Home kitaifa MWAKA WA KWANZA KWA JPM NA MITIKISIKO YA AINA YAKE

MWAKA WA KWANZA KWA JPM NA MITIKISIKO YA AINA YAKE

318
0
SHARE
Waziri mkuu akitoa heshimi kwa miili ya watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi Bukoba.

NA HILAL K SUED,

Tangu ujio wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, hakuna mwaka (ambao ni wa kwanza kwa rais mpya aliyechaguliwa mwaka uliotangulia) ulioingia kwa mtikisiko mkubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii kama mwaka huu wa kwanza wa Rais John Magufuli. Ni tofauti kabisa hali ilivyokuwa miaka ya kwanza ya urais wa Benjamin Mkapa (1996) na Jakaya Kikwete (2006).

Rais Magufuli aliuanza mwaka kwa mgogoro kisiasa wa kule Visiwani ulitokana na ufutaji ghafla wa matokeo ya uchaguzi wa Rais na Wawakilishi – uchaguzi uliokuwa umefanyika sambamba na uchaguzi wa Rais wa Jamhuri na Wabunge wa Bunge la Muungano tarehe 25 Oktoba 2015. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alifuta matokeo hayo kutokana na kile alichodai ‘kuwepo kasoro nyingi’ zilizogubika uchaguzi ule.

Kabla ya hapo Mgombea wa urais wa Zanzibar kuptia CUF, Seif Shariff Hamad, alitangaza mbele ya waandishi wa habari kuwa ameshinda kutokana na matokeo yaliyokusanywa kutoka vituoni. Kufutwa kwa uchaguzi huo kulizusha mgogoro mkubwa wa kisiasa, na ingawa ZEC ilitangazwa kurudiwa (Machi 20 2016) CUF ilisusia na hivyo ndiyo ikawa mwisho wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kama ilivyoanishwa chini ya Katiba ya Zanzibar iliyorekebishwa mwaka 2010.

Baadhi ya mataifa ya nje ikiwemo Marekani ilituhumu ‘ukiukwaji’ huo wa demokrasia huko Zanzibar na kuamua kusitisha misaada yake kwa Tanzania chini ya Shirika lake la Millennium Challenge Corporation (MCC). Sababu nyingine kwa Marekani kusitisha misaada ni upitishwaji wa ile Sheria ya Makosa ya Mitandao.

Tukiuacha mgogoro huo wa Zanzibar ambao bado haujapatiwa ufumbuzi wa kuhakikisha amani ya kudumu na utulivu katika visiwa hivyo ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mitikisiko mingine chini ya awamu ya Magufuli imekuja kimakusudi – na ilitokana na ahadi yake ya kuleta mabadiliko ya utawala wa nidhamu (pengine ni tofauti na utawala wa sheria) na lengo kuu hapa ni kwa watumishi wa umma ambao ana uwezo mkubwa dhidi yao kwani moja kwa moja wako chini ya muhimili wake – muhimili wa utawala.

Na ndiyo maana ziara yake ya kwanza akiwa Rais, alitembelea ofisi za Wizara ya Fedha, zilizopo jirani tu na Ikulu kuonyesha msisitizo wake wa nidhamu miongoni mwa watumishi wa umma, lakini pia kuonyesha yeye kutokuwa na mzaha kuhusu masuala ya fedha na ukusanyaji kodi za serikali.

Mtindo huu wa kurudisha nidhamu ndiyo ukawa mwongozo na kuchukuliwa na mtendaji wake mkuu, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa ambaye hakusita kutembelea ofisi mbalimbali za serikali na taasisi za umma, na mara nyingi kulazimika kuchukua hatua papo kwa papo kila alipogundua mambo yalikuwa yakienda ndivyo sivyo.

Sote twakumbuka ziara ya kwanza ya Waziri Mkuu Majaliwa katika bandari ya Dar es Salaam – ambapo aliwatikisa vigogo wa eneo hilo muhimu kwa uchumi wa taifa hili kutokana na usimamizi wao mbovu uliokuwa unasababisha serikali kupoteza fedha nyingi kama mapato yatokanayo na kodi za bidhaa zinazoingizwa nchini na ushuru mbalimbali.

