Home Habari WAFANYABIASHARA WALIA NA WAZIRI WA JPM

WAFANYABIASHARA WALIA NA WAZIRI WA JPM

372
0
SHARE

Uamuzi wake wadaiwa kuiokosesha Serikali mapato

NA JUSTIN DAMIAN


HADI kufikia Machi mwaka huu, serikali ya Awamu ya Tano inakisiwa kuwa itakuwa imepoteza kiasi kikubwa cha mapato yanayotokana na biashara ya viumbe hai.

Imeelezwa kuwa kwa mwaka biashara hiyo huliingizia Taifa kiasi cha sh. 17 bilioni ambazo ni fedha za mauzo ya viumbe hai vinavyosafirishwa nje ya nchi.

Taarifa za uhakika kutoka kwa wadau wa biashara hiyo, zimeonesha kuwa viumbe hai hasa aina ya vyura, buibui, jongoo na konokono ni miongoni mwa viumbe vilivyokuwa vikiliingizia Taifa fedha za kigeni.

Mmoja wa viongozi wa umoja unaowahusisha wafanyabiashara wa kusafirisha viumbe hai, Adam Waryoba aliliambia RAI kuwa serikali imeshaanza kupoteza fedha hizo zinazotokana na biashara hiyo tangu Machi mwaka jana.

Waryoba alisema upotevu huo umetokana na hatua ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, kutoa katazo  la kuuzwa nje viumbe hai.

Alifikia uamuzi huo kwa madai kuwa  biashara hiyo ilikuwa ikifanyika kiholela na kwamba Serikali ilikuwa ikiambulia mapato kidogo.

Waryoba alisema hatua hiyo imelifanya Taifa kukosa mapato mengi na hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu tayari itakuwa imepoteza kiasi cha  dola za Marekani 8,890,075, ambazo ni sawa na sh. 17 bilioni.

Mfanyabiashara huyo alidai kuwa mbali na katazo hilo kuikosesha mapato nchi, lakini pia limesababisha athari kwenye maisha ya  Watanzania wengi waliokuwa wakiishi kwa mapato yaliyotokana na biashara hiyo.

“Biashara ya viumbe hai, imekuwa ikifanyika hapa nchini tangu miaka 1970 ikitumia sheria ya uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 1974 ambayo ilifanyiwa marekebisho kwa sheria namba 5 ya mwaka 2009.

“Tangu kipindi hicho, biashara hii imekuwa ikiwaajiri maelfu ya watanzania hasa wa vijijini wanaohusika na kuwakamata wanyama hao,” alisema.

 

WAZIRI KADANGANYWA

Waryoba alisema kuwa upo uwezekano wa baadhi ya watendaji wa wizara kumdanganya Waziri juu ya biashara hiyo, jambo lililosababisha Prof. Maghembe kutoa takwimu zisizo sahihi bungeni.

Alisema wakati Waziri akitoa katazo la kusafirisha viumbe hai, aliliambia Bunge kuwa Serikali imefungia biashara hiyo kwa kuwa haina tija kwa Taifa na kutolea mfano wa bei ya malipo ya tumbili mmoja kuwa serikali inapata dola za Kimarekani tano ambazo kwa tumbili 700 serikali inapata dola 3,500.

Akitolea ufafanuzi hoja hiyo, Waryoba alisema takwimu hizo hazina ukweli wowote, na kwamba ukweli ni kuwa hakuna nyani anayetozwa dola tano za Kimarekani.

“Tozo za tumbili mdogo (Velvet monkey) ni dola za Kimareni 15 wakati tumbili mkubwa (Blue monkey) ni dola za Kimarekani 25,” alisema

 RAI limefanikiwa kuona risiti zilizotolewa na Wizara ya Mali Asili na Utalii zikionyesha malipo ya Dola za Kimarekani 15 na 25 kwa aina hizo mbili za tumbili ambazo hutumika katika utafiti wa dawa ya UKIMWI pamoja na shughuli nyingine za sayansi ya tiba.

