Home Makala TANZANIA YAMUUNGA MKONO BALOZI AMINA MOHAMED UWENYEKITI AU

TANZANIA YAMUUNGA MKONO BALOZI AMINA MOHAMED UWENYEKITI AU

293
0
SHARE

Uhusiano baina ya Tanzania na Kenya – nchi mbili wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) unazidi kuimarika tangu pale mapema mwaka huu Uganda ilipobadilisha uamuzi wake wa awali wa kupitishia Kenya bomba la mafuta yasiyosafishwa kutoka Uganda hadi Bahari ya Hindi.

Badala yake Uganda ilichagua bandari ya Tanga, Tanzania kupitisha bomba hilo na hivyo kutiliana mkataba mapema mwaka huu, hatua ambayo  wachunguzi wa mambo waliona haikuwa imeifurahisha Kenya ambayo iliiona kama vile Tanzania iliupora mradi huo ambao awali ulikuwa wa Kenya.

Katika hatua unayoweza kuita “sahau yaliyopita na tugange yajayo” wiki iliyopita Tanzania iliahidi kumuunga mkono mgombea wa kutoka Kenya – Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Balozi Amina Mohamed katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya uwenyekiti wa Umoja wa Africa (AU) katika uchaguzi ujao.

Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania wiki iliyopita ilisema serikali ya Tanzania inamuunga mkono Balozi Amina Mohamed, na wachunguzi wa mambo wanasema msimamo huu wa Tanzania ni tofauti na azimio lililotolewa na Jumuiya ya Maendeleo za Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Kwa upande mwingine uamuzi huu wa Tanzania unaondoa wasiwasi nchini Kenya kwani Tanzania ni mwanachama wa SADC wakati Kenya si mwanachama wa jumuiya hiyo. SADC ilikuwa imeamua kumuunga mkono mpinzani wa Balozi Mohamed, Dk Pelonomi Venson-Moitoi wa kutoka Botswana ambaye ni mgombea mwingine pekee mwanamke.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Dk Augustine Mahiga ambaye kwa sasa ndiyo mwenyekiti la Baraza la Mawaziri la Afrika ya Mashariki (EA Council of Ministers) amesisitiza msimamo wa Tanzania na ule wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuhusu ugombea wa Bi Mohamed katika nafasi ya Uwenyekiti wa AU.

Dk Mahiga alisema kwamba Balozi Amina Mohamed ndiye anayefaa kutokana na uwezo wake mkubwa katika masuala ya kidiplomasia na ya kiuongozi, sifa ambazo ni muhimu katika kuhamasisha msimamo wa pamoja katika masuala mbali mbali Barani Afrika.

Nchi nyingine wanachama wa EAC zilizomuunga mkono Balozi Amina ni Uganda, Rwanda na Burundi.

Kwa ujumla nafasi hiyo ya juu katika AU ina jumla ya wagombea watano. Watatu wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Equatorial Guinea Agapito Mba Mokuy, Moussa Faki Mahamat wa kutoka Chad na Prof Abdoulaye Bathily kutoka Senegal.