Home Makala Danny Paul Kyauka: Rais Magufuli geukia mimea tiba

Danny Paul Kyauka: Rais Magufuli geukia mimea tiba

426
0
SHARE

MAGONJWA mengi yanayoibuka katika zama hizi yanaelezwa kusababishwa na mtindo wa maisha ambao kwa namna moja au nyingine umechangia kuwepo kwa bidhaa feki ambazo zikitumiwa na binadamu huharibu na kuvuruga mfumo wa mwili.

Uwapo wa dawa feki, matumizi mabaya ya dawa kiholela bila ushauri wa daktari na hata kemikali zisizokuwa rafiki kwa mwili wa binadamu ni mojawapo ya mambo ambayo yanaelezwa sasa kuchangia ongezeko la tatizo la figo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hivi karibuni, ilionesha kuwa utafiti uliofanywa kati ya Agosti, 2014 hadi Februari 2015 katika Hospitali ya Bugando na Sekou Toure mkoani Mwanza kwa kuwapima watoto 513, ulibaini asilimia 16.2 walikuwa tayari wana matatizo ya figo.

Utafiti mwingine uliofanyika mkoani Kilimanjaro kati ya Januari na Juni 2014, uliohusisha watu 481 kutoka katika kaya 146, asilimia 7 walionekana kuwa na matatizo ya figo.

Pia inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia nane hadi 16 ya watu duniani wanaugua ugonjwa sugu wa figo na tatizo hilo linazikumba zaidi nchi zilizoko katika ukanda wa Jangwa la Sahara ambako asilimia 13 ya watu katika nchi hizo wana matatizo ya figo.

Ni dhahiri kuwa tatizo la figo limeendelea kukua siku hadi siku ndio maana kumekuwapo na watafiti mbalimbali wa mimea tiba ambao kwa namna moja au nyingine wamefanikiwa kukuza utafiti wao na kufanikiwa kutibu maradhi hayo.

Mmoja wao ni Danny Paul Kyauka, ambaye ni mgunduzi wa dawa ya kutibi maradhi ya figo, Billyd Formula Power. Mgunduzi huyo ambaye alipewa tuzo na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolijia mwaka 2005 kutokana na ugunduzi huo, anasema tangu aanze kutoa tiba ya maradhi ya figo hadi sasa hali imezidi kuwa mbaya kwani wagonjwa wanaongezeka kila kukicha.

“Wakati naanza kutoa matibabu nilikuwa natoa kwa watu wawili au watano kwa siku, lakini sasa kwa siku napokea wagonjwa 10 hadi 20 kwa siku, hakika hili ni tatizo ambalo linazidi kuongeza hasa ikizingatiwa kumekuwa na ujanja mwingi wa kujipatia fedha haramu kutoka kwa wafanyabiashara hivyo kuingiza soko bidhaa feki ambazo zinaathiri maisha ya Watanzania,” anasema.

Kwa kipindi cha miaka 20 ambacho ambacho Kyauka alikuwa akifanyia utafiti dawa hiyo, anasema alijaribu kwa wanyama mbalimbali ikiwamo, Mbwa na hata kuku na kubaini kuwa inatibu, hivyo kuipeleka kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa Tanzania (TFDA)  na kuhakikiwa hivyo kupokea pongezi kutoka  wizara ya Afya.

“Kabla ya kuwapatia matibabu wagonjwa wangu lazima wapatiwe vipimo katika hosptali mbalimbali kama vile Muhimbili na Regeancy lakini Regeancy ndio niko nao karibu kwani hata baada ya wagonjwa wangu kutibiwa huenda tena kuhakiki kwa vipimno katika hospitali hiyo,” anasema.

Watanzania wengi wamekuwa na hulka ya kutozingatia kufanya vipimo mapema hali inayochangia wale wenye matatizo ya figo kufikia hatua ya figo kufeli.

