Home Makala NDUNGULILE: HAKUTAKUWAPO NA UHABA WA ARVS

NDUNGULILE: HAKUTAKUWAPO NA UHABA WA ARVS

251
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI

SEKTA ya afya ni mojawapo ya sekta muhimu ambayo inatumika kama injini ya kuinua sekta nyingine hasa ikizingatiwa ili maendeleo yapatikane lazima wazalishaji wawe na afya njema.

Hili ni jambo ambalo limekuwa likizuia Taifa letu kupiga hatua na kuchangia kurudisha nyuma maendeleo kutokana na ukosefu wa huduma stahiki za afya.

Katika kudadavua mambo muhimu yanayoisibu sekta ya afya nchini na RAI na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa masuala ya Ukimwi, Afya ya kina mama na watoto ya Taasisi ya Mabunge duniani (IPU), Dk. Faustine Ndungulile ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni (CCM) pamoja na mambo mengine aliuchambua mwaka mmoja wa Rais John Magufuli madarakani.

RAI: Novemba 5 mwaka huu Rais Magufuli ametimiza mwaka mmoja madarakani, unautathmini vipi muda huo aliokaa mdarakani kwa kuzingatia ahadi yake ya kuboresha huduma za afya nchini?

NDUNGULILE: Katika mwaka wa kwanza wa serikali ya Magufuli kuna mambo mengi amefanya, kwanza kurudisha nidhamu katika utumishi wa umma, kubana matumizi katika mambo ambayo si ya lazima kama warsha, makongamano na safari zilizokuwa zinachukua fedha nyingi, pili ni vita dhidi ya rushwa, baadhi ya watendaji wa serikali wameondolewa, na wengine kufikishwa mahakama kutokana na matumizi mabaya ya ofisi, pia upande wa maendeleo tunaona amefanikisha mpango wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga na sasa litaunganishwa na Kongo.

Pia maamuzi ya ujenzi wa reli ya kisasa Standard gauge ni maamuzi makubwa sana na ya gharama kubwa. Suala la elimu bure amelianza lakini pia lina changamoto, amefanikisha kuanzisha mahakama ya mafisadi.

Pia amefanikisha ujenzi wa daraja la Kigamboni na mradi wa Udart umetoa ajira nyingi, amefanikisha upatikanaji wa ndege mbili na nyingine zitakuja kuna suala la ujenzi wa fly over haya yote yameanza kufanyiwa kazi, kwa kweli ni mambo mengi ndani ya mwaka mmoja ni vitu vyenye muonekano.

Ila changamoto hazikosekani kwa sababu mahitaji ya rasilimali fedha ni makubwa kuliko makusanyo yetu. Pamoja na kufanya yote haya kwa fedha za ndani bado hazitoshelezi, kuna mambo ambayo kwa ushauri tungependa yafanyiwe kazi, kwanza ni huduma ya maji na afya. Huduma hizi zinatakiwa kupewa msukumo kwa sababu zinagusa maeneo mengi ya nchi.

Pili kuhakikisha hospitali zetu zinakuwa na dawa za kutosha. Hili ni jambo ambalo anatakiwa kuijengea uwezo MSD kuwa na fedha za kununua madawa kwani inaidai serikali fedha nyingi sana. Pia tunatakiwa kushirikisha sekta binafsi badala ya kutegemea rasilimali kutoka serikalini inabidi kuangalia namna ya kushirikisha sekta binafsi ili fedha nyingine zinazobaki zitumike katika mambo ya msingi hivyo kwa mwaka mmoja kuna mafanikio ila changamoto hazikosekani.

RAI: Licha ya Gavana wa Benki kuu kubainisha kuwa uchumia wa Taifa unakua lakini wananchi wamekuwa wakilia ukata, unafikiri hali hiyo italisaidia Taifa letu kupiga hatua katika nyanja mbalimbali?

NDUNGULILE: Rais alisema miaka ya nyuma fedha ilikuwa inapatikana kiholela kwa mtu kujipangia safari, warsha na mengine, hivyo fedha ilikuwa inapatikana nyingi mtaani na huyo mtu alikuwa na watu waliokuwa wanamtegemea, sasa hivi serikali imezikusanya kwenye taasisi zote binafsi sasa zimepelekwa benki kuu.

Na zile warsha na semina zilizokuwa zinafanyika katika mahoteli binafsi sasa zinanyika ndani ya kumbi za taasisi za umma, hivyo ni kweli serikali sasa haifanyi biashara na taasisi binafsi ndio maana hali ni ngumu na mzunguko umeondoka. Lakini niseme huu ni muda wa mpito, serikali inajipanga ndipo ianze kushirikiana na sekta binafsi kwa nidhamu na mzunguko wa fedha utaanza kuonekana na kila mtu kuishi kwa kipato halali.

RAI: Mbali ya kuwa Mwenyekiti wa IPU ila pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma za jamii, unafikiri nini kimesababisha kuwepo na uhaba wa dawa na chanjo nchini na unaishauri serikali ichukue hatua gani ili hali hiyo isijirudie tena?

