Home Latest News RAIS USICHOKE KUSHUGHULIKIA WAOVU

RAIS USICHOKE KUSHUGHULIKIA WAOVU

290
0
SHARE
Rais John Magufuli

NA ARACHARD MUHANDIKI,

NATOA pongezi zangu za dhati kwa Rais Dk. John Magufuli, ameonesha nia na dhamira ya kweli ya kupambana na uhalifu na wahalifu kwa ujumla wake.

Katika kipindi kifupi cha utawala wake ameonesha sura ya kuuchukia uovu na waovu kwa maneno na matendo. Hatua yake hii inanipa faraja kubwa na ya kipekee.

Katika umri wangu wa miaka zaidi ya 70 sasa, sikupata kutarajia kuja kuona kiongozi wa kariba ya Rais Magufuli katika zama hizi za watu kupenda mali kuliko chochote.

Sikutarajia hilo kwa sababu ya historia na mwenendo wa baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali waliopita, wengi wao walipenda kujilimbikizia mali kuliko kuwapigania masikini.

Jambo la kufurahisha na kutia moyo ni namna Rais Magufuli anavyoweka mbele masilahi ya kundi kubwa la Watanzania masikini, hasa wakulima ambao wamekuwa wakinyonywa kwa muda mrefu.

Ukweli wa kunyonywa kwa wakulima unabebwa na mfano mdogo wa Chama Kikuu cha Ushirika Kagera maarufu kama KCU (1990) Ltd.

Chama hiki ambacho msingi wake ulikuwa ni kuwanufaisha wakulima wengi, kimetumika vibaya, baadhi ya watu wachache waliopewa dhamana ya kukiongoza walijilimbikizia mali, walikula bila kusaza.

Kundi hilo dogo ndilo lilikuwa miungu watu ndani ya Ushirika, wao ndio walikuwa waajiri wa vyama vidogo vidogo ambavyo ndivyo vinavyounda Chama Kikuu cha Ushirika, jambo ambalo ni tofauti, wao walipaswa kuwa waajiriwa wa vyama hivyo.

Hata hivyo, kwa sababu ya wakulima wengi kutojua haki zao, walijikuta wakiwasujudia na kuwaogopa viongozi hao wachache ambao walijinufaisha kwa kunyonya jasho la wanyonge.

Jambo la kufurahisha ni uamuzi sahihi uliochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuamua kuwaondoa viongozi wachache waliokuwa wakila na kusaza.

Hii ni hatua nzuri na bora kwa wakulima, huenda sasa haki yao iliyopotea kwa muda mrefu ikapatikana.

Pamoja na mambo yote hayo, bado naiona haja ya viongozi wapya wa KCU (1990) Ltd kutafuta namna bora ya kuwaondoa wawakilishi wengi wa vyama vidogo vidogo ambao wengi wao hawajui majukumu yao na badala yake walikuwa wakiweka masilahi yao mbele.

Hawakuwa na muda wa kupitia nyaraka muhimu za Ushirika wakati wa vikao, kwao muhimu ilikuwa ni posho za vikao na kwa sababu wajanja wachache walishaujua udhaifu huo, walichokuwa wakikifanya ni kuwapatia posho mapema ili wakimbilie madukani hatua inayotoa mwanya wa kupitishwa kwa mambo yanayowanufaisha wachache.

Kwamba haikuwa rahisi kuwahoji na yeyote aliyewahoji alitimuliwa kwenye mkutano kwa sababu alionekana ni adui wa kundi hilo ambalo leo hii limeondolewa madarakani na Serikali ya Awamu ya Tano.

Walikuwa na nguvu sana na nguvu zao zilihuishwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa hasa waliokuwa na dhamana na uwaziri. Jamaa hawa waliweza kuiba mabilioni ya fedha kwa kununua na kuuza mali za ushirika, ushahidi wa haya mambo upo na yanajulikana.

Nimefurahishwa na hatua ya Serikali ya kuwaondoa na kuweka uongozi mpya, lakini ninayo rai kwa uongozi wa sasa, unapaswa kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kwa kuhakikisha wanatoa elimu ya kujitambua.

Wakulima wengi hawajui haki zao, wanadhani KCU ni kikubwa kuliko wao, wanashindwa kujua kuwa bila wao hakuna Ushirika iwe kwa Kagera au  Tanzania kwa ujumla.

Mbali na hilo lakini pia iko haja na sababu ya mali za viongozi wa zamani kutaifishwa, wamekula na kukomba mali za wavuja jasho wa Kagera. Inatosha, sasa ni wakati wao kurejesha haki ya wakulima waliyoikalia kwa muda mrefu.

Namwomba Rais Dk. Magufuli asichoke kuwashughulikia watu waovu wanaowaibia masikini, natambua anayo majukumu mengi, lakini jukumu la muhimu kwake na ambalo naona ameanza kulitilia mkazo ni kuwapigania masikini ambao wamedhulumiwa haki zao kwa muda mrefu.

Mwandishi wa makala haya ni mkulima wa kahawa mkoani Kagera.