nyerere alifahamu ‘umahiri’ wa wababaishaji

Nyerere alifahamu ‘umahiri’ wa wababaishaji

406
0
SHARE

Na Markus Mpangala

MIONGONI mwa mambo ninayojutia maishani mwangu ni kutoweza kukuonana na Mwalimu Julius Nyerere, Abduwahid Sykes, Sewa Haji, Kirilo Japhet, Abeid Karume, Zuberi Mtemvu, Edward Sokoine, Oscar Kambona kwa kuwataja wachache.

Nina sababu nyingi, lakini kuu ni kwamba kila mmoja nilikuwa nahitaji kumsikiliza zaidi ya kusoma maandiko. Nilihitaji kumsikiliza Abdulwahid Sykes kwa masimulizi kutoka chama cha A.A kabla ya TANU, na harakati mbalimbali. Sababu kuu ni kwamba licha ya kusoma masimulizi yake mbalimbali, bado nina kiu ya kuonana naye. Bahati mbaya sina uwezo huo, alishatangulia mbele ya mola.

Nilitamani kuonana Kirilo Japhet ili animbie zaidi alichokiona na kujisikia kwenye harakati zake zote mpaka kupata nafasi ya kuwa Mtanganyika (baadaye Tanzania) wa kwanza kuhutubia kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Nilitamani kumwona Sewa Haji anipe mambo ya maana zaidi maishani mwake kuliko yaliyopo. Kwa kawaida natambua kuwa hayaandikwi yote, sasa name nilitamani yale yasiyoandikwa. Nilitamani kuonana na Oscar Kambona ajibu maswali yangu na kwanini ninazipinga fikra zake juu ya kuchagua itikadi ya kuongoza nchi.

Vilevile Kambona ningeonana naye ili anieleze kile alichofikiria zaidi katika utawala wa Nyerere na Tanzania kwa ujumla. Kambona ningemuuliza mambo yanayonitatiza, kwa mfano viweje wale wapinduaji wamtumie yeye kuiweka nchi sawa ama kwanini siku chache kabla ya kutokea jaribio la mapinduzi yale alipita kuzungumza na wa makamanda wa majeshi wa kigeni.

Kambona ningemwomba aniambie nyakati zake za furaha na Nyerere zilikuwaje na kipimo chake kilikuwa cha uzani gani. Abeid Karume angeliniambia ni kwanini azimio la Arusha alisema ‘mwisho wake kisiwa cha Chumbe’.

Ninatamani kuongea naye umahiri wake wa kucheza Bao, na namna alivyofurahia, huzuni na uwezo na kipi alijutia kushindwa kutekeleza. Ninajuatia kwasababu nimesoma maelezo mengi mno lakini yameshindwa kukata kiu.

Sokoine ninatamani kuongea naye nyakati zake za furaha. Nyakati zake za masomoni huko ng’ambo. Nyakati zake za uwaziri mkuu, na namna alivyoweza kuelewana na Nyerere au Rashid Kawawa. Zuberi Mtemvu ningetamani aniambie mchuano wa kuwania madaraka ndani ya TANU kabla ya kuanzisha chama chake.

Ninatamani angeongea yale yasiyoandikwa sababu yaliyopo bado yamenipa mwangaza lakini kiu ya mwisho ni kuwaona wahusika. Desturi ya masimulizi yanaweza kutiwa chumvi ili yawapendeze watu wenye kufangamana fikra ama kupunguza na kuondoa mambo muhimu ambnayo yanayonekana ya kawaida. Bado kiu hii haiwezi kutimia, kwakuwa wote wametangulia mbele ya haki.

Madhumuni ya kutamani kuonana na wazee hao na majuto yangu yameshamirishwa na kumtafakari Julius Nyerere, Baba wa Taifa letu. Nimemtafakari kuelekea Oktoba 14 na siku husika kwa kurudia kukisoma kitabu chake cha “Uongozi wetu na Hatima ya Nchi yetu”.

Maudhui ya kilichotokea na sababu za kuandikwa kitabu hicho kinanipa tafsiri kuwa kati ya mwaka 1990 hadi 1995 kulijaa ubabaishaji usiomithirika. Kuliibuka kundi la watu ambao walidhani wao ni mahiri lakini walijaa ubabaishaji.

