Home Makala TUING’ONG’E CCM ILA TUSIACHE KUISIFIA

TUING’ONG’E CCM ILA TUSIACHE KUISIFIA

804
0
SHARE

NA EMMANUEL SHILATU


MISINGI mizuri iliyojengwa na waasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere (Tanganyika) na Abeid Amani Karume (Zanzibar), imesababisha wananchi wa Tanzania kuishi kwa amani na utulivu, huku wakifanya mambo yao kwa uhuru, bila ya kuingiliwa.
Tofauti na mataifa mengine, Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote ndani ya nchi na hata kuishi au kufanya kazi, ama biashara bila ya bughudha yoyote mradi tu wanazingatia sheria za nchi.

Hali hii ni tofauti na nchi nyingine kama vile Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda, ambapo ukabila umetalaki kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, lakini kwa Tanzania hakuna ubaguzi wa rangi,dini wala ukabila.

Hiyo inatokana na uongozi imara, sera safi, upendo na ubora uliotukuka ndani jamii ya Kitanzania. Jambo linaloendelea kutia faraja, ni kuwa tangu CCM ianzishwe, imeendelea kuwa ni chama kinachotawala na kuongoza nchi. Na siri yote ya mafanikio hayo ni kutokana na kuwa nguzo imara ambazo ni wanachama, ilani ya chama, na viongozi wake.

Wanachama wake ambao ndio mtaji wa chama wapatao zaidi ya milioni nne na nusu, na mashabiki wapatao ama zaidi ya milioni 10. CCM ni chama kisichozingatia uwepo au hata harufu ya ubaguzi wa rangi, kabila au udini.

Hatua hio imewafanya Watanzania wengi, kuanzia vijana kwa wazee, wake kwa wanaume, kujivunia kuwa wanachama makini wa chama chenye mtazamo chanya wa kuwavusha kwenye neema.

Ili kuhakikisha CCM kinapata makada wa aina tofauti, bila kujali umri au jinsia, kilianzisha Jumuiya za Wazazi, Umoj wa Wanawake Tanzania (UWT), na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM)—jumuia ambazo ni viungo muhimu vya chama katika kuwaweka watu wote pamoja na hivyo kuendelea kuwa chama cha kishujaa katika kuwakomboa watu wake.

Pia kuna suala zima la uwepo wa ilani ya uchaguzi ambayo ni mkataba baina ya chama na wananchi, au viongozi na wananchi, ambao ndio wapiga kura wenyewe. CCM kinatoa ahadi mbali mbali za kutekelezwa katika muda wa miaka mitano.

Ni wazi kwamba ahadi hizo zimekuwa zikitekelezwa kwa kiwango kikubwa na cha kuridhisha, kiasi cha kuwafanya Watanzania waendelee kuwa na imani nacho kila uchaguzi mkuu unapowadia.

Hii inajidhihirisha wazi katika chaguzi za 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015, ambapo CCM kiliibuka na ushindi wa kishindo.

Nguzo nyingine kuu ya CCM ni viongozi wake. Ndani ya CCM wenye dhamana ya chama ni wanachama wenyewe na wala si viongozi. Hali hii imesaidia kutokuwa na hata chembe au harufu ya umimi, mtu kujiona kuwa ana haki miliki ndani ya chama, au kuwa ni kiongozi wa maisha. Ikumbukwe kuwa CCM ina haki zote kwa kiongozi yeyote aliyetokana na CCM.

Hiyo ni ishara kwamba ni chama chenye misingi imara ya uongozi, na ndio maana kumekuwa na mabadiliko ya uongozi ya mara kwa mara kwa kufuata misingi ya katiba ya chama. Kila baada ya miaka mitano hufanyika uchaguzi wa viongozi wa ngazi zote kuanzia mashina hadi Taifa na katika chaguzi hizo, ndipo watu huingia na kutoka.

Aidha, hali hii ni tofauti na vyama vingine nchini, ambavyo walivyoviasisi ni viongozi wa kudumu hadi hii leo. Wanapoambiwa kuna uchaguzi, baadhi yao hufanya mizengwe kwa wale wanaonyesha nia ya kuleta mabadiliko na hata kuwafukuza.

Kwa sasa CCM ipo chini ya uenyekiti wa Rais Dk. John Magufuli, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha chama kinaendelea kuongoza kupitia ridhaa ya wananchi.

Ridhaa hii inatokana na CCM kuendelea kuwa na uongozi imara, sera safi, maendeleo bora, na hivyo kuendelea kuwa tegemeo la kila Mtanzania anayependa haki na maendeleo pamoja na ustawi uliopo.