NDUNGULILE: Mimi ni daktari na mjumbe kama ulivyobainisha, niseme kuna tatizo la uhaba wa dawa, kwa sababu serikali ilisema kuwa dawa zinapatikana kwa asilimia 65, ila tulifanya utafiti mdogo tu na wabunge wenzangu wajumbe wa kamati na kubaini dawa zinapatikana kwa asilimia 25 hadi 30.

Kimsingi kwa kauli ya serikali hawajafanya makosa kuwa zinapatikana kwa asilimia 65, ila kama mtaalamu wa afya nikienda kwa undani na kudadavua naona si dawa zile muhimu, mfano unakuwa na duka unasema huna mchele, unga, sukari, mafuta na chumvi, ila una viberiti, tambi na mengine… niseme serikali kusema ina asilimia 65 ni kweli ila si zile dawa muhimu ambazo zinahitajika kwa wagonjwa mara kwa mara.

Kubwa ni kuiwezesha MSD, kwa sababu serikali imekuwa haipeleki fedha za kutosha, ilisema imepeleka Sh bilioni 20 na kuongeza bajeti ya dawa na kufikia Sh bilioni 251. Lakini tunaona kuwa kila mwezi serikali inatakiwa kuipa MSD Sh bilioni 20, sasa hivi tunamaliza robo ya kwanza na zile zilitolewa Sh bilioni 20 ambayo ni ya mwezi mmoja ilimegwa na kutatua suala la chanjo. Ndio maana tumeishauri serikali kuwapa fedha ya kutosha angalau Sh bilioni 60 hadi  80 ya kuanzia ili MSD wanunue dawa za kutosha, kwa sababu manunuzi ya dawa nchi hii kwa wastani hadi wazipate ni miezi tisa, tukichelewa tunawachelewesha wananchi wetu kupata huduma.

 

RAI: Kumekuwapo na taarifa za kuwapo kwa uhaba wa dawa za kufubaza makali ya Ukimwi ARVs ifikapo Desemba mwaka huu, unawaambia nini Watanzania?

NDUNGULILE: Nimekuwa katika tasnia hii inayohusiana na usimamizi wa masuala ya Ukimwi kwa zaidi ya miaka nane, pia nilikuwa mjumbe wa bodi ya taasisi ya kimataifa ya masuala ya Ukimwi hivyo nimekuwa na uzoefu wa masuala haya ya Ukimwi ndani na kimataifa.

Niseme kwamba si kweli kuwa kuna uhaba wa dawa za Ukimwi, kwa sababu utaratibu unaotumika sasa katika ununuzi wa dawa hizo, unaitwa Pod procurement mechanism (PPM), ni kwamba dawa zinanunuliwa kwa ufadhili wa taasisi kubwa mbili, Global Fund na Pepfar wa serikali ya Marekani, zile fedha hazitumwi kwetu zinakusanywa duniani na kupitia taasisi za kimataifa za ugavi zinanunua dawa na kuleta nchini, yaani serikali inachofanya ni kusambaza tu, na sasa dawa hizo zipo za kutosha hakuna uhaba wa dawa, kinachokuja na watu hawajakielewa vizuri ni kwamba serikali inataka kutoka katika mfumo wa awali ambao mtu alikuwa akiugua Ukimwi anapimwa CD4 mwanzo ilikuwa zinazingatiwa 250 baadae 350 na baadae 500, ila sasa kuanzia mwakani serikali inakuja na mpango wa Test and Treat kwamba ukipima na kukutwa nao unaanza tiba papo hapo.

RAI: Unafikiri uwepo wa taasisi nyingi binafsi za masuala ya Ukimwi zumechangia kupunguza changamoto za janga hilo au zimechangia kuongeza?

NDUNGULILE: Taasisi nyingi zinahitajika kwa sababu serikali haiwezi kufanya mambo yote peke yake. Kinachohitaji ni uratibu na ufahamu. Lazima kuwepo na taasisi inayosimamia mpango wa Taifa wa Ukimwi kutoa mwelekeo na wapi sekta iende, pili kuwa na mfumo wa pamoja wa utendaji kazi.

Kinachofanyika sasa navyojua kwa sababu ni mmoja wa waanzilishi wa mpango wa utoaji wa dawa hizo mwaka 2004, najua taasisi hizi zimepewa maeneo ya kufanya kazi kwa mgawanyo wa kikanda hivyo hazina mwingiliano. Changamoto ni usimamizi ndio maana hivi karibuni kulitokea taasisi zinazohamasisha masuala ya ushoga na kuibua mjadala mpana na kusababisha vilainishi kuondolewa na baadhi ya taasisi kutaka kufungiwa hii yote ni suala la usimamizi, tunatambua maambukizi ni makubwa katika makundi yote hayo kama wanaofanya ngono kwa jinsia moja, madawa ya kulevya na uchangudoa.

RAI: Mji wa Kigamboni ni mojawapo ya miji ambayo imeandaliwa mkakati kabambe wa kuendelezwa kiuwekezaji, umejipanga vipi kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa uhakika?

