Home Makala Tukianza utamaduni huu wa kufukua makaburi hatutabaki salama!

Tukianza utamaduni huu wa kufukua makaburi hatutabaki salama!

445
0
SHARE

NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

HATA kama wengine hawapendi kwa vile aliwazidi kila kitu isipokuwa kulimbikiza mali za umma na kuzifanya zao, lakini hatuwezi kuacha wosia wa Baba wa Taifa hili hayati Mwalimu Julius Nyerere kama kamusi rejea pale tunapoona baadhi ya viongozi wakiendesha mambo  hobela hobela, ovyo ovyo.

Kuna wakati aliwahi kusema bila kujali rangi ya ngozi, mtu mwenye mawazo ya kikaburu kama ya waliokuwa makaburu waliokuwa wakiikalia kimabavu  Afrika ya Kusini basi mtu huyo ni kaburu tu. Alikuwa akitoa maoni yake wakati nchi ikielekea kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Ni wakati huo ndipo pia alizungumzia nyufa mbalimbali katika nchi hii ambayo yeye na wazee wenzake walishiriki kuiasisi kwa kujenga misingi imara ili viongozi wengine watakaofuta pamoja na wananchi kwa ujumla wao  waweze kuiendeleza nchi juu ya misingi hiyo kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Dhambi ya ubaguzi ni sawa sawa na kula nyama ya mtu, ukila nyama ya mtu huwezi kuiachi utaendelea.” Hii ni sehemu ya nukuu katika moja ya hotuba za Mwalimu ambayo ina vimelea vya laana fulani hivi kwa viongozi waliokuwepo na waliofuata.

Nukuu hii ndio msingi wa makala haya ya leo hasa kutokana na mwelekeo wa baadhi ya viongozi wa Serikali ya awamu ya tano katika maamuzi yake ambayo hata kama yanaegemea sheria zilizopo lakini yanaonekana kukiuka desturi, mila na tamaduni zilizoanzishwa na waasisi wa  nchi hii.

Hivi karibuni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wiliam Lukuvi ametangaza kiama kwa wote wanaomiliki ardhi bila kuiendeleza, hasa wale ambao wamekamata viwanja bila kujenga, wengine wenye ardhi kubwa kwa ajili ya kilimo na mifugo lakini imebaki kuwa mashamba pori. Hawa ndio ambao kitanzi kilichotegwa kinawahusu.

Miongoni mwao ametajwa Waziri Mkuu mstaafu Frederik Tluway Sumaye. Huyu tunaambiwa ametelekeza kwa muda mrefu  eneo la ardhi analomiliki kihalali lililoko Mabwepande Wilaya ya Kinondoni bila kuliendeleza. Kwa wenye fikra huru jambo hili linaonekana kama ama kumkomoa au kumdhalilisha labda kwa vile sasa sio mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Huko nyuma hatukuwahi kusikia kiongozi mstaafu  sio kwa ngazi ya Waziri Mkuu, hata Mkuu wa Mkoa ambaye ameitumikia nchi hii akidhalilishwa hadharani namna hii kutokana na desturi mila na utamaduni.

Nataka nieleweke mapema kuwa sina nia yoyote ya kumtetea mtu awe kiongozi au mwananchi wa kawaida anayevunja sheria za nchi. Mantiki ya makala yangu ni kujua kama viongozi wa serikali wanakuwa wepesi kuamuru sheria kufuatwa na makundi yasiyokuwa na uhusiano na serikali au ni kufuata kile anachosema kiongozi aliyepo wakati huo au tunafuata katiba ya nchi.

Wakati fulani akiwa ziarani Mkoani Ruvuma, Rais mstaafu wa awamu ya nn,e Jakaya Kikwete, alipoona mashambulizi dhidi ya mtangulizi wake Benjamin Mkapa yanazidi kipimo akalazimika kuonya wakosoaji hao kuwa wamwache ‘mzee’ huyo akapumzike baada ya kulitumikia taifa katika kipindi chake cha uongozi.

Hata kama angekuwa na aina fulani viashiria vya kisasi katika utawala wake dhidi ya utawala ulimtangulia, bila shaka Kikwete alikumbushwa utamaduni au desturi anayopaswa kuifuata pamoja na mamlaka makubwa aliyokuwa nayo.

