Home Makala VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA IENDANE NA ELIMU BILA FITNA ZA...

VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA IENDANE NA ELIMU BILA FITNA ZA KISIASA – 1

236
0
SHARE
Baadhi ya raia wa Afghanistan wakitazama mimea ya 'opium' inayotumika kuzalisha dawa za kulevya

NA PROF HANDLEY MAFWENGA


TANZANIA inakabiliwa na biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya bangi, mirungi, heroin na cocaine ambapo mikoa ya Arusha, Morogoro, Iringa na Tanga ni hatari zaidi kwa zao za la bangi.

Uingizaji wa dawa za kulevya hufanywa kutoka nchi za Afghanistan, Pakistan, Iran, India, Brazil, Bolivia na Peru.

Aidha, baadhi ya nchi jirani ambazo hazina bandari hutumia bandari za Tanzania kupitisha madawa hayo kupitia Bahari ya Hindi, na hii inafanya baadhi ya dawa kubakizwa hapa nchini.

Vita ya dawa za kulevya nchini Marekani ilitangazwa na Rais Richard Nixon, mnamo mwaka, 1971, aidha, nchini Colombia ulitangazwa mpango mkakati wa kupunguza kasi ya biashara hiyo kwa miaka sita kufikia asilimia 50 mnamo mwaka, 1999.

Sababu zinazochangia kuwapo kwa biashara ya dawa za kulevya nchini ni pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi juu ya madhara ya biashara hiyo, uchu wa kujitajirisha kwa haraka na kushawishi vijana kujiingiza kwenye biashara ya dawa za kulevya, uwepo wa mipaka mingi isiyo rasmi ya ardhini na majini yenye changamoto nyingi katika udhibiti.

Soko la dawa za kulevya ni mnyororo wa uzalishaji unaojumuisha hatua mbalimbali, ikianzia uzalishaji katika nchi zenye vyanzo vya dawa hizo, ikifuatiwa na usafirishaji kwenda kwenye nchi za usambazaji. Baadaye dawa hizo husafirishwa na kusambazwa kwenye soko la wasafirishaji mpaka kuwafikia watumiaji.

Uzuiaji unaofanywa na nchi zinazozalisha hufanywa kwa njia mbili. Kwanza, ni njia ya kuondoa dawa hizo ambapo sera zinalenga upunguzaji wa ulimaji wa mazao haramu yanayozalisha dawa za kulevya kama cocaine, heroin, bangi n.k.

Pili, ni njia ya kuzuia ambapo sera zinalenga kuzuia njia zinazosafirisha dawa hizo kutoka kwenye nchi inayozalisha kuelekea kwenye soko la usafirishaji na uzuiaji wa usafirishaji wa dawa kwa njia ya bahari.

Sera zote hizi zinazuia ufanisi wa soko la usafirishaji wa dawa za kulevya kutoka kwenye nchi zinakozalishwa. Hata hivyo, biashara ya dawa za kulevya haiepukiki kwa vile watu wanaridhia kulipa gharama yoyote kwa ajili ya kupata dawa hizo wanazotaka kwa haraka bila kuchelewa na kwa urahisi wa hali ya juu; hii ni dhana ya nguvu ya soko ambapo kama mtu akihitaji dawa ndipo muuzaji huridhia kuuza.

PICHA Na 1: Hatua za Biashara za Dawa za Kulevya

Kuna njia mbalimbali hutumika kusafirisha dawa za kulevya; kuna njia ya masoko mbalimbali ambapo dawa husambazwa kwa wateja kupitia kwenye mnyororo wa soko la madalali.

Faida huzalishwa nchini, na kuhamishwa kwenye masoko kupitia hatua tofauti. Kwa hali hii, malipo hayafanyiki moja kwa moja kati ya mzalishaji au mkulima na mnunuzi.

Aidha, kuna njia iitwayo Kartelleni (Cartel) ambapo wadau wa kundi moja la wauzaji hudhibiti usambazaji wa dawa za kulevya kumfikia mteja na mara nyingi karibu zaidi na mzalishaji au mkulima.

Kwa hali hii, uzalishaji wa fedha za dawa za kulevya huanzia kwenye nchi dawa zinakonunuliwa na hupitia kwenye mtandao huohuo hadi kwa mzalishaji.

