Home Latest News MAMBO MUHIMU KWA JPM YA KUPAMBANA NA RUSHWA CCM

MAMBO MUHIMU KWA JPM YA KUPAMBANA NA RUSHWA CCM

459
0
SHARE
Rais John Magufuli

NA NASHON KENNEDY,

MWENYEKITI wa CCM Taifa, Rais John Magufuli ametangaza vita ndani ya chama hicho kikongwe cha siasa ambacho ni miongoni mwa vyama vikongwe Kusini mwa jangwa la Sahara vilivyoendesha harakati za ukombozi kwa baadhi ya nchi za Bara la Afrika.

JPM alitangaza vita hiyo hivi karibuni mara baada ya kuendesha vikao vyake vya kwanza vilivyofanyika jijini Dar es Salaam tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho mapema mwaka huu.

Pamoja na kufanya mabadiliko ya uongozi huku akimteua Humprey Polepole kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi ndani ya chama, mambo mengine aliyosisitiza Dk. Magufuli ni pamoja na kupambana na rushwa ndani ya CCM bila suluhu.

Juhudi za Rais Magufuli za kupambana na rushwa hazikuanza leo, alianza wakati akiwa Naibu Waziri na Waziri Kamili wakati wa awamu ya tatu na ya nne ya uongozi wa Marais wastaafu wa awamu hizo, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Moja ya mambo aliyokerwa nayo kwa wakati huo, ni pamoja na watu waliovunja sheria kwa kujenga kwa makusudi ndani ya hifadhi ya barabara na wale waliokuwa wakijihusisha na uvuvi haramu, ambapo baadhi ya vigogo nao wamekuwa ni wahusika wakubwa wa biashara ya uvuvi haramu ambapo hutumia makokoro ambayo hayaruhusiwi kwa mujibu wa sheria.

Tuliziona juhudi za Dk. Magufuli za kupambana na yote hayo kwa juhudi na maarifa licha ya kukumbana na changamoto za hapa na pale za kiutendaji, ambazo wakati mwingine ziliweza kumkwaza kwenye utendaji wake.

Suala la rushwa ni tete kwani hata vitabu vya maandiko matakatifu vinaonyesha ni jinsi gani rushwa iliweza kumshawishi mmoja wa wanafunzi na kipenzi chake Yuda ambaye alimuuza kwa rushwa.

Athari ya rushwa hata kwa mataifa makubwa duniani bado ni changamoto, lakini pia rushwa kwa nchi yenye watu maskini kama Tanzania madhara yake ni makubwa zaidi.

Lakini ifahamike kuwa madhara ya rushwa katika uchaguzi ni kuondoa uhuru wa mpiga kura, wagombea wenye vipaji na wenye uwezo wa kuongoza hushindwa kugombea kwenye uchaguzi kwa kukosa fedha, na hii huharibu dhana nzima ya uwakilishi kwa kuwa watakaokuwa wamechaguliwa hawana ridhaa kamili ya wapiga kura wao ( wananchi).

Rushwa pia ina madhara ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kiasi cha kuifanya jamii ya watu wanaoishi pamoja kuwa na kiu ya kusubiri kupewa na kufanya maamuzi ya mkato kwa kumpa haki mtu ambaye hastahili na kumchagua ambaye hastahili kwa ushawishi wa rushwa.

Matukio yote ya rushwa huonekana kwenye chaguzi mbalimbali za chama na serikali ambazo zimekuwa zikiendeshwa kuanzia ngazi za vitongoji, mitaa, vijiji, Kata, Wilaya, Mkoa hadi Taifa.

Uchaguzi ni hatua muhimu ya wananchi kuonyesha ukomavu wao wa kidemokrasia na kupitia taasisi zao za vyama wanalo jukumu la kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi kwa kuwachagua viongozi bora na sio bora viongozi kwa ajili ya ustawi wa maisha yao.

Wanatakiwa kufanya maamuzi yao bila vitisho wala kushurutishwa kwa rushwa au namna yoyote ile maana uchaguzi ni jambo linalohusu maisha yao. Mwananchi akimchagua diwani au Mbunge makini maana yake ni kuwa atakutana na fedha zake za kodi kwenye barabara, huduma bora ya afya na ujenzi wa miundombinu imara itakayomwezesha kusafirisha mazao yake kwenda kwenye soko na huduma zingine muhimu.

Mwananchi anapokubali kupokea hongo ya fedha, rushwa, t-shirt na kofia za vyama vya siasa, maana yake anauza uhai wake, wa watoto wake  na wajukuu wake kwa kipindi ambacho uongozi uliochaguliwa utakoma kuwepo madarakani.

