Home Habari CAG KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA RUSHWA

CAG KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA RUSHWA

462
0
SHARE

NAIROBI, KENYA


MKAGUZI Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Kenya, CAG, Ewdward Ouko, na aliyekuwa Naibu wake, Stephen Kinuthia, wamejiingiza matatani baada ya kudaiwa kutoa zabuni ya sh. milioni 100 za Kenya ambazo ni sawa na dola za Marekani 960,000 bila kufuata sheria na utaratibu.

Mamlaka ya Kupambana na Rushwa nchini humo (EACC) imetoa pendekezo la kukamatwa na kushitakiwa kwa wawili hao kutokana na uhusika wao wa kutoa zabuni ya ununuzi wa vifaa vya Kompyuta  kwa ajili ya Ofisi ya CAG.

EACC inataka Ouko ashitakiwe kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka na  kushindwa kimakusudi kufuata sheria na kanuni za manunuzi ya umma wakati ambapo aliyekuwa naibu wake Stephen Kinuthia ashitakiwe chini ya makosa kadhaa, yakiwemo matumizi mabaya ya madaraka, kushindwa kufuata sheria na kanuni za manunuzi ya umma na kufanya biashara ya bidhaa isivyo halali.

Hata hivyo uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) Keriako Tobiko, ambaye kufuatana na sheria anaweza kuamua kuwapeleka mahakamani wawili hao, kuagiza uchunguzi mpya au kuagiza jalada lifungwe kutokana na kutokuwapo ushahidi wa kutosha kuendesha mashitaka.

Katika ripoti yake kwa Tobiko ya Dsemba 16, mwaka jana EACC ilisema kuna ushahidi wa kutosha kwamba wawili hao, viongozi hao pamoja na wengine walijiingiza katika vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka na walitenda makosa ya kupoteza fedha ya serikali, hivyo wanatakiwa washitakiwe.

Uchunguzi wa EACC, kama utakuwa na ushahidi, utaathiri kwa kiasi kikubwa heshima ya taasisi iliyoundwa maalumu chini ya Katiba kwa nia ya kukagua matumizi ya rasilimali za serikali.

Uchunguzi huu ulianzishwa kufuatia barua ya Katibu Mkuu wa Hazina, Kamau Thugge, kulalamika kuwepo kwa ufisadi katika ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Thugge aliambatanisha barua kutoka kwa ‘mpiga filimbi’ aliyeibua tuhuma kadha zilizogusia manunuzi ya vifaa vya kompyuta kwa bei iliyokuzwa mno ya Shilingi 100 milioni za Kenya badala ya shilingi milioni 18 tu ambayo ndiyo ilikuwa bei ya sokoni ya vifaa hivyo.

Aidha, taarifa ya EACC kwenda kwa DPP ilisema kuwa vifaa hivyo vilinunuliwa kwa njia ya moja kwa moja bila zabuni na kwamba muuzaji alilipwa fedha bila ya kuwepo hati za kutosha.

Inasadikiwa kwamba msuka dili mkuu wa manunuzi hayo alikuwa ni, Stephen Kinuthia, ambaye alikuwa anahusika na masuala yote ya mahesabu na fedha na rasilimali watu na utawala katika ofisi ya CAG.