Home Latest News ILANI YA CCM BADO INA MAKENGEZA?

ILANI YA CCM BADO INA MAKENGEZA?

223
0
SHARE

 Na Chrysostom Rweyemamu,

KUMEKUWAPO na swali miongoni mwa Watanzania kuhusiana na mambo makuu mawili ambayo Mahakama Kuu ya Tanzania iliwahi kuyatolea uamuzi.

Mojawapo ya mambo hayo ni lile la takrima, ambalo si tu Mahakama Kuu ilitamka wazi kwamba ni rushwa, bali pia ilisema wazi kwamba sheria ya takrima ilikuwa inakiuka Katiba ya nchi, kwa  vile ilikuwa inawabagua Watanzania kutokana na ukweli kwamba ili uweze kukubalika kwa wapigakura, ilikuwa lazima utoe ‘chochote’.

Aidha, Mahakama Kuu ilisema kwamba sheria hiyo ilikuwa inawadhalilisha wananchi, kwa maana ya kuwapa vitu visivyo na maana kama pombe, sukari, kanga, sabuni, nakadhalika.

Jambo la pili ambalo Mahakama tajwa ililitolea uamuzi ni Sheria ya Uchaguzi ambayo ilikuwa inamlazimisha mwananchi kuomba uongozi kupitia vyama vya siasa.

Mahakama Kuu ililikataa hili kwa maelezo kwamba sheria hiyo ilikuwa inakiuka Katiba ya nchi, haki za binadamu na kuwabagua wananchi wasio na vyama kutopata fursa sawa ya kushiriki kwenye siasa za nchi yao.

Hata hivyo, Serikali ilikata rufaa kuhusu uamuzi huu,  na baadaye jopo la majaji likiongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu, Agustino Ramadhani, lilitengua kipengele hiki na kufuta ndoto ya mgombea binafsi bila kupitia chama chochote.

Uamuzi kuhusu yote haya  ndio unawafanya Watanzania wajiulize: Hivi  aliyevunja Katiba ya nchi ni nani?

Sheria ya Uchaguzi pamoja na marekebisho yake ilitungwa mara Tanzania ilipoamua kurudi kwenye mfumo wa zamani wa vyama vingi; na katika Sheria ya Uchaguzi, kipengele hiki kiliwekwa kwa makusudi ili kuwabana wana-CCM ambao hawakuridhishwa na mizengwe iliyokuwa ikiendeshwa kwenye chaguzi za ndani.

Waliofanyiwa mizengwe wakashindwa kuondoka CCM walikuwa wanabakia wakigugumia humo humo.  Watu wengi hawapendi lisemwe hili, lakini ukweli ni kwamba wengi wa viongozi wa CCM walishindwa kuondoka kwa kuwa hawakuona vyama vya siasa ambavyo wangejiunga navyo na kufanikisha malengo yao.

Wale walioondoka CCM kwenda Upinzani, wengi walirejea, isipokuwa wachache kama kina Augustine Mrema ambaye alibaki Upinzani lakini akaendelea kukipa CCM ushabiki.  Wengi hawakuiweza misuguano iliyovikumba vyama hivi vipya.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alitabiri kwamba chama cha upinzani chenye nguvu kitatokana na CCM.  Aliamini fika kwamba watu waliokuwa na wafuasi wengi ndani ya CCM wangekihama chama hicho na kuunda chama cha upinzani chenye nguvu.

Viongozi wa CCM, ili kudhibiti hali hiyo isitokee, wakatunga kifungu kwenye sheria ya Uchaguzi kwamba mtu hawezi kufanya shughuli za kisiasa bila kuwa na chama cha siasa.  Hiki ndicho kilichozuia mmeguko uliotarajiwa ndani ya CCM.

Sasa tunapofanya mrejeo kutokana na uamuzi huu wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa hatuachi kujiuliza:  Hivi aliyevunja Katiba hapa ni nani?

Rais Ali Hassan Mwinyi ndiye aliyefungua ‘pandora’s box’, yaani upenyo ulioambatana na makandokando yake chanya na hasi, ambao ulianzisha utitiri wa vyama vya siasa, na pia kufungua madirisha yote ya uchumi kwa sera yake ya “ruksa”.

Nchi ilikwenda mrama, rushwa ikaongezeka, matajiri wakaongezeka na kushirikiana na viongozi kuinyima Serikali mapato.

Kodi ikawa haikusanywi, misamaha ya kodi ikawa mingi mno mpaka nchi fadhili zikashtuka na kusimamisha misaada na mikopo.

Rais Mwinyi akalazimika kufanya mabadiliko katika Serikali ili kukidhi masharti ya wafadhili.  Hiki kilikuwa ni kipindi cha “lala salama” cha utawala wa Mwinyi.

