Home Makala RAIS MAGUFULI AACHE UTANI KIDOGO!

RAIS MAGUFULI AACHE UTANI KIDOGO!

485
0
SHARE

Na MARKUS MPANGALA


SAKATA la kusitishwa uzalishaji wa saruji katika kiwanda cha Dangote mkoani Mtwara limenifikirisha na kunirudisha kwenye mawazo ya vita kali ya kunufaika katika biashara na ufanisi wa viwanda.

Kwanza natambua namna Rais wa awamu ya Tano, John Pombe Magufuli anavyosisitiza suala la Tanzania ya viwanda. Pili, napenda kumkumbusha kuwa asidhani suala la Tanzania ya viwanda litakuja kirahisi, bali kwa vita. Asitegemee kuona ufanisi wa viwanda utakuja kirahisi kama anavyodhani kwakuwa tunafahamu namna vita kali iliyopo kwenye sekta hiyo.

Ni lazima Rais Magufuli atambue kuwa biashara na viwanda ni vita kali ambayo inaacha majeruhi wengi kote duniani. Kwenye suala la Tanzania ya viwanda hakuna mtu wala taifa ambalo litamchekea kwa gego na fizi. Hakuna tabasamu la upendo kutoka kwa akina Narendra Modi, Mfalme Mohammed wa Morocco au mataifa yoyote duniani.

Hakuna nchi ambayo itashirikiana na Tanzania kwenye sekta ya viwanda halafu tukategemea urahisi, kwani wengine watafanya ujasusi wa kibiashara (Economic Intelligence) kutumaliza.

Natambua kuwa Aliko Dangote alifanikiwa kujenga viwanda vitano vya saruji kati ya mwaka 2014 na 2015, katika nchi za Tanzania, Cameroon na Zambia bila shaka. Katika hatua hiyo Dangote anajua soko la saruji, anafahamu utamaduni wa kimafia wa ufanisi wa viwanda. Anajua ujanja wa kibiashara na maendeleo ya viwanda.

Hakuna njia rahisi ambayo tunaweza kufanikiwa  bila kutolewa jasho, kuliwa na ikiwezekana kudhulumiwa kidogo. Mathalani, katika soko la dunia bei ya korosha ni shilingi za kitanzania 19,000 kwa kilo moja. Lakini mkulima wa korosho kule Lindi anafanya sherehe baada ya kuiuza kwa shilingi 3,000 kwa kilo. Hii ndiyo tofauti ya maendeleo na utani wa kimaendeleo.

Dangote si mwenzetu kibiashara na viwanda. Anazijua rafu na vurugu zote zinazotawala sekta hiyo kwa hiyo ni lazima Rais Magufuli atambue kuwa yuko kwenye mapigano makali na mataifa makubwa nje na wadau wa viwanda wa ndani.

Ni lazima akubali kuwa vita vya kibiashara na viwanda haimaliziwi kwa matamko wala maneno matamu, bali ni suala la msimamo na kuyajua maslahi ya nchi pamoja na kuzungumza vizuri na wawekezaji kwa mujibu wa sheria. Ajue hakuna mwekezaji anayekataa ‘kupendelewa’ na ikibidi ‘apendelewe’ kwa maslahi ya nchi.

Suala la Saruji ya Dangote limenirudisha kwenye masimulizi ya mwanazuoni Yash Tandon kwenye kitabu cha ‘Trade Is War: The West’s War Against the World”.  Sura ya tatu ya kitabu hiki mwandishi ameipa jina la “EPAs; Europe’s Trade war on Africa. Anasema ili kuielewa Afrika, ni muhimu na wajibu kuielewa Ulaya. Ni sawa na kuelewa mtu alivyo masikini kuuelewa utajiri.

Anasema mahusiano ya Afrika na Ulaya yamejikita katika maeneo manne. Kwanza ni mkutano wa Berlin (Berlin Conference) iliyogawa Afrika, uvamizi na mapambano dhidi ya ukoloni.

Pili, uhusiano kya Afrika na ulaya unahusishwa kwenye madaraka (yaani Ulaya kuitawala Afrika katika kila nyanja). Tatu, uhusiano wa mabara haya umejengwa kitaasisi, kiutamaduni, tabia za pande zote. Nne, ujenzi wa ukoloni na mikataba mbalimbali ya kibiashara ndiyo inalitafsiri bara la Afrika leo.

