Home Makala Tamu na chungu za mwaka mmoja wa Dk. Magufuli Ikulu

Tamu na chungu za mwaka mmoja wa Dk. Magufuli Ikulu

1506
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE

NOVEMBA 5 mwaka huu, Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli anatimiza mwaka mmoja tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo.

Tangu kuingia madarakani kwa kiongozi huyo ambaye amekuwa akitumia kauli mbiu ya ‘Hapa kazi tu, kumekuwapo na mitazamo tofauti  kutoka kwa wananchi hususan wale wa kawaida. Rai limefanikiwa kupata maoni ya wananchi mbalimbali ambao wameelezea namna wanavyoutathmini mwaka mmoja wa Rais Magufuli.

ISAAC MSEMWA mkazi wa Mabibo

Licha ya kwamba kuna mambo mazuri ameyatekeleza Rais wetu ndani ya kipindi hiki kifupi, lakini bado kuna changamoto ambazo kama watu wa kawaida wanaziona ambapo iwapo zitafanyiwa kazi huenda kipindi hiki cha miaka minne aliyobakiza kufikia uchaguzi mwingine wa 2020 akafanikiwa.

Kwanza kabisa, viongozi wa serikali ni kama hawashirikishwi katika kutoa maamuzi na hivyo kujikuta wakati mwingine wakipingana na naye, mfano mzuri ni juu ya suala hili la kuwaondoa wamachinga ambapo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ameamuru waondoke ilihali, Rais alishawaruhusu kufanya kazi pasipo kubughudhiwa.

Ukiacha hilo kuna suala jingine ambalo ni juu ya uagizaji wa ndege za serikali ambao ni kama rais anafanya maamuzi mwenyewe ilihali kuwa kuna, Wizara husika ila kwenye mambo mengine yeye anakwenda vizuri isipokuwa awape nafasi ya kufanya maamuzi wale aliowateua.

JACKSON MAHENDERA

Kumekuwepo changamoto kadha wa kadha, lakini kuna mambo mengi ambayo yamefanywa na uongozi wa, Dk. Magufuli kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja hususan kwenye eneo la elimu.

Kama mwanafunzi ninajivunia mwaka huu mmoja wa Rais kuwa madarakani kwani amefanya kwa sasa, Walimu wanawajibika ipasavyo kwenye majukumu yao nikiwa na maana ya kuhudhuria kufundisha wanafunzi darasani.

Walimu wamekuwa makini kutekeleza majukumu yao kwa sasa ikilinganishwa na mwaka mmoja nyuma, hivyo mwamko wa walimu kufika kwenye vituo vyao vya kazi umekuwa ni mkubwa, kwani wanafika kwa wakati na hivyo hata wanafunzi kujikuta morali ya kujifunza na kuhudhulia vipindi darasani ikiongezeka.

Clifford Tilya

Bado bado kuna maeneo ambayo ameenda kinyume na ahadi zake alizozitoa kwenye moja ya mikutano yake ya kampeni.

Rais katika mkutano wake wa kampeni alipokuwa mjini Tabora mwaka jana alihaidi kuwa hakuna mwanafunzi wa chuo kikuu ambaye atachaguliwa alafu akashindwa kusoma kwa ajili ya mkopo.

Na kwamba wale wote watakaochaguliwa ni lazima wapate mikopo lakini hali imekuwa kinyume na matarajio kwani wanafunzi tumekuwa watu wa kuhangaika kwa sasa, kiwango cha wanaopata mkopo kinazidi kupungua tu hatuelewi nini tataizo mpaka tunakumbuka uongozi uliopita.

Jambo jingine ambalo bado hajafanikiwa ni kitendo cha kuwataka wanasiasa kufanya mikutano ya kampeni kwenye maeneo waliyochaguliwa tu, jambo ambalo ni sawa na kuminya uhuru wa Demokrasia.

Kwani hiyo ni aina ya udikteta sababu anachokifanya, Rais ni kuwalazimisha watu wafanye anachotaka yeye na siyo wanachotaka wao, hivyo akiamka asubuhi akipanga kitu hakuna wa kupinga, nafikiri katika kipindi cha miaka mingine inayokuja atalifanyia kazi hili suala, ili kuhakikisha kuwa anatoa nafasi ya watu kufanya maamuzi na kutoa maoni yao kwenye masuala mbalimbali.

NEEMA HAULE

Mambo yamekuwa magumu hasa kwa akina mama wajasiliamali ambao walikuwa wakitegemea vicoba ili kuendesha maisha yao.

Biashara kwa sasa haziendi kwani tulikuwa tukitegemea vikoba kuchukua mikopo na kisha kufanya biashara na kisha kurejesha mkopo huo.

Lakini sasa hivi mambo ni magumu wengi tumeambulia kuchukuliwa vitu vyetu vya ndani sababu mtu unachukua mkopo halafu biashara hazitoki na hivyo unajikuta kwamba muda wa marejesho unafika ukiwa hujafanya lolote.

