Home Makala UPITISHAJI MIHADARATI VIWANJA VYA NDEGE BADO NI CHANGAMOTO

UPITISHAJI MIHADARATI VIWANJA VYA NDEGE BADO NI CHANGAMOTO

271
0
SHARE
Rais John Magufuli akifanya ziara ya kushtukiza sehemu zilipo mashine za ukaguzi mizigo ya wasafiri uwanja wa ndege ea JNIA Dar es Salaam mwaka jana.

NA HILAL K SUED


Mwaka jana Rais John Magufuli katika pitapita zake kwenyw Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, alifanya ziara ya ghafla sehemu ya abiria wanaowasili na kuchekiwa mizigo yao na akaona kitu cha kusitisha, kwamba mashine za kukagua mizigo ya wasafiri zilikuwa hazifanyi kazi.

Lakini labda niseme tu kwamba hapo zamani mashine za kielektroniki (scanner) za kukagua mizigo ya wasafiri wanaotoka na kuinguia hazikuwapo kabisa uwanjani hapo na hivyo mizigo yote ilikuwa inakaguliwa kwa mkono na macho (physical examination), baada ya wasafiri kuamriwa kufungua mizigo yao. Mashine zimeanza kutumika takribani kwa muongo mmoja na nusu.

Lakini dhamira ya uwekaji mashine hizo bila shaka ilikuwa ni kutokana na kutoridhishwa na ukaguzi wa macho ya binadamu na pia kuokoa muda unaotumiwa katika ukaguzi wa mikono.

Miaka miwili hivi iliyopita wakati wa kikao cha wakuu wa mikoa iliyopo ukanda wa Bahari ya Hindi Tanzania Bara na Zanzibar, waliokutana Tanga kuweka mikakati ya kukabiliana na matumizi ya bandari bubu, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Shaaban Mwijaka, alitangaza kwamba Serikali ilikuwa mbioni kuagiza kutoka China na Marekani mashine za ukaguzi mizigo ambazo zingesaidia kubaini bidhaa haramu zinazoingizwa nchini.

Mashine hizo ambazo zingewekwa kwenye mipaka (entry, exit points) ikiwa ni pamoja na viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu, zilikuwa na uwezo wa kutambua hata unga wa meno ya tembo na nyara nyingine za Serikali zitakazokuwa zikivushwa kimagendo kwenda nje ya nchi.

Sina hakika iwapo mashine hizo tayari zimewekwa katika maeneo yote tajwa pamoja na kwamba katika Uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na ule wa Kilimanjaro zilikuwako kwa miaka kadhaa.

Lakini katika masuala haya mara nyingi huwa tunasahau kwamba mitambo yote hii huendeshwa na kusimamiwa na binadamu na kama hulka ya binadamu ilivyo, hususan hawa wa hapa kwetu Tanzania ya ufisadi na hujuma, basi mitambo hiyo si lolote si chochote.

Tunaweza kusema kwamba kuna watu wanaonufaika katika uletwaji wa mitambo hiyo; yaani ile ‘ten percent’ katika dili husika. Hakuna hapa duniani mitambo inayoweza kuzuia hulka ya ufisadi au hujuma. Ni kama vile hakuna mitambo inayoweza kumzuia mtu asiseme uongo. Na kwanini Serikali pia isiulizwe, ni lini italeta mitambo kwa ajili ya kusaidia maamuzi ya Takukuru?

Frederick William Robertson, Mwanafalsafa Mwingereza aliyeishi karne ya 19, aliwahi kunena kwamba kuna vitu vitatu hapa duniani ambavyo havipaswi kuvionea huruma vikiwamo, unafiki, udanganyifu na udikteta. Alitoa angalizo hilo kutokana na jinsi nchi yake na nchi nyingine za Ulaya zilivyokuwa

zinachimbia katika itikadi ya ubepari (capitalism).

Alisema changamoto kubwa inayoikabili itikadi hiyo ya ubepari; itikadi ambayo Tanzania tuliamua kuingia kichwa kichwa kwa zaidi ya miongo miwili sasa, ni kwamba masuala ambayo yalitakiwa kujenga na kulea uaminifu, badala yake yalijenga na kulea mazingira ya udanganyifu.

Ingawa vitu vitatu alivyovitaja Robertson; yaani unafiki, udanganyifu na udikteta vimekuwa hulka ya banadamu tangu alipoumbwa, lakini katika utawala wowote ule, udanganyifu ndiyo huwa chanzo cha hivyo viwili vingine.

Na pale ambapo udanganyifu hubainika, watawala wamekuwa wakihaha kutafuta njia za mkato za kujaribu kuufunika mbele ya macho ya umma, bila kutambua kwamba katika utawala wowote ule, ‘uaminifu’ ni suala la hatua za makusudi zinazopaswa kuchukuliwa katika kujenga misingi madhubuti ya usawa na haki.

