Home Afrika Mashariki JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI: DEMOKRASIA NA UTAWALA WA KIKATIBA BADO KIZUNGUMKUTI

JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI: DEMOKRASIA NA UTAWALA WA KIKATIBA BADO KIZUNGUMKUTI

808
0
SHARE

NA HILAL K. SUED

KUANZIA miaka ya 1920, Serikali za kikoloni wa Kiingereza zilizokuwa zikitawala nchi hizi tatu za ukanda wa Afrika ya Mashariki (Tanganyika (wakati ule), Kenya na Uganda ziliona umuhimu wa kuwa na njia bora ya ushirikiano miongoni mwao katika baadhi ya huduma za kipamoja kama vile mawasiliano na uchukuzi, ukusanyaji mapato, uchumi na uwekwaji takwimu na utafiti.

Tunaweza kusema kwamba hatua hii ilikuwa inavunja ule mkakati wao mkuu wa kikoloni wa ‘wagawanye na uwatawale’ (divide and rule) na badala yake wakaja na huu wa ‘waunganishe na uwatawale’ (unite and rule).

Lakini ushirikiano kamili ulianzishwa mwaka 1948 pale Serikali hizo ziliunda Tume ya Afrika Mashariki (East African High Commission- EAHC) katika kusimamia masuala hayo. Tume hiyo, ingawa ushirikiano wake ulikuwa ni wa katika ngazi ya utumishi zaidi (civil service) bali pia kulikuwapo na baraza la kutunga sheria (East African Legislative Assembly) ambalo wajumbe wake walikuwa wakiteuliwa na Magavana waliokuwa wakiyasimamia makoloni hayo.

Kwa mfano zile sheria za kuhusu ukusanyaji mapato, East African Customs Management Act na ile ya East African Income Tax Act, awali zilitungwa na EA High Commission na bado zinatumika sasa hivi baada ya kufanyiwa marekebisho kadha kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 70.

Baada ya nchi hizi tatu kuanza kupata uhuru mwanzoni mwa miaka ya 60, Tume hiyo ya EAHC  ilizaa jumuiya mpya, East African Common Services Organization (EACSO). Mwaka 1967 wakuu wa nchi hizi tatu huru walitiana saini mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, East African Community (EAC).

Miongoni mwa dhambi kubwa zilizotendwa na viongozi wa Bara hili tangu uhuru hakuna kama ile ya viongozi wa Jumuiya hiyo kuruhusu jumuiya hiyo kuvunjika miaka 10 tu ya uwepo wake, mwaka 1977.

Nasema hivi kwa sababu ushirikiano baina ya nchi za Jumuiya hiyo ambayo misingi yake tuliachiwa na wakoloni ulikuwa wa kipekee kabisa duniani, kimuundo na kiutendaji kwani ushirikiano baina ya nchi hizo ulikuwa mkubwa na wa karibu mno kuliko hata uliopo ndani ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) sasa hivi.

Mbali na kuendesha kipamoja mashirika ya kutoa huduma kama vile usafiri wa reli, ndege, shughuli za posta na simu na uendeshaji wa bandari, pia kulikuwapo mahakama moja ya rufaa kwa nchi zote tatu – Court of Appeal for East Africa na uendeshaji wa kipamoja taasisi kadha nyingine kama vile za utafiti wa malaria, uvuvi na uthibiti wa wadudu waharibifu wa mimea. Ilikuwa na Katibu wake mkuu na mawaziri waliokuwa wanasimamia idara (secretariat) mbali nbali.

Jumuiya hiyo ilivunjika mwaka 1977 kutokana na tofauti za kisiasa miongoni mwa viongozi wakuu wa nchi hizo ambao ndiyo walikuwa ‘mamlaka’ kuu ya kuiongoza Jumuiya hiyo (Authority). Na bila kutafuna maneno nadiriki kusema kwamba tofauti hizi zilitokana na migongano baina ya Tanzania dhidi ya nchi zile nyingine mbili.

Kwa Uganda ilianzia kwa ujio wa utawala wa Iddi Amin mwanzoni mwa miaka ya 70 ambao Tanzania haukuutambua na nchi mbili hizi zilipigana vita fupi ya mpakani mwishoni mwa 1971.