 

MADAI YA UJANGILI

 Waryoba alisema moja ya mambo yanayowashangaza ni hatua ya Waziri Prof. Maghembe kudai kuwa wafanyabiashara wa viumbe hai ni majangili, tuhuma ambazo hazina ukweli wowote kwani wao wapo kisheria.

“Waziri Maghembe amenukuliwa na vyombo vya habari mara kadhaa akisema wafanyabishara wa viumbe hai wamekuwa wakifanya ujangili, madai haya hayana ukweli wowote kulingana na taratibu za biashara hii.

“Leseni zinazotolewa kwetu hazihusishi wanyama (mammals), zinaeleza wazi kuwa sisi tutashughulika na vyura, mijusi, ndege na tumbili, jambo jema kwetu ni kuwa maeneo tunayokamata viumbe hivi ni ya wazi (open areas) ambako watu huishi na kufanya shughuli zao kama vile kwenye makazi ya watu, mashambani na  kwenye majalala.

“Sasa ni jangili gani ambaye anaweza kufanya ujangili kwenye maeneo ya namna hii, nina uhakika  Waziri analifahamu hili vizuri, lakini kwa makusudi kaamua kuuficha ukweli,” anafafanua.

Mbali na madai hayo, lakini pia Waryoba alisema ziko kauli nyingine za Waziri zinalitia aibu Taifa.

“Waziri aliwahi kunukuliwa akisema biashara ya viumbe hai imekuwa ikifanyika kiholela na kwamba wanyama wanaotoka Tanzania wanapeleka magonjwa nje ya nchi.

“Ilikuwa ni kauli ya kustaajabisha, lakini cha kushangaza Waziri hakuwa kutoa mfano hai hata mmoja” alisema.

Hata hivyo ripoti za kimataifa zinazotolewa na taasisi inayojihusisha na biashara ya viumbe hai ya Convention on International Trade on Endangered Species of Wild Flora and Fauna (CITES) zinaonyesha Tanzania inaongoza karibu kila mwaka kwa umakini na ubora katika biashara hii.

“Nimekuwa nikifanya biashara hii kwa zaidi ya miaka 30 na mpaka sasa hakuna nchi yoyote duniani imewahi kukacha kufanya biashara na Tanzania kwa kukiuka sheria na taratibu za biashara hii,” anaongezea Waryoba.

Baraka Bishanga ambaye pia ni mfanyabiashara wa viumbe hai alisema wameshangazwa na uamuzi wa serikali, kwani wao siku zote wamekuwa wakifanya kazi zao kwa kufuata sheria.

“Nachelea kusema kuwa Waziri hana nia nzuri na sisi. Hakuna tukio lolote ambalo anaweza kusimama na kusema ni uvunjifu wa sheria au taratibu ambalo limesababisha Wizara yake kufunga biashara hii.

“Ni biashara halali ambayo inatufanya tundeshe maisha yetu na familia zetu. Ningetegemea Waziri msomi kama Prof Maghembe aje na mifano hai ambayo inaweza kuwashawishi watu.”

Hata hivyo inaelezwa kuwa uamuzi wa kufungia biashara hiyo una sura ya mgogoro wa kibiashara kati ya wazawa na raia wawili wa Urusi.

Inadaiwa kuwa sababu kubwa ni baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa zabuni ya kutafuta nyani kwa ajili ya majaribio ya kisayansi yenye lengo la kutafuta dawa ya UKIMWI.

“Baada ya zabuni kutolewa Warusi hawa wawili ambao wana kampuni zilizosajiliwa hapa Tanzania waliingia katika vita baada mmoja wao kukosa.

“Alijaribu kufika mpaka ubalozi wa Tanzania katika jiji la Moscow akitaka kumshawishi balozi wetu amsaidie aweze kupata zabuni hiyo, lakini ilishindikana.

“Baada ya hapo akaona bora wote wakose na ndipo aliposaka njia nyingine zilizofanikisha kusitishwa kwa biashara hiyo,” imeelezwa.

 

TOZO ZA SERIKALI

 Waryoba anasema, wao wamekuwa wakitoa tozo hata kabla ya kufanya biashara kwa kulipishwa ada ya ukamataji viumbe hao, ambayo huitoa kabla ya kwenda kukamata tofauti na inavyokuwa kwenye biashara nyingine za Maliasili ambazo hulipiwa ada baada ya mzigo kupatikana.

