Home Makala GEORGE MTASHA: JPM ANALINDA MADINI KWA VITENDO NA PENDO...

GEORGE MTASHA: JPM ANALINDA MADINI KWA VITENDO NA PENDO FUNDISHA

1025
0
SHARE

GEORGE Mtasha, si jina geni jijini Mbeya, huyu ni mjasiriamali, anayejitafutia ridhiki yake kwa halali bila hila. Hatua yake ya kusaka pato lake kwa njia halali inampa nguvu na jeuri ya kukubaliana na maamuzi mengi yanayofanywa na serikali ya awamu ya Tano dhidi ya Wafanyabiashara wadogo na wakubwa.

Moja ya mambo yanayomuunganisha Mtasha na harakati za Rais Dk. John Magufuli ni uamuzi wa kupiga marufuku mchanga wa madini kwenda kuchenjuliwa nje ya nchi.

Rais Magufuli alipiga marufuku hiyo machi 3, mwaka huu, kwa kuweka wazi kuwa ni vema shughuli ikafanyika nchini kwa sababu kitendo cha kusafirisha mchanga huo nje ya nchi kinatoa nafasi ya wafanyabiashara wa madini wasio waaminifu kujinufaisha.

Alisema uchenjuaji wa mchanga wa madini nje ya nchi unaikosesha Serikali mapato ikiwa ni pamoja na wizi madini hayo na kwamba hiyo ndio sababu kubwa ya yeye kukataa kusaini mkataba wa EPA.

Alisema, kupitia mkataba huo, ni vigumu kwa kampuni za Tanzania kushinda zabuni katika nchi za Ulaya, lakini ni rahisi kwa kampuni za Ulaya kushinda zabuni Tanzania kutokana na kukomaa kiteknolojia, na hata zinaposhindanishwa kampuni za Tanzania na Ulaya ni rahisi kwa kampuni za Ulaya kushinda, jambo litakalochangia kuua kampuni za ndani.

Uamuzi huo wa Rais inawezekana umewaudhi wafanyabiashara wachache wakubwa, lakini kwa kiasi kikubwa umewafurahisha wafanyabiashara wengi wadogo.
Miongoni mwa waliofurahia ni wachimbaji wadogo wa madini aina ya dhahabu waliopo katika mgodi wa Makongolosi, Wilayani Chunya, mkoani Mbeya.

Wao wanasema wasafirishaji wa mchanga walikuwa wakiitumia nafasi ya kusafirisha mchanga nje, kuiba baadhi ya madini hatua ambayo pia ilikuwa ikiwasaidia kukwepa kodi.

Mtasha, ambaye alizungumza na RAI anasema ili nia njema ya Rais Magufuli ya kuwa na Tanzania ya viwanda ifanikiwe, ni lazima wafanyabiashara walipe kodi stahiki.

Serikali kupitia idara husika zinapaswa kusimamia mapato, kitendo cha kuzuia mchanga kwenda nje kuchenjuliwa ni hatua kubwa ya kufanikisha upatikanaji wa mapato stahiki ambayo yatasaidia kusukuma maendeleo mbele.

Anasema, baadhi ya makampuni ya kigeni yamekuwa yakitumia nafasi hiyo kujinufaisha wao binafsi pamoja na kukuza uchumi wa nchi zao kwa kupitia maligahafi za Tanzania.

“Wilaya ya Chunya imebarikiwa kuwa na madini tena madini mbalimbali, Dhahabu inapatikana, Shaba, Kopa na hata Almasi inasemekana inapatikana katika eneo la Lupa Wilayani Songwe.

“Lakini pamoja na utajiri mkubwa wa rasilimali hizi bado wilaya, Mkoa na hata nchi imekuwa hainufaiki na kubwa zaidi hata wachimbaji na wananchi wa maeneo husika wameendelea kuwa masikini na hii inatokana na unyonyaji mkubwa unaofanywa na watu wanaomiliki makampuni makubwa ya uchimbaji.

Mtasha, anaweka wazi kuwa kampuni hizo zimekuwa zikisajiliwa na kupewa leseni kutoka ofisi za madini, lengo likiwa ni uchimbaji, ajabu ni kwamba zinapofanya ununuzi wa marudio ya mchanga hazichangii kitu chochote kwa serikali zaidi ya kulipia kibali cha usafirishaji.

“Mabaki ya mchanga ambao husafirishwa nje na wageni hao, ndani yake kunakuwa na madini mengi sana ambayo kama ungepimwa ndani ya nchi basi Watanzania wangeweza kunufaika na rasilimali hizo.

“Makampuni yote unayoyaona yanakuja kununua marudio yaani mchanga ambao ulikwisha chenjuliwa, wanachokifanya ni kuchukua mchanga na kwenda kuupima maabara, wanabaini kwamba ndani ya mchanga ule kuna kiasi fulani cha dhahabu sasa hawaji kukuambia wewe kiasi cha madini walichokibaini hiyo ni siri yao,” anasema.