Ipo tofauti kati ya kemikali bashirifu na madawa ya kulevya ambapo kemikali bashirifu husaidia kupunguza uwepo wa dawa za kulevya na zimekuwa zikizalishwa Marekani na kwa baadhi ya nchi za Ulaya kwa ajili hiyo.

Kemikali bashirifu ni za kawaida za viwandani ambazo mara nyingi hutumika kutengeneza dawa za kulevya. Kemikali hizi hutokana na mimea na nyingine hutengenezwa viwandani. Mfano; utomvu wa tunda la mmea wa mbaruti afyuni (opium poppy) huchanganywa na kemikali na kutengeneza heroin.

Dawa ya kulevya aina ya amfetamini hutokana na mchanganyiko wa kemikali, ikiwamo ephedrine. Katika Kesi ya People of The Philippines, G.R. No. 199403 dhidi ya Gomer S. Climaco ya Mwaka, 2012;  Gomer alishitakiwa kwa kukiuka Kifungu Na 5 na Na 11 cha Sheria ya Umma Na 9165 (The Comprehensive Dangerous Drugs Act of 2002) kwa kuwa na dawa na kuuza dawa ya amfetamini kimakosa; Mahakama ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka 12 na siku moja na faini ya ₱300,000.00.

Hata hivyo, mahakama ya rufaa ilimuona hana hatia baada ya kukosekana ushahidi kwa vile Gomer alijumuishwa kwenye kesi hali hajui kuwa yupo kwenye orodha ya watu 20 walioshitakiwa na hakukutwa na kidhibiti.

Kemikali bashirifu kama vile potassium permanganate hutengeneza sabuni, dawa za fangasi, hutibu vidonda vya mdomoni, huzuia matunda kuoza, hutumika kuua wadudu kwenye mboga za majani, na hutumika kutengenezea vidonge vya vitamin C n.k  Hata hivyo, hutumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya cocaine.

Acetic anhydride ni kemikali bashirifu inayotengeneza vidonge vya Aspirin, mikanda ya picha, gundi, fremu za miwani n.k. Hata hivyo, hutumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya heroin.

Zipo pia kemikali bashirifu kama Ephedrine na Pseudoephedrine ambazo hutengeneza dawa ya kikohozi, nusu kaputi itumikayo wakati wa upasuaji, dawa ya kuzuia shinikizo la chini la damu na dawa za kupunguza uzito.

Hata hivyo, hutengeneza pia dawa za kulevya aina ya metamfetamini na methcathinone. Phenylacetic acid ni kemikali bashirifu inayotengeneza dawa ya kupunguza uzito, dawa ya mafua, pafyumu, tiba ya kaswende, kisonono, donda koo, homa ya uti wa mgongo, homa ya mapafu n.k.

Aidha, madawa ya kulevya aina ya amfetamini hutokana na kemikali hizo. Kemikali bashirifu kama safrole, isosafrole na piperonal hutengeneza dawa ya kuua wadudu na manukato, pia ni kiungo kwenye kutengeneza majani ya chai na bia.

Hapa pia tunapata aina ya dawa ya kulevya ambayo ni kichangamshi kinachoitwa Methylenedioxymeta mfetamini. Tatizo kubwa la kemikali zinazozalishwa zimekuwa haziuzwi moja kwa moja kwa walaji, kwani kunakuwa na madalali.

Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Kemikali Bashirifu wa mwaka 1988 unazitaka nchi wanachama kuwa na mamlaka za kusimamia udhibiti wa kemikali bashirifu katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa kemikali zilizoorodheshwa kwenye mkataba huo, ikiwa ni pamoja na uchepushaji wa kemikali hizo.

Kwa mujibu wa mkataba huo, jukumu la kudhibiti kemikali bashirifu katika ngazi ya kimataifa imepewa Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya.

Aidha, kuna orodha ya kemikali ambazo haziko katika udhibiti wa kimataifa, lakini zinafuatiliwa kwa ukaribu na Bodi ili kutambua kemikali mbadala zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya.

Kwa upande wa Tanzania, imekuwa ikidhibiti kemikali bashirifu kupitia Wizara ya Afya kwa kutumia taasisi zake za Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Hata hivyo, kumekuwapo na uingizaji haramu wa kemikali bashirifu, soko haramu la kemikali bashirifu na uelewa mdogo wa umuhimu wa kuchukua vibali. Ieleweke kuwa, kemikali bashirifu zote zina matumizi halali, isipokuwa pale ambapo hazina vibali au hutumika katika maabara haramu.