Ya Kikwete tuyaache maana Rais wa awamu ya tano DK John Magufuli alishatamka hadharani na kwa mujibu wa katiba juu ya haki na stahili zote za viongozi wastaafu.Pamoja na kwamba bado kuna usiri katika hili, ambacho hakijaelezwa bayana ni iwapo wastaafu hao ni lazima wawe wanachama wa CCM!

Maswali ni mengi, kwamba kama angekuwa bado mwanachama wa CCM, Sumaye angepewa notisi ya siku 90 awe ameendeleza ardhi hiyo vinginevyo atanyang’anywa? Je ni kiongozi yupi mwingine mwenye ardhi ambayo haijaendelezwa mwenye wadhifa kama wa Sumaye atatajwa?

Vipi kuhusu Waziri Mkuu mwingine Edward Lowassa ambaye naye kama Sumaye aliachana na chama kilichowapa madaraka hayo? Marais wastaafu wote wameendeleza ardhi wanazomiliki? Vipi kina Malecela, Salimu Ahamed, Warioba, na Msuya?  Je, ni utamaduni mpya  wa kushughulikiana?

Kwa watu kama Freeman Mbowe ni jambo la kawaida kwa sababu hajawahi kuwa CCM na zaidi ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Hai hakuwahi kushika madaraka Serikalini .

Kama anachofanyiwa Sumaye ni matokeo ya siasa za visasi kama alivyonukuliwa akisema , basi ni jambo la hatari sana kwa mustakabali wa taifa, tunaotesha mbegu mbaya sana ya chuki na ulipizaji wa visasi na haitaishia kwa wanachama wa vyama vya upinzani bali utasambaa hadi kwa wanachama wa CCM.

Hakuna mwingine wakujitokeza kulikemea hili zaidi ya Rais Magufuli, akiruhusu aina hii ya laana haitamwacha salama hata yeye  kwa sababu ni sawa na kula nyama ya mtu, hakika hatoacha kwasababu akistaafu yeye na viongozi wa serikali yake nao wataandamwa tu na watakaopokea kijiti cha uongozi/utawala.

Yapo mambo yanapoamuliwa yanaonekana kuwa ya kawaida tu. Lakini matokeo yake yanapoonekana wazi baada ya muda hakuna anayejiuliza chanzo. Mambo yanapoharibika wote tunabaki kusingizia vitu visivyohusika. Mfano wa hili wapo baadhi ya watu ambao wakati wa utekelezaji wa Azimio la Arusha kuna dhuluma ilifanyika ndio maana nchi hii imedumaa.

Serikali haina dini, haiamini Mungu japo hapa ndipo unafiki ulipolala, hembu tujiulize hata kama kwa akili ya kawaida huwezi kukubali hili lakini huenda ni kweli, hivi tumeshawahi kujiuliza wale ambao mali zao zilitaifishwa zikiwemo nyumba nakadhalika wakati wa utekelezaji wa Azimio waliinenea nini nchi hii baada ya jasho lao kunyang’anywa?

Kama sheria ni msumeno basi ikate kila upande, Rais Magufuli kila mara anapojitokeza hadharani anasisitiza mshikamano, uzalendo, umoja na upendo miongoni mwa Watanzania. Anakemea wanaopalilia ubaguzi wa aina yoyote hasa ukabila, udini, ukanda, rangi na hadhi za watu katika jamii.

Sijui huko sirini ndani ya moyo wake maana hata kama aliwahi kusema yeye hajaribiwi kama ambavyo Mungu hajaribiwi lakini bado anabaki kuwa binadamu mwenye madhaifu kama walivyo wengine.

Jirani zetu Zambia ni mfano katika aina hii ya laana ya kulizana kisasi, Frederik Chiluba alimtupa mahabusu Rais wa kwanza wa taifa hilo Keneth Kaunda hadi pale Nyerere alipokwenda ‘kumkemea’ ndipo akamwachia.

Nani anajua kama matukio yanayoendelea katika nchi hiyo hivi sasa ikiwemo vifo vya viongozi wakuu vinatokana na laana baada ya Kaunda kutoa machozi yake? Sote tutafakari.