Home Latest News VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA IENDANE NA ELIMU BILA FITINA ZA...

VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA IENDANE NA ELIMU BILA FITINA ZA KISIASA – 2

686
0
SHARE
Tunda aina ya Opium linalotengeneza dawa za kulevya

NA PROF HANDLEY MAFWENGA,

WAATHIRIKA wakubwa wa dawa za kulevya duniani ni watu kati ya miaka 15 hadi 64 ambao hutumia bangi, heroin, cocaine na amfetamini. Cocaine katika bara la Afrika imekuwa ikisafirishwa kwa njia ya anga, barabara na maji. Mfano mtuhumiwa Jabir Mohammed alikamatwa na heroin akiwa ameficha kwenye soli za viatu vyake Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi Februari 2, 2007. Aidha, watuhumiwa wengine, akina Aktash Akasha, Ibrahim Akasha, Ghulam Hussein na Vijaygiri Goswami kesi zao zilihamishiwa Marekani kwa ajili ya kosa la dawa za kulevya. Kesi zao zilitikisa Ukanda wa Afrika Mashariki.

Bangi inazalishwa kwa wingi katika maeneo yote ya Bara la Afrika. Nchi za Morocco na Afghanistan ni chanzo cha bangi iliyosindikwa kote duniani. Hispania imeendelea kuwa sehemu ya kuingizia bangi iliyosindikwa kwenda Ulaya. Dawa za kulevya aina ya Metamfetamini husafirishwa kutoka Afrika Magharibi, hasa katika nchi za Benin, Ivory Coast, Gambia, Ghana, Nigeria, Senegal na Togo kwenda Asia Mashariki, Asia Kusini na Oceania. Mirungi ni mimea isiyodhibitiwa kimataifa isipokuwa ina kemikali zinazodhibitiwa kimataifa ambazo ni “cathinone” na “cathine”. Mimea hii huzalishwa na kutumiwa kwa wingi hasa katika maeneo ya Afrika Mashariki. Nchi zinazozalisha, kusafirisha na kutumia mirungi ni pamoja na Djibout, Ethiopia, Kenya na Somalia. Mirungi ni halali katika nchi za Djibouti, Ethiopia, Kenya na Somalia na imeharamishwa katika nchi za Tanzania, Eritrea, Rwanda na Sudan. Soko kuu la mirungi ni Somalia, Ethiopia na Yemen.

Hadi kufikia mwaka 2014, maambukizi ya VVU miongoni mwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano yameongezeka barani Afrika. Nchini Ghana maambukizi mapya yalikuwa asilimia 4, Senegal  asilimia 9.2, Nigeria asilimia 9 na Kenya asilimia 4.

Eneo la Amerika ya Kati na Caribbean kuna magenge ya usafirishaji wa dawa za kulevya ambayo yana mitandao Marekani na Ulaya. Kiasi cha asilimia 90 cha cocaine yote inayosafirishwa kwenda Marekani hutokea Colombia kupitia ukanda wa Mexico. Nchi za Jamaica, Saint Vincent na Granadine ni vyanzo vikuu vya kuzalisha na kusafirisha bangi. Kiasi cha bangi kinachozalishwa katika nchi hizi hutumika ndani ya nchi hizo na kiasi kingine husafirishwa kwenda Marekani, Ubelgiji, Ujerumani, Uholanzi, Uingereza na Ireland ya Kaskazini. Nchi nyingine inayozalisha na kusafirisha bangi kwa wingi katika eneo hili ni Costa Rica.

Kwa upande wa Tanzania, dawa zilizohusishwa kwenye biashara hii haramu ni bangi, mirungi, heroin na cocaine. Bangi ni dawa ya kulevya inayopatikana kwa wingi zaidi ya dawa nyingine hapa nchini. Hii inachangiwa na hali ya hewa na maeneo ya miinuko yanayoruhusu kustawi kwa mmea wa bangi kama vile Iringa, Mara, Arusha, Tanga, Morogoro n.k.  Mirungi imekuwa ikiingizwa kutoka Kenya kwa njia ya barabara, heroin hutokea nchi ya Afghanistan kwa njia ya maji, hasa kupitia bandari bubu na kusafirishwa kwa njia ya anga kuelekea nchi za China na Afrika Kusini na Cocaine hupitia viwanja vya ndege zikitokea Bara la Amerika ya Kusini kupitia nchini Brazil.

Matumizi ya dawa za kulevya ni mzigo kwa taifa kwa kupunguza nguvu kazi na husababisha uharibifu wa mali.  Gharama za utoaji wa elimu kwa umma na uteketezaji wa mashamba ya bangi. Biashara ya dawa za kulevya husababisha mfumuko wa bei unaotokana na fedha za biashara hiyo kuingizwa kwenye mfumo halali. Utakatishaji fedha katika nchi nyingi duniani hufanywa kwa chanzo cha dawa za kulevya. Dawa za kulevya husababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii, kama vile vitendo vya wizi, uporaji, biashara ya ngono, ushoga, ugaidi na ubakaji. Aidha, bangi likilimwa kwenye vyanzo vya maji na kwenye ardhi oevu husababisha kukauka kwa mito na kuleta ukame.

Wafanyabiashara wa dawa za kulevya hujitumbukiza kwenye vitendo vya kihalifu kama utekaji nyara, kufadhili ugaidi, mauaji ya kikatili, vita ya wenyewe kwa wenyewe na ujambazi, hivyo kusababisha uvunjifu wa amani. Kwa mfano, Mtandao wa Kuuza Madawa ya Kulevya wa mjini Medellin, Colombia ulidaiwa kuwaua majaji 15 na wapelelezi wa Asasi ya Usimamizi wa Dawa za Kulevya (DEA-Drug Enforcement Agency) ya Marekani.