Tunaomba alegeze kamba kidogo kwani tutashindwa kusomesha watoto kwa namna hali ilivyo, asifanye tujutie maamuzi yetu, tunatambua kuwa bado ana muda wa kutosha wa karibu miaka minne kufanya marekebisho kwa ajili ya kuboresha maisha ya watanzania kwani kwa namna hali ilivyo ni mateso matupu hakuna tena anayechukua mkopo kutokana kwamba biashara hakuna tena, vikundi vingi vya vikoba vimevunjika ili hali kwamba aliahidi kutusaidia, hivyo tunajikuta hatuna pakukimbilia kwani hata tukimwambia, Diwani naye amekuwa hana msaada wowote.

LEONARD MUNISI

Kwa wastani rais amefaulu na sehemu moja amefeli kutokana na maamuzi mengi kuwa mzigo kwa watanzania.

Mwanzo alianza vizuri huko kwenye maeneo kama, Bandari, watumishi hewa na kwingine, lakini jambo linalotupa maswali kama wananchi ni kusikia kuwa serikali kwa sasa imekuwa ikikusanya mpaka Trioni 1.8, ila ukingalia dawa hakuna, huduma nyingine zimebaki kuwa mzigo kwetu wananchi.

Angalia suala kama la sukari ambapo kipindi anaingia madarakani kilo moja ilikuwa Sh 1,800 hadi 2,000 lakini sasa hivi imepanda mpaka 2,500 hadi  3,000 jambo ambalo ni mzigo mkubwa kwa sisi wananchi wa kawaida ambao tulikuwa na imani naye.

Siyo sukari tu kwani hata huduma nyingi bei zimepaa kiasi kwamba baadhi ya familia kwa sasa zimeondoa kabisa ratiba ya chai kutokana na gharama za upatikaji wa sukari.

Kwa maana hiyo kama wananchi wa kawaida inakuwa ni vigumu kumudu maisha hasa wenye familia, kwani majipu tayari yameshatumbuliwa ila sasa hatujui iwapo tutakula usaa au nini kwani hali ni mbaya.

Hivyo tumeshuhudia utumbuaji huu lakini kwetu sisi kama wananchi bado haujawa na faida ya moja kwa moja kwani bidhaa nyingi bado zimebaki kuwa bei juu kinyume na matarajio tuliyokuwa nayo kwa rais wetu.

AISHA KARATA

Binafsi namshukuru Dk. Magufuli kwa mwaka huu mmoja aliokuwa madarakani kutokana na kuimarisha huduma muhimu ikilinganishwa na hapo awali.

Nampongeza rais kutokana kwamba kuna mazuri mengi ambayo ameyafanya ndani ya kipindi kifupi cha mwaka mmoja, kwani maeneo kama Tabata ni sehemu ambazo tulikuwa hatujui maji ya bomba yanafananaje lakini leo ninavyoongea na wewe kuna bomba la maji kila nyumba.

Haya barabara za rami hadi uchochoroni zinajengwa, usafiri umeimarika kwa kipindi kifupi, sasa utasemaje kwamba hajafanya mazuri? Leo mimi nafanya biashara zangu najua mwanangu aliyeko kidato cha nne anasoma bila kuhangaika kutafuta pesa ya ada.

Naweza kusema kuwa kwa wale wanaomchukia basi ni wale ambao walikuwa wakiendesha maisha yao kwa ofa na fedha zisizokuwa halali, lakini kwa wale ambao walikuwa wanajituma na kujishughulisha maisha hayajawa magumu sana kama inavyoelezwa.

GELARD MKAMBA

Hali ni ngumu mno kwa upande wao wa biashara ya kitoweo cha nyama kutokana kwamba kwa kipindi hiki tangu kuingia madarakani kwa Dk. Magufuli kila siku idadi ya walaji wa nyama imekuwa ikishuka kwa kasi.

Sasa hivi ikitokea mteja akakupa elfu 5,000 utafute chenchi utazunguka mtaa mzima kwani watu hawana pesa, kila kukicha idadi ya wateja wanaonunua kitoweo cha nyama inashuka wengi wanakimbilia kwenye maharage, dagaa na mboga za majani.

Kuna wateja ambao walikuwa wanachukua kilo 10 kila wiki kwa ajili ya matumizi ya nyumbani lakini siku hizi wakijitahidi sana ni kilo moja na nusu, hivyo hiyo inaonyesha ni kwa namna gani hali ilivyo mbaya.

Wanunuzi wa nyama kwa sasa wamekuwa ni watu wenye migawaha tu kama hoteli lakini kwa wananchi wa kawaida idadi imepungua mno. Ilizoeleka zamani kwamba siku za jumapili wengi wanapokuwa nyumbani hununua nyama lakini siku hizi badala yake watu wanapenda kununua maharage na njegele jambo ambalo halikuwapo zamani.

Hivyo binafsi kama mfanyabiashara naona kabisa kuwa mambo bado ni magumu japo tunajipa matumaini kuwa huenda mambo yakabadilika baadaye lakini bado hali ya kibiashara haikuwa vizuri kwani kila kukicha tunapunguza kiwango.