Sote tanakumbuka ziara yake hiyo ‘iliondoka na vichwa’ vya baadhi ya vigogo – wale wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA). Na hapo hapo ndiko kukaanza kwa zoezi lile maarufu la Rais Magufuli la ‘utumbuaji majipu’ – kuwaondoa madarakani watendaji wanaotuhumiwa kwa ufisadi na utawala mbovu.

Zoezi hili lilishika kasi kiasi kwamba hata wakuu wengine wa idara, vitengo na taasisi za umma – kama vile mawaziri, makatibu wa Wizara, Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wengine wakaanza ‘kuwatumbua’ wale wa chini yao wanaowaona hawafai.

Kama kawaida malalamiko yakaanza kujitokeza kupitia mitandaoni na kwenye vyombo vingine vya habari – kwamba kuna ‘utumbuaji’ mwingine ulikuwa wa visasi, majungu na uonevu mkubwa na kwamba ni vyema ‘utumbuaji’ huu ukafuata sheria na kanuni za utumishi zilizopo.

Malalamiko haya yalikuja kuwekewa mkazo na Makamo wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye akiwa ziarani mkoani Geita katika hafla moja kuhusu watumishi wa Idara ya Afya alisema kabla ya kutumbua ni muhimu kanuni za utumishi zikazingatiwa. Kuanzia hapo ‘utumbuaji’ majipu kiholela ukaanza kukoma.

Lakini haya yote ni tofauti kabisa na alivyofanya mtangulizi wa Rais Magufuli, Jakaya Kikwete katika mwaka wa kwanza wa urais wake (2006) katika azma kama hiyo ya kusisitiza nidhamu na ufanisi katika sekta ya utumishi wa umma.

Yeye aliamua kufanya semina elekezi kwa watendaji wakuu wa serikali katika Hoteli ya kitalii ya Ngurdoto mkoani Arusha lengo likiwa mbali na kuwepo kwa nidhamu na uadilifu katika utendaji wao, pia kupewa miongozo ya namna ya kuwaondoa wananchi kutoka dimbwi la umasikini.

Kwa wasiojua – Hoteli ya Ngurdoto iko mlimani na ni kwa ajili ya watalii wenye fedha ‘za kuchezea’ – hivyo mandhari yake ni tofauti kabisa na hali halisi inayowakabili mamilioni ya Watanzania.

Watendaji wa serikali walihudumiwa kwa wiki nzima wakila na kunywa katika hali ambayo wasingeweza kuwafanya wauhisi ule ‘umasikini’ wa wananchi wengi, umasikini ambao ndiyo walikuwa wanatumwa kwenda kuuondoa wakitoka hapo.

Kuna waliohoji: Kwa nini wasipelekwe kukutana Boma la Ng’ombe, Usinge au Kijichi ili wapate kuiona hali iliyopo ili waweze kuiondoa?

Wengi waliona aina hii ya ufujaji wa fedha za umma ni kiashirio cha unafiki wa wale wanaoshika usukani wa nchi hii masikini – kwamba ili kupambana na umasikini, lazima kwanza uonyeshe utajiri.

Kwa matajiri pengine ni haki kuonyesha utajiri, lakini masikini ataonyesha vipi utajiri ambao hana? Kwa ujumla katika kipindi cha Awamu ya urais wa Jakaya Kikwete wananchi walianza kuelewa kwa nini Tanzania ilikuwa masikini.

Angalia tofauti: Magufuli alianza urais wake kwa kufuta sherehe za mwaka wa 54 uhuru (Desemba 9 2015) pamoja na karamu ya chakula inayoandaliwa pale Ikulu na kukaribisha wageni mbali mbali na badala yake akaagiza fedha hizo (kiasi cha sh 4 bilioni) zipelekwe katika upanuzi wa barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Na katika mwaka wa kwanza wa Rais Magufuli ni pale kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam likawa chini ya upinzani yyani kwa mara kwanza mpizani alichaguliwa kuwa Meya wa jiji. Halmashauri nyingine za manispaa ya jiji hilo – Ilala na Ubungo nazo zikajikuta zinaongozwa na vyama vya upinzani.

