Home Makala Mabenki na dhana ya kutokuwa rafiki kwa walio masikini

Mabenki na dhana ya kutokuwa rafiki kwa walio masikini

301
0
SHARE
Mohamed Yunus – Mbangladeshi aliyebuni benki ya mikopo midogo midogo kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya kiuchumni na ya kijamii kwa kutokea chini.

NA HILAL K SUED

Mabenki si rafiki kwa watu masikini. Katika orodha hiyo pia imo serikali na wanasiasa. Si rafiki kwa vitendo – labda ni kwa nadharia tu.

Kwa upande mwingine viongozi wa dini, wahisani, watoa zaka, wamasikini wenyewe na Muhammad Yunus ndiyo marafiki wakubwa wa watu masikini.

Muhammad Yunus ni Mbangladeshi na anasifika kwa ubunifu wake mkubwa katika kuanzisha na kufaulisha mfumo wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na watu wengine ambao ni masikini sana kuweza kupata mikopo kutoka mabenki ya kawaida – kwa kifupi Microfinance – unaotumika katika nchi nyingi duniani na kunufaisha kiuchumi mamilioni ya watu walio masikini. SACCOS ni mojawapo wa mfumo wa microfinance.

Mwaka 2007 Yunus, na benki yake ya Grameen Bank aliyoianzisha alitunukiwa Nishani ya amani ya Nobel kutokana na ”jitihada zake katika kusukuma maendeleo ya kiuchumni na ya kijamii kwa kutokea chini.”

Mark Twain, mtunzi wa riwaya Mmarekani aliyeishi katika karne ya 19 aliwahi kuwashambulia wamiliki wa mabenki kutokana na tabia yao ya kutojali kitu chochote. Aliandika: “Mmiliki wa benki ni mtu anayekuazima mwamvuli wake wakati jua linawaka, lakini anakunyang’anya punde tu mvua ikianza kunyesha.”

Na kama mabenki yanajigamba kwamba ni rafiki kwa wateja wao, kwa nini basi huzifunga kwa kamba kalamu zao kwenye kaunta zake?

Ukweli ni kwamba wamiliki wa mabenki wanafahamu historia huzidisha sana thamani ya vitu na kwamba kuficha fedha ni kitu cha mwisho mtu wa busara anaweza kukifanya.

Na hivyo ndivyo mabenki yalivyokuja kukua na kuendelea hadi sasa – kuwalazimisha watu hao “wa busara” kutoa fedha zao na kuzipeleka benki, kazi ambayo huwapa riba kwa kuzitunza – na baadaye kuzikopesha fedha hizo hizo kwa watu matajiri (siyo kwa watu masikini, angalia) na kuwatoza riba kubwa. Kwa ufupi mabenki hutoa huduma za kifedha kwa ajili ya kujipatia faida tu. Sasa mtu masikini yuko wapi hapo?

Kwa kawaida, mabenki hupata faida kutokana na tozo za miamala na riba yanayotoza kwa mikopo inayotoa. Hata hivyo katika miaka ya karibuni, hasa kutokana na viwango vidogo vya riba ambavyo hupunguza sana viwango vya upatikanaji wa faida kutokana na mikopo inayotoa. Mapato makubwa ya mabenki sasa hivi hutokana na tozo za miamala na uwekezaji katika miaradi yenye kubeba athari kubwa (riskier investments).

Na itakuwa si makosa kusema pia kwamba mabenki huibia watu – ingawa si kwa namna watu wanavyoiba kutoka mabenki. Katika enzi hizi za uhalifu wa kiteknolojia, wahalifu wengi pamoja na yale makundi ya kihalifu wameacha uhalifu wao wa kawaida wa kuvamia mabenki kwa kutumia silaha na kujikita katika wizi wa kutumia kalamu au compyuta.

