Home Makala SURA MBILI ZA RAIS WA NCHI

SURA MBILI ZA RAIS WA NCHI

165
0
SHARE

NA MARKUS MPANGALA


NIMEMSIKILIZA kwa makini Rais wa Benki ya Dunia, DK. Jim Yong Kim, katika hotuba aliyoitoa Machi 20, mwaka huu eneo la Ubungo Maji jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya juu.

Katika hotuba yake alidai kuvutiwa na Mwalimu Julius Nyerere wakati akiwa mwanafunzi.

Dk. Yong Kim alinukuu mojawapo ya kauli za Mwalimu Julius Nyerere isemayo: “Without freedom you get no development and without development you very soon lose your freedom.” Kwa tafsiri yangu ni kwamba “Bila Uhuru huwezi kupata maendeleo na pasipo na maendeleo katu huwezi kuwa huru”.

Sina hakika kama kweli alivutiwa na Nyerere toka akiwa mwanafunzi au ghiliba tu kwa kuwa alitakiwa kuwasili nchini. Yote mawili yanawezekana.

Hoja kuu ambayo naiwasilisha leo ni kwamba katika ulimwengu wetu huu, kila mwanadamu anatakiwa kuwa huru. Kila mwananchi anatakiwa kuwa huru katika uamuzi wake wa kujitafutia pato. Kila Mtanzania anao wajibu wa kuhakikisha anakuwa na uhuru wa kiuchumi ambao unampatia uhuru wa kujieleza.

Endapo hajitoshelezi katika suala hilo, basi kwa kawaida huwa anakosa ule uhuru wa maendeleo. Watu wanapokosa uhuru wa maendeleo maana yake wanakosa kabisa uhuru wa kujieleza. Na hata wakijieleza wanapoteza kujiamini na kuona hawawezi kufanya chochote kwa kuwa wao hawana uhuru wa kujitosheleza kiuchumi.

Hasara ya taifa la watu wasiojitosheleza kiuchumi wanaweza kurubuniwa na yeyote kisha wakauchukua uamuzi wao kama nyenzo ya kujaribu kupata uhuru wa kujieleza.

Dk. Kim ameeleza hilo kama njia ya kuwasilisha umuhimu wa uhuru wa kiuchumi na kujieleza. Kwamba kama watu wako huru kujieleza, basi watakuwa na uhuru wa kufikiri njia za kujipatia pato.

Hatutarajii kuona watu wakishindwa kujieleza sababu ya kubanwa. Hatutarajii kuona Serikali ikifurahia watu wake kushindwa kujieleza wala kuwa na uduni wa Uhuru wa kiuchumi. Yote mawili haya yanaendana.

Hakuna mahali ambapo uchumi ulistawi kwa watu kuacha kufikiri njia za kujiongezea pato. Hakuna nchi inayoendelea kwa kuwafanya watu waishi kama zama za ‘vijiji’ vya ujamaa ambavyo havikuwa na Uhuru wa watu kujitosheleza.

Baada ya maelezo hayo ndipo tunatazama upande wa pili, je, sisi tuko huru kiasi gani kiuchumi? Fikra zetu zimekuwa huru kwenye maendeleo ya nchi yetu? Je, tunao uhuru wa kutosha wa kujieleza au kutoa hisia zetu juu ya mambo yoyote? Iko hivi; katika ulimwengu huru kutokubaliana na upande fulani kisiasa au makundi, haina maana kuwa ule upande unafanya mambo mabaya pekee bali wakati mwingine ni wewe mhusika ndiye hukubaliani na kule kwingine tu kwa minajili ya kuridhisha fikra za upande wako.

Pande mbili zinapopingana haina maana kuwa lazima mmoja uwe mbaya. Inakupasa kujua madhumuni ya unalokubaliana nalo ni halali kimantiki au ni kwa sababu ya kuridhisha nafsi au pengine kujipoza kwa kitu fulani kilichokutokea maishani dhidi ya kundi fulani. Mathalani maneno ya Dk. Kim amepiga ngumi ya shavuni ambayo hata Rais John Magufuli anatakiwa kuyafikiri.

Kwamba kama hakubaliani na uhuru mwingi wa kujieleza wa wananchi wake, basi anatakiwa kufahamu anachochea kuminywa kwa uhuru wa kujipatia maendeleo. Na kwamba Dk. Kim anatufunza kuwa ili kufanikisha maendeleo, ni lazima kuzielewa pande hizo mbili kwa kuwa zinashabihiana.

Ukiminya uhuru wa watu kujieleza basi unaminya uhuru wao wa kujifikiria kimaendeleo. Huo ndo ukweli na Dk. Kim, ameutoa kwa makusudi akifahamu hali zetu. Kwamba tumekuwa watu tusiothamini uhuru wa maendeleo lakini tunapewa uhuru wa kumpongeza kiongozi tu.

Kwa muktadha huo, unaweza kujionea sura kadhaa za rais wa nchi kupitia mambo hayo mawili; uhuru wa maendeleo na kukosa uhuru unaochochea uduni wa maendeleo.