Si mara ya kwanza hapa nchini Serikali kutangaza azma ya kuweka mashine za kisasa katika vituo vya mipakani (entry/exit points) katika ‘jitihada’ za kuzuia uingizaji bidhaa haramu, hususan dawa za kulevya hasa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Mihadarati hiyo imekuwa ikipita uwanjani hapo kwenda nje (na bila shaka kuingia nchini) pamoja na kuwapo vizuizi stahiki, kwa maana ya mashine/mitambo maalumu ya kukagua mizigo ya abiria na abiria wenyewe. Haikupaswa kupita kamwe labda vitu viwili viwe vimetokea: kuharibika kwa mashine au usimamizi mbovu wa mashine hizo.

Miaka minne iliyopita, baada ya kukamatwa kwa kilo 150 za dawa za kulevya katika mabegi sita katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo (Johannesburg) Afrika ya Kusini kutoka kwa abiria, Watanzania waliosafiri kutoka Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema Serikali imeamua kufunga uwanjani hapo mashine mpya na za kisasa zaidi zenye uwezo wa kubaini aina yoyote ya dawa za kulevya na nyara za Serikali.

 Mwakyembe alisema lengo la kuweka mitambo hiyo mipya ni kudhibiti uingizwaji na upitishwaji wa mizigo uwanjani hapo, ambapo kuanzia pale itakapofungwa mizigo yote inayoingia na kutoka itakaguliwa. Bila shaka mojawapo ya zile mashine alizoagiza (iwapo kweli ziliagizwa), ni zile ambazo magufuli aliziona mwaka jana zikiwa hazifanyi kazi.

Lakini kwa ujumla, suala la kujiuliza ni je, tatizo lilikuwa ni ukosefu wa mashine za kisasa zaidi za kukagua mizigo au ni uzembe tu (laxity) kwa upande wa wasimamizi wa mitambo hiyo, uzembe wa kimakusudi tu unaotokana na ufisadi ambao sasa hivi umekithiri katika safu za watendaji wa Serikali na taasisi zake?

 

Na kama jibu ni kuwepo kwa vishawishi vya ufisadi, hali ambayo wengi wanaamini ndivyo imejikita uwanjani pale, basi hii ina maana kwamba hakuna mashine/mitambo duniani inayoweza kufanya kazi kwa usahihi iwapo wasimamizi wake hawatataka iwe hivyo.

 

Kwa ujumla kamwe ufisadi hauwezi kupigwa vita kwa njia za mkato hususan hizi za kutumia mitambo kwa sababu ni hulka iliyojijenga akilini mwa watumishi wa umma na washiriki/maswahiba zao wa kibiashara.

 

Mathalani, mashine zinazoangalia mizigo pale uwanja wa ndege zinaweza kughushiwa zisifanye kazi sawasawa au zisifanye kazi kabisa kama kuna ‘mzigo’ mkubwa unaotaka kupitishwa. Kadhalika inategemea na yule msimamizi wa mashine hizo anayechungulia mizigo kupitia TV screen; anaweza akaamua kwamba ‘hakuona’ kitu chochote haramu ambapo pengine si kweli.

 

Mbali na mitambo hiyo ya kukagua mizigo, kuna kamera za kunasa matukio (CCTV Cameras) ambazo zipo nyingi tu pale uwanjani, ndani na nje. Je, nazo hizo hazikufanya kazi katika kuwanasa wale waliopitisha mabegi yale sita ya mihadarati siku ile na akina nani waliokuwa nao na/au waliowasindikiza uwanjani? Au hata baadaye kuwabaini kutokana na kumbukumbu za camera hizo?

 

Sote tunafahamu kwamba masilahi ya watu binafsi ndani na nje ya nchi yanayotokana na ushawishi wao wa kifedha, huwafanya kutumia njia haramu kupata mianya ya kibiashara, zikiwemo biashara haramu na ukwepaji kodi na katika hali hii, taasisi za umma za usimamizi hujikuta zinasalimu amri katika ufisadi huu na hivyo kugeuzwa na kuwa taasisi danganyifu.

Miaka kadhaa iliyopita, ilibainika kwamba Serikali ya Pakistan ilikuwa inatumia mashine za kutambua mabomu yaliofichwa kwenye mizigo n.k. ambayo zilikuwa ni feki. Mashine hizo aina ya ADE-651 ziliagizwa kutoka Uingereza kutoka Kampuni ya Jim McCormick ambaye baadaye alishtakiwa nchini humo kwa udanganyifu na kuhukumiwa kufungwa miaka kumi jela.

Aidha, inasadikiwa mlipuko wa bomu lililotegwa na wapiganaji wa Taliban katika Uwanja wa Ndedge wa Jinna mjini Karachi na kuua makumi ya watu ulitokea wakati mashine hizo feki ndizo zilikuwa zinatumiwa pale.

Kutokana na tukio hilo na baadaye kugundulika kwamba mashine zile zilikuwa feki, maofisa kadhaa wa Wizara ya Ulinzi na Usalama walitiwa mbaroni kwa kuagiza vifaa hivyo.

Aidha, ilidaiwa kwamba mashine hizo pia zilikuwa zimeingizwa na kutumiwa na vyombo vya usalama vya Iraq, ingawa ilichukuwa muda mrefu kutambulika kama ni feki.