Home Makala MWACHENI JPM AWANYOOSHE

MWACHENI JPM AWANYOOSHE

1239
0
SHARE

Na ABRAHAM GWANDU, Arusha


GARI linapoharibika kutokana na ajali baada kutumbukia korongoni, mathalani taa zimevunjika, magurudumu yametoka, bodi imebonyea, mmiliki hapeleki fundi mle ili alitengeneze bali atalikwamua kwanza ndipo mengine yafuate.

Wakati wa kulitoa korongoni mwenye gari hatojali sana uharibifu mwingine utakaoongezeka wakati wa zoezi hilo. Kama anatumia mtambo maalumu wa kunyanyua vitu vizito, mikwaruzo na kugongesha ni vitu ambavyo haviepukiki. La msingi ni kulitoa huko liliko.

Akishalikwamua sasa atamwita fundi ili afanye tathmini ya uharibifu uliosababishwa na ajali, ili hatimaye zoezi la matengenezo lifanyike na kisha kulirejesha gari katika hali yake ya awali, tayari kwa kulitumia kama mwanzo.

Kama ni gari la familia, kiongozi wa familia atakuwa mkali kutokana na hasara aliyopata kwa hiyo mambo mawili ni hakika. Moja ama dereva aliyesababisha ajali atafukuzwa  au atakumbushwa masharti ya kuliendesha gari na hata kuwekewa masharti mapya ili kumwadabisha.

Taifa letu ni kama gari lililopata ajali, kinachofanyika sasa ni kulikwamua hapa lilipokwama. Wengi tunanung’unika jinsi Serikali inavyotenda na kutekeleza mambo yake. Kuna wanaodai katiba ya nchi inavunjwa makusudi na hakuna anayewajibika au kuwajibishwa.

Wakati mwingine sheria na kanuni zinakiukwa waziwazi, wafanyakazi wa umma wanahaha, hawajui kesho yao. Mitaani wanasema wote tunaisoma namba barabara.

Usalama wao haupo katika sheria za nchi bali wanasubiri hatma yao kwa kuangalia uso wa kiongozi. Akiwa na makunyanzi wanajua kabisa hakuna ‘msaliemtume’ isipokuwa ni kurudi kijijini kwenda kuungana na wale waliobaki huko tangu kuhitimu elimu.

Hawa wanaozungumza chini chini na kulaumu hatua zinazochukuliwa maarufu kama kutumbua majipu hawatuambii ilikuwaje kama nchi tukaacha kutumia sheria nzuri tulizojitungia , kanuni na miongozo tuliyoweka kiasi cha kufikia hatua ya kutumbukia korongoni.

Ni sahihi kabisa kwamba nchi ina katiba yake, ni kweli kwamba kuna sheria tena nzuri tu, zipo kanuni, kuna sera na miongozo kadha wa kadhaa. Lakini hatujiulizi madudu yote yanayoibuliwa leo yamesababishwa na katiba, sheria, kanuni na blablaa zipi kama sio hizi?

Kweli fedha zimekosekana mtaani, lakini hakuna maana yoyote kwa fedha zilizotokana na mbinu chafu kuzunguka mtaani. Nyumba zilikuwa zinaota kama uyoga, anasa na starehe ndio ukawa mtindo wa maisha kwa tabaka fulani la watu.

Ilifika wakati mtumishi wa umma asiyeiba alionekana mjinga na asiyejua faida ya kuajiriwa na kuwa mtumishi wa uma. Bandari, TRA, BOT na mashirika mengine yenye kuzalisha faida yakawa shabaha ya wote wanaosaka ajira ili baada ya kipindi kifupi waingie mtaani kutamba.

Sasa ndio tumefahamu chanzo cha shabaha na matambo, kumbe ilikuwa ni jeuri iliyotokana na kuchepusha fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya wananchi. Kumbe ni fedha za wizi wa makontena bandarini, kumbe ni fedha zinazopelekwa katika mabenki ya biashara ili zizunguke halafu baada ya muda maofisa hao wanagawana faida.

