Home Makala TUACHE SIASA ZA KUVIZIANA, TUWE WAKWELI KUISAIDIA NCHI YETU!

TUACHE SIASA ZA KUVIZIANA, TUWE WAKWELI KUISAIDIA NCHI YETU!

337
0
SHARE
Mrisho Gambo (kushoto) akisailimiana na Rais John Magufuli

NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA


LENGO la chama chochote cha siasa ni kushika madaraka na kuongoza dola bila kuzingatia sana njia na uhalali wa kufikia lengo hilo, mambo mengine yote ikiwemo kutekeleza ahadi za wakati wa kampeni yanafuata baadaye.

Ni mwaka moja sasa tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani na Chama Cha Mapinduzi ndicho kimeshika hatamu. Katika kipindi hicho tumeshuhudia mambo mengi yakitokea ikiwemo mageuzi makubwa ya kiuongozi ambayo yaliadimika katika miaka ya hivi karibuni.

Kabla sijaendelea, nikurudishe katika tukio kubwa la kiulimwengu la uchaguzi mkuu wa Marekani uliofanyika wiki mbili zilizopita ili kuweka msingi wa makala haya ya leo. Taifa la Marekani ni taifa kongwe, utawala wake ni mkongwe na kwakweli wanao uzoefu katika demokrasia na utawala ndio maana inajinasibu kuwa baba wa demokrasia ulimwenguni.

Yapo mambo ambayo yanaipa sifa Marekani, moja ni kwamba hakuna utitiri wa vyama vya siasa kama ilivyo kwa mataifa ya Afrika, pili ni kwamba uchaguzi unapomalizika tu dakika moja baada ya matokeo kuanza kujulikana yule mshindani aliyeshindwa haraka anampongeza mshindi na kuahidi kufanya naye kazi kwa masilahi ya taifa lao.

Kama nilivyosema hapo juu uchache wa vyama vya siasa unawapa fursa nzuri raia wa nchi hiyo kufanya uchaguzi sahihi na kwa umakini. Na hili la pili la kukubali haraka kushindwa na kumpongeza mshindi ni hatua ya kuimarisha msingi imara wa uzalendo na kuipenda nchi yao ambao wameujenga kwa miaka mingi.

Inawezekana upo msururu wa masuala lakini itoshe hayo mawili kuitofautisha taifa hilo na nchi nyingi za Afrika. Ni kweli mataifa ya Afrika yanaumri mdogo tangu zijitawale kulinganisha na nchi za Ulaya na Marekani lakini mabadiliko ya sayansi na teknolojia yameziharakisha nchi zote duniani kuwa ‘sawa’ kwa hiyo hakuna nchi kubwa kwa maana hiyo.

Tanzania kama zilivyo kwa nchi nyingi za kiafrika nayo ina siasa na demokrasia ya aina yake. Ni hapa ambako kiongozi wa ngazi ya juu serikalini anaweza kusema jambo lolote kana kwamba yeye ndiye muumba mbingu na ardhi.

Ni hapa Tanzania ambako kiongozi hawezi kukubali kushindwa uchaguzi isipokuwa mara zote kura zake huibwa na washindani wake. Ndio nchi ambayo upinzani siku zote ni uadui, wapinzani hawana haki kamili kuitwa raia wa nchi kama ilivyo kwa wale ambao wamejipa milki ya nchi.

Mathalani katika nchi hii wakuu wa mikoa na wale wa wilaya lazima watokane na chama kilichoshinda uchaguzi na kuunda dola. Kwa sasa CCM ndio inaongoza dola na kutawala.

Tumeshuhudia viongozi hawa ambao wanadhaniwa kuwa viongozi wa umma wakishindwa kuwajibika vyema kwa wananchi na badala yake wameegemea upande wa chama chao.

Ni jambo la kushangaza kidogo kuona viongozi hawa wanaoteuliwa kufikia hatua ya kudharau na kubeza viongozi waliochaguliwa na wananchi kama wabunge ,madiwani na wenyeviti wa vijiji na mitaa.

