Home Afrika Mashariki VIZUIZI EAC VYAPUNGUZWA

VIZUIZI EAC VYAPUNGUZWA

279
0
SHARE

Na Grace Shitundu

KATIKA kuhakikisha Watanzania wanafaidi fursa zilizomo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Serikali imepunguza vizuizi 47 vya ukaguzi ili kurahisisha mazingira ya biashara kwa nchi wananchama.

Hatua hiyo imekuja baada ya wafanyabiashara mbalimbali kulalamikia wingi wa vizuizi hivyo hali iliyokuwa ikisababisha baadhi yao kutumia njia za ‘panya’ kusafirisha bidhaa kwenda nchi wanachama.

Akizungumza na RAI katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bernard Haule, alisema vizuizi hivyo vimepunguzwa kutoa 50 hadi kufikia vitatu pekee.

Alisema awali wafanyabiashara walikuwa wakilalamika juu ya kuwapo kwa vikwazo visivyo vya kiforodha vikiwamo vituo vya ukaguzi visivyopungua 50.

“Tulikuwa na vizuizi 50  hali iliyokuwa ikiwafanya wafanyabiashara kuona ni kero hivyo tulipunguza hadi 35 halafu 10 na sasa vitatu.

“Vizuizi hivi vitatu ambavyo ni Vigwaza, Manyoni na Nyakanozi vitakuwa vituo vya pamoja vya ukaguzi (One Stop Posts – OSBP) ambazo mfanyabiashara atakaguliwa kila kitu ambapo hiyo ni kwa upande wa Tanzania,” alisema Haule.

Haule alisema hatua hiyo imekuja baada ya wanachama wa EAC kila mmoja kuainisha vikwazo visivyo vya kiforodha ambavyo vilikuwa ni changamoto  kwa wafanyabiashara na kuwekeana ratiba ya kuviondoa..

Akizungumzia suala la kodi Haule aliwatoa hofu watanzania kwa kuwa kuna Cheti cha Uasili kinachowapa upendeleo wananchi wa nchi wanachama.

“Kwa sasa hakuna  sababu ya wafanyabiashara kupitia njia za panya kwa kuwa cheti cha uasilia kinawapa nafasi ya kuvusha bidhaa bila ya kulipa kodi,” alisema

Akitoa ufafanuzi juu ya wafanyabiashara wanaohusika na  cheti cha uasilia, haule alisema ni wale wanaotaka kuvusha bidhaa ambazo thamani yake haivuki Dola 2,000.

Alisema kila nchi mwanachama imeunda kamati ya kitaifa ya kushughulikia vikwazo hivi sambamba na Kamati  ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Katika kukabiliana na vikwazo hivi nchi Wanachama pia zimeamua kuanzisha vituo vya pamoja vya ukaguzi mipakani.

“Tayari vituo vya Holili, Sirari na Mutukula vimekamilika

Huku vile vya Namanga, Taveta, Rusumo, Horohoro na Kabanga vikiendelea na hatua za ujenzi, alisema Haule.

Alisema uanzishwaji wa vituo hivi utasaidia kurahisisha taratibu za ukaguzi na huduma kwa wafanyabiashara.