Home Habari kuu RAIS MAGUFULI HANA BREKI KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE

RAIS MAGUFULI HANA BREKI KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE

684
0
SHARE

RAIS John Magufuli amezidi kudhirisha kasi na viwango vyake katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ndani ya Serikali anayoiongoza tangu alipoingia madarakani Novemba 5 mwaka 2015. RAI linachambua.

Kasi ya Rais Magufuli imeonekana kuwa kubwa kuliko ilivyotarajiwa na baadhi ya Watanzania hivyo kuibua mijadala mbalimbali hususani baada ya kuupokea mwaka 2017 kwa staili ya kipekee.

Licha ya kuwa siku ya mapumziko, Januari mosi Rais Magufuli alitangaza kuendelea kuwatumbua watumishi wa serikali.

Magufuli ambaye alishiriki ibada ya kuukaribisha mwaka mpya katika kanisa kuu la jimbo la Bukoba, alizungumzia uamuzi wa Mamlaka ya udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), kutangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia nane.

Ewura ilikubali maombi ya Shirika la ugavi wa umeme nchini (TANESCO) ambalo liliwasilisha nia hiyo mapema Septemba mwaka jana ambapo pamoja na sababu mbalimbali ilikubali kupandisha gharama ya asilimia nane badala ya 18 waliyotaka waombaji.

“Ninamshukuru sana waziri wa nishati na madini ameshatengua maamuzi hayo kwa hiyo umeme hakuna kupanda, haiwezekani wakati kuna mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika mikakati mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme mpaka vijijini, na umeme unaenda kwa watu maskini walioumbwa kwa mfano wa Mungu alafu mtu pekee kwa sababu ya cheo chako unasimama unakwenda kupandisha bei ya umeme, ndio maana  Baba askofu nalizungumza hili kwamba majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua,” alisema Magufuli.

Saa chache baada ya kauli hiyo ya Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba na kumteua Dk. Tito Esau Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi wa shirika hilo.

Hii ni dhahiri kuwa kwa mwaka 2017 Mkurugenzi huyo wa Tanesco, Mramba anakuwa mfanyakazi wa kwanza kutumbuliwa na Rais Magufuli.

Ikumbukwe kuwa katika kipindi cha muda wa mwaka mmoja aliokaa madarakani, Rais Magufuli ameshatumbua zaidi ya watumishi 300 kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo tuhuma za utovu wa nidhani na matumizi mabaya ya madaraka.

Mwaka 2016 ulikuwa na matukio mengi kisiasa, kijamii, kiuchumi na hata kiutamaduni hivyo Watanzania wengi kudhani kuwa mwaka 2017 unaweza kuwa wa utulivu na watu kuanza kufanya kazi kama ilivyo kauli mbiu ya Serikali ya Rais Magufuli, ‘ Hapa kazi tu’.

Akihutubia Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika hotuba yake ya kwanza, Rais Dk. John Magufuli alisema atatumbua majipu na sasa bado anaendelea nayo hadi mwaka huu wa 2017.

Rais Magufuli ambaye wengi wanamfananisha na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake haitawavumia watendaji wasiokuwa waaminifu, waadilifu na wanaoendekeza rushwa na ufisadi.

Lengo la msimamo wake huo ni kuirudisha nchi katika misingi ambayo iliwekwa na Mwasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere.

Hata hivyo akiwa Mkoani Kagera ameendelea kudhihiria kuishi mapito ya Mwalimu Nyerere kwa kuonesha tabia yake ya ukali na kueleza ukweli baya.

Licha ya Rais Magufuli kutoonekana katika mkoa huo tangu palipotokea tetemeko la ardhi lilisobabisha vifo vya watu zaidi ya 20 na maelfu ya watu kukosa makazi kutokana na nyumba zao kubomoka kutokana na tetemeko hilo, Rais Magufuli amewapa aina tofauti ya pole yenye kuwataka wananchi hao kufanya kazi badala ya kuitegemea serikali pekee.

Hatua hiyo ilikuja baada ya wananchi wengi waliopatwa na mkasa huo kusubiri serikali iwajengee nyumba baada ya watu mbalimbali kuguswa na janga hilo hivyo kuchangia fedha zaidi ya Sh bilioni nne.

