Home Latest News WALICHOKIHUBIRI SI WANACHOKITENDA

WALICHOKIHUBIRI SI WANACHOKITENDA

305
0
SHARE
Magari yakipita kwa shida katika mtaa wa Kasanga Kata ya Gerezani Kariakoo jijini Dar es Salaam kutokana na ufinyu wa eneo la kuegesha magari.

NA JIMMY CHARLES,

JANUARI 15, 2013 wakati huo Mbunge wa sasa wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) akiwa mbunge wa Ubungo jimbo ambalo kwa sasa linashikiliwa na Saed Kubenea (Chadema), alipata kuandika makala ndefu iliyohuisha sera ya Majimbo.

Katika andiko lake hilo la Mnyika, kichwa cha makala kilichosomeka ‘Sera ya majimbo ni siri ya maendeleo ya nchi na wananchi’.

Mnyika alijitahidi kuelezea sera ya Majimbo ambayo ni moja ya sera za chama chake cha Chadema.

Alifanya hivyo kwa nia ya kumpinga Profesa Sospeter Muhongo ambaye wakati huo alikuwa akiiongoza wizara anayoiongoza sasa ya Nishati na Madini.

Prof. Muhongo, alisema sera ya majimbo inaweza kuligawa Taifa na kwamba haipo duniani kote, msingi wa madai hayo ulikuwa ni mgogoro wa kimaslahi wa gesi uliowahusisha wakazi wa Mtwara na serikali yao.

Mnyika aliieleza misingi tisa  ya sera ya majimbo na umuhimu wake. Ili kuweka kumbukumbu sawa nitafanta rejea ya misingi saba kati ya tisa na ili kuchagiza andiko langu hili nitaanza na msingi wake wa mwisho na kuendelea na mingine.

Katika andiko la Mnyika, msingi wa mwisho ambao nina hakika haukuwa wa mwisho kwa umuhimu ni ‘wananchi kunufaika kutokana na matunda ya raslimali za eneo lao’.

Msingi wa kwanza kwake ulikuwa ni ‘kujenga uwezo wa kisiasa,uongozi na uwajibikaji. Hoja ikiwa ni mfumo wa sasa ambao unatoa mwanya kwa raslimali zote kumilikiwa na “Dar es salaam” kwa maana ya serikali kuu, hali aliyodai kuwafanya wananchi wasinufaike na raslimali za maeneo yao kikamilifu.

Kwamba Sera ya majimbo inaelekeza taifa kuwa na viongozi wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi katika ngazi mbalimbali. Hii ina maanisha kwamba kwa muktadha wa sera ya majimbo ofisi na vyeo vya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, katibu tarafa vitafutwa.

Msingi wa pili ni kushusha na kugawanya madaraka. Alisema uzoefu unaonyesha kuwa majimbo yanapopewa madaraka nayo yanatoa madaraka kwa ngazi ya chini yake na kuendelea mpaka chini kabisa.
Msingi wa tatu ni kupanua umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania na kuvunja dhana ya ukabila. Mfumo wa sasa wa kugawa wilaya pamoja na sababu zingine zinazotolewa na serikali umekuwa ukilalamikiwa kuwa umejikita katika kugawa wilaya kwa mujibu wa makabila.

Msingi wa nne ni kuweka utamaduni wa ushindani na upekee ndani ya nchi. Kama ambavyo nchi zinavyoshindana ndivyo ambavyo majimbo yenye taratibu tofauti za kibiashara, ajira, uwekezaji, makazi na kadhalika zitakavyoshindana. Serikali ya majimbo inatoa mwanya kwa majimbo kujiamulia mwelekeo wake katika masuala fulani fulani.

Msingi wa sita ni kupanua vyanzo vya mapato. Majimbo yanapopaswa kujitegemea kwa aina fulani moja kwa moja yanapaswa kuanza kutafuta njia za kujitegemea. Hii itasaidia vyanzo vya mapato kupatikana. Hii ni kutokana na kanuni ya mwitu.

