Home Latest News RAHCO: TUTAIUNGANISHA D’SALAAM KWA RELI KUPUNGUZA MSONGAMANO

RAHCO: TUTAIUNGANISHA D’SALAAM KWA RELI KUPUNGUZA MSONGAMANO

349
0
SHARE
Ofisa Uhusiano wa RAHCO, Catherine Moshi

NA VERONICA ROMWALD,

KAMPUNI hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO) ilianzishwa na serikali mwaka 2002 baada ya kubinafsishwa kwa shirika la reli Tanzania (TRC).

TRC ilipobinafsishwa serikali ilipeleka mswada bungeni ambapo iliazimia kuanzishwa kwa shirika la kusimamia miundombinu ya reli nchini hivyo mwaka 2002 baada ya kutungwa kwa sheria ya reli RAHCO ikaanzishwa rasmi.

RAHCO ilipewa jukumu la kusimamia miundombinu ya reli, kuiendeleza na kulipa madeni yote yaliyokuwa yakidaiwa TRC pamoja na kuingia mikataba na makampuni ambayo yanataka kufanya kazi kwenye njia ya reli.

Ofisa Uhusiano wa RAHCO, Catherine Moshi, anasema mbali na  RAHCO, serikali pia ilianzisha TRL na kutengenezwa makubaliano na kila moja kupewa majukumu yake.

“Sisi (RAHCO) kazi yetu ni kujenga, tukishajenga, tunaruhusu watu mbalimbali kuja kuwekeza kwenye reli, lakini kwa kuwa miundombinu yetu haipo sawasawa ndio maana mnaona ipo TRL peke yake. TRL ni operator, kimsingi alitakiwa awe anatulipa kiasi cha fedha ‘concession fee’ kwa mujibu wa makubaliano.

“Iwapo wangekuwa wanatulipa ingesaidia RAHCO kupata mapato yake ya kujiendesha na hata tusingekuwa na sababu ya kusubiri fedha ya serikali,  tungekuwa na miundombinu mizuri tungeweza kujiendesha kama ambavyo mnaona kwenye barabara, kule TANROAD anajenga na anasimamia, hivyo tungekuwa na ma-oparator weng na tungekuwa na miradi mingi,” anasema.

Anasema ingawa yote ni mashirika ya serikali hata hivyo kumekuwa na mwingiliano wa kimajukumu ambayo kwa namna moja au nyingine hukwamisha maendeleo ya sekta hiyo.

“Nimeeleza awali kwamba RAHCO ina jukumu la kujenga miundombinu ya reli lakini kuna baadhi ya mambo yanaleta mgongano kidogo, kwa mfano linapokuja suala la kurekebisha miundombinu ya reli wakati mwingine wale wa TRL wanasema si jukumu lao, lipo chini ya RAHCO wakati mkataba ule unaeleza ukarabati utafanywa na TRL iwapo gharama ni chini ya Dola 100,000.

“Ikiwa zaidi ya hapo jukumu hilo linakuwa la RAHCO kwa mfano madaraja yanapobomoka au reli zinaposombwa na maji ya mafuriko, ni jukumu letu RAHCO, kwa hiyo kuna changamoto kadhaa zinajitokeza lakini zinashughulikiwa na tunasonga mbele kuwatumikia wananchi,” anasema.

Anasema  suala la wizi wa miundombinu ya reli nalo ni changamoto inayowakabili katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.

“Hapo zamani kuna mataruma ambayo yaliuzwa kwa sababu yalionekana kuwa yamechoka, sasa tangu kuuzwa kwa mataruma yale kuliibuka wizi na yaliendelea kuibiwa hata yale ambayo hayajachoka.

“Kutokana na hali ile hata tukiyakuta huko mtaani wengi wanasema walinunua zamani, lakini si kweli na ndiyo maana wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Tulichogundua ni kwamba wengi wanaojihusisha na wizi huo walishawahi kufanya kazi na sisi, ama waliajiriwa au walikuwa vibarua kwenye maeneo ambayo miradi ilikuwa inapita, hivyo wanaelewa wanachokifanya, nimebahatika kupita katika maeneo kadhaa nchini nimekuta watu wamejengea fensi na wengine vyoo, sijui shughuli zingine wanazoenda kufanya na hayo mataruma ni zipi,” anasema.

Anasema ili kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya reli wanashirikiana kwa karibu na wenzao wa TRL kwa sababu wao ndiyo wapo wengi na wapo katika maeneo ya miradi.

Ujenzi wa standard gauge

Catherine anasema mradi huo ni mpya utagharimu Sh trilioni 15 unakuja na mikakati yake mipya na kwamba unatarajiwa kuwa na umbali wa kilometa 1219 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

“Rais Dk. John Magufuli anataka hadi kufikia 2019 mradi uwe umekamilika, ili tuendane na kasi hiyo na tufanikishe suala hilo, mradi huu umegawanywa katika ‘phase’ nne, ya kwanza itatoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ya pili itatoka Morogoro hadi Makutupora (Dodoma), ya tatu kutoka Makutupora hadi Tabora na nne Tabora hadi Mwanza,” anasema.

Anasema zabuni ya ujenzi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro tayari imeshatangazwa na kwamba mshindi atatangazwa mapema ifikapo Januari, mwakani.

“Reli ya standard gauge itaanzia pale bandarini, lengo hapa ni kwamba njia hiyo itumike kusafirisha mizigo na abiria, jambo hilo litasaidia kuimarisha uhifadhi wa barabara zetu pia,” anasema.

Anaongeza “ Bado hatujajua reli hiyo itapita wapi na wapi, lakini jambo ambalo watu wanapaswa kufahamu ni kwamba katika kila sehemu ilipojengwa reli tuna hifadhi ya ardhi usawa wa mita 15 kulia na mita 15 kushoto kutoka katikati ya reli mijini na mita 30 kulia na mita 30 kushoto vijijini.

Dar es Salaam kuunganishwa na reli

Catherine anasema RAHCO ina mpango wa kujenga reli katika jiji hilo, na tayari kampuni ya Gibbs ya kutoka nchini Afrika Kusini ipo kazini ikifanya tathmini ya njia zitakazojengwa.

“Sasa hivi kuna treni mbili tu, lakini tayari kuna njia 10 ambazo iwapo zitaanza zitakuwa zimesaidia kupunguza machungu ya foleni, kutakuwa na ruti ya kutoka katikati ya mji hadi Kibaha kupitia Mbezi- Luguruni, mjini kati,  Uwanja wa Ndege hadi Chanika kupitia Pugu.

“Mjini kati hadi Bagamoyo kupitia Bunju, mjini kati hadi Chamazi kupitia Mbagala, Msasani, Kinondoni, Magomeni, Ilala hadi Shimo la Udongo, Kunduchi, Mtongani, Salasala, Goba hadi Mbezi Luis. Bunju, Luguruni, Segerea hadi JKNIA, Chamazi.

“Mjini kati, Gezaulole kupitia mji wa kigamboni, ipo pia itakayounganisha mji wa Chalinze na Rufiji, tunatarajia pia kujenga reli katika mji wa Dodoma ambako serikali imepanga kuhamia,” anasema.