Home Makala TUSIULIZE ‘UHURU’ UTAONDOKA LINI!

TUSIULIZE ‘UHURU’ UTAONDOKA LINI!

316
0
SHARE

MIAKA nenda rudi umekuwa wimbo huo huo, hali ikirudiwa na kurudiwa. Kelele zimepigwa mpaka masikio yakaziba, na fedha za umma zimeendelea kuibwa!

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kila mwaka amekuwa akianika uoza na jinsi fedha za umma zinavyoibwa, lakini ‘hola’!

Kuna wakati ilisemwa kuwa watuhumiwa wa EPA, wengi wao wakiwa vigogo, waliambiwa kuwa wakirejesha fedha watasamehewa!

Na waliorejesha hawakufanywa kitu! Eti hizi ni sheria za hapa tu nchi ya Bongo, sheria ambazo haziko kokote duniani! Mtu anaiba fedha za umma halafu anachekewa! Sasa kwanini wajanja wasiibe?

Watanzania bwana ni watu wa ajabu. Mwizi aliyekalia ofisi ya umma anaporomosha jengo la mabilioni, huyu anaitwa mjanja, na anasifiwa kwa kujenga hekalu hilo la nguvu kwa fedha zao (Watanzania) zilizoibwa!

Eti waziri fulani anatumia cheo chake kukwapua fedha za umma, anapolazimishwa kuachia ofisi hiyo, anapokewa kishujaa na watu wa jimbo lake! Viongozi wangapi wamefanya kufuru hiyo na Watanzania wanawaangalia tu na kuwashangilia? Si watu hawa wanalelewa? Sasa kwa nini wasiwaibie ili wapate sifa? Si  Watanzania wanapenda na kufurahia kuibiwa bwana, eti?

Mfumuko wa bei wakati Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, anaingia madarakani ulikuwa takribani asilimia 3.5, baada ya miaka 10 ya uongozi wake, mfumuko wa bei ulipaa na kufikia asilimia zaidi ya 20!

Bei ya vyakula, vifaa vya ujenzi na vitu vingine muhimu katika maisha ya binadamu vilipaa kuliko uwezo wa Watanzania walio wengi! Ilikuwa balaa juu ya balaa! Lakini ni kweli hayo?

Na watu wachache waliendelea kuiba fedha za umma na kuendelea kusifiwa! Viongozi wenye dhamana waliwaangalia tu kama sinema! Waliweka chachu katika mfumuko wa bei!

Kwanini watu hawa wasiibe kama adhabu yao, ilipolazimika, ilikuwa kuondolewa tu kwenye ofisi za umma, basi! Hakuna adhabu nyingine iliyofuata baada ya hapo! Walioziba nafasi zao waliendeleza wizi huo huo! Eti nchi hii ilikuwa ni Shamba la Bibi?

Aidha, Watanzania walikuwa ‘wema’ kupita kiasi kuhusu fedha zilizopotea kwa njia ya misamaha ya kodi kwa miaka nenda rudi na kufikia Sh trilioni zisizohesabika! Kwamba kama makusanyo yangedhibitiwa kusingekuwa na haja ya kuomba fedha kutoka nje. Tungeweza kuendesha mambo yetu wenyewe bila kulazimika kukinga mabakuli kwa Wazungu! Lakini wajinga ndio waliwao, eti?

Nchi hii ilikuwa Shamba la Bibi ambako kila mjanja alivuna anavyopenda bila wasiwasi, na baada ya kuvuna alisifiwa na Watanzania wenyewe kwa ujanja huo hasi?! Eti acha fedha za umma ziibwe!

Kabla ya Uhuru wetu, watawala wa kikoloni walikuwa wakihamisha rasilimali zetu na kuzipeleka makwao kwa ajili ya kujenga nchi zao. Wananchi waliteseka kwa kuwafanyia kazi wakoloni. Walinyanyaswa vya kutosha!

Baada ya Uhuru, watawala weusi walianza kusahau manyanyaso waliyoyafanya wakoloni na kuanza kuwanyanyasa ndugu zao! Polepole wakaanza kuwaibia, na kasi ya kuiba ikawa inaongezeka! Badala ya kodi zao kuwaletea maendeleo, iliishia mifukoni mwa ‘wajanja’ waliokabidhiwa ofisi za umma wakati wao wakiishi maisha hohehahe!

Maana ya Uhuru ilipotea, na mwishowe Watanzania waliaanza kuhoji lini ‘Uhuru’ walioupata utaondoka kama alivyoondoka mkoloni!

Hivi sasa Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli imekuwa tofauti kwa kiwango kikubwa. Amekuwa akiwatumbua wale wanaotumia vyeo vyao kujinufaisha binafsi. Aliowatumbua si haba.

Lakini kazi ameimaliza? Maana kuna wananchi wengi wanaongoja waendelee kuguswa na utumbuaji wa Dk. Magufuli.

Wako waliojihusisha au kufaidika na utapeli wa Escrow ambayo imeijeruhi nchi kupindukia. Wananchi wanasubiri Rais Dk. Magufuli atumbue watu hawa kwa faida ya nchi.

Awafanye wajione kama maana ya Uhuru haijapotea, ili wasije mwishowe wakaanza kuuliza na kuhoji lini ‘Uhuru’ walioupata utaondoka kama alivyoondoka mkoloni!

Rais Dk. Magufuli bila shaka hatakubali hali iwe hivyo, na hatabadili nia hadi mwisho wa safari. Aidha, hataonyesha kupwaya.

Macho ya Watanzania hivi sasa ni kodo kwa hili.