Hata hivyo mitikisiko mingine ya Urais wa Magufuli ulitokea katika Muhimili mwingine muhimu wa Dola – ule wa Bunge ambapo kwa mara ya kwanza tangu ujio wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, serikali ilisitisha utangazwaji ‘live’ wa majadiliano ya vikao vya Bunge. Sababu kubwa iliyotajwa ni kupunguza gharama.

Kama kawaida Wabunge wa upinzani waliipinga hatua hii wakisema inawanyima wananchi kufuatilia yanayozungumzwa Bungeni na wawakilishi wao. Walisema hatua hiyo ni uingiliaji wa Muhimili wa Dola kwa ule wa Bunge kwani aliyetangaza kusitishwa matangazo live ni Waziri wa Serikali (Waziri wa Habari) na siyo Bunge lenyewe.

Mtikisiko mwingine kwa upande wa Muhimili wa Bunge chini ya Urais wa Magufuli nao ulikuwa ni wa kwanza katika Bunge la vyama vingi – kufungiwa kwa Wabunge 11 wa upinzani kuhudhuria vikao kadha vya Bunge kutokana na makosa mbali mbali, yakiwemo kufanya vurugu Bungeni, kutoa kauli zilizodaiwa ni za uongo na kadhalika na kadhalika. Hadi sasa kuna baadhi ya Wabunge hao wanatumikia adhabu zao.

Aidha katika mwaka huu wa kwanza wa Rais Magufuli kuna wananchi kadha wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kumtusi/kumkejeli Rais mitandaoni – chini ya Sheria ya Makosa ya Mitandaoni ilyopitishwa na Bunge wiki chache kabla ya uchaguzui mkuu wa mwaka jana.

Lakini mtikisiko mkubwa wa aina yake, mtikisiko ambao uliwagusa wananchi wengi ni lile suala la sukari. Mapema mwaka huu rais magufuli alitangaza kupiga marufuku uingizwaji wa sukari kutoka nje, kwa kusema inayozalishwa nchini inatosha na ikawaonya wafanyabiashra wote wa sekta hiyo kutoificha bidhaa hiyo.

Ghafla sukari ikaanza kuadimika na kupanda bei maradufu, kutoka sh 2000 kwa kilo hadi sh 6000 kwa baadhi ya maeneo nchini. Msako mkali wa maghala mbali mbali nchini ukaanzishwa ‘kuwabaini’ wote walikuwa wanaficha bidhaa hiyo muhimu.

Ingawa matani na matani ya sukari yaligundulika katika maghala mbali mbali, wamiliki wa bidhaa hiyo walijitetea kwa kusema kamwe hawakuwa wanaificha, bali walikuwa wakiiuza kwa mnunuzi yoyote wa jumla (wholesale) kwani wao walikuwa hawauzi rejareja.

Ilivyoonekana ni kwamba Rais Magufuli alikuwa ameshauriwa vibaya kuhusu hali ya uzalishaji wa sukari nchini, kwani ni kweli ilikuwa haitoshelezi mahitaji ya nchi hivyo lazima sukari ya ziada iagizwe kutoka nje.

Lakini yote hayo ni tisa … kumi ni ule mtikisiko wa kihalisia uliotokea mapema mwezi Septemba mkoani Kagera pale mji wa Bukoba na maeneo ya jirani yalipotikiswa na tetemeko kubwa la ardhi la ukubwa wa 5.7 katika kipimo cha Richter.

Hilo lilikuwa ni tetemeko kubwa zaidi kutokea katika historia ya nchi hii tangu uhuru na zaidi ya watu 13 walipoteza maisha, takriban 200 wengine walijeruhiwa na mamia ya majengo makazi ya watu, shule, miundombinu viliharibiwa na maelfu ya watu kukosa makazi.