Home Makala MWALIMU KESSY- VITA DAWA ZA KULEVYA SI YA MKOA NI KIMATAIFA

MWALIMU KESSY- VITA DAWA ZA KULEVYA SI YA MKOA NI KIMATAIFA

272
0
SHARE
Dk. Nderakindo Kessy

NA GABRIEL MUSHI


VITA dhidi ya dawa za kulevya imezidi kupamba moto, huku kukiwa na mabadiliko kadha wa kadha ndani ya Serikali katika kushughulikia tatizo hilo.

Licha ya awali watuhumiwa wa dawa hizo kutangazwa hadharani na kwenye vyombo vya habari na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, hali sasa imekuwa tofauti kwa Kamishna mpya wa mamlaka ya kuzuia dawa hizo, Rogers Sianga, ambaye sasa ni mwendo wa kimyakimya.

Pamoja na mambo mengine, wapo viongozi na wanazuoni mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa ushauri kwa Serikali namna ya kushughulikia tatizo hilo, mbali na hao, wiki hii Dk. Nderakindo Kessy, ambaye ni Mbunge wa Afrika Mashariki (EALA), naye ametoa neno kwa serikali.

Dk. Nderakindo, ambaye hupenda kuitwa zaidi ‘Mwalimu’, amezungumza na RAI na kubainisha mambo mbalimbali, ikiwamo mipango yake ya baadaye kisiasa, hasa ikizingatiwa yupo ukingoni kufikia kikomo cha nafasi hiyo ya ubunge wa EALA.

RAI: Kumekuwapo na mapambano dhidi ya watumiaji na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, unazungumziaje mwenendo wa Serikali katika kudhibiti tatizo hilo?

MWALIMU KESSY: Tatizo lolote ambalo linamuathiri binadamu, njia yake kuu ni kuzuia tatizo hilo, si kutibu, kwa hiyo hapa namaanisha kuwa kuwafuata watumiaji wa dawa na kuwapeleka mahakamani haitazuia tatizo lolote katika kudhibiti dawa hizo. Inabidi kuiga mfano wa EAC ilivyofanikiwa kuzuia malaria baada ya kuja na mbinu ya kuzuia ugonjwa huo na si kuutibu. Tunaona kuwa sasa idadi ya wagonjwa wa malaria imepungua. Vivyo hivyo kwa suala la kuzuia dawa za kulevya… Huwezi kulishughulikia katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee na kuona kuwa umelitokomeza, kwa sababu hili ni tatizo la dunia, kwa hiyo ili Serikali ifanikiwe kuzuia biashara hiyo haramu, ni vema kuhakikisha vyombo vya dola vinashirikiana na vile vya mikoa mingine na pia vya kimataifa ili kupambana nalo.

RAI: Umedumu kwenye nafasi ya ubunge wa EALA tangu 2012,  je, ni vitu gani ulivyojifunza baada ya kuhudumia nafasi hiyo kwa muda wote huo?

MWALIMU KESSY: Yapo mengi niliyojifunza, ila kubwa ni kutenga muda wa kutosha kujisomea makabrasha ambayo yanatolewa  ndani ya Bunge. Unaweza usichangie hoja kwa muda yanapotolewa, lakini ukishayapitia ndipo ukapata wazo zuri la kuchangia. Ili uweze kuwa mzoefu inabidi zile ripoti zinazotolewa katika kamati mbalimbali lazima uwe unazipitia kwa muda wako binafsi ili hata mwaka unaofuata uwe na uzoefu wa kutosha kuchangia.

Kwa hiyo, lazima uwe na nidhamu ya kusoma kama mwanafunzi uingiapo katika Bunge hili, ni kazi nzito kweli kwa sababu makabrasha ni mengi. Na katika nafasi ya ubunge hakuna bosi anayekusimamia kukulazimisha kufanya jambo fulani. Ni wewe mwenyewe kuanza kujitoa na kujua jukumu lako ni nini.

