Home Latest News KATIBU MKUU UJASIRI WAKO UTATUOKOA, TUSAIDIE WANACCM

KATIBU MKUU UJASIRI WAKO UTATUOKOA, TUSAIDIE WANACCM

273
0
SHARE
Rais John Magufuli akimsikiliza kwa makini Abdulrahman Kinana

KWA heshima kubwa na unyenyekevu pokea salamu ya chama chetu Katibu mkuu jasiri uliyetuvusha enzi za mkuu wetu mstaafu, pole sana na majukumu ya kukijenga chama chetu kikongwe chenye heshima iliyotukuka Afrika na duniani kote, pamoja na ukimya wako mkubwa nasema pole na majukumu baba yangu katibu mkuu wetu.

Katibu mkuu wetu jasiri uliyewatandika mawaziri mizigo kipindi kile bila huruma kwa masilahi ya chama chetu na Taifa letu kipindi hiki ujasiri wako ni muhimu sana tafadhari Katibu mkuu naomba uvae bomu ukaseme japo na Mwenyekiti wetu mpendwa wanachama na watanzania tutakuombea bomu lisikulipukie, tafadhari katibu mkuu wetu nenda kamsihi m/kiti wetu najua wewe ni jasiri sana.

Katibu mkuu wetu mwenye heshima na ujasiri wenye ujazo wa kumwagika kaseme na m/kiti wetu haya machache tafadhari.

Mosi, Kamwambie watumishi wa umma wamepoteza matumaini hawajui hatima yao, Katibu mkuu sema bila woga mwambie watumishi wa umma mioyo yao imejaa hasira dhidi yake, hasira na chuki vimekolezwa na uhakiki wa watumishi hewa wenye tija uliofunga na kusitisha masilahi ya walio waadilifu, mwambie uchangiaji wa mbio za mwenge na kulazimishwa kukesha kwenye mwenge vilichochea chuki na moyo wa visasi kwa watumishi, Katibu mkuu wetu jasiri sana sema na m/kiti wetu hasira za watumishi hazionekani usoni lakini ni kali kuliko za simba aliyekoswa risasi.

Pili, Katibu mkuu wetu mwambie wanachuo na wasomi hawamuelewi kabisa bado unaitafuta kwa tochi njia yake anayotumia kutuvusha tena wanachuo wamejaa chuki na hasira inayongoja kulipuka, Katibu mkuu wetu tafadhari jifunge bomu ukaseme na m/kiti wetu nenda tafadhali tunakuombea usilipuke mwambie bodi ya mikopo imekoleza hasira kwa wanachuo, msisitize suala la katiba mpya limechemsha hasira ya wasomi wenye kuifikria kesho ya vizazi vingine.

Tatu, Katibu mkuu wetu msihi m/kiti wetu awaruhusu watani zetu wapaze sauti zao, wapige kelele na kutangaza mambo yao kwa wananchi wayazoee, wananchi wakizoea watapuuza kama kwa baba yetu mstaafu kuwazuia kunaleta maswali magumu yasiyojibika siku za usoni, mwambie watani zetu watatushtaki kwa wananchi na kutupakazia kuwa tumewazuia/tuliwazua wasiseme madhaifu, tafadhari mwambie siasa ni kusemana kwa kupokezana tafadhali katibu mkuu wetu kaseme nae.

Nne, Katibu mkuu wetu mwenye busara ya aina yake mwambie waheshimiwa wanaogopa kurudi majimboni maswali ya ahadi zake hayajibiki, wapiga kura wanadai viwanda, wanakijiji wanadai mipesa yao, wapiga kura wamechachamaa kwa waheshimiwa wao wanataka majibu ya ahadi za m/kiti wetu kipindi cha mapambano, tafadhali, chonde chonde katibu mkuu wetu kaseme nae sisi tunaogopa nenda baba yangu kaseme nae tunakuombea.

Tano, Katibu mkuu wetu mwambie m/kiti wetu benki zimesitisha mikopo kwa muda usiojulikana, mwambie tafadhali wewe ni jasiri sana uliwaseme wale mizigo sema nae m/kiti wetu tena mwambie wahitimu wameamua kujiajiri tatizo mitaji benki zimesitisha kukopesha tena nasikia chanzo ni mkazo wa m/kiti mwambie usiogope maana tupo nyuma yako kwa maombi.