Lakini hapa inatubidi tuseme wazi kuwa kipindi cha pili cha ‘Mzee Ruksa’ kiliipeleka nchi pabaya.  Ni kipindi hiki ambapo zilifumka kashfa kama ile ya Loliondo, akina Chavda kupewa mashamba ya umma ‘bure’, kushamiri kwa mihadhara mingi ya kashfa za kidini na mikataba mingineyo ambayo haikuwa na faida kwa nchi.

Ukienda ndani zaidi unafikia uamuzi kwamba Mzee Ali Hassan Mwinyi hakuwa amebuni ilani na jinsi ya kuendesha nchi.  Alikuwa akitekeleza sera za chama chake CCM!

Kikaingia kipindi cha Rais Benjamin William Mkapa.  Kwenye Ilani ya CCM, mambo yaliyokuwa yakizungumzwa sana ni kero ya rushwa.  Mkapa akaapa kuwa “hatakuwa na suluhu na rushwa”, lakini baadaye akawa kigeugeu kwa hili na akatamka bayana kwamba Ilani ya CCM ilikuwa haitekelezeki.

Yeye alisema, ni lazima tuambizane ukweli, sera yake ikawa ya Uwazi na Ukweli. Ni katika kipindi hiki sheria ya Takrima ambayo Mahakama Kuu ilisema ni kinyume cha Katiba ya nchi  ilipopitishwa na Bunge.

Katika kipindi cha Mkapa tulishuhudia kuuzwa kwa mashirika karibu yote ya umma, kuingia mikataba mibovu na makampuni ya kimataifa yanayochimba migodi na mingineyo inayochota rasilimali ya nchi.

Wakati huo huo Mzee wa “Ukweli na Uwazi” akakazania kutupeleka kwenye utandawazi.

Huyu naye hakuwa ametunga Ilani yake binafsi, alikuwa akitekeleza Ilani ya chama chake, CCM.  Sasa hapa tunasemaje? Ni nani aliyevunja Katiba ya nchi au kwenda kinyume cha Ilani ya chama?  Ni Mwinyi au Mkapa?

Miaka 10 ya Mkapa ilikwisha wakati tofauti ya ongezeko la kipato miongoni mwa makundi mbalimbali katika jamii ikiwa imeongezeka sana.  Viongozi wengi, huku wakilindwa na sheria hizi mbovu za Takrima na sheria ya Uchaguzi wakajihakikishia kwamba wanaendelea kutawala.

Wakatunga kipengele kingine ambacho kilihusu kuwa kupinga matokeo ya uchaguzi sharti mlalamikaji awasilishe kwanza Sh milioni tano!

Kipengele hiki ndicho kilitumika kuwanyima haki Watanzania kupinga matokeo ya uchaguzi waliyoyaona kuwa si halali. Hiki Kipengele pia kiliwanyima wananchi haki ambayo ni ya kikatiba!

Baadaye akaja Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia alitekeleza Ilani hiyo hiyo ya chama kile kile – CCM.  Je, na yeye alivunja Katiba kwa mwendelezo ule ule?

Maana CCM walisema Serikali inatekeleza Ilani ya chama tawala!  Mwinyi alilaumiwa kwa kuiachia nchi iwe holela (ruksa) kiasi hicho, Mkapa alilaumiwa kwa mambo kadhaa, ikiwamo kuuza mashirika ya umma na pia mikataba mibovu; na wote wawili walikuwa wanatekeleza Ilani ya chama kilichowasimamisha na hatimaye wakanyakua madaraka ya dola.

Katika utendaji kazi wa Rais Kikwete, naye alitekeleza Ilani ya CCM kama watangulizi wake, lakini wakati huo huo chama chake kilisambaratika na makundi ndani ya chama hicho yalitaka kutoana roho!

Mfumuko wa bei ulikwenda juu sana, kauli mbiu ya “Kasi Mpya, Ari Mpya na Nguvu Mpya” iliyeyuka kama barafu na “Maisha Bora kwa kila Mtanzania” ikawa ndoto!

Aidha, CCM ilitekwa na wenye fedha zilizotokana na ufisadi na uporaji wa rasilimali za nchi.

Sasa Ilani hii ya CCM ilikuwa na sura ngapi?  Au ilikuwa na makengeza kama ambavyo macho yenye makengeza huwa hayana uhusiano katika kuangalia kitu kimoja!

Na Rais Dk. John Magufuli ambaye ni Rais na Mwenyekiti mpya wa CCM atakuwa na makengeza haya? Amekwisha kusema kuwa anataka CCM safi, na kuna mambo mazuri amekwisha kuyafanya. Tusubiri tuone.