Home Makala UKATA UNAVYOWATESA WAUZA VIFAA VYA UJENZI

UKATA UNAVYOWATESA WAUZA VIFAA VYA UJENZI

566
0
SHARE

NA MANENO SELANYIKA


KATIKA miaka ya hivi karibuni Watanzania wamekuwa wakijitahidi kuboresha makazi yao lakini harakati hizi zimekuwa zikikwamisha na changamoto nyingi ambazo zinawakabili wananchi katika kuzifikia ndoto zao.

Mojawapo ya changamoto hizo ni gharama za vifaa vya ujenzi ambavyo watu wengi wanaishia kuwa na viwanja au maeneo na mashamba makubwa lakini wameshindwa kuyaendeleza kutokana na bei za vifaa kuwa juu.

Mbaya zaidi katika uongozi wa awamu hii ya tano chini ya Rais John Magufuli, baadhi ya watanzania  wameshindwa kuendeleza ujenzi  wa nyumba kutokana na hali ya ukata wa fedha ambayo imewakabili asilimia kubwa ya watanzania.

RAI wiki hii limekutana na baadhi ya wananchi wakiwemo mafundi na wauza vifaa vya ujenzi ambao hutegemeana katika kazi zao ambapo wanasema hali ya kifedha imekuwa ngumu hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Tano.

Katika kukabiliana na changamoto za ujenzi wa nyumba za kisasa na kwa bei nafuu kampuni ya Shikamana Group Limited ya Jijini Dar es Salaam, imejitolea kusaidia wananchi wenye kipato cha chini na kati ili wawe na makazi mazuri na yaliyo bora.

Kampuni hiyo inahusika na upimaji wa ardhi, uthaminishaji na uendelezaji wa majengo.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Swalehe Salmin anasema kuna wananchi wengi wamenunua viwanja lakini wameshindwa kuviendeleza kutokana na uhaba wa fedha hasa katika kipindi hiki.

Anasema wengi hununua maeneo kwa fedha za mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha lakini huishia kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa deni alilokopa.

Mkurugenzi huyo anasema ana muda wa zaidi ya miaka mitatu katika kazi hiyo ambapo katika uongozi huu kidogo kumekuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa fedha kwa wateja wake hivyo biashara hiyo imekuwa ngumu kidogo.

Anasema jumla ya viwanja 200 vyenye ukubwa tofauti tofauti ameviuza kwa watu mbalimbali lakini kati ya hivyo ambavyo vimeendelezwa ni vichache sana.

“Cha ajabu zaidi tangu mwaka huu uanze sijawahi kuuza wala kufanya biashara yoyote kutokana na hali ngumu ya maisha,” anasema Salmin.

Anasema licha ya ukata uliopo kampuni yake imejiwekea malengo ya kujenga nyumba 15 maeneo mbalimbali Jijini  Dar es Salaam, na kuzikabidhi kwa wahusika.

Salmin anaishauri serikali itoe elimu kwa wananchi kuhusu mchakato mzima wa umiliki wa ardhi ili kuepuka migogoro mbalimbali.

Aidha, baadhi ya mafundi ujenzi wa majengo nao wanalalamika hali ya ujenzi wa nyumba sio kama kipindi cha miaka miwili iliyopita kwani kwa sasa wanaohitaji kujengewa nyumba ni wachache.

Shukur Jabir, ni miongoni mwa mafundi hao, anasema wateja wanaohitaji kugengewa nyumba hasa za kisasa ni wachache sana baada ya huu uongozi wa Rais Magufuli kuingia madarakani.

“Kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete kulikuwa na mzunguko wa fedha na kazi za ujenzi zilikuwa ni nyingi hapa mjini,” anasema Jabir.

Ahmada Masoud, ambaye ni mfanyabiashara wa mbao na vifaa vingine vya ujenzi kwenye soko Kuu la Kariakoo anasema ana zaidi ya miaka 20 katika kazi hiyo ambapo anakiri kuwa sasa hali ya kibiashara ya vifaa hivyo imedoda ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Kwa sasa hali ya kibiashara sio nzuri sana mafundi ndio wateja wangu hapa ila sijawahi kuona ugumu wa biashara kama mwaka huu yaani wamekimbia wanasema hakuna hela matajiri hawana kitu hivyo tunakoelekea ni hatari sana,” anasema Masoud.

Anasema licha ya ugumu wa maisha bado bidhaa hiyo gharama yake ipo juu ambapo ubao mmoja bei ya chini ya Sh 15,000 wakati ya juu ni Sh 18,000 kwa bei za rejareja.

Mbaraka Athuman, ni mfanyabiashara wa duka la marumaru, ambaye huuza kwa bei za jumla pamoja na rejareja. Bei ya juu ni Sh 89,000 na chini ni 41,600 kwa boksi moja la marumaru.

Anasema kupungua kwa wafanyabiashara wa bidhaa hiyo dukani kwake kumetokana na masuala mbalimbali likiwemo wateja kuwekeza fedha zao shuleni.

“Mimi nina muda wa miaka minne hapa japo hali sio nzuri sana ila kuna wakati mwingine napata fedha na kipindi kingine nakosa, lakini mwaka umeanza yawezekana wateja wamewekeza fedha zao katika elimu au wameishiwa,” anasema.

Anatoa rai kwa serikali kuwa hainabudi kurejesha fedha  kwa wananchi ili kuwapo na mzunguko ili wafanye kazi kama za ujenzi na kuleta maendeleo kwao na kwa Taifa kwa ujumla.