Home Makala UKOMO WA MADARAKA HUEPUSHA VURUGU ZA KISIASA

UKOMO WA MADARAKA HUEPUSHA VURUGU ZA KISIASA

256
0
SHARE
Marais wa zamani wa Afrika; Kutoka kushoto ni Kenneth Kaunda (Zambia) aliyekubali kushindwa uchaguzi, Julius Nyerere (Tanzania) aliyeondoka madarakani kwa hiari, Jomo Kenyatta (Kenya) aliyefariki akiwa madarakani na Milton Obote (Uganda) aliyepinduliwa akiwa madarakani.

NA HILAL K SUED


Mabadiliko ya upepo wa kisiasa (political wind of change) yaliyoikumba dunia mwishoni mwa miaka ya 80 (zaidi ya robo karne iliyopita) yaliyoanzia Ulaya Mashariki, yalileta uboreshaji fulani ya mifumo ya tawala za nchi kadhaa barani Afrika, zilizokuwa zimejikita katika udikteta wa chama kimoja au wa mtu mmoja kwa kuruhusu uwepo wa mifumo ya vyama vingi, Tanzania ikiwemo.

Ndipo hapo ikasisitizwa uwepo wa ukomo wa vipindi vya watawala na nchi kadhaa, ikiwemo Tanzania zikafanya hivyo, kwamba mtawala (rais) asiongoze kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Hii iliigwa kutoka mfumo wa utawala wa Marekani, ingawa wao ni vipindi viwili vya miaka minne minne.

Lakini pamoja na kuwepo kwa ukomo wa vipindi vya urais, Tanzania bado inatawaliwa na chama kile kile tangu wakati wa uhuru, ikiwa ni zaidi ya miaka 55 iliyopita.

Inawezekana hapo awali wakati wa ujio wa mfumo wa vyama vingi na miaka kadhaa baadaye, CCM ilikuwa bado ni kipenzi cha wananchi wengi, hasa katika ile methali ya ‘zimwi likujualo halikuli likakumaliza’ lakini jinsi miaka inavyozidi kupita, hali hii inazidi kupata changamoto nyingi.

Miaka kadhaa iliyopita, mhadhiri mmoja mwandamizi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na ambaye sitamtaja jina, aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari, akisema kwamba ingawa yeye bado ni mwanachama wa CCM, lakini pamoja na wenzake wengine pale chuoni na kwingineko, wanajitahidi kuhakikisha CCM inaondoka madarakani kwa amani, ili ikae pembeni na kujitafakari.

Alisema ana hakika CCM inaweza ikarudi madarakani, mara hii kwa nguvu, mawazo na sera mpya na kuongeza kusema kwamba yeye na kikundi chake wako tayari kukisaidia chama hicho, kwani bado kina sera nzuri za kutetea utu wa binadamu na wanyonge kama kilivyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Mhh!!!!CCM irudi madarakani baada ya kuondoka? Hilo naona ni kitu kigumu kutokea, hasa ukitazama vilivyokuwa vyama tawala vingine katika nchi kadhaa barani Afrika, ambavyo vilitokomea nyikani baada ya kuondoka.

Mifano ni UNIP ya Zambia na KANU ya Kenya. Hivi ni vyama vile vilivyoondoka kupitia sanduku la kura, lakini kuna vingine haikuwa kwa njia ya aina hii ya kidemokrasia, kama vile Burundi, Ivory Coast, Ghana, Siera Leone, Liberia, Madagascar, Rwanda, Congo DRC na nyingine nyingi barani humu.

Mwasisi wa Taifa la Zambia, Kenneth Kaunda angekuwa na matshi binafsi, hadi leo angeweza kuwa rais wa Zambia. Kwani si ndicho hicho kilichopo nchi jirani ya Zimbabwe?

Vyama na Serikali zao zilibadilishwa kwa ghasia kubwa na hata vita za wenyewe kwa wenyewe za umwagaji mkubwa wa damu. Hii yote ilitokana na kushamiri kwa mifumo ya demokrasia iliyokuwa dhaifu, ingawa pia ni tamaa tu ya madaraka.

Nitatoa mfano; mwaka 2012 aliyekuwa Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, alitupwa nje ya kinyang’anyiro cha kuwania urais kwa kipindi cha pili, baada ya kushindwa na Francois Hollander. Katiba ya Ufaransa imeweka ukomo wa vipindi vya urais viwili vya miaka mitano mitano kama ilivyo Tanzania.

Kama Ufaransa ingekuwa na demokrasia dhaifu kama vile za baadhi ya nchi nyingi tu barani Afrika, Sakorzy angefanya juu chini abakie madarakani.

Ama angeondoa ukomo wa vipindi vya urais na kujitangaza rais wa maisha au kila mara angekuwa anashinda chaguzi kwa njia za haramu na ghilba. Na hayo yote yangeshindikana, basi angefanya juu chini mwanawe mmoja anamrithi. Jitihada zote hizi zikiwa na lengo la kujilinda, kwa kuhakikisha haingii uraiani na akiingia basi asiweze kushtakiwa na kutupwa gerezani.

Nchi za Tunisia, Misri na Libya ni mifano ya miaka ya hivi karibuni. Marais Ben Ali na Hosni Mubarak wa Tunisia na Misri mtawalia walitinga mahakamani mara tu baada ya kuangushwa ingawa Ben Ali aliwahi kutorokea Saudi Arabia.

Kesi yake ilisikilizwa na hukumu kutolewa akiwa hayuko nchini. Mubarak alihukumiwa kifungo cha maisha, lakini mapema mwaka huu alishinda hukumu hiyo katika rufaa ingawa bado yuko kizuizini kwa mashtaka mengine.