Wakati maofisa hao wakigongesha bilauri ya mvinyo baada ya kuagawa faida iliyotokana na fedha za miradi ya wananchi, huko vijijini ambako miradi hiyo ilikuwa inufaishe, walengwa wanakufa na kiu ya kukosa maji, walengwa wanajifungulia njiani au sakafuni, walengwa hawana namna ya kufikisha mazao yao sokoni, watoto wa walengwa hawana vitabu shuleni. Ni sawa sawa na kumkaanga samaki kwa mafuta yake.
Juzi hapa Rais DK John Magufuli alivunja bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kisa cha kuivunja kwa mujibu wake ni kitendo cha kubariki fedha za TRA kuwekwa kwenye akaunti ya muda maalumu ‘fixed deposit account’ katika benki za biashara.

Hatua hiyo ya Rais, ni kengele ya kuwakumbusha watumishi wa umma juu ya agizo lake la kuhakikisha fedha zote zinawekwa kwenye akaunti maalumu ndani ya benki kuu ya Tanzania (BOT) ili zipangiwe matumizi kutoka huko.

Kwa mantiki hii bila shaka baada ya mwaka mmoja madarakani, wengi tunaanza kuelewa dhamira ya kiongozi huyu ambaye sio malaika lakini huenda akawa zimwi litujualo bila shaka hawezi kututafuna tukaisha.

Nikiri kabisa kuwa mimi sio muumini wa aina ya uongozi wa Rais Magufuli, uongozi wa amri mithili ya jeshini inayotaka kutekeleza kwanza kisha maswali kama utakubaliwa basi yafuate baadaye. Ila kwa mahali tulipokuwa tumefikia unaepukaje ‘staili’  hii ya uongozi?

Walioifikisha nchi hapa ilipo wamesomeshwa bure katika shule na vyuo vya umma. Wezi na watendaji wabovu wanaotumbuliwa leo wengi wao walipitia JKT mwaka mzima  kwa mujibu wa sheria. Huko walifundishwa uzalendo na kuipenda nchi, hawakufundishwa kwenda kuiba fedha za umma.

Sasa kama ‘askari’ hawa waliofunzwa nidhamu na uzalendo wakati wa kupigana vita dhidi ya maadui watatu wa taifa ambao ni umaskini, ujinga na maradhi wanaasi na kugeuka kuwa mamluki wanaosaidia adui, dawa yao ni ipi kama sio hii ya kutumbuliwa!

Kama nilivyosema Rais sio malaika, ni dhaifu pengine madhaifu yake yakawa makubwa mno ila yanafichwa na dhamira hii njema kama punje ya haradali kwa nini wazalendo tusimsaidie kwa kuonyesha majipu yalipo?

Nchi hii ni kubwa, macho ya Rais hayawezi kuona kila kona ya nchi, ni jukumu la wasaidizi wake kuonyesha matatizo yalipo, kama hawa wasaidizi wakikengeuka na kuwa askari waasi na mamluki basi ni jukumu letu sisi wananchi wazalendo kumsaidia ili walau kuirejesha nchi katika misingi yake.

Hatuwezi kufikia ndoto ya kuwa nchi ya viwanda, (sio vile vya Waziri Mwijage) hapana, viwanda vikubwa kama zilivyo nchi zilizofanya mapinduzi ya viwanda bila sote kuunga mkono hatua za kurejesha nidhamu na uwajibikaji kote nchini.

Ni heri nchi ikaendeshwa kwa amri za Rais kwa muda mfupi, kisha baadaye tukazirudia sheria zetu ambazo tulizipuuza bila kujali kwa vile nchi iligeuka kuwa nyumba ya kambale kila moja ana ndevu, au kama alivyowahi kusema mbunge God-bless Lema kuwa nchi imekuwa ghetto la wahuni.

Kwa hali iliyokuwa imefikia, ndugu Rais, tunyooshe tu maana hamna namna nyingine. Wakati wewe ukiendesha winchi unayotumia kulikwamua taifa letu, sisi nasi tunakusaidia ili usijekuligongesha likaharibika zaidi. Inawezekana tutimize wajibu wetu pale tulipo.