Home Afrika Mashariki TANZANIA HAIKUJIANDAA KUINGIA EAC

TANZANIA HAIKUJIANDAA KUINGIA EAC

489
0
SHARE

TUNU NASSOR NA MANENO SELANYIKA

JUMUIYA ya Afrika Mashariki ilianzishwa ikiwa na malengo mengi, likiwamo la kujikomboa kiuchumi kwa nchi wanachama.

 Malengo hayo yalikuwa ni kupunguza gharama za kufanya biashara kwa kuondoa milolongo na gharama za utendaji na usimamizi.

Pia kuongeza vivutio vya uwekezaji wa nje na ndani kati ya nchi wanachama pamoja na kujenga mfumo wa kuzuia biashara ya magendo katika jumuiya hiyo, kujenga mfumo madhubuti wa kusimamia mapato na kuongeza mzunguko wa biashara kutokana na kupungua kwa michakato katika utendaji.

Aidha, kuwezesha soko la pamoja kwa kujenga soko moja la ndani na kuondoa vikwazo visivyo vya kodi ili kuwezesha mzunguko huru wa bidhaa za ndani ya jumuiya.

Katika kuyafikia malengo hayo, ilianzisha himaya moja ya Forodha (SCT) ikiwa na misingi mitatu ambayo ni mzunguko huru wa bidhaa, mifumo ya usimamizi wa mapato na mfumo wa kisheria na kitaasisi miongoni mwa jumuiya.

 Katika utekelezaji wa sheria hiyo, bidhaa zinazozalishwa ndani ya jumuiya hazitozwi ushuru wa forodha zinapohamishwa kwenda nchi mwanachama ilhali zimekidhi vigezo vya kikanuni za usajili za jumuiya.

Bidhaa hizo zinaweza kutozwa kodi za ndani, kama zipo, zinazotozwa katika biashara ya kimataifa pindi zinapoingia ndani ya mipaka ya nchi husika.

Kwa Tanzania, matarajio ya manufaa yatokanayo na kuwapo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki  yamefifia kutokana na kudaiwa kuwa na maandalizi hafifu.

Rai imezungumza na wadau wa uchumi ambao wanazungumzia kwa undani utekelezaji wa malengo hayo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Johnson Minja, anazungumzia manufaa tunayoyapata kama nchi katika Jumuiya hiyo.

Anasema bado Tanzania haijapata faida ya moja kwa moja kutokana na maandalizi duni yaliyofanyika.

“Hatukuwa na maandalizi ya kutosha wakati tunaingia katika jumuiya hii kwa kuwa wenzetu wakenya walikuwa tayari wamewekeza katika viwanda na hivyo sisi kumejikuta tumegeuzwa kuwa soko lao,” anasema Minja.

Anasema sheria ya uingizaji bidhaa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutumia viwango sawa vya forodha imekuwa ikitumika nchini pekee huko Kenya wanatumia bei zao.

“Uchunguzi tulioufanya na baadhi ya viongozi wa Serikali ambao tulienda nao mpaka Kenya tukakuta wenzetu hawautumii mfumo huo bali wanatumia bei elekezi ambayo inawapa nafuu wafanyabiashara wao na kusababisha bei za bidhaa za nje nchini Kenya kushuka,” anasema Minja.

 Anasema bidhaa zilizoingizwa toka nje ya Umoja wa Forodha na kuruhusiwa kwa matumizi ya ndani ya nchi ziko huru kuzunguka ndani ya jumuiya, hivyo kusababisha Wakenya kuuza bidhaa zinatoka nje nchini kwa bei rahisi kutokana na wao kutotumia sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki.

Minja anaona ni vyema Serikali ikazungumza na wadau wa uchumi na kujipanga upya namna ya kutumia fursa zilizopo katika Jumuiya hiyo.

“Wenzetu Wakenya wanakaa na Serikali yao na kujipanga namna ya kutumia fursa za jumuiya hii lakini sisi tumekuwa kama watoto yatima tusiokuwa na baba wala mama,” anasema Minja.

Naye Mhadhiri kutoka Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi, anasema kuna fursa nyingi za kiuchumi  katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Suala linalotushinda Watanzania ni kwamba tumeingia katika Jumuiya hii pasipo kujiandaa namna ya kutumia fursa hizo kama soko la pamoja, ajira, na uhuru wa uwekezaji.

“Tujiulize kwanini kampuni nyingi za Kenya zipo nchini lakini ya Watanzania hayapo huko kwao na ndipo utagundua kuwa hatujajiandaa kuingia katika Jumuiya hii,” anasema Dk.Ngowi.

Anaongeza kwamba iwapo sheria zitafuatwa vizuri, Serikali itaongeza kipato kutokana na malipo ya kodi na tozo mbalimbali zitokanazo na viwanda na biashara.

“Bado tuna nafasi kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa nchini kwa kuwa upatikanaji wa masoko kutokana na soko la pamoja la bidhaa baina ya nchi hizo upo,” anasema Dk.Ngowi.

Aidha, anasema kwa kuwa lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hii ni kulinda viwanda na kushawishi uwekezaji wa nje na ndani, ni bora kila nchi ifanye juhudi za kiushindani katika masuala ya uwekezaji na mitaji.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Tony Swai, anasema ni vema wafanyabiashara wakakaa na Serikali kuona namna ya kutatua changamoto iliyopo.

“Kamishna wa forodha hajakataa kukaa na wafanyabiashara ili kuweka bei elekezi, bali wafuate taratibu zilizowekwa katika kufikisha ujumbe,” anasema Swai.

Anaongeza kuwa Serikali haiwezi kukurupuka katika utendaji wake wa kazi, hivyo madai hayo huenda yakawa yanafanyiwa kazi.

“Kama kuna uhitaji wa kutumia bei elekezi kama wenzetu, ina maana inabidi suala hili lifikishwe bungeni ndipo lipatiwe ufumbuzi ninaamini kuwa Serikali inaendelelea na taratibu zake,” anasema Swai.