“Ninatibu figo ambayo imeanza kufeli, kwa sababu kuna hatua mbalimbali, kuna hatua ambayo haiwezekani kutibu, kwa mfano wale ambao wamefikia hatua ya kusafishwa damu wako wachache wanapona ila ni wale ambao figo hazijakufa kabisa. Wale ambao wanaanza kufeli, figo yenye mawe tunatibu kwa asilimia 99, kwa sababu ile dawa inayayeyusha yanatoka kwa njia ya haja ndogo, figo iliyoathiriwa na mikwaruzo au malengelenge zote tunatibu.

Kwa mfano hizi figo zenye madhara na kuvimba zinakuwa na maumivu, ila inayofeli haina maumivu ila inakuwa na dalili ni kama kuvimba tumbo, kichwa kuuma, uoni hafifu, kichefuchefu kutapika, hiyo ni kwenye upande wa figo, kuchoka, kichwa kuuma, mwili mzima kujaa kutoka jasho sana, kichefuchefu kutapika,” anasema.

Mbali na figo, Kyauka pia anatibu homa ya ini ambayo nayo imekuwa tatizo katika nchi nyingi duniani.

“Natibu homa ya ini kuanzia A,B na C, labda kama ini limefikia hatua mbaya ya kansa hapo halitibiki.

“Homa ya ini, kuambukizana ni rahisi kwa sababu haina dalili sana katika kipindi cha awali,  inaweza kujulikana ukimtolea mgonjwa damu au iwe imefikia hatua mbaya sana ndipo unakuwa na dalili za kukosa choo, kuwashwa, kuchoka, homa,  macho kuwa njano, tumbo kuvimba,” anasema.

Hata hivyo, wagunduzi aina ya Kyauka, bado hawajapewa kipaumbele nchini licha ya kufanikiw akuokoa maisha ya Watanzania kutokana na ugunduzi wa dawa zake ambazo zimekuwa kimbilio kwa wagonjwa wengi.

“Dawa nyingi duniani ni mimea, zikitoka kwenye miamba au mawe vilevile ni chache kwa sababu tunaona wachina wana mashamba ya miti dawa. Watanzania tumelogwa sijui na nini kwa sababu tuna kila kitu lakini tunashindwa kutumia.

“Hivyo tusiite hizi ni dawa mbadala kwa sababu hizi ni dawa zinazotibu kabisa na wazazi wetu walianza nazo, piahizi dawa za kisasa zina madhara kibao, watu wanapofuka, wanapata uziwi na mambo mengine,” alisema.

Changamoto anazopitia

Dk. Kyauka, alishauri serikali kuharakisha mchakato wa kusajili dawa za tiba asili na tiba mbadala nchini, ili zifikie hatua ya kusafirishwa kwa wingi nje ya nchi. Alitoa mfano wa dawa ya figo ya Billyd Formula Power (aliyoigundua), kwamba imeshindwa kusajiliwa baada ya kukosekana kwa chombo cha kufanya hivyo.

“Pia sijaweza kuajiri vijana wengi kwa sababu bado sijasajiliwa na kama tunavyofahamu Tanzania yenye haijasahi kusajili dawa yoyote hivyo namini kuwa Rais Magufuli akigeukia katika sekta hii ya mimea tiba tunaweza kupata ahueni ili na sisi tuonekana kuwa na mchango katima Taifa hili.

“Bado sijafanikiwa kufikia soko la kimataifa ipasavyo licha ya kupeleka dawa zangu katika nchi za Oman na Dubai, naamini iwapo serikali ingeniunga mkono ningekuwa na uwezo wa kuiletea serikali mapato mengi kutokana na ugunduzi wangu hasa ikizingatiwa hakuna dawa ya kutibu homa ya ini.

Aidha, akizungumzia matarajio yake anasema ni kuboresha huduma na kuwa na kiwanda, kwa sababu hizi dawa hazipo duniani, ningeweza kuajiri watu wengi sana. Wizara inanipongeza lakini bado hakuna jitihada.

MWISHO