Na kutokana na Tanzania kutoitambua Uganda mikutano ya wakuu watatu wa jumuiya hiyo (E.A Authority) ilikuwa haifanyiki na hivyo Jumuiya nzima ikaanza kukosa muongozo kutoka juu, hali ambayo ilikuwa inaiathiri sana afya yake.

Na tofauti zetu na Kenya zilikuwa za kiitikadi zaidi lakini pia zilizidishwa na ugomvi wetu na Uganda, ugomvi ambao hatimaye uliishia kwenye vita kubwa ya umwagaji damu ya 1978-79 ambayo hatimaye ilimuondoa Idi Amin madarakani. Na hili ndilo Kenya walilitumia katika azma yao ya kuona Jumuiya ile inavunjika. Tusisahau kwamba Tanzania iliingia vitani na Uganda wakati hatuna maelewano mazuri na Kenya kutokana na kuvunjika kwa Jumuiya.

Kwa hiyo hata kuvunjika kwake hakukuwa kwa utaratibu uliofaa kwani kila nchi zilianza kuhodhi mali za mashirika ya Jumuiya yaliyokuwa nchini mwake.

Kwa mfano Kenya ilizuia ndege za lililokuwa shirika la ndege la Jumuiya hiyo – East African Airways (EAA) na vichwa vya treni, mabehewa na meli za lilikouwa Shirika la Reli la Jumuiya (East African Railways Corporation – EARC). Makao makuu ya mashirika mawili hayo yalikuwa nchini Kenya.

Sote twakumbuka kwamba meli ya MV Victoria iliyokuwa katika kitengo cha huduma za majini (Marine Services) ndani ya EARC ilizuiliwa kwenye bandari ya Kisumu, Kenya kwa miaka kadha tangu Jumuiya ilipovunjika na hatimaye ilipewa Tanzania baada ya mgawanyo wa mali za Jumuiya huyo mapema miaka ya 80.

Swali kubwa sasa hivi ni kwamba hivi sisi wakazi wa nchi za Afrika ya Mashariki tulijifunza chochote kutoka historia? Je, tulijiwekea mifumo yoyote mathubuti ya kuzuia haya yasitokee tena? Na hasa pale Jumuiya hiyo imekua baada ya kuongezeka kwa nchi za Burundi na Rwanda (2007) na Sudan ya Kusini mwaka jana?

Vipo vizuizi vyovyote, kimuundo na vya kisheria, vya kuzuia nchi mwanachama mmoja kudai sehemu ya ardhi ya mwanachama mwingine (kama vile Idi Amin alivyodai sehemu ya ardhi ya Tanzania) au hata yenyewe kutumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe?

Kutokana na ‘shahada’ zao za kisiasa zenye mashaka mashaka, viongozi hawa wako tayari kuruhusu matendo yao yatathminiwe na wenzao (peer review) katika Jumuiya bila pingamizi?

Wengi hawaamini hivyo. Sasa hivi kuna mgogoro wa kisiasa nchini Burundi unaokaribia miaka miwili na viongozi wa Jumuiya, waliokutana Arusha Machi mwaka jana, walionekana kutokuwa na namna thabiti ya kuutatua. Changamoto kuu ni kwamba viongozi wengi hawa hawana sifa za kufanya hivyo. Hakika, walilizungumzia hilo suala lakini yaliishia katika mazungumzo ya mezani tu. Ngoja tuone.

Na hapo ni pamoja na miaka kadha iliyopita kuanzishwa kwa mkataba wa pamoja (Protocol) wa kusimamia masuala ya utawala bora na utoaji wa maamuzi ya haraka kuhusu masuala ya migogoro ya siasa, masuala ambayo yalitajwa kuwa muhimu katika ajenda ya ushirikiano wa kisiasa (political integration agenda) wa nchi hizi.

Haya yalitarajiwa kutoa suluhisho la kudumu katika uendeshaji wa chaguzi – suala nyeti kwa nchi zote wanachama. Kwa mfano Ibara ya 2 na 3 ya Mkataba huo zilizitaka nchi wanachama kudumisha misingi ya demokrasia, kusimamia utawala wa katiba na kufanya chaguzi zilizo huru na haki na katika kubadilisha serikali kwa njia ya amani.