Hili ni tusi kama kweli tunafuata misingi iliyowekwa na waasisi wa demokrasia. Imefika mahali kazi ya viongozi hawa ni kuvizia wenzao wa upinzani ili siku inayofuata waende kwa wananchi na kueleza jinsi wapinzani walivyoshindwa kutumia nafasi ya kuchaguliwa kwao.

Baadhi ya viongozi hao siku za karibuni wamekuwa na tabia ya kuwaamuru watumishi wa sekta mbalimbali za umma na kuambatana nao katika ziara zao za Mikoa ama Wilaya. Mfano RC anaita mwakilishi wa shirika la umeme (Tanesco), au mtu wa wakala wa barabara na hata wale wa maji na hospitali.

Wakifika huko kwenye ziara inapofika zamu ya wananchi kusema kero zao maana kipengele hicho lazima kiwepo na kinawekwa kimkakati basi RC au DC huamuru kwa ukali wawakilishi hao kueleza siku ambayo wamaliza tatizo husika vinginevyo wamejifukuza kazi. Haya ndiyo yanayofanyika na ni siasa za kuviziana.

Wale wa upinzani nao hawana ubunifu, wakisikia RC au DC kafanya ziara kwenye Mtaa, Kijiji, Kata au Jimbo badala ya kushukuru hatua iliyofikiwa na kuwaeleza wananchi hao kuwa utatuzi wa kero iliyokuwa ikiwakabili umetokana na msukumo wake juu ya mgawanyo wa fedha zinazotokana na kodi zao, wao hukimbilia kusema kuwa wanahujumiwa na kutafuta huruma kutoka kwa wananchi.

Tabia hii iko kuanzia ngazi ya chini kabisa ya utawala wa wananchi mpaka ngazi ya juu kabisa. Wananchi hawaelewi hasa kinachoendelea, wanashuhudia tu jinsi ambavyo viongozi wao wakipita kwenye magari makubwa ya anasa huku wakiwa wamefunga vioo.

Matokeo ya haya hakuna maendeleo ya kweli yanayofikiwa, sio kutoka serikalini wala kutoka kwa viongozi wa upinzani. Hali huwa hivi kila baada ya miaka mitano, muongo moja , nusu karne na tusipoangalia tutafika karne moja yaani miaka 100 tangu tujitawale nchi hii itabaki ikiwa imedumaa.

Hakuna mzalendo wa kweli, kila anayepata nafasi hufanya mambo kana kwamba hapajawahi kuwa na Rais, mbunge au diwani katika nchi au eneo husika. Nchi haina ajenda yake inayoisimamia, mifumo yote imeparaganyika, na hasa mfumo wa elimu na mfumo wa uongozi na utawala.

Maajabu ya karne kwenye mfumo wa elimu, tukiacha wale wanaoitwa vilaza, ni Tanzania pekee ambako msomi wa kiwango cha Profesa anashindwa kuwa mbunifu hata akajiajiri na kuajiri maelfu ya vijana matokeo yake wanakimbilia maisha rahisi ya siasa, kuwa diwani au mbunge ili akafanye iasa za kuvizia. Hapa sijataja viwango vinavyofuata kwenda chini hadi ‘msomi’ wa gumbaro.

Kuparaganyika huku kumesababisha hata wasomi wetu kushindwa kujieleza kwa lugha walizotumia kujifunzia darasani. Bila shaka hizi ni hujuma toka na mkoloni aliyetutawala, ni bahati mbaya sana kama vile zumbukuku eti tunamwita jina zuri la mshirika wetu wa maendeleo, mara mfadhili na kadhalika wakati ni huyu huyu aliyechangia nchi kudumaa na kuwa kama ilivyo sasa.

Badala ya siasa hizi ambazo kila kiongozi mwenye mamlaka katika eneo lake la kazi anatafuta mnyonge wake ili alipize kisasi au aonyeshe umwamba, ni vizuri tukaiga wenzetu waliotutangulia.

Tukipata nafasi tusijione miungu watu, tukumbuke ahadi mojawapo ya mwana Tanu kuwa cheo ni dhamana tu, itafika siku ama utakufa au utakataliwa na wananchi usiwaongoze au utafukuzwa na aliyekuteuwa.Tuwe wakweli badala ya unafiki huu wa kujiita wazalendo uchwara.