Home Makala MATUMIZI YA SIMU ZA KISASA YAIMEIFANYA DUNIA KUWA KIJIJI

MATUMIZI YA SIMU ZA KISASA YAIMEIFANYA DUNIA KUWA KIJIJI

480
0
SHARE

Na Balinagwe Mwambungu


Tunapoungumzia simu, watu wengi, hasa vijana wa Kitanzania, inawezekana wanadhani simu kama tunazotumia hivi sasa ndizo zilikuwapo hapo zamani.

Kulikuwapo simu za upepo lakini pande mbili husikilizana kwa sauti, zikitumika na Shirika la Posta na Simu, Polisi na Jeshi la Wananchi. Aidha kulikuwa na simu zilizoitwa za upepo (signal) ambazo pande mbili zilisikizana na milio tu. Baadaye ikaja simu ya mezani na telex.

Simu ya mezani nayo ilikuwa inapatikana sehemu za shughuli za Serikali, Shirika la Posta na Simu na kwenye vibanda maalumu vilivyojengwa na Shirika la Posta na Simu.

Kwa hiyo mtu akitaka kuwasiliana ni lazima funge safari kwenda mjini na kulipia gharama za simu. Vijijini na baadhi ya miji ya wilaya hapakuwapo simu kabisa—taarifa zilipelekwa kwa njia ya barua au simu ya upepo kupitia Kikosi cha Signal cha Jeshi la Polisi.

Ujio wa simu za kiganjani, sio tu umerahisha maisha ya watu wote, umesaidia sana kukuza taaluma ya habari—kwa maana ya upatikanaji, na usambazaji wa habari. Nakumbuka enzi za ukusanyanji wa habari kwa kutumia simu ya mezani—mwandishi ukipangiwa kazi ya kutafuta habari mikoani, ilikuwa ni kazi ngumu. Mwandishi kwa mfano, anapiga simu Extelecom House na anamwomba opareta amuunganishe na Mkuu wa Mkoa wa Kagera na opareta anakujibu:

“Kuna uchelewesho wa saa 8 utasubiri?” Anajibu: “Nitasubiri.” Hapo ujue hawezi kucheza mbali na chumba cha habari, japo hakuwa na uhakika wa kumpata anayetaka kuongea naye. Mara nyingi, kama habari iliyokuwa inaitafutwa ni kubwa, Mhariri anamtuma mwandishi kwenda mkoa husika. Hii iliwasaidia sana wandishi kwa upande mwingine, kufahamiana na viongozi na kuijua nchi yetu.

Nimeitaja mkoa wa Kagera kwa kuwa ni mikoa uliopembezoni mwa Tanzania. Mikoa mingine ambayo ilikuwa haifikiwi kirahisi kwa simu ni Kigoma, Rukwa, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Simu za masafa marefu ziliunganishwa kwa nyaya zilizoshikiliwa na nguzo—na unaweza ukaona jinsi ilivyokuwa gharama kujenga njia ya simu kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, Dar es Salaam- Sumbawanga, Dar es Salaam-Arusha- Dar es Salaam-Musoma!

Wandishi waliokuwa mikoani, walikuwa wanatuma habari kwa simu ya mezani akimsomea mwenzake aliyeko ofisini Dar es Saalam kwa sauti. Wakati huo kompyuta zilikuwa hazipo—anayepokea habari anachapa kwenye taipureta! Baadaye ikaja telex ambayo ilikuwa inanukuliwa na mashine kwa kutoboa matundu kwenye uzi wa karatasi.

Uzi ule wenye matundu huingizwa kwenye mashine nyingine ambayo hutafsiri yale matundu kuwa maneno. Chumba cha Telex kilikuwa kina maopereta ambao walikuwa ni sehemu ya Chumba cha Habari.

Wandishi wa habari wa sasa—kila mmoja ana simu ya kiganjani na anaweza akatafuta  stori kirahisi kabisa akiwa mahali popote.

Simu za mkononi zinapatikana sehemu zote nchini—hakuna pembezoni tena. Mbamba Bay na Lituhi, kwenye ukanda wa Ziwa Nyasa, Kibwesa kando ya Ziwa Tanganyika na visiwani kama Mafia, Mkoa wa Pwani, Ukerewe, Ukara huko Mwanza na Bugarama mpakani mwa Burundi na Wilaya ya Ngara, Murongo-Kaisho kule Karagwe, Shirati mpakani mwa Tanzania na Kenya anaweza kuongea na mtu aliyeko Rongai, Wilayani Rombo na Tandahimba mkoani Mtwara. Haya ndio mageuzi ya teknolojia ya simu.

Baadaye Shirika la Posta na Simu (TTCL), liingiza teknojia mpya kwa kutukumia setelaiti (Satellite)na kuhama toka simu ya kukoroga na kuingia simu ya kuzungusha namba (dialing) hadi tunaingia simu za kiganjani. Hapana shaka ujio wa simu za mkononi umetutoa kwenye kujenga nguzo za simu nakufunga waya ili kuiunganisha miji yote ya Tanzania—ilikuwa kazi ngumu na ilihitaji fedha nyingi sana.

Simu za kigajani zimebadilisha kabisa mfumo wa namna watu wanavyo husiana. Watu hutumiana ujumbe kwa njia ya meseji, e-mail, twitter, Facebook na whatsup. Simu za kiganjani zimekuwa njia rahisi na ya haraka ya kupashana habari na kufanya biashara. Simu imekuwa nyenzo kubwa ya kupashana kwa njia ya picha na video. Simu pia imekuwa kifaa cha kutunzia kumbukumbu.