“Waambie hao wanasiasa wawajengee hizo nyumba zenu wenyewe.. kwa hiyo kila mmoja katika upande wake abebe msalaba wake mwenyewe kwa sababu jukumu la serikali ni kurejesha miundombinu ya serikali, siyo kujenga nyumba za wananchi,” alisema.

Hata hivyo, licha ya kukumbwa na janga la tetemeko mkoa huo pia umekumbwa na uhaba wa chakula kutokana na ukame kama ilivyo mikoa ya Tanga, Dodoma na Singida.

Rais Magufuli pia alitolea kauli suala hilo na kueleza kuwa  “asitokee mtu kuwadanganya kwamba serikali itagawa chakula., hauwezi kugawa chakula ardhi ni ya kijani, sasa mkuu wa wilaya nataka nikueleze hapa.., sitaleta chakula hapa, hakuna chakula cha serikali, serikali haina shamba. Nimekuja kuwapa ujumbe huu, na mwenye kusikia asikie” alisema Rais Magufuli.

Kauli hizo za Rais Magufuli zimetafsiriwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na kijamii kuwa hana breki na ni hulka ya ukali hasa ikizingatiwa huu ndio mwanza wa mwaka ambao ameutumia kwenda kuwatembelea wahanga wa mkoa wa Kagera.

Rais Magufuli ni mkali

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa, alisema umefika kwa watanzania kutambua kuwa Rais John Magufuli ni kiongozi mwenye hulka ya ukali hivyo yapaswa kuishi naye kwa umakini na kukubaliana na aina ya ukali wake.

Dk. Kahangwa alitolea mfano wa ziara ya Rais Magufuli mkoani Kagera kuwa hadhani kama alikwenda kutoa pole bali ni kueleza ukweli kwani akama anavyosema kuwa yeye ni mtumbuaji hivyo hajali maumivu ya mtumbuliwaji.

“Rais wetu hana lugha ya kubembelezana, anaisimamia serikali kwa msimamo hata alipokuwa waziri tuliona matendo yake hivyo hatupaswi kulalamika kama watu wanavyofanya kwenye mitandao.

“Hatuwezi kuilazimisha serikali iwajengee nyumba wananchi kwa maana hiyo wale waliochangia inabidi kuelewa kuwa sasa umefika wakati wa kuichangi jamii na si serikali. Ni sawa na kusema serikali inatoa kibali na kufungisha ndoa lakini si kukuandalia harusi,” alisema.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alisema Watanzania wengi walifikiri mambo mengi aliyoyafanya katika mwaka wake wa kwanza labda alikuwa anajifunza namna ya kushika madaraka hayo ya urais kumbe sivyo.

“Ameendelea kufanya maamuzi yenye  utata, na sasa sio kwamba anakosea tena labda anajifunza tunaona kuwa amedhamiria kuyafanya.

“Kwa mfano staili hii ya utumbuaji majipu tunaona mbele ya safari haitakuwa na maana kwa sababu itakuwa vigumu kumwajibisha mtu. Hivyo vijana wa mtaani wanasema labda anajitafutia umaarufu.

“Lakini pia niseme nimesikitishwa sana na ziara yake Kagera kwa sababu kule si kwenda kuwafariji wahanga kwa sababu kwa akili ya kawaida huwezi kuwatolea kauli zenye utata kama zile watu walioathirika kisaikolojia kutokana na mtikisiko huo,” alisema.

Naye waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya nne na Dk. Militon Mahanga alisema watumishi wa serikali waachwe watumbuliwe ili Watanzania waelezwe kwa mbwembwe hadharani.

Mkurugenzi wa Tanesco atumbuliwe tu na wananchi tuelezwe kwa mbwembwe hadharani. Na hata Mkurugenzi Ewura naye aje atumbuliwe tu na wananchi tuelezwe utumbuaji huo kwa mbwembwe hadharani. Lakini wakati hazina watakapopeleka ruzuku Tanesco ili iweze kutoa huduma za umeme kwa wananchi, basi na hatua hiyo tuje tuelezwe kwa mbwembwe hadharani huku tukielezwa ni ruzuku kiasi gani hicho na maeneo ya huduma na maendeleo ya wananchi yatakayoathirika kwa ruzuku hiyo kupelekwa Tanesco,” aliandika Dk. Mahanga katika ukurasa wake wa Facebook.