Home Makala KIINI CHA MAPINDUZI ZANZIBAR NI UNYONGE

KIINI CHA MAPINDUZI ZANZIBAR NI UNYONGE

200
0
SHARE
John Okello akikabidhiwa silaha

NA MWANDISHI WETU


MWISHO wa unyonge ni uasi. Hivi ndivyo unavyoweza kuyasemea Mapinduzi tukufu ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964.

Idadi kubwa ya wananchi ilidhulumiwa, ilinyonywa na kulazimishwa kuishi maisha ya kitumwa ndani ya nchi yao.

Hatimaye unyonge uliwachosha, walichoka kuendelea kunyonywa bila matumaini ya kunyonya. Usiku wa Januari 12, miaka 53 iliyopita kundi la watu 300 waliamua kuasi na kukitwaa kisiwa cha Unguja.

Kiongozi wa kukataa unyonge alikuwa ni mtu mweusi tii, mwenye misuli inayoonesha uimara wake kutoka nchini Uganda, John Okello, ambaye kwa nyakati hizo hakuwa na nafasi yoyote si serikalini bali hata kwenye shughuli zake za kawaida.

Okello alikuwa akiishi Pemba, ambako alifika hapo akitokea nchini Uganda. Okello alipokelewa na vijana wa Zanzibar ambao wengi wao walikuwa ni makuli na wabeba mizigo iliyokuwa ikiingia na kutoka Zanzibar kwa njia ya Meli.

Kutokana na vijana wengi kumkubali Okelo, waliamua kumfanya kiongozi wao katika harakati zao za kusaka haki.

Kundi hilo lilifanya mikutano yake kwa siri kubwa, nae kwa kujua dhamira ya vijana wa Kizanzibar, alibeba dhamana ya kufanya mapinduzi na kuwapa matumaini ya mabadiliko watu wake wafuasi wake.

Okello alikuwa akifanya kazi pamoja na vijana hao kwa muda mrefu, kazi zao hazikuwa za staha, mara nyingine walilazimika kufanya kazi kwenye mazingira ya hatari, huku wakipokea amri za kiongozi yeyote ambaye ataweza kuwalipa.

Hali hiyo iliwachosha, hivyo waliamua kufanya uasi kwa nia ya kusaka malisho bora na yenye staha.

Kwakuwa hali ya kisiasa haikuwa nzuri ndani ya Zanzibar na Pemba  tangu kufariki kwa Sultan Khalifa mwaka 1960, aliyetawala Zanzibar kuanzia mwaka 1911-1960, ilikuwa ni rahisi kwa vijana hao kupenyeza harakati zao.

Baada ya kifo hicho kulifanyika uchaguzi ambao ulitawaliwa na udanganyifu mkubwa katika majimbo ya uchaguzi mwaka 1961. Vyama vikuu vilishindwa kujipatia wingi wa kura kwa kila kimoja.

Waingereza waliamua kuyaondoa majeshi yao kikiwemo kikosi maalumu cha Kiarishi ambacho kilikuwa kimewekwa karibu na uwanja wa gofu na mpaka wa mji mkongwe mapema mwaka 1963.

Wakati mfalme mpya, Jemshid akipandisha bendera ya Taifa huru la Zanzibar Desemba  12, 1963, aliadhimisha uondokaji wa Gavana wa kiingereza na mwisho wa ukoloni visiwani humo.

Uchaguzi mwingine uliofanyika mwishoni mwa mwaka 1963 ukiipa ushindi mdogo wa kura Muungano wa chama cha Chama cha Kizalendo Zanzibar (ZNP) na Chama cha Watu wa Pemba na Unguja (ZPPP) na chama cha Afro Shirazi (ASP) ambacho kilipaswa kuwamo ndani ya Serikali iliyo chini ya nusu ya wabunge kwa mtindo wa Bunge la Kiingereza na Sultani akiwa kama mtawala asiye na maamuzi ya mwisho.

Zanzibar ambalo lilikuwa taifa kamili mwanachana wa Jumuia ya madola na mwanachana mpya wa Umoja wa Mataifa lilidumu kwa siku 33 tu.

Majadiliano makali ya kisiasa na maandamano yalikuwa ni matukio ya kawaida siku hizo. Kulikuwa na makudni ya watu mbalimbali mitaani waliokuwa wakiimba na kusifu majina mbalimbali ya viongozi wa kisiasa, huku yakivuka vizuizi vya barabara vilivyokuwa vikilindwa na askari wa Kiingereza.

Vikundi mbalimbali vilijadiliana juu ya mambo yanayowakabili ikiwa ni pamoja na haki dhidi ya fursa, wageni dhidi ya wenyeji wa zamani, Ubepari dhidi ya Ujamaa, Wafanyabiashara dhidi ya wamiliki ardhi, Waunguja dhidi ya Wapemba, Waasia dhidi ya pazia la nyuma la vita baridi na harakati za utaifa na kuondosha ukoloni ambazo zilikuwepo kipindi hicho ndani ya Afrika.

Okello hakuwa na jawabu la mambo hayo nyeti, lakini alikuwa na kipawa cha kutambua kwamba vikundi hivi vinavyoshindana vinatoa nafasi nzuri kwa mtu wa harakati kama yeye.