Kwa miongo kadhaa sasa, chaguzi nyingi zinazofanyika ndani ya CCM zimekuwa zikigubikwa na rushwa ambayo imekuwa ikifanyika kisayansi zaidi. Zipo rushwa ambazo hutolewa kama mikopo ya kwenda kwenye Saccos na zingine hutolewa kama zawadi au misaada ya ujenzi wa majengo ya taasisi za umma na baadhi ya wagombea ambao sio waaminifu.

Kwa kifupi rushwa ndani ya CCM ina sura za kutisha, hubadilika mithili ya rangi ya kinyonga, na watoaji wa rushwa hiyo ni watu wenye mbinu nyingi kulingana na mazingira ya mahali, nyakati na sehemu na kwa nani anayetarajiwa kukabidhiwa rushwa hiyo.

Na ndio maana ilifika mahali rushwa ndani ya chaguzi za chama ilipata baraka kutoka kwa vigogo huku ikipewa majina laini likiwemo jina la takrima, ambalo kwa miaka kadhaa tulijuhudia mijadala mikali ya ndani ya chama hata bungeni ya kutoa baraka kwa jina hilo.

Katika uchaguzi Mkuu wa Chama uliopita, mimi nilikuwa miongoni mwa wagombea wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia Wilaya ya Ilemela. Kwenye kinyang’anyiro hicho sikuweza kubahatika kuchaguliwa katika nafasi hiyo, na badala yake Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Ilemela ulimchagua Israel Mtambarike kuwa MNEC wa Wilaya ya Ilemela, na viongozi wengine wa Chama Mkoa na wilaya zingine walichaguliwa.

Safari yangu haikuishia hapo, katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka jana, niligombea nafasi ya udiwani kupitia CCM katika Kata ya Kisaka, wilaya ya Serengeti, ambapo nilishiriki kikamilifu kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya chama, ingawa vilevile kura hazikutosha na hivyo niliishia kwenye kura za maoni.

Kuna mambo kadhaa ambayo niliyagundua ambayo hasa yamekuwa yakiendeshwa na chama katika kuwapata wagombea wake huku yakiwa na changamoto kubwa ya tatizo la rushwa. Kiuhalisia rushwa ndani ya CCM ni mbegu iliyoota kuanzia kwa wana CCM wenyewe, viongozi na hata marafiki na wapenzi wa CCM.

Ni kitu cha kawaida sana pale wana CCM wanapomjua mtu anayetaka kutia nia ya kugombea ikiwa hata kwa tetesi, wao humuendea na kumwambia anawaachaje. Ushawishi wa rushwa ndani ya CCM huanza kujengwa kisaikolojia  kwa wagombea kabla hata ya kuitishwa kwa vikao muhimu vya chama.  

Ningeshauri kwa wanachama wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa wa rushwa ndani ya chama, na wao wadhibitiwe kwa kufutiwa uanachama wao.

Uchambuzi na kigezo muhimu kwa mgombea ndani ya CCM sio sifa za uongozi na uwezo wa kuongoza bali ni uwezo wa fedha alio nao hata kama aliwahi kukosa sifa za yeye kuwa mgombea.

Kwa bahati mbaya sana kinachotazamwa na viongozi wa Chama katika ngazi za Kata na Wilaya hata mkoa kwa nafasi za udiwani na ubunge ni uwezo alio nao mgombea.

Mgombea wa nafasi ya ubunge au udiwani lazima awe ama mfanyabiashara au mwenye ukwasi wa fedha ndiye anayepewa nafasi na baraka ya kuchaguliwa kuwa Diwani ama Mbunge.

Na tathimini ndogo niliyoifanya kwa mtu ambaye anawania nafasi ya udiwani hadi apate ushindi wa kiti hicho lazima atumie kiasi cha fedha ambacho hakizidi Sh Milioni 250-300 na kwa nafasi ya ubunge sio chini ya Sh Milioni 300 hadi Milioni 400.

Swali la kujiuliza hapa kwa mwanachama mwenye sifa ya uongozi kwa nafasi zote mbili na akawa hana uwezo wa kifedha ni kukosa nafasi hizo. Kwa lugha nyingine ni kuwa kwa miaka kadhaa nchi imewapoteza viongozi wengi wenye sifa kwa kukosa fedha kwa ajili ya kutoa rushwa au kununua uongozi.

Hapo utashuhudia ofisi nyingi za chama ngazi ya wilaya na Kata zinageuzwa kuwa ofisi za wagombea wenye fedha. Wao ndio wanaofadhili fedha za kuendesha vikao, kutafuta miziki na kufadhili burudani kwa ajili ya kampeni ili mradi azma yao ya kutaka kuongoza inafikiwa.

Kwa mfano katika uchaguzi wa mwaka 2015 wa ngazi ya udiwani, ambapo binafsi nilikuwa mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM ambapo baadhi ya viongozi wa chama hukosa sauti ya kusimamia maadili na kanuni ndani ya chama na hivyo kuruhusu wagombea wenye fedha kufadhili baadhi ya mambo muhimu.