RAI: Kumekuwa na msukumo kutoka kwa baadhi ya wabunge kuwa lugha ya Kiswahili itumike kama lugha rasmi kwenye jumuiya na hata ndani ya Bunge, mchakato huu umefikia wapi?

MWALIMU KESSY:  Nadhani haikueleweka vizuri katika vyombo vya habari kulipoibuka suala hili, kulikuwa na hoja kuwa Kiswahili kiwe lugha rasmi kwa sababu tunajua idadi kubwa ya wanajumuiya (EAC) hawazungumzi Kiingereza, sehemu kama Uganda wanazungumza zaidi Kiingereza lakini si asilimia kubwa ya Waganda au hata Wakenya hawazungumzi Kiingereza. Tukiangalia Kiswahili chimbuko lake ni lugha zetu sisi wote wanajumuiya, hivyo hii ni lugha yetu sisi Waafrika, ikianza kutumika itakuwa ni rahisi kwa jumuiya kutoa taarifa.

Kwa maana hiyo ule mchakato ulikuwa ni hoja iliyotolewa na haijafikia kwenye muswada na ikishapitishwa na Bunge na kusainiwa na wakuu wa nchi kuwa sheria ndipo itaanza kutumika, kwa sababu kinachotakiwa ni kutumika kama lugha rasmi ya jumuiya si Bunge pekee.

RAI: Kumekuwapo na miswada mbalimbali iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni, ukiwapo wa kuzuia ukeketaji kwa nchi wanachama, je, miswada hii inatumika vipi na kuwiana na sheria za nchi hizi?

MWALIMU KESSY: Sheria zinazopitishwa na Bunge ni lazima zioane na sheria za nchi wanachama. Kwa mfano, Tanzania kuna sheria ya walemavu, kwa hiyo sheria itakayopitishwa na  Jumuiya haitaleta mabadiliko katika sheria ya kuzuia ukeketaji Tanzania… kwa sababu tayari sheria ya Tanzania ilishajumuisha sheria hizi. Sasa sijui nchi nyingine kama tayari zimeshapitisha sheria za aina hiyo au la.

RAI: Kumekuwapo na utaratibu wa kufanya vikao vya Bunge kwa mzunguko katika kila nchi wanachama, Je, utaratibu huu ulikuwa na lengo gani na kuna haja ya kuendelea?

MWALIMU KESSY: Ukitazama katika mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya EAC, kuna nafasi za mzunguko kama Mwenyekiti wa jumuiya, makamu na hata Katibu, sasa suala la vikao lilitolewa na Bunge la pili. Lengo ni kuwajulisha wananchi kuwa Bunge lipo, ila kwa sasa Bunge hili la tatu chini ya Spika mpya, kamisheni imekuja na programu ambayo wabunge wanakwenda kwenye nchi yao husika kuhamasisha, hata New Habari tulifika kuhamasisha, madhumuni ya kuzunguka katika vikao ilikuwa kuleta awareness, sasa kumetokea ugumu wa bajeti nafikiri kusiwe na umuhimu tena wa kuzunguka kwa sababu lengo la uhamasishaji tayari linafanywa kwa njia nyingine.

RAI: Kumekuwapo na kilio cha uhaba wa fedha ndani ya Jumuiya kwa sababu asilimia 60 ya bajeti ya jumuiya hutegemea nchi wahisani, hususan Ujerumani na asilimia 40 ndio zinatoka kwa nchi wanachama, hali ikoje kutokana na ukata huu?

MWALIMU KESSY: Tukijiuliza sisi wenyewe je, Serikali yetu ina fedha ya kutosha? Jibu ni hapana… nadhani hata Bunge la Jamhuri bajeti yao haitolewi kwa muda muafaka, kwa hiyo kiujumla hali ya kiuchumi ni changamoto nyingine kwa sababu vianzio vyetu ni vilevile.

