Home kitaifa KICHEKO NA MAUMIVU YA SHERIA ZILIZOTIKISA MWAKA 2016

KICHEKO NA MAUMIVU YA SHERIA ZILIZOTIKISA MWAKA 2016

416
0
SHARE
Waandishi wa habari wakiwajibika.

NA GABRIEL MUSHI, 

MWAKA 2016 hakika hautahasahaulika katika sekta mbalimbali nchini ambazo kwa namna moja, au nyingine ziliguswa na marekebisho ya sheria pamoja na miswada ya sheria iliyopitishwa na Bunge mwaka huu.

Baadhi ya sekta hiyo ni tasnia ya habari, mawasiliano, utalii na wadau wa bandari. Hata hivyo sekta ya habari iliibua mjadala zaidi baada ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016, kupitishwa na Bunge.

Muswada huo ambao ulianza kujadiliwa zaidi ya miaka 23 iliyopita, hatimaye ulipitishwa mwaka huu kukiwa na baadhi ya vipengele ambavyo kwa namna moja au nyingine vinaiumiza au kuiboresha sekta hiyo kwa ujumla.

Baada ya Bunge kupitisha muswada huo, naye Rais John Magufuli hakuchukua muda kwani aliusaini na kuwa sheria ambayo sasa inasubiri kutungiwa kanuni na kuanza kutumika.

Sheria hiyo iliibua mvutano ambao uliilazimu Serikali kufanya maboresho 32 kwenye muswada huo na kuingiza vifungu vipya vitano ambavyo vitatoa ahueni kwa wanahabari.

Sheria hiyo sasa itawafanya wanahabari kuhakikisha wanazingatia sheria kwenye kazi zao, na watakaokwenda kinyume cha sheria, wakijikuta wakifungiwa na Bodi Huru ya Habari kwa muda wa miezi mitatu.

Licha ya baadhi ya wabunge kuchambua madhara ya sheria hiyo na kuainisha namna unavyobana uhuru wa vyombo vya habari nchini, hoja zao hazikufua dafu katika Bunge ambalo limetawaliwa na wabunge wengi wa upande wa chama tawala CCM, ambao kwa namna yoyote kwa uwingi wao hupitishwa miswada ambayo wanaona ina manufaa kwa serikali.

Itakumbukwa kuwa mwaka 2000, muswada huo ulifufuliwa tena lakini maoni ya wadau yalichukua muda mrefu na kusababisha kutofikishwa bungeni na baadaye mwaka 2015, uliwasilishwa kwa mara nyingine na kuibua mvutano mkali ambao ulisababisha uondolewe tena bungeni kabla ya safari hiyo, kuhitimishwa mwaka huu na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Utalii, mawasiliano

Hata hivyo, katika hatua nyingine mwaka huu sekta ya utalii na mawasiliano nazo pia ziliguswa baada ya Bunge kufanya marekebisho ya sheria ya Kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Serikali ilifanya marekebisho ya VAT, sura 148 yaliyotangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipokuwa akisoma bajeti ya serikali bungeni kwa mwaka huu wa fedha 2016/17.

Baada ya marekebisho hayo kupitishwa maumivu makali ya kodi yameanza kuwaumiza wananchi.  Kwa sababu kwa upande wa mawasiliano tayari maumivu kwa watumiaji wa simu ambao wanakadiriwa kuwa milioni 39.8 nchini yameonekana dhahiri kwa kuwa sasa wameanza kukatwa asilimia 18 ya VAT kwa kila muda wa maongezi wanaonunua kupitia vocha, kurushiwa au kupitia njia za benki za simu kama vile Airtel money, na Tigopesa.

Licha ya Serikali kupitia waziri wa fedha kudai kuwa kodi hiyo hakatwi mwananchi, hali imekuwa tofauti kwani huduma za mawasiliano nchini zimeendelea kuwaumiza wananchi kutokana na makato hayo.

Vivyo hivyo kwa upande wa tozo ya huduma za utalii nchini ambayo imekuwa sekta muhimu katika kuchangia pato la Taifa kwa sababu kwa sekta hii kwa mwaka 2015, imeweza kuchangia katika uchumi wa Taifa dola za Kimarekani bilioni 2.23.

Kama ilivyo ada Bunge lilipitisha tozo ya kodi ya ongezeko la thamani VAT kwa asilimia 18 kwenye huduma za utalii.

Huduma hizo ni katika shughuli za kuongoza watalii, kusafirisha watalii, utalii wa majini, kuangalia wanyama na ndege wa porini, kupiga picha, kutembelea hifadhi na usafirishaji wao.

Baada ya bunge kupitisha sheria hiyo mpya kuanzia Julai mosi mwaka huu, Serikali imeanza kutoza kodi ya VAT kwenye shughuli za utalii.

Hutua hiyo ya Serikali kwa imekuwa ikilalamikiwa na kuzua wasiwasi wa kupungua kwa idadi ya utalii nchini.

Mmoja wa wadau waliokuwa wakipinga tozo hiyo ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Nchini (TCT), Mohamed Abdulkadir, anasema sekta ya utalii inaweza kuliingizia taifa mapato mengi zaidi sio tu kwa kupitia makusanyo ya kodi, bali pia katika nyanja zingine zinazoendana na utalii.

“Tanzania itapoteza idadi kubwa ya watalii wanaokuja nchini kwani biashara ya utalii ina ushindani mkubwa na mabadiliko yoyote ya bei huleta ukakasi au huvuruga mipanago kwani huwa ni ya muda mrefu. Kodi ya ongezeko la thamani itaongeza gharama ya watalii kuja Tanzania kwa zaidi ya asilimia 18,” anasema Abdulkadir.

Baadhi ya wadau hao, wanaeleza kuwa tayari nchi mshindani mkuu katika biashara hii ni nchi ya Kenya ambayo imeondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye utalii iliyokuwa inatoza kwa asilimia 16, ili kuichuuza Tanzania.

Pamoja na mambo mengine pia, mwaka huu ulitikiswa na tozo ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye huduma za mizigo inayokwenda nchi za nje kupitia Bandari ya Dar es Salaam (transit cargo) ambayo pia ilitajwa kuwa moja ya sababu lukuki zilizowakimbiza wafanyabiashara kutumia bandari hiyo.

Licha ya sheria hiyo inayowataka kulipa gharama hizo kufanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bunge mwaka 2014, na kuanza kutumika Julai mwaka 2015, maumivu yake yalianza kuonekana mwaka jana na kuanza kupamba moto mwaka huu, hali iliyoilazimu Serikali kuingilia kati suala hilo.

Marekebisho yaliyofanyika, yaliondoa msamaha kwenye huduma zote zinazohusiana na shughuli za kuhudumia mizigo ya nje inayopita nchini. Vile vile, kuonekana kuwa tozo hiyo inatoa mwanya kwa washindani wa Tanzania ambao ni Kenya. Nchi nyingine kama Msumbiji na Afrika kusini.

Ni dhahiri kuwa sasa wakati umefika kwa Serikali pindi inapopitisha miswada ya sheria au marekebisho, baadhi ya vifungu vya sheria vifanyiwe tathmini ya kutosha, ili kulinda masilahi ya wananchi wake.