Aidha swala la maadili halipewi uzito unaostahili. Suala hili hujitokeza mara nyingi wakati wa kura za maoni na hivyo kusababisha mchakato huo katika ngazi ya kata kuwa na mzigo mkubwa wa gharama kutoka kwa wagombea.

Mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM ni wa gharama kubwa kuliko hata uchaguzi mkuu wenyewe wa kuelekea kwenye uchaguzi wa kapu kwa kushirikisha vyama vyote vya siasa.

Mathalani katika uchaguzi huo wa udiwani, ambapo tulikuwa wagombea saba kila mgombea alichangia gharama ya Sh 112,500 kama gharama ya uchaguzi ikiwemo ya Sh 10,000 ya kuchukulia fomu.

Hakuna sababu yoyote ya jimbo moja liwe la ubunge au udiwani kuwa na wagombea 10-12. Katika chaguzi hizo katika hatua ya awali hakuna vigezo mahususi vya kumpata mgombea, ingawa CCM imekuwa ikitumia hoja kuwa ni ushiriki mpana wa kuwapata wagombea wake.

Mfano kadi za wagombea wa chama haitazamwi kikamilifu na hili ndilo eneo muhimu la kuanza kudhibiti viongozi bora, mfano baadhi ya wanachama wanaoenda kugombea hulipia ada zao kwa mara moja katika kipindi cha miaka mitano.

Ili JPM aweze kufanikisha vita ya rushwa ndani ya CCM, ni sharti akijengee uwezo wa kutosha chama( kiuchumi) kuanzia ngazi ya Kata na Wilaya ambako huko ndiko kuna chaguzi na uongozi muhimu wa chama.

Chama kiwe na miradi na vitega uchumi vya kutosha ili kuwezesha viongozi wake kutokuwa na ushawishi wa kuomba rushwa hata kwa mambo ya utendaji yaliyo ndani ya uwezo wao.

Mfano katika kupitisha majina ya wagombea nafasi za ubunge kuna udhaifu mkubwa ambao huonyeshwa na Makatibu wa CCM wa wilaya ambao ndio watendaji wakuu wa shughuli za kila siku za chama.

Baadhi ya viongozi na watendaji walio ndani ya CCM,  hufikia hatua ya kuwalamba miguu wagombea nafasi za ubunge walio na fedha kwa kuishia kupendekeza majina yao kwenye vikao vya maamuzi kwa kuwashawishi wajumbe.

Kwa upande wa Kata, kwa wanachama wanaowania nafasi za udiwani, Makatibu wa CCM wa Kata nao kutokana na kuwa hoi kiuchumi na kukosa vitega uchumi ndani ya chama, tegemezi lao katika utekelezaji wa majukumu hata yale ya kawaida ya chama hutegemea wagombea wanaojitokeza kuwania nafasi ya udiwani.

Hakuna sababu ya mwanachama wa CCM kutumia gharama zake kwenye mchakato wa kuomba uongozi mwisho wa siku hataweza kutekeleza majukumu yake kwa kufuata kanuni, taratibu za chama zilizopo maana yeye atakuwa ameununua uongozi na hali kama hii ndiyo inayoendelea kukigharimu CCM.

Ni vyema mfumo wa kuwapata wagombea ndani ya CCM ukabadilishwa, watume majina yao mapema( wajisajiri mapema) chama kipate muda mpana wa kuwachunguza mienendo na tabia zao, ikiwa ni kwa kiwango gani wanakubalika kwa jamii kabla ya kutumia ushawishi wa rushwa ili waweze kuchaguliwa.

Chama kipige marufuku watu wanaotumia umaarufu wao wa fedha na utajiri katika kuwania nafasi za uongozi. Mara nyingi baadhi ya wafanyabiashara waliochaguliwa kuwa ama wabunge au madiwani, baadhi yao wamepata kutumia nafasi hizo kwa kupitisha na kufanya mambo yao, lakini walio wengi hawakuwa na dhamira ya dhati ya uongozi.

Kwa awamu hii ya tano, Mwenyekiti wa CCM ni vyema akatenganisha siasa na uongozi, ili watu wenye dhamira ya dhati ya kufanya siasa kama zilivyo taaluma zingine wafanye siasa, na wanaofanya biashara waifanye kwa uhalali ili serikali iweze kukusanya kodi.

Ifanyike tathimini ya kina kila unapofika wakati wa uchaguzi kwa kila mgombea ili kujiridhisha kama ana dhamira ya dhati ya uongozi kwa nafasi anayoomba. Yote haya yakifanyika kwa dhati kwa kutanguliza uzalendo tutakuwa tumemsaidia JPM katika vita dhidi ya rushwa kwa kuijenga CCM mpya ambayo wanachama wake watakuwa hawaimbi tena wimbo wa rushwa kwa kikolezo cha unaniachaje!

Mungu ibariki Tanzania!

0756 823 420