Home Makala KWANINI MADABIDA HAKUSAMEHEWA KAMA KIMBISA?

KWANINI MADABIDA HAKUSAMEHEWA KAMA KIMBISA?

262
0
SHARE

NA GABRIEL MUSHI


MWISHONI mwa wiki iliyopita, Watanzania wameshuhudia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikianza safari ya mageuzi baada ya kutimua wanachama wake 12, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba.

Mbali na Sophia ambaye tayari alishatangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka huu, pia wamo wenyeviti wa CCM wa mikoa minne ambao nao wamefukuzwa kwa makosa ya usaliti na kukifanya chama hicho kinuke mbele ya wananchi.

Wenyeviti hao na mikoa yao katika mabano ni Ramadhan Madabida (Dar es Salaam,) Jesca Msambatavangu(Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga) na Christopher Sanya (Mara).

Wanachama wengine waliofukuzwa ni Wilfred Ole Mollel ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini, Mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Babati Mjini, Ally Sumaye na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Wilaya ya Arumeru, Mathias Manga.

Katika orodha hiyo, pia wamo wenyeviti wa wilaya wa chama hicho; Omari Awadhi (Gairo), Ally Msuya (Babati Mjini), Makolo Laizer (Longido), na Salum Madenge (Kinondoni-Dar es Salaam).

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkutano wa Kamati Kuu ya NEC uliofanyika mjini Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alibainisha kuwa uamuzi huo ni mwanzo tu wa kuelekea katika mageuzi.

Hata hivyo, mjadala umebakia miongoni mwa Watanzania kuhusu kufukuzwa kwa kada mkongwe wa chama hicho, Ramadhani Madabida, huku Adam Kimbisa akisamehewa.

Itakumbukwa kuwa Dk. Emanuel Nchimbi, Kimbisa na Sophia Simba, walikuwa katika kundi lilopinga kitendo cha Kamati ya Maadili chini ya Mwenyekiti wake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete cha kukata majina yote ya wagombea urais, likiwemo la aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, bila kuwaita na kuwahoji kisha kupeleka majina matano tu ili yajadiliwe na Kamati hiyo.

Kati yao waliojitokeza hadharani na kudai kuwa kanuni za chama hicho zilikuwa zimepindishwa, ni Kimbisa pekee ambaye amesamehewa. Dk. Nchimbi ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Brazil, amepewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi.

Kwa upande wake Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), amesamehewa lakini Madabida ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam ambalo ndilo jicho la Tanzania, akitimuliwa na kufutiwa uwanachama.

Pamoja na mambo mengine, zipo sababu kadhaa tano ambazo zimesababisha Madabida kuadhibiwa na kuzua taharuki kwa baadhi ya wananchi.

‘Team Lowassa’

Mosi, alikuwa miongoni mwa makada waliodaiwa kumuunga mkono Lowassa katika uchaguzi wa kumteua mgombea wa kiti cha urais 2015. Licha ya jambo hili kutowekwa wazi, Madabida alikuwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Duru za kisiasa zinasema kuwa alikuwa mmoja wa makada wa CCM waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa.

Itakumbukwa kuwa Sophia Simba ambaye amedumu kwenye ubunge kwa miaka 22 na uenyekiti UWT miaka 10, licha ya kuwa na nyadhifa ndani ya CCM, alionesha mapenzi ya waziwazi kwa Lowassa na kuendelea kutoa matamko yenye utata. Hiki ndicho kisa cha chama hicho kumng’oa huku Kimbisa akibakishwa licha ya kwamba alionesha kumuunga mkono Lowassa, lakini alibaki kimya baada harakati za Uchaguzi Mkuu kuanza.

Upotevu wa majimbo

Pili; upotevu wa majimbo katika Mkoa wa Dar es Salaam unaweza kuwa sababu kubwa kwa Madabida kuondolewa. Upinzani ulinyakua majimbo sita kati ya tisa.

Itakumbukwa kuwa CCM imekuwa ikijivunia Jiji la Dar es Salaam kama ngome yake. Kwa mara ya kwanza upinzani umetoa Meya wa Jiji na majimbo mengine yametoa mameya wa manispaa.

CCM ilipoteza majimbo ya Kibamba, Kawe, Ubungo, Kinondoni, Ukonga, Temeke na kuambulia majimbo ya Kigamboni, Ilala na Segerea.

Wakati CCM ikiangukia pua Mkoa wa Dar es Salaam, Kimbisa alifanya vema kwa upande wa Mkoa wa Dodoma na kuendeleza rekodi ya kuwa moja ya mikoa ambayo kwa miaka 20, CCM imekuwa ikipeta.

Dodoma ambayo ina majimbo 10 katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Kimbisa alifanikiwa kuuongoza mkoa huo na kutetea majimbo yote, licha ya awali kuonesha kuwa alikuwa akimuunga mkono Lowassa. Hii ni sababu tosha iliyochangia kwa kiasi kikubwa kusamehewa kwake.

Kupoteza Madiwani

Kupoteza madiwani ilikuwa ni sababu ya tatu ya kufukuzwa kwa Madabida. Ukawa ilivuna madiwani 87, huku CCM ikiambulia madiwani 76. Hali hii iliifanya CCM kuwa katika wakati mgumu katika kutetea nafasi mbalimbali za umeya.

Kupoteza halmashauri

Nne; kupoteza halmashauri kama ilivyotanabaishwa awali, tayari jiji lipo chini ya Ukawa likiongozwa na Meya Isaya Mwita. Ukawa pia walichukua halmashauri za Ilala na Ubungo.

Tofauti hiyo pia ilimweka katika nafasi finyu Madabida kubakishwa, ukilinganisha na Mkoa wa Dodoma ambako Kimbisa alifanikiwa kuuweka chini ya himaya ya CCM.

Licha ya kuwapo sarakasi mbalimbali katika chaguzi za Meya, Madabida hakufua dafu katika maeneo mengi, zaidi ya Kinondoni ambako CCM ilifanikiwa kutwaa nafasi ya umeya kwa kutumia mbinu na nguvu kubwa kama ilivyofanya katika Jiji la Tanga.

Kashfa

Tano; Kashfa ya Kiwanda cha kutengeneza dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI), ambayo iliibuka mwaka 2011 na kumhusisha Mkurugenzi Mkuu Madabida, inatajwa pia kuchagiza anguko lake.

Itakumbukwa kuwa kiwanda hicho kilituhumiwa kusambaza dawa feki za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (ARVs) na mwaka 2014, Madabida na wenzake walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu kwa mashtaka matano ya usambazaji wa ARVs.

Pia walishtakiwa kwa kuisababishia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hasara zaidi ya Sh milioni 148.3. Hata hivyo, mwaka jana TPI walishinda kesi hiyo na kufungua kesi ya madai ambayo walishinda.

Aidha, Rais John Magufuli alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari, kuwa hatathubutu kulipa tozo ya Sh bilioni 60 kama fidia kwa TPI hata kama walishinda kesi.
TPI kinamilikiwa na watu watatu akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, wamezuiwa kufanya shughuli za uzalishaji kwa miaka minne kufutiwa hati ya mfamasia wa kiwanda hicho, Zarina Madabida, kwa sababu ya kuzalisha ARVs feki.
MWISHO