Pia tayari kuna teknolojia imeweza kuanika kuwa wapi kuna ufujaji wa fedha na pale ambapo haikutumika ilivyopaswa wale wadhamini wanaanza kuweka alama ya kuuliza ili kutaka kupata taarifa sahihi. Kwa mfano, nchi wachangiaji zimekuwa zikisuasua kutokana na mzunguko mbaya wa fedha.

Wamekuwa wakitoa fedha kwa awamu, kwenye mkataba waliweka kwamba ifikapo Desemba 31 kila nchi iwe imeshapeleka asilimia 100 ya fedha zake ili ziweze ku-adjust zile programu. Lakini kuna nchi nyingine mpaka Januari mwaka huu au Desemba hazijatoa chochote, yaani ni ziro kabisa.

Kuna baadhi ya nchi zimetoa asilimia 10 au 18 pekee na kuendelea. Kwa hiyo inakuwa kweli inaleta usumbufu katika utekelezaji wa majukumu kwenye kamati na Bunge kwa ujumla, ndiyo maana Katibu wa jumuiya alikuja kuonana na Rais Magufuli hivi karibuni na alitueleza jambo alilozungumza naye ni kuhusu uchangiaji wa fedha hizo.

Kwa upande wa wabunge, ni suala la ucheleweshwaji wa mishahara labda kwa mwezi mmoja, ila hakuna tatizo kubwa. Vilevile kwa upande wa posho nalo ni jambo muhimu kwa lazima, wabunge wasafiri walipie hoteli na mambo mengine.

RAI: Mojawapo ya mambo yanayoshughulikiwa na EALA ni kero za EAC, ni kwa kiasi gani mmefanikiwa kutatua kero za jumuiya hii?

MWALIMU KESSY:  Yapo mambo mengi, mojawapo ni kuweka mazingira rahisi kwa wageni wanaokuja labda kutalii, pia raia wanaokaa mipakani kuandaliwa mazingira rafiki ya kurahisisha biashara. Pia tumewasaidia wawekezaji wenye makampuni makubwa, angalau kuna sheria zinawawezesha kufanya biashara kwa kuchagua eneo moja la biashara kwa sababu ni kama jumuiya moja.

Hili suala la mtangamano litatuletea faida sana, kwa mfano suala la makataba wa EPA, ndiyo kuna mapungufu yake na faida zake, ila tukiweka vitu vizuri pengine itatusaidia.

Nadhani kuna mambo pia ya amani na usalama katika miaka yetu ambayo ni suala la ugaidi, kwa sababu kuna kitengo katika jumuiya kinachoshughulikia amani na usalama katika jumuiya.

RAI: Unazungumziaje mwenendo wa chama chako NCCR- Mageuzi, kwa sababu kimeonekana kudhoofika ndani ya Ukawa, unadhani ni muda mwafaka sasa kuingia ndani ya Chadema na kuwa chama kimoja?

MWALIMU KESSY: Watu walisema NCCR ni ndogo kwenye Bunge la Katiba, lakini hatimaye ikafanya vizuri, pia kwenye Bunge la sasa yupo Mbunge mmoja tu lakini anafanya vizuri vilevile. Nisema kuwa mchango wa NCCR- Mageuzi ni mkubwa kwa sababu NCCR- Mageuzi ni mwenyekiti mwenza na katibu mkuu ndani ya Ukawa. Tunaona kuwa chama hiki kimeshika nafasi zote hizo, utasemaje kuwa kimedhoofika ndani ya Ukawa? Labda tuseme uwakilishi bungeni ambao tulikwamishwa kwa sababu uchaguzi mkuu si wa huru na haki, itikadi yetu ni ya utu, tunaamini katika utu, tunaamini chaguzi zetu lazima zifuate mienendo ya kiutu.