Lakini hakuna anayeamini iwapo kweli haya yanweza kutekelezeka na viongozi wote wa Jumuiya ambao kila mmoja wao anaamini kwamba masuala ya uendeshaji chaguzi ni masuala ya ndani ya nchi zao. Hakuna kufundishana hapa! Masuala ya uendeshaji chaguzi katika misingi inayotakiwa yanawahusu Wamarekani, Waingereza na Wafaransa, siyo wao!

Hebu angalia: Wakati viongozi hao watano wa Jumuiya walipokutana Machi mwaka jana katika Hoteli ya kifahari ya Ngurdoto, Arusha (ambako eti pia walizungumzia changamoto ya kuondoa umasikini katika nchi zao) kulikuwa na migogoro ya kisiasa katika kila nchi hizo iliyofikia uzito wa viwango tofauti.

Ni vigumu kuniaminisha kwamba Yoweri Museveni anaweza kusuluhisha mgogoro wa kikatiba unaoitafuna Burundi unaotokana na ukomo wa vipindi vya urais ambapo yeye mwenyewe (Museveni) haamini suala zima la ukomo. Vivyo hivo kwa Paul Kagame wa Rwanda.

Iwapo ubora wa hali ya juu katika usuluhishi wa migogoro katika nchi za Afrika ulionyeshwa na Umoja wa Afrika (AU) takriban miaka 10 iliyopita uliofanikisha kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Burundi, sembuse Jumuiya hii ya nchi sita tu sasa hivi? Inawezekana kazi ikawa rahisi zaidi.

Kwa upande wa Kenya ambayo polepole imekuwa ikisimika katiba yao mpya waliyoipata kwa njia ya umwagaji damu, chokochoko za kisiana na wanasiasa zinaanza kujitokeza kuelekea uchaguzi mkuu Agosti mwaka huu. Siasa chafu, ufisadi wa kiuchumi na kisiasa na kurushiana maneno kumeanza, ni kama vile wamesahau kabisa yaliyotokea baada ya uchaguzi wa Desemba 2007. Wakuu wengine wa Jumuiya hiyo wanafanya nini kuzuia hilo lisitokee tena?

Tanzania pia ina sehemu yake ya siasa haribifu pamoja na majigambo ya majukwaani kwamba ni kisiwa cha amani katika bahari ya machafuko. Kuna suala lilitokana na kufutwa ghafla kwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar yaliyoonyesha kuupa ushindi upinzani. Pengine mgogoro huu haukufikia kiwango cha kutaka kuingiliwa na viongozi wengine wa Jumuiya, lakini inawezekana pia ukafikia hatua hiyo. Hakuna anyejua katika mienendo ya siasa.

Na iwapo utafikia hapo, je Rais John Magufuli anaweza kutamka kwamba mgogoro wa Zanzibar ni wa Zanzibar na kwa kuwa kikatiba yeye mwenyewe (kama rais wa Tanzania) hawezi kuingilia, hivyo hauwezi pia kuingiliwa na wakuu wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki?

Mapema miaka ya 2000 Katibu Mkuu wa EAC (wakati huo) Amanya Mushegga wa kutoka Uganda, aliwahi kusema kwamba iwapo Burundi na Rwanda wangeruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ile ya zamani na kwamba Jumuiya hiyo isingeachiwa kuvunjika mwaka 1977, matatizo ya kikabila yasingejitokeza katika nchi hizi mbili na kwamba hata mauaji ya kimbari ya Rwanda yasingetokea mwaka 1994.

Lakini kauli hiyo ilikuwa ni ya kufikirika tu (hypothetical) kwani mwaka 2007, Rwanda na Burundi zilijiunga na Jumuiya hii ya sasa lakini bado haijasaidia kutuliza migongano ya kikabila ndani ya nchi hizo, hasa Burundi.

Na yote haya yanatokea pamoja na uanzishwaji wa ule mkataba wa pamoja (Protocol) unaosisitiza utawala bora na unaozitaka nchi wanachama kudumisha misingi ya demokrasia na kuheshimu haki za binadamu.