Na mwaka 1998, Helmut Kohl baada ya kuwa Kansela (Waziri Mkuu) wa Ujerumani kwa zaidi ya miaka 17, alijiuzulu kwa aibu baada ya kubainika kwamba chama chake cha Christian Democratic Union (CDU) kilikuwa kinapata michango ya siri kutoka kwa wafanyabiashara. Wengi walisema kutokana na kung’ang’ania madarakani muda mrefu, madhambi yake yalianza kuchimbwa na hatimaye kuwekwa hadharani.

Na madhambi ya namna hiyo na mengine ndiyo huingizwa kile kinachoitwa kulindana katika utawala, hali inayoelezwa mara kwa mara kuwa sababu mojawapo kwa chama kama CCM kukaa madarakani muda mrefu. Rais anayepokea kijiti huamua (na hata kutangaza hadharani) kwamba hatamchukulia hatua mtangulizi wake kwa ‘madhambi’ yoyote ya kiutawala na mengine anayodaiwa kufanya akiwa madarakani.

Hili la kulindana limewahi kuzungumzwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, baada ya kumrithi Benjamin Mkapa na pia Rais wa sasa John Magufuli baada ya kumrithi Kikwete.

Akiwahutubia waandishi wa habari pale Ikulu Juni mwaka 2007, mwandishi mmoja alimuliza Rais Kikwete kwamba iwapo ana mpango wa kumchukulia hatua za kisheria Rais aliyemtangulia, Benjamin Mkapa, kwa tuhuma kwamba akiwa madarakani yeye na mkewe walianzisha kampuni ya kibiashara na hivyo kujishughulisha na biashara na kwamba huenda aliutumia wadhifa wake wa urais kwa kuipendelea kampuni hiyo ili kujinufaisha binafsi.

Kikwete alijibu kwamba ingawa kulikuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa ‘kosa’ hilo alilofanya mtangulizi wake, lakini suala zima la kuwachukulia hatua za kisheria marais wa zamani kwa makosa ambayo waliyatenda wakiwa madarakani, kunaweza kuwafanya baadhi yao kubadilisha vipengele vya katiba za nchi zao kwa lengo la kuongeza vipindi vya kutawala.

Juni mwaka jana katika hafla moja jijini Dar es Salaam iliyohusu masuala ya ulinzi na usalama, huku rais aliyemtangulia Jakaya Kikwete akiwa karibu yake, Rais Magufuli alitamka bayana kwamba hatamgusa mtangulizi wake kuhusu tuhuma zozote za ufisadi alipokuwa madarakani na aendelee na maisha yake ya ustaafu kwa amani kabisa.

Ni vyema nikataja hapa kwamba ‘wanaosamehewa’ hapo ni pamoja na ndugu, jamaa, familia na maswahiba wa huyo mtangulizi wake.

Kama vile ‘hukumu’ ya hatia ya jinai alivyotoa kwa watendaji wakuu wengine (mfano kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, marehemu Wilson Kabwe) ‘hukumu’ ya kutokuwapo kwa jinai kwa Jakaya Kikwete ilishangaza wengi.

Kauli ya Magufuli ilikuja miaka kumi kamili baada ya huyo mtangulizi wake, Kikwete, kutoa kauli ikimhusu mtangulizi wake Benjamin Mkapa. Hakuna dalili iwapo kutakuwepo na ukomo wa ‘mchezo’ huu.

kwa upande mmoja, hii inaelezea kwa namna na kiwango fulani, kwa nini marais wa zamani hapa nchini hawataki ‘kustaafu’ kiukweli na kula pensheni zao kwa taratibu, kwani daima utawaona nyuma ya mabega ya waliomo serikalini wakichungulia kile kinachoendelea.

Lakini mfano mwingine mzuri wa watawala kung’ang’ania madarakani, ni jirani zetu Kenya katika uchaguzi wao miaka tisa iliyopita, uchaguzi uliosababishwa na maamuzi yasiyokuwa ya haki ya tume yao ya uchaguzi, maamuzi ambayo yalidaiwa kusukumwa na utawala wa rais aliyekuwa mafarakani, Mwai Kibaki kutaka aendelee kuongoza.

Watu walikufa na wahusika wakuu pia walitinga katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) huko The Hague, Uholanzi ingawa sasa hivi ndio viongozi wakuu wa nchi hiyo, kwa maana ya rais na makamu wa rais, ambao wanagombea tena uchaguzi Agosti mwaka huu. Haya maajabu hutokea barani Afrika tu.

Baada tu ya kuanguka kesi ya wawili hao kutokana na mashahidi kadhaa wa upande wa mashtaka kujitoa, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Kofi Anan na ambaye alihusika katika kuleta ufumbuzi wa mgogoro wa nchi hiyo, alisikika akisema kwamba mahakama hiyo ilifanya makosa makubwa kuwapa dhamana watuhumiwa. Wangenyimwa dhamana leo hii wasingekuwa viongozi wakuu wa Kenya, achilia mbali kutaka kugombea tena.

Na kwa Kenya hayajaisha, kama vile msemo ule wa mitaani kwamba ‘mambo bado asubuhi kabisa.’ Sasa hivi figisu figisu za kampeni za uchaguzi zimeshika kasi na itakuwa wanafanya makosa makubwa iwapo wanasiasa wa Kenya watakuwa wameyasahau yale yaliyowapata 2007.

Kuna baadhi ya watu wanasema wasuluhishi walisahau kuweka katazo katika mkataba wa maridhiano, kwamba wanasiasa wakuu wote waliohusika katika vurugu zile wasigombee uchaguzi kuwania nafasi za juu kwa miaka kumi.