Kifupi nilivutiwa na sera hii na kujiaminisha kuwa inaweza kuwasaidia Watanzania wengi bila kujali hali zao kuweza kufaidi kipande cha keki cha nchi yao.

Nilijiaminisha hivi kwa sababu niliiona haja ya kuwapa fursa wananchi katika kujiamulia na kushiriki moja kwa moja kwenye kujenga uchumi wao. Sikuweka wala kukaribisha dhana ya utengano.

Miaka mitatu baada ya andiko hilo la Mnyika, nimeshitushwa na kile kilichofanywa na Mameya wa jiji la Dar es Salaam, ambao wengi wao ni kutoka ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),unaokijumuisha Chadema.

Mameya hao kwa kujua ama kutokujua wamekwenda kinyume na msingi wa tisa (kwa Mujibu wa andiko la Mnyika) wa sera yao ya Majimbo, ambayo  inaweka wazi kuwa ‘wananchi wanapaswa kunufaika kutokana na matunda ya raslimali za eneo lao’.

Mameya hao wameipa zabuni  ya kukusanya tozo mpya ya maegesho ya magari katikati ya jiji la Dar es Salaam, kampuni ya kigeni ya Kenya Airport Parking System (KAPS).

Na tayari bei ya maegesho hayo imeshakwea hadi kufikia sh. 500 kutoka sh. 300 ya awali. Hoja yangu hapa si kupandishwa kwa bei ya maegesho, fikra zangu ni sababu ya kugawa zabuni hii kwa wageni.

Inaelezwa kuwa kampuni hiyo imeahidi kukusanya fedha nyingi tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba hakuna kampuni yoyote ya wazawa ambao ndio walengwa wa sera ya Majimbo yenye uwezo wa kukusanya kiasi hicho.

Kama dhamira ya Chadema na washirika wake ni kuwakomboa Watanzania hawa ambao wanatajwa kunyonywa kwa miaka mingi, iweje nao wapiti kwenye mapito yale yale ya wanaowaita wanyonyaji?

Hawa wageni watakusanya fedha hizo wapi na hao wazawa wangezikusanya wapi au hawa wageni wataongezea fedha zao kutoka mifukoni?

Ipo haja ya kulitazama hili, kamwe sipingi kwa kampuni hiyo kupewa kazi, ninachokipinga ni Mameya hawa ambao wanatoka ndani ya vyama vinavyojipambanua kutetea maslahi ya Watanzania kwenda kinyume na kile wanachokisema.

Maeneo kama haya ndiyo yalikuwa muhimu kwa Chadema na Ukawa kwa ujumla kujichukulia sifa, kwamba wangehakikisha wanafanya kila linalowekeza kuziwezesha kampuni za ndani ili ziifanye kazi hiyo na kama hilo lingekuwa gumu basi wasingeona ukakasi kazi hiyo kufanywa na KAPS kwa kushirikiana na kampuni ya wazawa.

Mameya wa Ukawa wanaoliongoza jiji la Dar es Salaam, walipaswa kutumia mbinu za kiongozi wa kwanza mweusi wa chama cha Democratic Alliance (AD) cha Afrika Kusini, Mmusi Maimane ambaye sera zake za kuwapa nafasi zaidi wazawa zilikiwezesha chama chake kunyakuwa mikoa mingi ya Western Cape.

Siioni kazi kubwa ambayo itafanywa na wageni hawa katika kukusanya ushurui wa maegesho, ambacho watakifanya wao ndicho watangekifanya wazawa, labda kama hawa wageni watakuwa na ukatili wa kutoza tozo hata lisilostahili.

Kitendo cha kuruhusu tozo la maegesho kukusanywa na wageni ili hali wenyeweji wenye uwezo wa kufanya hivyo wapi, kumeitoa doa dhamira njema ya kuwakomboa Watanzania inayohubiriwa na Ukawa.

Kitendo hicho kimewafanya kuyasema wasiyo yatenda.

Mungu Ibariki Tanzania.