Mantiki ninayopita ni kwamba Nyerere alikuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na hoja kinzani. Aliwajua wapinzani wake wa hoja. Aliwajua uwezo wao na namna walivyoshindwa kumkabili. Tofauti ya Nyerere na wakinzani wake wa hoja ilikuwa moja tu;’ uwezo wa kuichakata hoja na kuona mbali bila darubuni.

Jambo jingine nililobaini kutokana na kitabu hicho, ni pale alipoelekeza shutuma za moja kwa moja kwa Rais na Waziri mkuu. Ninawaomba radhi wazee wangu Ali Hassan Mwinyi na John Malecela.

Nilichobaini katika uongozi wao hakukuwa na msimamo madhubuti zaidi ya ubabaishaji na kushindwa kujiweka sawa mpaka wanapokwenda kuomba msaada wa Nyerere ili awasaidie kuwanyamazisha wabunge wa CCM.

Kiutawala mpaka Rais na Waziri mkuu walipomfuata Nyerere ili aokoe jahazi maana yake waziri mkuu hakuwa thabiti katika nafasi yake kumshauri Rasia. Nyongeza ni kwamba Rais alimteua waziri mkuu ‘mbnaya’ asiywe na uwezo wa kumshauri namna nzuri au bata kupingana naye kwa hoja kabla ya kupata suluhisho.

Waziri mkuu hakutaka kuchukua ‘risk’ ambayo ingeliweza kuonyesha uthabiti wa serikali ya awamu ya pili. Aidha, ilionyesha bayana kuwa uongozi wetu ulikuwa umetanguliza matakwa ya kisiasa na kukidhi haja zao badala ya matakwa ya ustawi wan chi ili kuepuka kurundika mzigo wa mgogoro wa kisiasa ambao ungeliweza kujitokeza.

Kusema hivyo sina maana kuwa Nyerere hakuwa na makosa kwa upande wake (yapo na kiasi Fulani ninayo mambo ambayo sikubaliani naye kabisa, ndio maana ninatamani ningeonana naye kwanza tuelezane).

Nitatoa mfano katika hilo; “Rais alieleza kuwa walikuwa wamekubaliana kwamba vipindi vya kuwa Rais ni lazima vitamkwe, lakini walikuwa hawajaafikia uamuzi viwe vipindi vingapi.

Awali baadhi ya viongozi wa Chama walikuwa wameanza kampeni za kutaka Rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa kuwa Rais. Nilipotambua hivyo nilikuwa nimekwenda mara moja kwa Rais na kumsihi azizime kampeni hizo; na viongozi wahusika nilitafuta nafasi nao nikawaomba wasilifufue jambo hili.

Nikadhani tumeelewana hivyo. Kwa hiyo nilistuka niliposikia kuwa kumbe suala hilo la vipindi vya urais bado linazungumzwa, na ati bado uamuzi wa vipindi vingapi haujafikiwa!”(Uk.9).

Picha tunayopata hapa Rais Mwinyi hakuwa amepata ushauri mzuri. Lakini kutokana na busara aliyonayo ilimwongoza kuafiki kuiweka nchi kwenye njia salama kwa kutoruhusu kampeni hizo kuendelea kumyumbisha ndiyo maana mwaka 1995 aliachia nagzi. Hii ilikuwa busara ya hali ya juu na msingi wa ustawi wa taifa letu. Kosa la Mwinyi ni kuteua waziri mkuu ambaye hakuwa mshauri hodari. Hilo ni lake Mwinyi.

Kwa vyovyote vile kuibuka wimbi la wabunge wa CCM kuchuana kwenye madaraka ilikuwa ishara tosha nchi yetu ilitumbukia mikononi mwa wababaishaji. Nyerere alistaafu urais wmaka 1984, na uongozi wa chama mwaka 1990.

Kwa mantiki hiyo kundi kubwa lilipoibuka kumyumbisha Rais Mwinyi lilikuwa halina uwezo wa kimantiki wala kifikra kukabiliana na Nyerere. Kilichopo ndichi kinachotutafuna leo hii; ufuasi wa watu au wanasiasa ulikuwa umeota mizizi katika kipindi hiki kuliko wakati wowote. Wanafunzi wa Nyerere waliokuwa uongozi walikuwa wafuasi wake kiuongozi badala ya itikadi, falsafa na fikra ambazo zingestawisha nchi. Hawakujiamini mbele ya Nyerere.

Itaendelea wiki ijayo…