Home Habari MOHAMED DEWJI ATAJWA TENA KUWA BILIONEA NAMBA MOJA KIJANA BARANI AFRIKA

MOHAMED DEWJI ATAJWA TENA KUWA BILIONEA NAMBA MOJA KIJANA BARANI AFRIKA

880
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU


KWA mara ya tatu mfululizo jarida maarufu la Forbes la Marekani linalotoa ripoti ya masuala mbalimbali limemtangaza mfanyabiashara na mwanasiasa wa zamani wa Tanzania, Mohamed Dewji kuwa bilionea namba moja kijana barani Afrika.

Jarida hilo ambalo limekuwa likitoa orodha ya mabilionea duniani pia limemworodhesha Dewji kwenye nafasi ya 16 ya mabilionea wa Afrika huku mfanyabiashara bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote akiendelea kushikilia namba kwa miaka sita mfululizo kutokana na kuwa na utajiri unakadiriwa kufikia kiasi cha Dola za Marekani bilioni 12.1.

Hii ni mara ya tatu kwa Dewji ambaye amekuwa akijihusisha na biashara mbalimbali ikiwemo vyakula na vinywaji kutajwa na jarida hilo kuwa bilionea kijana Barani Afrika, ambapo mwaka juzi alikuwa katika nafasi ya 21, ambapo mwaka jana utajiri wake ulikadiriwa kufikia dola bilioni 1.1.

Forbes linabainisha kuwa kwa mwaka huu, utajiri wa Dewji maarufu kama MO umeongezeka hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.4.

Dewji ambaye ana umri wa miaka 41, ameingia kwenye orodha hiyo ya matajiri wa Afrika kupitia kampuni yake ya Mohamed Enterprises (Metl Group), ambayo imekuwa ikifanya biashara katika nchi mbalimbali Afrika.

Dewji mwenye familia ya watoto watatu anaelezwa kuwa na mafanikio makubwa kutokana na kuwa na nidhamu katika biashara na mali zake, ambazo zilianzishwa na  wazazi wake.

Mbali na vyakula na vinywaji, lakini pia mwanasiasa huyo na mbunge wa zamani wa Singida Mjini amekuwa akifanya biashara ya nyumba, mazao na viwanda vya mafuta.

Kwa sasa Dewji ndiye Ofisa mtendaji Mkuu wa Metl, hatua aliyoifikia baada ya kuendeleza mali za baba yake yake ambaye alianzisha kampuni hiyo kwenye miaka ya 1970.

Kinywaji chake cha Mo Cola, kimekuwa kiuzwa bei ya chini ikilinganishwa na kile cha Coca Cola, huku mshindani wake mkubwa nchini Tanzania akiwa ni  Said Salim Bakhresa ambaye ni mtengenezaji wa kinywaji cha Azam Cola.

Dewji alistaafu ubunge mwanzoni mwa mwaka 2015 baada ya kukamilisha vipindi vyake viwili vya uongozi.

Katika siasa hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, Dewji alikuwa mstari wa mbele katika kukisaidia  Chama Cha Mapinduzi (CCM), hali iliyochangia ushindi wa chama hicho kwa wabunge na hata urais.

Mfuko wake wa Mo Foundation umekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa unatoa ufadhili kwa wanafunzi wanaotoka familia duni kuweza kupata elimu.

Mabilionea wengine waliotajwa na jarida hilo mbali ya Dangote ni Michael “Mike” Adenuga wa Nigeria ambaye utajiri wake unatokana na kuwekeza zaidi kwenye mawasiliano, mafuta na makazi, ukikadiliwa kufikia dola za Marekani bilioni 10.3.

Nafasi ya tatu imeshikwa na Nicholas “Nicky” Oppenheimer wa Afrika Kusini ambaye utajiri wake ni dola za Marekani bilioni 6.6 unaotokana na dhahabu.

Bilionea mwingine ni Christoffel Wiese pia kutoka Afrika Kusini ambaye utajiri wake umetokana na  uuzaji wa bidhaa mbalimbali kwa mfumo wa rejareja ambapo unafikia dola bilioni 7.3 na nafasi ya tano kwenye orodha ya matajiri barani Afrika imechukuliwa na Johann Rupert mwenye utajiri wa dola bilioni 5.4.