Na kwa upande mwingine, siku hizi mabenki yanapendelea zaidi wakopaji (borrowers) kuliko wawekaji (savers). Aidha ni rahisi zaidi ‘kuwachuna’ wakopaji kwa sababu hawa si makini sana katika kusimamia fedha zao.

Mabenki yana historia ndefu sana na katika nchi nyingi yamekuwa yakitoa mwelekeo wa kiuchumi na kisiasa kwa karne nyingi. Tanzania polepole imekuwa ikiingia katika enzi hii ya siasa za kimabenki – au tuseme mabenki ya kisiasa? Hata hivyo ni kwa njia tofauti kabisa.

Katika kipindi cha pili cha utawala wa Awamu ya Nne – aliyekuwa Rais Jakaya Kikwete alitangaza kwamba serikali yake ilitenga sh 500 milioni kwa kila mikoa 21 ya Tanzania Bara kwa ajili ya kukopesha kwa watu wa kipato cha chini. Baadaye kiwango hicho kiliongezwa hadi sh bilioni moja kwa kila mkoa.

Hadi sasa safi kabisa – yaani kauli hiyo ilionyesha kwamba rais alikuwa anajali sana watu masikini – kwani alikuwa ni swahiba wao kwa hali na mali. Kwani kwa kuwa alikuwa anashindwa kuanzisha ajira milioni moja kwa ajili yao, asingeweza kushindwa kuhamasisha sh bilioni 21 kwa ajili ya watu masikini.

Aidha, ni wachache wangeweza kupinga kwamba kutokana na namna kauli ile ilivyotolewa, ilikuwa kama vile mtu ataamka asubuhi moja na kukuta muisururu mirefu ya watu katika sehemu za ulipapaji fedha hizo ili kujipatia fedha hizo tena bila ya masharti yoyote makubwa. Na bila shaka watu wengi walichukulia tangazo hilo kama ndiyo mwisho wa matatizo yao ya kila siku ya maisha.

Lakini baadaye walikuja kujua ukweli – ukweli hasa. Walikuja kutambua kwamba waombaji wa fedha hizo – zilizopachikwa jina la ‘Mabilioni ya Kikwete’ – sharti wapitie njia za kawaida za kupata mikopo – kama vile zile za watu matajiri wanavyokopa – ili kupata mikopo hiyo.

Swali ambalo wengi walijiuliza ni kwa nini masharti haya hayakutangazwa wakati tangazo hilo ya ‘mabilioni ya Kikwete’ ilipotolewa? Kwani kilichofuata ni kwamba maafisa wa mabenki walionekana kupata tabu kueleza kwa wananchi wakisema “samahani, masharti ya utoaji mikopo lazima yafuatwe.” Masharti haya ni kama vile dhamana na kadhalika.

Wadadisi wa mambo waliona kuwa suala zima lile la ‘mabilioni ya Kikwete’ lilikuwa ni la kisiasa zaidi na lililenga si tu kujijenga kisiasa, bali pia kuuondoa umma katika matatizo mengi ambayo utawala ulikuwa unakabiliana nayo wakati ule.

Aidha, tangazo hilo la mikopo lilikuja wakati zoezi kabambe lilikiwa likifanyika la kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo – wamachinga – pamoja na vioski vyao kutoka kati kati ya jiji la Dar es Salaam na hivyo ilikuwa ni namna ya kutoa faraja kwa waathirika wa zoezi hilo. Kwa Dar es Salaam ujumbe ulikuwa ni kwamba “utapata mkopo ukiondoka katikati ya Jiji na kwenda sehemu nyingine iliyotengwa.”

Ilikuwa ni wakati huo huo serikali ilipotangaza azma ya kuwajengea wamachinga majengio ya kudumu (Machinga Complex) ingawa uamuzi huo ulikuwa wa kisiasa zaidi kuliko kibiashara kwani hadi sasa fauida ya majengo yaliyojengwa maeneo ya Ilala kwa gharamna kubwa bado haijaonekana, mbali na mradi mzima kukumbwa na ufisadi, kama ilivyoripotiwa.