Aliitumia nafasi hiyo kujipanga na hatimaye yeye na kundi lake waliweza kutwaa vituo muhimu vya kienyeji vya habari na kambi za Polisi.

Mara tu baada ya vituo vya habari na Kambi za polisi pamoja na silaha kudhibitiwa na  Okelo, hakukuwa na mtu ambaye angeweza kumshinda.

Viongozi wa A.S.P ambao wengi walikuwa nje ya Zanzibar walifadhaishwa na matendo ya Okello.

Hata hivyo wapo waliowaunga mkono waasi hao. Mamia ya wafuasi wa vyama walipigwa na butwaa juu ya wale ambao walikuwa na shuku ya kukata fundo hilo gumu la majadaliano ya kidemokrasia na kukimbilia moja kwa moja kwenye utawala.

Hawa walitafuta njia ya kuiandaa jamii kwenda sambamba na kanuni zao. Kanuni siku hizo zilikuwa ni ghali sana kama sarafu ya Marekani. Ubinadamu ulikuwa ni kitu adimu sana.

Baadhi ya viongozi wa ASP baada kuona kwamba serikali itakuwa haina udhibiti na uwezo kujilinda na kutokuwa na imani na matokeo ya chaguzi huria zilizofanyika, viongozi walitafuta njia za haraka za kuhalalisha udhibiti  wa yale ambayo yaliitwa sasa “Mapinduzi”.

Makundi ya watu wenye fujo yalikuwa huru. Sheria na amani zilikuwa hazipo katika mitaa ya Zanzibar.

Walimiliki ardhi na wafanya biashara waliburutwa kutoka majumbani na madukani mwao, uporaji na mauaji yalienea katika eneo lote la Mji mkongwe mzima.

Waarabu na Waasia , waliokuwa wakiunga mkono vyama vyengine waliuliwa kwa makundi. Kwa usiku mmoja maisha ya watu wengi  yalipotea hatimae maelfu ya watu waligeuka kuwa wakimbizi kwa kuikimbia nchi yao.

Okello mwenyewe alijipachika cheo cha Jemedari Mkuu akishirikiana na bataliani zake zenye fujo, walianzisha utawala wa vitisho ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Alitangaza vitisho visivyo vya kawaida na ahadi ya kifo kwa wote watakaojaribu kumpinga yeye,  aliamini kuwa alikuwa akipokea maelekezo kutoka kwa Mungu na akionyesha uwezo usiokuwa wa kawaida kwa kutumia nambari, kwa mfano tarehe Januari 13, 1964, alitangaza ujumbe ufuatao.

” Serikali sasa inaendeshwa na sisi ikiwa mtakuwa wakaidi na kukataa kutii amri, nitachukua hatua kali mara 88 zaidi ya hatua ninazozichukua hivi sasa na  ikiwa yeyote atashindwa kutii amri ya kutotoka nje ya nyumba kama walivyofanya wengine.sitokuwa na njia nyengine zaidi ya kutumia silaha nzito. Sisi, ni jeshi lenye nguvu ya 99,099,000″.

Vitisho vyake na uwezo wake wa kuvitekeleza viliwatia hofu raia, hasa makundi mbali mbali ya jamii zilizo ndogo.  Januari 14, 1964 alitangaza maneno ya kufadhaisha kwa kusema kuwa: Huyu hapa ni Jemedari Mkuu wa Unguja na Pemba, nafikiria kuelekea kijiji cha Mtendeni kukiangamiza ikiwa watu wa hapo hawatafuata amri. Baada ya dakika 40 nitawamaliza nyote hasa Wangazija na kwa vijana wote wa kiarabu wanaoishi Malindi, nitapita Malindi nikiwa nimesheheni silaha ambazo mimi mwenyewe ndie nizijuazo. “Nataka kuona kila mmoja abakie na chupi na kulala chini. Nataka kuwaona wao wanaimba… Baba wa Waafrika. Mungu Mbariki yeye na malengo yake na yale ya Jemedari Mkuu.”

Wakati unyanyasaji uliposimama jamii za tamaduni tofauti za Zanzibar zilikuwa zimeparaganyika.

Taifa la chama kimoja lilitangazwa. Lakini bado taifa hili likihofia uwezekano wa kufufuka upinzani kutoka kwa wapinzani waliokimbia nchi.

Wanamapinduzi hawa baadae walijihakikishia udhibiti zaidi baada ya kusaini mkataba wa Muungano wa Tanganyika. Hii ingeruhusu maelfu ya marafiki wa kisiasa wa Tanganyika kuingilia kati upinzani wowote wa baadae katika visiwa hivi.

Askari polisi wa Zanzibar walibadilishwa kwa askari polisi kutoka Tanganyika ambao ni watiifu kwa chama na pazia la siasa za utengano ziliwakumba Wazanzibari ambazo zilitakiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 20.

Jambo la kufurahisha ni namna Hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyoweza kutokomeza matendo yote dhalimu visiwani humo kwa kuingiza Zanzibar kwenye Muungano na Tanganyika.

Viongozi wa kweli na wenye kujali hali za watu wameibuka Tanzania na hii imewafanya wakimbizi waliokimbia wakati wa mapinduzi kurejea visiwani. Uvumilivu na amani sasa vimerejea Zanzibar.

Ingawa Okello alileta vitisho, lakini angalau aliweza kukomesha unyonge kwa wanyonge.