Home Afrika Mashariki UELEWA WAKWAMISHA VIJANA KUJITANUA AFRIKA MASHARIKI

UELEWA WAKWAMISHA VIJANA KUJITANUA AFRIKA MASHARIKI

284
0
SHARE

Na Peter Kasera

MWANZA ni moja ya mikoa inayokuwa kiuchumi kwa kasi, sababu kubwa ikiwa ni jiografia yake.

Ukiwa ndani ya Mwanza ni rahisi kufika  Entebbe, Uganda, itakuchukua dakika 30 tu kwa usafiri wa ndege, huku ikikuchukua dakika 45 kutua Kigali, Rwanda na huenda ukalazimika kutumia dakika 60 kufika Bujumbura, Burundi.

Mbali ya hilo, lakini pia Jiji la Mwanza lina faida kubwa ya kuiunganisha Tanzania na nchi za Maziwa Makuu.

Wafanyabiashara kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hufika jijini humo kufanya biashara.

Biashara kubwa inayofanyika hapo ni ununuzi wa samaki wanaotoka Ziwa Victoria. Ujio wa wafanyabiashara hao kutoka nchi jirani unachangia kukuza pato la mtu mmoja mmoja na mji wa Mwanza kwa ujumla, kwani wafanyabiashara hao mbali ya kufuata samaki, lakini pia wao huja na bidhaa kutoka kwao, ambazo wanalazimika kuziuza jijini hapo.

Hali hiyo huibua ushindani wa kibishara, hatua inayowatia unyonge wafanyabiashara wadogo ambao hawana uelewa wa kutosha wa kupambana sokoni.

Awali wafanyabiashara wa ndani waliweza kulindwa na sheria mbalimbali, kakini sasa hali ni tofauti, ujio wa soko la pamoja la Afrika Mashariki umefungua milango ya kuwapo kwa soko huru kwa wafanyabiashara wote.

Bidhaa zinazozalishwa Kenya, Uganda, Rwanda na hata Burundi zinaweza kuingia nchini bila vizuizi. Vile vile zile zinazozalishwa Tanzania zinaweza kwenda kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashriki bila vikwazo.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa vijana wengi wa Tanzania wana hofu juu ya ushindani mkubwa wa ajira na bidhaa zinazozalishwa ndani ya jumuiya. Pamoja na hilo, pia hawana elimu ya kutosha kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na mbaya zaidi wengi wamekuwa wakisubiri kuletewa taarifa na fursa zilizopo katika Jumuiya hiyo badala ya wao kutafuta taarifa na fursa zaidi ya walizo nazo.

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Samwel Chacha anaeleza kuwa: “vijana wengi wamekuwa wakitazama Jumuiya kwa jicho  la kawaida, hali inayowafanya  kushindwa kupambana na kutumia fursa zilizopo ndani ya Jumuiya.

“Vijana wa nchi jirani hutafuta taarifa na fursa ndio maana tunaona wanafanikiwa na kufaidika ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Vijana wa Kitanzania wanakosa elimu kuhusu ujasiliamali na pale inapotokea kupatikana namna ya kuwawezesha, elimu itolewayo inakuwa ni ya kiwango cha chini, ukilinganisha na aina ya soko lililopo na wanalotakiwa kuingia kushindana.”

Chacha anasema sifa kubwa ya mjasiriamali ni kuona fursa, wakati wengine wanaona matatizo.

“Fursa yoyote lazima iwe na changamoto zake, changamoto mara zote hazikimbiwi bali inatakiwa kupambana nazo ili mwishowe upate matokea mazuri.

“Tanzania imejaliwa kuwa na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo na nchi yetu inao uwezo wa kuwa mzalishaji na mlishaji wa nchi zote zilizomo katika Jumuiya hii. Ukifika katika wilaya ya Rorya ambayo iko mpakani na Kenya, utashangaa kuona kuwa bidhaa nyingi zinatoka Kenya. Hii ni pamoja na chakula.

“Hali hii inatokana na vijana wa upande wa Tanzania kubakia kuwa watazamaji na kuona urahisi wa kuchukua bidhaa kutoka Kenya kwa kuwa ni karibu pasipo kutambua kuwa hata huko Kenya huzalishwa na wazalishaji wakubwa ni vijana kama wao. Inaonesha kabisa kuwa mfumo wa maisha ya Kenya umewafanya vijana wa nchi hiyo kutambua kero zinazowakabili na kisha kuzigeuza kuwa fursa.”

Chacha anasema kwa upande wa vijana  walioko upande huu wa Tanzania bado ni wazito na wagumu kubadilika hali inayowafanya kushindwa kutanua kazi zao ili ziweze kuvuka upande wa pili wa mpaka na kupata soko lililopo huko.

“Vijana hawa waliopo Rorya kimsingi wanawakilisha tabia ya vijana wengi wa Tanzania. Namna maisha yalivyo hapa kwetu yamewafanya vijana kutokuwa na morari na kujijengea tabia ya uthubutu wa kufanya mambo kwa ajili ya kujielendeleza kiuchumi.”

Ofisa Tawala Wilaya ya Rorya, Moses Kyawa, anasema vijana wanatakiwa kutafuta taarifa mbalimbali zinazohusu Jumuiya ili kuweza kupanua elimu waliyonayo kuhusu ushirikiano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na fursa zilizopo na jinsi ya kuzikabili.”

Pia, anawaasa vijana kujiunga katika vikundi mbalimbali vya ujasiriamali, ili kwa pamoja waweze kushindana kwa ukamilifu na wafanyabiashara wa nchi zingine. Umakini, uzalishaji bora wa bidhaa ni muhimu katika kuhimili ushindano wa namna huo.

Kwa ujumla dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kukuza kipato, kuinua hali ya maisha ya wananchi wa nchi wanachama wa Afrika Mashariki, kukuza uchumi na kujenga ushindani wa kanda katika ngazi ya kimataifa, katika kutekeleza azma hiyo, nchi wanachama zinatakiwa kunufaika kutokana na mahusiano mazuri ya kibiashara. Ni katika misingi hiyo ni wajibu wa kila kijana wa Tanzania kutambua fursa na wajibu alionao katika jumuiya ili kuinua uchumi wake binafsi na wa Taifa kwa ujumla na kuacha kuwa na hofu kabisa.