Home kitaifa MASOKO YA MIPAKANI FURSA KWA JUMUIYA

MASOKO YA MIPAKANI FURSA KWA JUMUIYA

343
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

MASOKO ya mipakani katika Mkoa wa Kigoma yamekuwepo na yanaendelea kustawi kutokana na mwingiliano wa kibiashara baina ya wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya karibu na mipaka.

Miongoni mwa masoko hayo yanayoendeshwa rasmi ni pamoja na soko la Mnanila lililopo Manyovu, Wilaya ya Buhigwe, Muhange Wilaya ya Kakonko na Mabamba Wilaya ya Kibondo.

Masoko yote haya yapo kwenye mpaka wa Tanzania na Burundi nchi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwa sasa wananchi wanaoishi mpakani wamefikia hatua ya kuweka siku maalumu ya soko kwa kila upande.

“Siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa tunauza bidhaa zetu katika soko la Mabanda lililoko Wilaya ya Makamba nchini Burundi wakati siku zilizobaki katika wiki, soko linafanyika hapa Manyovu,” anasema Simon Seberero kutoka Burundi.

Wananchi walio wengi wanafanya biashara ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku, hivyo bidhaa nyingi zinazopatikana katika masoko ni zile zinazozalishwa ndani ya nchi yakiwamo mazao ya chakula na bidhaa za matumizi mengine ya nyumbani.

Watanzania huwa wanapeleka zaidi ndizi, nyanya na matunda yakiwamo mananasi wakati wale wa Burundi biashara yao kubwa ni ndizi, kuni na mkaa.

Seberero anasema wananchi wengi kutoka Burundi huwa wanatumia njia za panya kuvuka mpaka kuleta biashara zao Tanzania kama inavyosemekana kufanyika pia kwa wenzao kutoka Tanzania wakati wa kuingia Burundi.

“Mara nyingi huwa tunavuka kwenye saa 11 alfajiri kwa kutumia njia zetu wenyewe ili kuleta biashara zetu za mkaa hapa Manyovu,” anasema Seberero.

Kwa mujibu wa Jesca John, mkazi wa Manyovu mkaa unapatikana kwa shida sana katika mazingira ya Manyovu na gunia linauzwa shilingi 8,000 hadi 10,000 kutegemeana na bei ya soko.

“Lakini kuni ambazo huuzwa kati ya 2,000 hadi 3,000 zipo; watu wana misitu yao; kwa hiyo wanaleta tu kuni, ila uhitaji wao ni mdogo,” anasema Jesca.

Akizungumzia zaidi kuhusu biashara yake ya mkaa Seberero ambaye anatoka vijiji vya mpakani mwa Burundi na Tanzania anasema inamsaidia kupata pesa kidogo ya kuweza kuendesha maisha kuliko kukaa bila ya kufanya kazi yeyote.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Manyovu, Isaya Mwamakungi, alisema suala la kupita njia za panya ni woga wao tu na kutojua fursa zilizopo za biashara kwenye EAC.

“Kwa mfano, hapa Manyovu tumejitolea kuwapa mafunzo akina mama namna ya kuendesha biashara kihalali ili waweze kufaidi fursa za  biashara kwenye EAC. Lakini, leo wakija, kesho huwaoni tena, sasa inakuwa shida,” anasema Mwamakungi.

Taasisi ya Foundation for Civil Society  ilichogundua ni kwamba mbele ya ofisi za Serikali ikiwa ni pamoja na za TRA kuna wafanyabiashara wadogo wanafanya biashara ya wazi ya kubadilisha fedha. Wanabadilisha shilingi ya Tanzania na faranga ya Burundi kwa kiwango kinachokubalika.

Maofisa wa Serikali na wadau wengine walipohojiwa walisema njia nyingi za panya katika Mkoa wa Kigoma zinatoa changamoto kubwa kwa utekelezaji wa Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Soko la Pamoja na Umoja wa Forodha.

Uanzishwaji wa Itifaki ya EAC ya Soko la Pamoja ambayo ni ya pili kwenye ushirikiano wa kikanda ilianza kutumika tarehe 1 Julai, 2010 inatoa “Uhuru kwenye maeneo manne” usafirishaji huru wa bidhaa; kazi; huduma; na mitaji miongoni mwa nchi wanachama wa EAC.

Soko la Pamoja linawakilisha hatua ya pili ya mchakato wa ushirikiano wa kikanda kufuatia Umoja wa Forodha ambao ulianza kutumika kikamilifu  mwezi Januari, 2010.

Soko la Pamoja ni hatua muhimu kuelekea kupata mafanikio ya kufikia hatua nyingine katika mchakato wa ushirikiano, yaani, Umoja wa Fedha (Monetary Union) na Shirikisho la kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Madhumuni ya kuwa na Soko la Pamoja ni kuharakisha nyanja za kiuchumi na kijamii kwa faida ya nchi wanachama na raia wake kama inavyofanyika katika mpaka wa Manyovu.

Hata hivyo, imebainika kwamba watu wengi ikiwamo Jumuiya ya wafanyabiashara hawana uelewa wowote kuhusu Itifaki za Jumuiya ya Afrika Mashari za Soko la Pamoja na Umoja wa Forodha.

Wakazi wa Kigoma na jumuiya ya biashara walipohojiwa  walisema hawajui cho chote kuhusu fursa za biashara zinazopatikana kwenye EAC.

Esther Jacob, Mkulima wa Manyovu anasema watu wengi katika mkoa wa Kigoma hawana uelewa kuhusu fursa za biashara zilizopo kwenye EAC  kutokana na ukosefu wa elimu kuhusu suala hilo.

Kauli hiyo imeungwa mkono na mkulima mwingine Scolla Julius ambaye alisema kama wangekuwa na uelewa kuhusu fursa za biashara zilizopo kwenye EAC wangeweza kuvuka wenyewe mpaka na kwenda kuuza bidhaa zao Burundi badala ya kuwauzia wafanyabiashara.

“Kitu muhimu cha kufanya ni kwa Serikali kutoa elimu kuhusu fursa za biashara zilizopo kwenye EAC kwa wananchi, hususani sisi tunaoishi mipakani, angalau itasaidia,” anasema Scola.

Pamoja na changamoto hizo upo uwezekano wa kutolewa kwa elimu ya aina hiyo ambayo itawapa mwanga wananchi kuhusu fursa za biashara kwenye EAC na hivyo kuweza kuongeza ufanisi katika kusimamia masoko ya mipakani.

Masoko hayo ni kama fursa wakati huu wa kuelekea kwenye kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwenye nchi za EAC na kwa hiyo, ni muda mwafaka, kwa nchi wanachama kuchukua hatua za makusudi za kuimarisha masoko ya mpakani kuanzia kwa kufanya kampeni kwa kutoa elimu  katika masuala ya msingi juu ya somo husika na hasa jinsi gani masoko ya mpakani yatakuwa na manufaa chini ya Itifaki ya EAC ya Soko la Pamoja.