Alisema uamuzi wa Waziri umeipotezea serikali fedha za moja kwa moja kiasi cha dola za Marekani 1,066,709 ambazo ni sawa na sh. 2.3 bilioni kwa mwaka ambazo hulipwa kabla ya viumbe hao kukamatwa.

Mapato mengine ni pamoja na kiasi cha shilingi bilioni 1,315,132,000 ambazo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ingepata kutokana na vibali vya kusafirisha viumbe hao pamoja na chanjo ambazo zingetolewa na Wizara ya Mali Asili na Utalii ingejipatia shilingi milioni 32 kupitia vibali mbalimbali katika biashara hii.

Taarifa inayotoa mgao (quota) wa viumbe ambao wameidhinishwa kukamatwa na kuuzwa nje na Wizara ya Mali Asili na Utalii, inaonyesha mauzo ya nje kama isingekuwa katazo la Waziri Megembe yangefikia dola za Kimarekani milioni 8,890,075 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 17.

 

HAWAKUSHIRIKISHWA

Baadhi ya wafanyabishara ya viumbe hai wanasema Waziri alichukua uamuzi huo bila kuwashirikisha, jambo ambalo limewasababishia hasara kwani hawakuweza kumalizana na wateja wao ambao tayari walishaingia nao mkataba ikiwa ni pamoja na  kuchukua malipo ya awali (advance payment).

James Kilasara mmoja wa wafanyabiashara hao anasema katazo hilo lilikuja ghafla wakati baadhi ya wafanyabiashara wakiwa katika kazi yao hiyo huku baadhi wakiwa wamechukua mikopo benki kwa ajili ya kufanikisha biashara.

“Tunavyo vibali halali ambavyo vilikuwa vinaisha Desemba 31, mwaka jana. Waziri alitakiwa kuwa na roho ya kibinadamu kwa kutupatia walau muda wa kumalizana na wateja ambao tumengia nao mikataba.

“Leo hii baadhi yetu tayari tunaviumbe ambao wanahitaji matunzo pamoja na chakula jambo ambalo ni gharama. Baadhi ya wateja wanatuona matapeli na inaharibu taswira ya nchi, Waziri alitakiwa atumie busara katika jambo hili,” anaeleza.

Machi 3, mwaka jana Waziri Maghembe aliagiza ndege iliyokuwa imebeba tumbili 62 ambao walikuwa wakisafirishwa nje ya nchi kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro kukamatwa na wahusika katika sakata hilo kuwekwa ndani.

Watuhumiwa hao saba wakiwamo raia wawili wa Uholanzi, wafanyakazi wanne wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mfanyabishara mmoja wa Kiatanzania walilazimika kosota rumande kwa miezi saba.

Hata hivyo baada ya kesi hiyo kusikilizwa, Mahakama iliwaachia huru wote baada ya kujiridhisha kuwa hakukuwa na uvunjaji wa sheria katika sakata hilo na kwamba vibali vilikuwa ni halali.

Mahakama pia iliagiza watumishi wa umma waliosimamishwa kazi kurudishwa kazini mara moja.

 

WAZIRI MAGHEMBE AZUNGUMZA

Ili kupata ukweli wa madai hayo RAI lilimtafuta Waziri Prof. Maghembe kwa njia ya simu ili alitolee ufafanuzi.

Moja ya mambo ambayo gazeti hili lilihitaji ufafanuzi kama kuna kikao cha pamoja kilifikia uamuzi wa kufungia biashara hiyo.

Akijibu madai hayo, Waziri alisema  katika kufikia maamuzi hakukuwa na ulazima wa kufanya kikao cha pamoja.

“Nani kakuambia ni lazima kikao kifanyike ndiyo maamuzi yafanyiwe? Ninachokuambia ni kuwa uamuzi wa kufungia umefanywa na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema waziri Magembe kwa ukali.

Juu ya serikali kupoteza kiasi hicho cha fedha, Waziri hakuwa tayari kulijibia hilo.