Katika sehemu hii mwandishi amegawa maeneo matatu:

Mosi, masuala ya historia baina ya Mabara haya katika mikataba (The Historical Context). Anasema tukitazama mkataba wa Cotonou (2000) kati ya Afrika na Ulaya hakuna tofauti na ule ulioletwa mwaka 2001 yaani EPA.

Hapa anaelezea namna mataifa ya Ulaya yalivyonufaika na rasilimali za Afrika kimaandishi ambayo inadaiwa kuwa ushirikiano wa kiuchumi. Kwamba bidhaa za Ulaya zina uwezo kupenya katika soko la Afrika ambalo linazingirwa na mikataba hiyo, hivyo kutokuwa na ufanisi wa uzalishaji viwandani.

Vilevile anazungumzia mbinu za kudhibiti fedha za Afrika kama vile mikopo na mitaji ikiwemo kupenyeza ushawishi katika siasa za nchi yoyote. Anaonyesha namna Afrika ilivyotumika kuisaidia ulaya wakati wa vita vya pili vya dunia. Anasema Afrika ilikuwa inatoa chakula, bidhaa, fedha na kadhalika.

Vita kubwa walivyonavyo Ulaya na Marekani dhidi ya Afrika ni kuhusu masoko na rasilimali zake. Kwa maana hiyo mchuano wa rasilimali unazidi kuwapa mwanya wa kutengeneza mikataba yenye kubadili maneno tu, huku madhumuni yakiwa yaleyale.

Anakumbusha juu ya unyonyaji wa mkataba wa EU-ACP Cotonou (huu ni tofauti na ule wa Cotonou, isipokuwa malengo ni yaleyale). Hapa tuelewane pia, tunajua kulikuwa na makoloni, mkishasaini mkataba wao wa biashara, wao wanagawana nchi za kujikita. Ufaransa anabaki na Francophone, Uingereza na Anglophone, Ureno na makoloni yake. Marekani huwa na ubia na mataifa rafiki (Uingereza, Ujerumankli n.k).

Sehemu ya pili ameipa jina la ‘Contemporay Euro-Africa Trade Reletions’. Anasema kutoka mikataba hiyo kukaja kuibuliwa mingine ya REPA, EPA, IEPA, FEPA, CEPA, lakini maudhui na madhumuni ni kuendelea kudhibiti soko, mitaji, na fedha.

Hapa inabidi tuelewane, baada ya kuunda mikataba hiyo wanachofanya ni kutengeneza asasi za kutoa ushauri. Asasi hizo ndo zinakuja kushauri, zinawanasa wanasiasa (wabunge) wenye ushawishi, watu binafsi wenye ushawishi, madalali (lobbyists) ambao wanatia ushawishi kwenye taasisi za serikali zilizolengwa. Na hata kwenye sakata la Dangote wapo watu sampuli hiyo.

Ndio maana hapa mpaka leo rais mstaafu Benjamin Mkapa anasikitika kuwa ubinafsishaji ulipaswa kuwa na chombo cha uhakiki wa Sera hiyo (Hata hivyo alishanaswa, japo alitaka mabadiliko, hivyo asingeweza kuponyoka wala kufikiri suala la chombo hicho).

Kwa kawaida tukibinafsisha hapakuwa na chombo cha ukaguzi wala uhakika wa maendeleo ya mashirika au viwanda vilivyobinafishwa. Anatolea mfano ACP-Wide Consultant, ACP Action Plan na nyinginezo.

Hapa ndipo twaweza kuona taasisi moja ilikuwa ikitoa ushauri kwenye sekta ya madini (ilitoka Canada). Na hapa ndipo anaingia rais mstaafu Kikwete kama mtu aliyetegemewa mno kutia saini mkataba wa EPA baada ya utawala wa Mkapa kutia ngumu.

Tunakumbuka kwenye mkutano WEF (World Economic Forum) pale Mlimani City jijini Dar es Salaam miaka ya nyuma Mkapa alitoa hotuba kali kuzionya nchi za Afrika juu ya EPA. Yawezekana Kikwete alisoma mchezo, kaendesha suala hilo kijanja janja hadi kamaliza muda wake bila kusaini.

Tunaweza kuyapata maelezo hayo katika ukurasa wa 73 wa kitabu hicho ambapo mwandishi ameipa jina la ‘How the people of East Africa Trounced the Economic Commision’. Ili kushamirisha hoja yetu ya leo inabidi tukumbushane masharti ya mkataba wa FEPA(Framework Economic Partnership) ambao ulikuwapo kabla ya EPA (Economic Partnership Agreement).