RAI: Unakaribia kufikia kikomo cha muda wa ubunge wako ndani ya EALA, ni yapi matarajio yako kisiasa?

MWALIMU KESSY: Hakuna raia ambaye anakwenda kusomea kuwa mbunge, siri ya kuwa mbunge unaipata ndani ya ubunge. Kwa mantiki hiyo, Taifa limeshaniamini na kunipa ubunge kwa miaka mitano, nimepata uzoefu wa muda wa miaka mitano. Uzoefu huu ni rasilimali kwa Taifa langu kwa sababu liliwekeza kwangu.

Sasa ninao uwezo wa kurudi kuutumia ule uzoefu ipasavyo, hivyo basi nategemea kurudi tena, nipo katika mchakato ndani ya chama change, nitachukua fomu na uteuzi utafuata na baadaye tutakwenda kujinadi kule bungeni Dodoma, nadhani itakuwa Aprili, mwaka huu. Ninaamini nimefanya kazi nzuri na nitakuwa mmoja wa watu watakaorudi kule bungeni EALA.

RAI: Katika siku za karibuni kumekuwa na taarifa za kukanganya kuhusu uamuzi uliotolewa na mahakama dhidi ya Spika aliyeng’olewa madarakani, Magreth Zziwa, ni upi ukweli kuhusu mgogoro huu?

MWALIMU KESSY: Ukisoma ile hukumu kwa undani nikiwa kama mwanahisabati, ni kwamba ukianza na mwanzo mbovu, utaishia na mwisho mbovu.

Katika ule mchakato wa kumwondoa spika, spika mwenyewe alizuia ule mchakato wa kumng’oa, yaani Zziwa aliuzuia ule mchakato kwa kutumia ofisi yake vibaya kwa kutaka kuwa jaji kwenye hukumu yake mwenyewe, sasa ukiisoma ile hukumu utaelewa kuwa wabunge tulifuata sheria zilizopo bila ya yeye kuwapo, kwa hiyo mchakato huo umeonesha kuwa spika alianza mwenyewe kutumia vibaya madaraka yake. Ndiyo maana akawekwa spika wa muda ili maamuzi yachukue nafasi.

Kiujumla niseme kuwa hukumu ile haimrudishi spika Zziwa madarakani, ukisoma jinsi mchakato ulivyo kiujumla ulikuwa dhaifu, na udhaifu wake ulianzishwa na spika yeye mwenyewe.  Ila mahakama imesema waziwazi hata katika madhaifu. Kwa sababu spika alichaguliwa kwa kupigiwa kura ya siri na kuondolewa ameondolewa kwa kura ya siri vilevile.

RAI: Katika uongozi wa serikali ya awamu ya nne, kulitokea jumuiya ndogo iliyojumuisha nchi za Kenya, Rwanda na Uganda na kuzua minong’ono ya uwezekano wa kuvunja jumuiya kwa mara nyingine, je, hali hiyo iliwaletea changamoto gani kama wawakilishi?

MWALIMU KESSY:  Kuna kitu kinaitwa valuable geometry, kwamba inategemea na mazingira ya kidemokrasia ni kwa namna gani watu wa ukanda mmoja huweza kushirikiana, hata Umoja wa Ulaya (EU) kuna baadhi ya nchi zinaweza kuamua kushirikiana badala ya kushirikisha nchi zote za jumuya.

Kwa mfano, Burundi haihusiani sana na Ziwa Victoria, iwapo kutakuwa na mkakati namna ya kutumia ziwa hilo si lazima Burundi ihusishwe, vilevile kwenye EAC ndogo kuna mambo waliamua kukubaliana kutokana na ukanda waliopo, hususan kwenye usafiri wa reli, kasoro iliyojitokeza ni kwamba, katibu mkuu wa jumuiya alikuwa anahudhuria vikao vya marais hao watatu.  Ndiyo maana ikazusha hofu ya kutengeneza EAC nyingine ndogo.