Hakuna binadamu aliyemkamilifu kwa kila kitu, isipokuwa Mungu pekee. Kwa kulitambua hilo, CCM kiliona si vizuri endapo wataendelea kuwa peke yao. Mwaka 1990 uliletwa mswada na mwaka 1992, walio wachache (20%) wakapatiwa ushindi na mfumo wa vyama vingi.

Hivyo CCM ndiyo mkunga na mwanzilishi wa mfumo huu. Tangu kuasisiwa kwake, CCM kimeendelea kuwa mkunga na kinara ndani ya utiriri wa vyama vya kisiasa takribani 20 hapa nchini.

Pia CCM kimeendelea kuwa chama cha maskini, na hii inajidhihirisha zaidi kupitia shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na Serikali zinazokuwa madarakani ambazo zote zina walenga watu maskini na watu wote katika ujumla bila ya kujali rangi, dini wala kabila.

Lengo la kuanzishwa kwa CCM ilikuwa  kumkomboa Mtanzania—haswa  mkulima na mfanyakazi (kupitia nembo ya jembe na nyundo), ili kumfanya aweze kupiga hatua kimaendeleo. Hivyo hatutakosea endapo tutasema kuwa CCM ni chama cha kimapinduzi ya kweli na dhahiri. Mathalani, CCM daima kimekuwa chama tawala kinachopinga maradhi, ujinga na umasikini. Vile vile CCM, kimeendelea kuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Mathalani katika elimu, kupitia mipango yake MMEM (Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi) na MMES (Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari), kumuwezesha kuwepo na ongezeko la idadi ya Wanafunzi katika shule.

Hii inatokana na uwepo wa sera ya kuhakikisha kuwa kuna shule za msingi katika kila kijiji na uwepo wa shule za sekondari katika kila kata.

Hali hii imesaidia uwepo wa shule za msingi 15,816 na shule za sekondari za kata 2,171. Pia Serikali za CCM zimechakalikia uwepo wa vyuo mbali mbali ambapo mpaka sasa kuna jumla ya vyuo 47 kutoka vyuo 3 vilivyikuwepo wakati tunapata uhuru.

Mfano ya vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), na matawi yake ambayo ni Chuo cha Uwalimu Dar es Salaam (DUCE) ; na Chuo cha Uwalimu Mkwawa (MUCE), Chuo cha Madaktari Muhimbili; Chuo cha Ardhi (ULASS).

Vyuo vingine vikuu ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine; Chuo Kikuu cha Mzumbe, na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambacho ni chuo kipya chenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 40,000.

Mwaka 1961, upatikanaji wa maji vijijini ulikua asilimia sita sasa ni asilimia 68. Upatikanaji wa maji mijini mwaja 1961, ulikua asilimia 25 sasa ni asilimia 83.

Upande wa huduma za kiafya; kulikuwa na hospitali 48 mwaka 1961, sasa zipo 109. Mwaka 1961 zahanati zilikua 239, sasa zipo 6114.

Upande wa elimu, shule za msingi mwaka 1961 zilikua 3000, sasa zipo 16538. Walimu wa shule za msingi walikua 9885, sasa wapo 88905. Shule za sekondari zilikua 41, sasa zipo 4753. Walimu wa sekondari walikuwa 764, sasa wapo 88908.

Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), mwaka 2016 ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 2.56 kutoka asilimia 67.53 mwaka 2015, na kufikia asilimia 70.09 mwaka 2016.

Upande wa miundombinu, mwaaka 1961 kulikuwa na barabara za lami 1300 zenye urefu wa kilomita 33,600,  na sasa kuna kilomita 124,234 na zingine zinaendelea kujengwa.

Serikali za CCM zimefanikiwa kuleta unafuu katika elimu na hata kuleta unafuu wa wanafunzi na kwa wazazi ama walezi, kwa kuhakikisha kuwa elimu ya msingi ni lazima kwa kila mtoto wa miaka saba na inatolewa bure; kila Mtanzania awe na elimu angalau ya Kidato cha Nne; kuondoa kero ya ada za mitihani kwa shule za msingi na sekondari.

Wakati tunapata uhuru kulikuwa na Watanganyika milioni 9. Kati ya hao ni watu wasiozidi 300,000 waliobahatika kupata elimu ya darasani na waliokuwa darasani kipindi hicho hawakufika wanafunzi 1,500. Itaendelea wiki ijayo