Anasema, wao watakachokueleza ni kwamba mchanga wako unamadini mengi aina ya shaba au sampo ni ndogo, lakini ukizalisha mchanga wenye dhahabu nyingi tutakulipa vizuri hivyo kwa mchanga huu, utalipwa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa tani zaidi ya 200.

Anasema, wanunuzi hao wamekuwa wakikadiria bei kwa macho lakini ndani ya mchanga ule unakuta kuna kilo 14 za dhahabu ambayo ina asilimia 98 sasa ukifanya hesabu za kawaida unaweza kukuta gramu moja ya dhahabu unauza kwa shilingi 80,000 kwa soko la dunia.

Hivyo kilo kumi ya dhahabu, unaweza pata milioni 800 lakini kumbuka wewe ulipewa milioni 100 tu kwa kuuza mchanga huo wa marudio.

“Hata ndege alizotuletea rais hazipati faida ya namna hiyo, lakini huyu aliyenunua mabaki ya mchanga anapata faida ya milioni 800 kwa roli 200 za mchanga,”anasema.

Anasema, katika hesabu hiyo kilo nne, zinawekwa pembeni kwa ajili ya matumizi madogo madogo lakini ukweli ni kwamba wageni wamekuwa wakilimaliza Taifa, hivyo ni vema sasa Serikali ikaangali njia mbadala itakayosaidia kuwabana wanunuzi wa mchanga.

Akizungumzia mikakati yake katika kukuza uchumi wa Taifa pamoja na kujiongezea kipato, Mtasha ambaye pia ni mwanasiasa mkongwe kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anasema kuwa ameamua kuthubutu kwa kufungua kiwanda cha uchimbaji wa madini.

“Awali kazi yangu ilikuwa ni kuchimba madini kwa kutumia njia za kawaida, lakini katika kipindi cha mwezi mmoja ninatarajia kuanza kuchimba madini kwa kutumia njia za kisasa zaidi kwa kutumia kiwanda kidogo nitakachokifungua mwezi Mei mwaka huu,”anasema.

Anasema, kiwanda hicho kitaongeza uzalisha lakini kubwa zaidi ni kwamba ameamua kumuunga mkono Rais katika kutekeleza sera ya viwanda.

“Kwa kuwa serikali inataka nchi ya viwanda na hii ni sehemu ya viwanda, nitachimba madini katika mgodi wangu na kuongeza uzalishaji mwingine,”anasema.

Anasema, kiwanda hicho kitaingiza mapato Serikalini kupitia mrahaba wa madini atakayo zalisha.
“Kwa sasa nalipa pato mara moja tu kupitia uzalishaji wa mawe, lakini kiwanda kitaongeza asilimia nyingine nne za uzalishaji hivyo itakuwa asilimia nane, hilo niongozeko kubwa na nchi itaendelea kunufaika na kuboresha miundombinu yake.

Aidha, serikali kupitia ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, katika kuhakikisha inawasaidia wachimbaji wa madini, wakubwa, wakati na wadogo, imeamua kusogeza huduma kwa kufunga mtambo mpya na wa kisasa wa Energy Dispensive X-Ray Fluorescence(ED-XRF) kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara.

Maabara hiyo paoja na usimamizi wa sheria zilizo chini ya wakala, pia itafanya kazi za kuchunguza zinazofanywa na maabara za kuhakiki ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa viwandani kama vile, dawa za kulevya, vyakula,dawa za binadamu, sampuli za mazingira, sumu, vinasaba na sampuli za migodi.

Akizungumzia hili, Mkemia Mkuu wa Serikali,Profesa. Samweli Manyele, anasema mtambo huo utatumika katika kufanya uchunguzi wa sampuli za migodi migodini kama vile miamba, udongo,masalia ya mchanga baada ya wachimbaji wadogo kuchenjua na maji taka yaliyo na sumu aina ya sianidi.

Lingine mtambo huo, utapima hewa ya “Carbon” ili kuweza kutambua kiwango cha dhahabu na madini mengine ya thamani kabla ya kuwekeza katika uchimbaji na uchenjuaji huo.
Mkemia huyo, anaongeza kwa kusema kuwa mtambo huo utatumika kubaini ubora na usalama wa bidhaa za chuma, bidhaa za petrol ikiwemo mafuta na dizeli, petrol na vilainishi ili kupima kiwango cha madini ya sulphur na Phosphorus.
Hata hivyo, akizungumzia ujio wa mtambo huo, mlipuaji mawe yenye dhahabu kwa kutumia baruti katika mgodi wa PML wa Makongorosi Wilayani Chunya, Daniel Ngusa, yeye binafsi anaishukuru serikali kwa kusogeza huduma hiyo kwani asilimia kubwa ya wachimbaji wadogo wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea badala ya kitaalamu.
“Unakuta mtu anaingia shimoni kupasua au kulipua miamba pasipo kufanya uchunguzi wowote wa kimaabara hivyo hujikuta akitumia muda mwingi kupasua mawe ambayo hayana mali, hivyo mtambo huo utasaidia kurahisisha kazi kwani kabla ya kulipua, muhusika tayari anafahamu kama jiwe hili litanitolea mali,”anasema.
Mwisho.