Home Makala Sera za Trump kwa Afrika ni kama hazipo

Sera za Trump kwa Afrika ni kama hazipo

465
0
SHARE

NA HILAL K SUED

INATARAJIWA masuala kuhusu Bara la Afrika yatateremka chini katika orodha ya vipaumbele vya sera za utawala wa Donald Trump. Hii ni kutokana na ukweli kwamba siku zote masuala ya sera za nje za Marekani huongozwa na masuala ya ndani na nje ya nchi hiyo.

Na yanapokuja masuala ya ndani Trump hataruhusu kufunguliwa milango ya ushawishi unaofanywa na Waafrika waishio Marekani (African diaspora), jamii ambayo kihistoria ndiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma agenda ya Bara la Afrika iingie katika sera za Marekani – kama ilivyokuwa kawaida huko nyuma.

Hii pengine inatokana na ukweli kwamba jamii hii (African dispora) iliyoko Marekani haikumsaidia kabisa Trump katika kampeni zake za uchaguzi kwa hivyo hakutarajiwi kuwepo kwa malipo ya fadhila. Aidha, inatarajiwa kwamba mwanga ambao Bara la Afrika ilikuwa nao pia utapungua sana hususani katika masuala ya kijamii, na pia jamii nzima ya Kiafrika nchini Marekani.

Aidha, hakutarajiwi kuwepo na uvumilivu wa fikra kwamba jamii ya Kiafrika nchini Marekani ni ‘eneo la sita’ la Bara la Afrika. Umoja wa Afrika (AU) unawatambua watu wa asili ya Afrika ambao huishi nje ya Bara kama ‘eneo la sita’ – maeneo mengine yakiwa Kusini, Mashariki, Kati, Magharibi na Kaskazini ya Afrika.

Yote haya hayatatiliwa maanani sana na rais mpya wa Marekani. Na isitoshe Trump anatarajiwa kutokuwa mvumilivu na huenda hata kutojali masuala ya siasa za ndani katika nchi za Afrika – labda tu itokee kwamba – na hili aliisha lielezea vyema katika hotuba yake ya ushindi – masuala yenyewe yatakuwa na mwelekeo katika masilahi ya Marekani yenyewe.

Kwa mfano, haitarajiwi Trump atavutiwa sana na yanayotokea Somalia au Ethiopia au maeneo mengine ya Bara la Afrika yenye migogoro. Hii inatokana na ukweli kwamba Trump hana uwezo mkubwa wa kufuatilia mambo kwa undani wake, hivyo inatarajiwa mambo haya ataishi nayo kwa mtazamo wa kijuu juu tu.

Na suala lingine linalotarajiwa kuuondoa utawala wa mpya wa Marekani kutoka desturi na mazoea kuhusu mahusiano yake na Bara la Afrika linatokana na kitendawili kwamba nani atachaguliwa kuwa Msaidizi wa Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani kuhusu masuala ya Afrika (Assistant-secretary of state for Africa).

Katika siasa za nje za Marekani kwa miaka 40 iliyopita ilikuwa rahisi, kila pale nafasi hiyo inapokuwa wazi, kujua nani atachaguliwa katika nafasi hiyo. Mifano ni pamoja na

Chester Crocker, Hank Cohen na Susan Rice.

Lakini sasa ni Donald Trump na hakuna kabisa kielelezo ni nani atashika nafasi hiyo. Na kwa kuzingatia hili, itakuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika, ikiwemo Afrika a Kusini kuwa na uelewa, umakini na uwazi katika chaguzi zao za watu watakaokuwa mabalozi wao nchini Marekani.

Teuzi hizi zitakuwa ni muhimu katika kufungua milango ya utawala mpya wa Trump. Kitu cha hovyo ambacho nchi za Afrika zinaweza kufanya, pamoja na ugumu wa hali yenyewe ilivyo, ni kuonyesha kutoridhishwa kwao na ujio wa Trump – au kuziba pua zao kwake.

Kwa upande mwingine masuala ya usalama ndiyo yatapewa kipaumbele mkubwa katika sera za Trump kwa nchi za nje. Na tunapozungumzia hili moja kwa moja linagusa Kamandi ya Marekani kwa Afrika (US African Command), iliyoanzishwa mwaka 2007.

Kamandi hii – kwa kifupi Africom – ni miongoni mwa maeneo sita ya kijiographia duniani yaliyobuniwa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) na liko chini ya Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo kuhusu masuala ya mahusiano ya kiulinzi na nchi za Bara la Afrika kupitia Umoja wa Afrika (AU) na taasisi zingine za ulinzi na usalama Barani Afrika.

Na linapokuja suala la sera za Marekani kwa Bara la Afrika, Africom ndiyo itaibuka na kuwa kiini cha mahusiano hayo. Na kutokana na msimamo mkali dhidi ya mataifa ya Kiisilamu, Africom ndiyo itakuwa kama jibu kwao.

Ni vyema nchi za Kiafrika zikakabiliana na hali hii vilivyo kwa sababu ni suala ambalo ndiyo kiini cha itikadi kuu ya Marekani duniani kwa wakati huu na linaweza kuyaweka mataifa ya Bara la Afrika katika migongano na China. Lakini iwapo nchi za Afrika zitaikabili vilivyo marekani kuhusu sera zake kupitia Africom ni suala la kusubiri tuone.

Lakini kwa hali yoyote ile, ni muhimu kwa nchi za Afrika kuwa angalifu sana katika kusimamia mahusiano yake na Marekani na China kwa wakati mmoja. Kwa muda mrefu Marekani imekuwa na sera za kutojali sana kuhusu Afrika, wakati China imekuwa ililikumbatia Bara la Afrika kwa ukaribu zaidi.

Lakini si kwamba hali hii ni mbaya sana kwa Afrika. Inatarajiwa Marekani itajaribu kukabiliana na hatua ambazo China imepiga ndani ya Bara la Afrika, suala ambalo viongozi wa Afrika wanaweza kulisimamia kiurahisi tu.

Ile Sheria ya Maendeleo na Fursa kwa nchi za Afrika – African Growth and Opportunity Act (AGOA), ambayo ilianza kutumika miaka 16 iliyopita ililenga kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya Marekani na nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.

AGOA ilikusudia kutoa chachu maendeleo ya kiuchumi, kusaidia mishikamano ya kiuchumi na kuwezesha eneo la Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara kushikamana na uchumi wa dunia.

Hata hivyo bado AGOA inao uzima — angalau kidogo. Lakini ni wazi kwamba Trump ni mtu ambaye atalinda nchi yake, hivyo hatavumilia upanuaji au uongezaji wa AGOA, ah hata hali yoyote ya sintiofahamu itokanayo. Hii ina maana kwamba sera za biashara za Trumb sharti ziangaliwe kwa makini.

Aidha kunatarajiwa kuwepo kwa upunguaji wa misaada ya Marekani kwa Afrika. Kwa baadhi ya nchi za Afrika, misaada kutoka Marekani ni kitu muhimu sana.

Chukulia nchi ya Malawi kwa mfano nchi ambayo bila shaka Trump atataka kitu kama mrejesho kutoka nchi hiyo – hasa ikizingatiwa kwamba yeye mwenyewe Trump ni mfanyabiashara aliyekuwa na mafanikio makubwa.

Hivyo atataka nchi za Afrika nazo zifanye namna yoyote ya uwekezaji nchini Marekani.

Makala hii imendikwa kutokana na vyanzo mbali mbali vya Intaneti.