Siku hizi simu imekuwa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na anaitumia kufanya mambo mengi sana. Kusahau simu nyumbani wanasema ni sawa na kuondoka nyumbani pekupeku. Simu ni kila kitu—ina radio, kamera na sasa hivi unaweza kuangalia kipindi cha televisheni kwa njia ya simu popote ulipo!

Hapa Tanzania, benki zinalalamika kwamba simu imepunguza san wateja wao —hawaweki tena fedha benki kama zamani, na hata huduma ya kuhamisha fedha kupitia benki imepungua.

Pamoja na faida kubwa zilizoletwa na mapinduzi ya teknolojia ya simu za kiganjani, wataalamu wanasema kwamba simu ya kiganjani pia imeleta matatizo ya kijamii na kiafya.

Simu imemrahishia mwanadamu njia ya kuwasiliana, kwa njia ya mtandao, imeifanya dunia kuwa kijiji na hivyo kutumika kama njia ya kueneza tabia na mienendo chanya na hasi miongoni mwa jamii.

Familia hutofautiana kwamba watoto wadogo wasipewe simu ya kiganjani na nyingine zinasema simu ni ya lazima kwa mtoto—hasa katika nyakati hizi za vitendo vya kigaidi na utekaji nyara. Kwa hiyo mtoto akiwa na simu ni rahisi kumfikia—au mtoto mwenyewe akipata tatizo, mara moja huwarifu wazazi wake.

Simu imeunganisha vitu vingi kiasi kwamba imekuwa kama kompyuta ndogo ya mfukoni. Simu inaweza kukuongoza na ukafika sehemu ngeni unayotaka kwenda.

Faida nyingine ya simu ni msaada mkubwa kwa kuwa zinatumia GPS na ni rahisi kumfuatilia mtu mwenye tabia ya uhalifu. Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama, kufuatilia mienendo ya wahalifu kama wanapanga mipango yao kwa njia ya simu.

Ndiyo maana Mamlaka ya Mawasiliano na Udhibiti (TCRA), baada ya kuingia kwenye mfumo wa digitali, ni lazima mtumiaji wa simu ajiandikishe kwa kuwa simu inatunza kumbukumbu. Ni kosa la jinai kutumia line ya simu bila kuandikisha.

 

Lakini wasosiolojia wanasema simu ya kiganjani, imepunguza uhusiano wa moja kwa moja—yaani kuonana ana kwa ana na watu wanaotuhusu—hivyo kutuondolea utu wetu wa maongezi na kubadilishana mawazo (socialization) na marafiki, wanafamilia, na ndugu wengine.

Simu imekuwa chanzo cha mifarakano katika jamii—imeleta kutoaminiana kati ya mke na mume, rafiki wa kike na wa kiume—kila mmoja hatataki mwenziwe aperuzi simu mwenzake.

Aidha, wasosiolojia wanasema watu wanaathirika kwa kutawaliwa (addicted) na simu kama vile mlevi wa pombe au mihadarati—mtu wa aina hiyo anahitaji ushauri nasaha pia.

Kwa upande wa sule, badhi ya walimu, huwakataza wanafunzi kubeba simu shuleni, au kama ni shule za bweni, hukabidhi kwa walimu hadi muda wa kuaporudi makwao. Hii inatokana na ukweli kwamba simu inaweza kumvuruga mtoto asiwe msikivu wakati wa masomo.

Pia imeelezwa kuwa ajali nyingi za barabarani husababishwa na uzembe wa madereva. Pamoja na kukatazwa kisheria kutotumia simu wakati dreva anaendesha gari, sio wengi wanatii katazo hili.

Lakini pia, wanasayansi wameorodhesha mambo kadhaa yenye madhara kwa watumiaji wa simu za kiganjani—kwamba simu hutoa mionzi (radiation) ambayo husababisha saratani ya ubongo na ngozi.

Wenye ugonjwa wa shinikizo la damu wanashauriwa kupunguza matumizi ya simu za kiganjani.

Simu za kiganjani zinachangia kupunguza mbegu za kiume ‘sperm count’ na hivyo vijana wa kiume wanaonywa kwamba wanaweza kupata utasa na kwa wasichana ugumba.

Aidha, mionzi ya simu hizo inaathiri ubongo na kuufanya upoteze kumbukumbu, hupunguza umakini na uwezo wa kupambanua mambo.

Simu ni muhimu sana katika maisha yetu ya kwa hivyo, kama walivyosema wataalamu, matumizi ya muda mrefu ya simu za  mkononi yanaweza kuepukwa ili kupunguza madhara hayo.

Wataalamu wanashauri kuwa kina mama na kina dada, wasiweke simu kifuani na kina kaka wasiweke simu kiuononi wala isikae sana mfukoni.

Ushauri wa jumla ni kwamba watumiaji wa simu wabebe kwenye mifuko  ambayo hupunguza athari.

Simu ya kiganjani imeiunganisha dunia, mtu anaweza kuongea na mtu mwingine katika mabara yote matano kwa urahisi kabisa, lakini pamoja na hayo,
tunapaswa kuitumia simu ya kiganjani kwa umakini ili tuepukane na madhara yake.