NDUNGULILE: Kimsingi Kigamboni sasa ni wilaya, halmashauri mpya inayojitegemea. Ina watu 250,000, tuna vituo vya kutolea huduma za afya 28, 18 ni vya serikali vingine sekta binafsi, kuna hospitali moja na vituo vya afya viwili. Lakini havitoshi kwa sababu Kigamboni inakua sana.

Kwa kuanza tutaboresha hospitali ya vijibweni kwa kipindi hiki ili itumike kama hospitali ya wilaya. Sasa tunaitumia hospitali ya Temeke ambayo inahudumia watu zaidi ya milioni 1.6 ni wengi sana, tunataka kupunguza kwa kuboresha hosptali hiyo kwa sasa ili tuendelee kutafuta uwezo kujenga hosptali ya wilaya. Juhudi zinaendelea kupandisha hadhi vituo vya afya ili kukidhi mahitaji

RAI: Juni mwaka huu Kamati ya Bunge ya Ardhi na Maliasili ilibainisha kuwa serikali imeutelekeza mradi wa wakala wa uendelezaji wa mji mpya wa Kigamboni (KDA), je, ni kimeusibu mradi huu?

NDUNGULILE: Niseme kwamba mradi wa mji mpya Kigamboni umekuwa na changamoto nyingi na huu mwaka wa nane. Mradi umekwama na hakuna kinachoendelea ndio maana katika bajeti ambayo tumeipitisha hivi karibuni, KDA haina hata senti tano, pili KDA haina watumishi wa kutosha kwa sababu hawafiki 10.

Tumeiomba serikali pia nimekuwa nikimkumbusha waziri Lukuvi kuhusu maamuzi ya vikao tulivyokaa wadau wa kigamboni, madiwani na wenyeviti wa mitaa kwamba kwa kuwa Kigamboni imekuwa wilaya inayojitegemea, halmashauri inayojitegemea na mamlaka inayoweza kujipangia mji, kuwa na mamlaka mbili ambazo za kupanga mji ndani ya eneo moja inaweza kuleta mgongano.

Kwamba moja inaripoti serikali kuu lakini haina fedha wala rasilimali watu, inaweza kutuchelewesha kwa sababu sasa ni mwaka wa nane hakuna kitu, lakini pia hiyo KDA inasimnamia asilimia 12.7 ya ardhi ya Kigamboni na ni kata sita kati ya tisa za Kigamboni, hivyo inaifanya Halmashauri kusimamia kata tatu tu ambazo ni sawa na asilimia 88 ya ardhi, hivyo majukumu ya halmashauri yatakuwa yamefinywa sana.

Na itakuwa inasimamia maeneo ya kata za pembezoni wakati hizi kata sita ndio kata zenye vyanzo vya mapato. Tumeiomba serikali itukabidhi sisi ule mradi ili wakati tunasimamia uendelezaji wa Kigamboni tunaangalia kwa ujumla wake, tumekubaliana hivyo kwa vikao, wananchi wakapendekeza na kutoa maazimio na kumkabidhi waziri, sasa litaenda kwenye baraza la mawaziri ili lipitishwe na kuungwa mkono.

RAI: Unafikiri ubadhirifu ulioikumba miradi hiyo nayo imechangia mpango huo kudorora?

NDUNGULILE: Huu mradi wa Dege village ambao ni ubia kati ya Azimio na NSSF, ni mkubwa umekuwa ukifanywa na NSSF kwa kujenga nyumba pamoja na daraja la Kigamboni. Pia kuna taasisi kubwa ya michezo Real Madrid na Hospitali ya Apolo ambavyo vyote ni miradi ambayo tulitarajia kukamilika.

Kwa sababu ujenzi wa nyumba 7500 ungependezesha sana mji huu, ningependa kuiambia serikali itekeleze miradi hii mapema. Kuna changamoto za ubadhirifu na ripoti ya ukaguzi italetwa bungeni hivyo tutaishughulikia ila niwaambie mradi huu utaendelea kwa sababu hatuwezi kuacha yale magofu pale kwani tutabaini mapungufu na kuwachukulia hatua wahusika.

RAI: Kumekuwa na taarifa kuwa wabunge wa CCM mmeonywa kutoikosoa serikali hasa baada ya kuonesha makali yenu katika wiki ya kwanza ya Bunge linaloendelea mjini Dodoma, je, ni kweli?

NDUNGULILE: Ni suala la tafsiri tu kuwa wabunge wa CCM wameonywa kutoikosoa serikali, kwa sababu kwa mfano ule muswada wa sheria ya huduma za habari 2016, una mabadiliko makubwa sana, waandishi wa habari wenyewe walikuwa hawaelewani mfano kuhusu elimu limeondolewa, suala la kuungana na TBC wakati wa taarifa halipo, dressing code halipo, suala la kufutiwa leseni ya uandishi kwa kufanya kosa hilo halipo, kiujumla wajibu wa mbunge ni kuisimamia serikali hakuna kikao chochote ambacho kimekaa na kutuagiza kuwa tusiikosoe serikali, zaidi wanaleta viroja tu kuwa tumepewa Sh milioni 10 na mambo mengine.