Sita, Katibu mkuu wetu mwambie m/kiti wateule wake wamekuwa makatili, wanajiona bora kuliko watendaji wengine, wanatunisha misuli na kuwachapa watendaji wataalam badala ya kushirikiana nao, mwambie m/kiti wetu wateule wake hawana hata huruma ya wapiga kura wake, mwambie yaliyotokea kanda ya ziwa ni tone la maji katika bahari, huku kusiko na kamera wanyonge wananyongwe kweli kweli. Katibu mkuu wetu sema na m/kiti wateule wake watamgharimu msimu wa mapambano kurudi kwenye kiti.

Saba, Katibu mkuu jasiri wa viwango mwambie m/kiti wetu wapiga kura wake wamemkumbuka mstaafu wanatamani kumuomba msamaha kwa mabaya waliyomsema, tafadhali hili halifurahishi mwambie ajitahidi kuwafanya wampende yeye kuliko kutamani waliomaliza warudie, mwambie ni hatari wapiga kura kujutia ni chanzo cha balaa kwenye mapambano yajayo.

Nane, Jasiri uliyetukuka katibu mkuu wetu mwambie m/kiti wetu aruhusu Bunge liwe ‘live’ kama yeye alivyo ‘live’ , mwambie wapiga kura ni wadadisi sana huku wanauliza mbona m/kiti anajirusha ‘live’ inamaana gharama za kurusha ‘live’ zipo kwa wabunge tu, mbona hata mazungumzo ya hapa na pale anajirusha ‘live’ au yeye ndiyo mwenye haki pekee, tafadhali mwambie usiogope kama wenzako wewe ni jasiri mno.

Tisa, Katibu mkuu wetu mwambie m/kiti wapambe wake tuliompigania kipindi cha kusaka kiti tunaulizwa maswali mazito yenye mitego kuyajibu lazima uwe jasiri usiyeogopa kusema uongo, wanauliza msimamo wa m/kiti ni upi kusitisha sherehe za uhuru kuokoa matumizi au kufanya sherehe za uhuru pasipo matumizi ?, msimamo wake kuondoa mzigo wa kodi kwa wanyonge au kuchukua kidogo cha wanyonge kijenge uchumi wetu, wanauliza upendeleo hasa kanda ya ziwa wachuuzi wamepoteza mali za walizopata kwa jasho lenye damu wasababishi wamesemwa tu lakini wale walimu waliomchapa mtoto kwa dhamira nje walichukuliwa hatua haraka sana, tafadhali katibu mkuu wetu ujasiri wako ni muhimu tusaidie .

10, jasiri mwenye msimamo nakusihi na kukuomba mwambie m/kiti wetu wakumbuke katiba yetu, sheria zetu na taratibu tulizojiwekea wenyewe katika kufanya mambo, msihi akumbuke Sheria ya manunuzi, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, akumbuke uhuru na mipaka tafadhari sema usiogope kama hao wengine wewe ni jasiri kila mtu anatambua ujasiri wako ulivyo, mwambie kama kanuni zetu, sheria zetu, katiba yetu ni kikwazo cha kufika tuendapo afuate utaratibu kuvitoa kama ni kero lakini akumbuke kuna kesho ya m/kiti mwingine mwenye dhamira na malengo yake.

Mwisho, Katibu mkuu wetu mwenye heshima hapa na kwingineko kote ujasiri wako ndiyo kitu pekee kinachoweza kutuvusha na kutuokoa, tafadhari tunaomba ujasiri wako urahisishe mapambano ya kiti msimu ujao, tafadhali mwambie tunampenda sana, tunatambua juhudi zake, tunaheshimu dhamira yake njema, tunajua anakusudia kufanya mema lakini siku hazigandi, tena mwambie ikiwezekana amfuate mstaafu amdokeze mbinu zake asipambane mwenyewe huenda kuna mikoba hajakabithiwa tafadhari msihi. Katibu mkuu wetu nenda kwa unyenyekevu, nenda kwa mwendo wa pole hasira zake zisikuumize bado tunahitaji utendaji wako uliotukuka, uliweza kupiga safari nchi nzima kujenga chama chetu, uliweza kukemea mizigo iliyomlemea mstaafu wetu, uliweza kusema na kuwakemea wavuruga chama hakika nina hakika hili la kusema na m/kiti wetu mpendwa ni jepesi mno kwako.

Mungu akutangulie katika kusema na m/kiti wetu, nina hakika utaupata ujumbe wangu na kuufanyia kazi nimesema kwa niaba ya mioyo ya wapiga kura sijasema kwa ubinafsi maana naogopa msimu ujao tusiruke sarakasi kwenye majukwaa kuomba kura. Mungu akubariki Katibu mkuu wetu jasiri, kila kheri katika utendaji wako mtukufu.

Ndimi mwanachama mtiifu Lamu Elizayo Pascal Kilimba
lamuelizayo@gmail.com
+255766033331