Home Makala Nini hatma ya Afrika Kusini baada ya kujiondoa ICC?

Nini hatma ya Afrika Kusini baada ya kujiondoa ICC?

294
0
SHARE

Afrika Kusini imetangaza kujiondoa katika Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC) mapema wiki iliyopita. Zoezi hilo limefanyika baada ya kuwasilisha hati yenye kusudio la kujitoa katika mahakama hiyo, zilizowasilishw akatika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Kufiatia uwasilishwaji wa hati hiyo, Afrika Kusini inabakia na kazi moja tu, yaani kuipeleka hoja hiyo katika Bunge la nchi hiyo na kisha Bunge hilo liridhie kujitoa rasmi. Hoja hiyo imekwishakuandaliwa na itawasilishwa wakati wowote katika Bunge.

Kutokana na Chama Tawala cha nchi hiyo, ANC kuwa na wabunge wengi, ni dhahiri kuwa hoja hiyo itapita huku ikkabiliana na upinzani mdogo ambao utashindwa kwa kura. Baada ya kura hiyo, Afrika Kusini taifa linaloshikilia nafasi ya pili kwa uchumi barani Afrika, litakuwa linaandika historia inayotia shaka kuhusu kuheshimu haki za binadamu pamoja na mchango wake kwa watu wanaodhulumiwa haki hizo duniani.

Tukio hili la Afrika Kusini limefanyika huku tayari kukiwa na tukio kama hilo lililofanywa na Burundi. Burundi imekuwa nchi ya kwanza kujitoa katika mahakama hiyo ya ICC. Wiki iliyopita Bunge la Burundi lilipitisha hoja ya kujitoa katika ICC na siku moja baadaye Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza, akasaini sheria hiyo ya kujiondoa katika mahakama hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya haki za binadamu katika Afrika wanaelezea kuwa, maamuzi haya ya Afrika Kusini pamoja na Burundi, yanaashiria kuwa mwanzo wa nchi nyingine zilizopo Afrika kufuata nyayo hizo.

Sababu kubwa zinazotumika na nchi za Afrika kutaka kujitoa katika mahakama hiyo ni kuwa, viongozi wengi wa Afrika ndio ambao wamekuwa walengwa wa kesi za mahakama hiyo, tofauti na viongozi wa mabara mengine. Viongozi wa Afrika licha ya kuwa huonesha kuhusika na matukio haya ya uvunjaji haki pamoja na kushiriki uhalifu wa kivita, wanataka wasiwe na chombo cha kushtaki uhalifu wao.

Kenya inatajwa kuwa nchi itakayofuata kujitoa katika mahakama hiyo. Pia zinatajwa nchi ambazo viongozi wake wanaonekana wazi kuwa wanang’ang’ania kubakia madarakani licha ya kuchokwa na raia wao, pamoja na wale ambao wapo madarakani kwa matumizi ya nguvu katika kusimamia chaguzi zinazowapatia nafasi ya kuongoza.

Kitendo cha Afrika Kusini kujitoa kinaelezwa kukolezwa na tukio la kukata kumakamata Rais wa Sudan Omar Al Bashir, mwaka jana alipokwenda nchini humo kuhudhuria Mkutano wa Viongozi wakuu wa nchi za Afrika (AU) ambapo mahakama kuu ya nchi hiyo ya Afrika Kusini Juni 11, 2015 ilitoa amri ya kutaka Rais huyo wa Sudan akamatwe lakini serikali ya nchi hiyo ilikaidi amri hiyo kwa kisingizio kuwa imetoa kinga kwa kila kiongozi mkuu wa nchi na serikali aliyekuwa anahudhuria mkutano huo.

Shirika la Kimataifa la Amnesty limepinga kitendo hicho cha serikali ya Afrika Kusini kutangaza kujiondoa katika Mahakama ya hiyo na kusema kuwa, ni fedheha na usaliti mkubwa kwa mamilioni ya waathirika wa makosa uhalifu wa kivita pamoja na wanaodhulumiwa haki zao duniani.

“Uamuzi huu wa Afrika Kusini ni usaliti kwa mamilioni ya watu wanaokabiliwa na madhira ya uvunjaji wa haki za binadamu ambao walitegemea na hutegemea jumuiya ya kimataifa kuwasaidia kupata haki yao,” anasema Netsanet Belay, Mkurugenzi wa Utafiti na Uenezi wa Amnesty kanda ya Afrika.

Balozi wa Kudumu wa Afrika ya Kusini aliyepo makao Mkuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani aliwasilisha hati iliyosainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Maite Nkoane-Mashabane mchana wa Alhamis iliyopita, katika Umoja wa Mataifa. Msemaji wa Umoja wa mataifa Stephane Dujarric alithibitisha kuwa hati hiyo ilipokelewa na kwamba itaanza kutekelezwa Oktoba 19, 2017.

Kwa mujibu wa Amnesty, kitendo hiki cha Afrika Kusini kujitoa katika mahakama hiyo ni kukimbia jukumu lake na kusaliti heshima ambayo nchi hiyo imejiwekea katika kupigania haki za binadamu. Amnesty inaeleza kuwa, Afrika Kusini inasahau historia yake na uamuzi huu ni mfano wa kidonda kwa wale walioshiriki katika kuisaidia nchi hiyo kutokomeza uvunjaji wa haki za raia wake wakati wa Ubaguzi wa rangi.

Kwa mujibu wa Mkataba wa Rome ambao ndio umeianzisha mahakama ya ICC, kila nchi iliyosaini mkataba huo, haitaruhusu uhalifu unaotambulika katika sheria za kimataifa ikiwemo, ubaguzi wa rangi na hivyo ni lazima kwa nchi hizo kuruhusu uhalifu wa aina hiyo kushtakiwa katika mahakama ya ICC.

Chama cha upinzani nchini humo cha Democratic Alliance (DA), baada ya kupata taarifa hiyo, kilianza harakati za kutaka mahakama nchi humo kuzuia hatua hiyo kwa kile walichokieleza kuwa ni kupingana na Katiba ya Afrika Kusini inayozungumzia na kuweka misingi ya haki za binadamu.

Mataifa mengi yalishangilia wakati mkataba wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo ulipopitishwa jijini Rome mwaka 1998. Mkatabahuo ulikuwa na malengo ya kukabiliana na matukio makubwa yanayohatarisha usalama wa watu duniani. Matukio hayo ni pamoja na mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita pamoja na uvunjifu wa haki za binadamu. Kabla ya wiki iliyopita baada ya Burundi na sasa Afrika Kusini, nchi wanachama wa mahakama hiyo zilikuwa 124.