 

Masharti ya FEPA;

1.Kupunguzwa ushuru wa bidhaa za nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya kwa asilimia 80.

  1. Kuruhusu kuingizwa bidhaa kutoka Ulaya zenye thamani kubwa kwa asilimia 17.4 na kukinda soko lake.

 

  1. Kuleta chakula cha ziada kama kunatokea matatizo ya kisiasa kwa nchi za wanachama wa EAC.

 

  1. Kwa mujibu wa ibara ya 13 ya mkataba ilitaka kutoongezwa ushuru bidhaa za nje kwa miaka 25.

 

  1. Ibara ya 15 ya FEPA ongezeko la kodi katika usafirishaji wa bidhaa za EAC kwenda Ulaya halitaruhusiwa.

 

  1. Ibara ya 16 ya FEPA ilisema ushirikiano wowote Kati ya nchi za EAC na China, India au Brazil ni lazima uzishirkishe nchi za jumuiya ya Ulaya.

 

Tumekataa EPA tumetumbukia KTC

Katika msingi huo tunakubaliana kuwa mkataba wa EPA ulikuwa mbaya. Tunakubaliana kuwa EPA ni mkataba ambao haufai kwa maendeleo yetu ya viwanda.

Tunakubaliana kuwa EPA hauna maslahi kwa sababu kwanza tuko katika kundi la nchi za zenye kiwango kidogo cha maendeleo ambapo tunapewa uhuru kwenye soko la Jumuiya ya Ulaya na Marekani.

Katika moja ya vipengere vya mkataba kinadai kama nchi itapata hasara kwa kuingia mkataba huu basi nchi hiyo ipandishe tozo ya VAT kufidia.

Kwamba wanatuambia tukapopata hasara ya kusamehee wao kodi basi wananchi wetu wabebe hasara hiyo kwa kuongezewa VAT, bila shaka wanajua hasara iliyotarajiwa kwetu. Aidha, hasara hiyo ilitakiwa kudumu kwa miaka 25 ya mkataba ulivyotaka. Je Magufuli anafahamu namna vita vya kibiashara vinavyokwenda?

Wakati tunajiuliza hilo ni vizuri kuikumbuka Kurasini Trade Center (KTC) ambayo tumeingia nayo mkataba na serikali ya China. Kwamba Kurasini Trade Center ni soko la biashara la wachina ambapo wataingiza bidhaa zao bila kodi na kuziuza pale. Bila shaka chochote kile tulichokataa kwenye mkataba wa EPA ndio wachina tumewapa kuendesha soko letu bila kulipa kodi.

Tutashuhudia bidhaa kutoka China zikipatikana hapo badala ya kwenda huko China. Tumeambiwa wafanyabiashara wa kigeni kutoka Zambia na watu wa nchi jirani watakuja Kurasini kununua bidhaa badala ya wao kwenda China.

Kwa maana hiyo Tanzania tunakuwa kituo kikubwa cha biashara za China. Nini maana yake? Kwamba bidhaa zitatoka viwandani China siyo Tanzania. Bidhaa za viwanda vya Tanzania zitauzwa wapi? Ni namna gani Rais Magufuli na serikali yao wameona vita hivi vya kibiashara? Unatuambia unataka viwanda wakati unafungua soko la viwanda vya mwenzio auzie kwako bure?

Kuna manung’uniko juu ya hiyo KTC. Inaelezwa kuwa itaua soko la Kariakoo. Sasa hivi kabla ya kuanza KTC, wachina wamelishika soko la Kariakoo lakini kuna unafuu kwa sababu wao na wazawa wote wanacheza kwa sheria sawa.

Litakapoanza soko la Kurasini maana yake itakuwa ngumu kwakuwa watakuwa hawalipi kodi bidhaa zao na itawapa nafasi kwenye bei kuwa rahisi. Kwahiyo tunajua kuwa soko litakuwa na Wachina na bidhaa zao kutoka katika viwanda vyao. Ni kwa vipi sisi tutamudu kuingiza bidhaa zetu katika soko hilo?

Sote tunatambua kuwa Wachina, Wavietnam, na watu wa India wote bado wana njaa, na wanatuona sisi kama washindani wao, kamwe hawawezi kukubali tuwe na viwanda kuwazidi. Katika mazingira tuliyonayo tutamudu vipi vita vya biashara na viwanda kama ya Dangote inatutosha jasho?