Chukulia mfano, upo katika nchi ambayo kelele na mashinikizo ni mengi. Upo katika nchi ambayo kiongozi fulani wa nchi hiyo anatuhumiwa jambo lolote. Wananchi wamejieleza. Wanafikiri na wanajua wanayo haki hiyo. Lakini upande wa pili wanajikuta nguvu zao zinatumika bure kwani matarajio yao hayatimii.

Matarajio hayatimii kwa kuwa rais wa nchi anakuwa amekataa kuyatimiza. Je mambo yanayoliliwa na wananchi ni halali? Jawabu la jambo linalotokea juu ya kiongozi kutuhumiwa ni kusafisha uchafu unaomwandama.

Kwa kawaida kiongozi akituhumiwa ni lazima ajitokeze kujieleza na kukiri makosa ama kufafanua. Tumeona maeneo mbalimbali kuwa viongozi wanatuhumiwa na kujieleza. Tumeona wenye makosa wakijieleza na kufafanua.

Lakini inapotokea katika nchi fulani kiongozi hajibu wala haonekani kuwa na muda wa kujitetea juu ya tuhuma, watu huamini kuwa ni tuhuma za kweli au wamedharauliwa. Kwa maana hiyo tuhuma hizo zinaota mizizi.

Zinawagusa na kuwafikia hata watu wasiokuwa na shaka na kiongozi. Pamoja na kiongozi mhusika kutojibu tuhuma zake, kabla hayajaketi sawasawa anaibuka na tuhuma nyingine. Katika tuhuma za pili zinaonyesha kuwa akitenda mambo ambayo hayaoneshi taswira nzuri kwa jamii.

Makundi mawili huibuka katika muktadha huo. Kundi la kwanza litatafuta uhalali wa tukio au uharamu. Kundi hilo linachofanya ni kujadili matokeo ya tukio tu, halina cha mno.

Kundi jingine linarudi nyuma na kujiuliza kwanini tukio limetokea? Kwanini mhusika ametenda tukio hilo? Je, tukio hilo ni la kawaida au lina ishara zote zenye nadharia za propaganda za aina fulani juu ya kugeuzwa mwenendo fulani na kuupeleka sehemu fulani au kumnasua kiongozi fulani anayekabiliwa na tuhuma fulani? Je, wahanga wa tukio wanasema nini juu kutokea jambo hilo? Tukitoka hapo tunakuja katika nadharia za usalama, je, inawezekanaje tukio moja likachukua muda mrefu kuzungumzwa kana kwamba hakuna uhuru mwingine wa kujitafutia pato? Bado tunarudi kwa Dk. Kim, tunapoteza uhuru wetu pale tunapokosa maendeleo pamoja na kupoteza uwezo wa kufikiri. Kupoteza uhuru huko ni pamoja na uwezo wa kufikiri sawasawa kutokana na kukosa ‘viungo’ vya kutosha (mifano) ambayo inajenga dhana husika ya tukio.

Mwishowe unabakiwa na makundi mawili kama tulivyoona hapo juu. Baadaye utagundua kuwa makundi hayo yanajadili masuala ya uongozi wa nchi kwa namna yake.

Yanajadili juu ya uhalali wa uamuzi wa kiongozi lakini yanakosa vielelezo vya kutosha kufikia hitimisho kwa kuwa wamepangiwa ‘script’ nzima juu ya kuongea na wamebashiriwa aina ya maongezi ya mijadala yao.

Hakuna kitu kibaya maishani kama kutabirika kwa kiongozi au mwanadamu yeyote. Lakini hilo halizuii kiongozi kuwa msikivu kwa watu. Mosi, matukio ya kiongozi mmoja yametufunza kuhusu mambo muhimu ya rais wa nchi.

Yanatupatia sura za rais wa nchi katika muktadha wake. Pili, katika sura hizo mbili kutokana na hoja ha kwanza ni kwamba rais huwa na mambo mawili makuu: kwanza, kwa wananchi wake anakuwa ‘Rais ametusikiliza’ hasa pale anapochukua uamuzi unaopendeza jamii anayoiongoza.

Pili, ‘Rais kaongea leo’. Huyu anakuwa rais anayezungumza kinyume na matarajio ya wananchi juu ya jambo fulani. Huyu anakuwa ametoa kauli nzito za kuashiria uongozi wa nchi.

Huyu ndiye anaweza kuwapoteza au kuwainua wananchi wake katika kuupata uhuru wa kufikiri juu ya maendeleo, sababu saikolojia ya kawaida inakata tamaa au kuimarika.

Faida ya hilo ni kwamba watu hao hao watamsifu au kumkejeli rais kuwa ni mtu mwenye msimamo au hana msimamo kwani anayumbishwa kirahisi.

Watamsifu kuwa ni kiongozi thabiti au dhaifu. Katika nukta hii tayari makundi mawili yanaibuliwa na yanakinzana na kuanzisha hoja nyingine kati ya sifa za uthabiti wa rais na kuyumba kwake.

Sasa sijui Rais Magufuli ameyumba au amekuwa thabiti. Labda nitaelewa tuko upande gani huko tuendako.