Mwaka jana kabla ya rais ilikuwa ni kawaida kuuza 50 lakini sasa ukiuza kilo 10 unashukuru, utumbo kwa sasa ndio umekuwa na soko kuliko ilivyokuwa awali kwani mtu anaona bora anunue kilo moja ya utumbo Sh 3,000 kuliko kununua nyama Sh 8,000, lakini tunaendela kusubiri tuone mbele ya safari kwani naamini kuwa anaweza kufanya makubwa na maisha yakabadilika na kuwa rahisi kwa watanzania wote.

GREENWELL SICHONE

Maisha siyo magumu wala rahisi katika kipindi hiki cha mwaka mmoja bali yamesalia kuwa vilevile. Hali imekuwa ngumu kwa wafanyakazi wa serikali na wale waliokuwa wakipata pesa kwa njia za panya.

Kwa watumishi wa serikali tunaweza kusema kuwa mwaka huu mmoja wa rais madarakani umekuwa mchungu zaidi kwao ikilinganishwa na sisi wananchi wa kawaida.

Kwani tumeshuhudia kwa sasa ongezeko kubwa la vijana wa kike na wa kiume waliokuwa wakifanya kazi kama wafanyakazi wa ndani kwenye majumba mbalimbali wakiongezeka hii inatokana kwamba wengi wameachishwa vibarua vyao kutokana na ukata unaowakabili waajiri wao.

Hivyo tuna imani kuwa ataendelea kufanya mambo mazuri zaidi ikiwamo kutengeneza taifa lenye nidhamu na siyo kusukumana kama ilivyokuwa zamani, lakini ni lazima pia aangalie kuwa kuna kundi kubwa la watu ambao walikuwa wakila kupitia watumishi hawa wa serikali hivyo ni lazima alitazame hilo pia.

STEVEN DIDAS

Mwaka mmoja wa uongozi wa, Dk. Magufuli mambo mengi yamebadilika jambo linalofanya upatikanaji wa kipato kuwa mgumu.

Sijui kwe sekta nyingine mambo yakoje, lakini kwetu sisi tunaojihusisha na ujenzi hali siyo nzuri hata kidogo kwani sasa hivi unafanya kazi ya Sh 100,000 lakini unalipwa Sh 20,000 tena mtu anakulipa huku akilalamika kweli kweli kuwa umemdhurumu.

Zamani kwa mwaka nilikuwa najenga nyumba zisizopungua nne, lakini tangu uongozi huu uanze  nimefanikiwa kupata kibarua cha kujenga nyumba moja peke yake, hivyo mwaka huu umekuwa na machungu yake kwa watu tunaotegemea ujenzi.

SADIKI MWAMWAJA

Mwaka huu mmoja huu rais amekuwa na mtazamo tofauti kwani awali aliahidi kuwa ni mtetezi wa wanyonge kutokana na kuhaidi kuwapa mazingira bora ya kufanyia kazi lakini kwasasa kadri mambo yanavyoenda hali inazidi kuwa mbaya zaidi.

Rais katupa uhuru wa kufanya biashara lakini mara tunaondolewa, mfano kama mimi hapa nauza sumu ya panya, nguo za mtumba na vitu vingine vidogo unadhani nikienda huko mawasiliano hao wateja nitawapata wapi wakati natakiwa nikae kando ya barabara ili niwauzie wapita njia.

Hivyo upande wetu tunaona bado hakuna msaada kabisa kwenye mwaka huu mmoja hatujui labda kwa baadaye.

 

HABIBU SIMBA

Mambo mengi aliyofanya yamekuwa na tija kwa taifa kwa namna moja au nyingine lakini amebana sana pesa.

Rais amejitahidi amefanya vizuri lakini hana budi kuachia pesa maana katika mwaka wake mmoja maisha yamekuwa magumu mno kiasi kwamba hatuelewi nini hatima yetu. Tunasisitizwa wanawake tufyatue tu watoto elimu ni bure, lakini kama unakosa hata nauli ya watoto kwenda shule unafikiri hao waatoto utawasomeshaje licha ya kwamba ada ni bure.

Hivyo angelegeza kidogo kwenye eneo hili la kubana pesa ili kuweze kuwa na mzunguko ambao utasaidia hata sisi watu wa chini kupata chochote cha kuweza kuendesha maisha.

Shabani Seleman

Kipindi hiki cha miezi 12 tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu kimekuwa kigumu mno hasa kwetu sisi walala hoi, kwani hakuna tena kitu cha bei rahisi, jambo linalosikitisha zaidi ni kuwa hata unapokuwa na mgonjwa wako pale Hospitali ya Taifa Mhimbili kisha akafariki basi utahangaika mno.

Licha ya kwamba wazee miili yao inatolewa bure, lakini mambo hayako hivyo kwa sasa kwani kinyume na mambo tuliyokuwa tunaelezwa kuwa wazee watapata huduma bure lakini mambo ni kinyume, hivyo tunaomba Rais aliangalie hili kwani  huduma ya afya kwetu sisi wazee mambo bado ni mabaya ukilinganishwa kuwa uongozi wake huu pesa hakuna basi inakuwa tabu.