Home Makala MADAKTARI WETU WATAKUWA SALAMA KENYA?

MADAKTARI WETU WATAKUWA SALAMA KENYA?

192
0
SHARE
Rais John Magufuli

NA MARKUS MPANGALA,


 

KENYA itaingia kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu ifikapo Agosti 8. Katika kipindi hicho cha kuelekea uchaguzi mkuu, Serikali yao imeingia kwenye mgogoro na Chama cha Madaktari wa nchi hiyo ambao umedumu kwa kipindi cha miezi mitatu.

Mgomo wa madaktari unatokana na kiwango cha malipo na masilahi mengine. Licha ya majadiliano ya hapa na pale pamoja na kufikishana mahakamani, bado haijapatikana suluhu kati ya Serikali na madaktari wake.

Kutokana na hali hiyo, huku baadhi ya wananchi wakipoteza maisha, Serikali ya Kenya imeamua kuomba msaada kwa Serikali ya Tanzania ili ipatiwe madaktari. Nayo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, imeamua kuitikia wito wa Rais Uhuru Kenyatta wa kupatiwa madaktari 500 ili kutatua nakisi inayowakibili.

Takwimu zinaonyesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Kenya kiliongezeka hadi asilimia 40 mwaka 2011 kutoka asilimia 12.70 ya mwaka 2006. Ukosefu wa ajira kutoka mwaka 1999 hadi 2011 kilikuwa asilimia 22.43.

Tofauti ya viwango hivyo vinaashiria kuwa Kenya haijatatua tatizo la ajira kama ilivyo kwa Tanzania ambapo hadi Desemba mwaka 2014, tatizo  hilo ni asilimia 10.3.

Ninakubaliana na uamuzi wa Serikali kupokea maombi ya Kenya na kuyafanyia kazi. Ninakubaliana na madaktari takribani 157 waliotuma maombi ya kazi hiyo kupitia Wizara ya Afya, Jinsia na Watoto.

Ninaamini hatua hiyo itasaidia kupatikana kwa madaktari wapya (ambao kwa muda mrefu hawakuajiriwa serikalini). Pia ninaamini hata wale ambao hawakuwa na ajira, wanaweza kuitumia fursa hii kuingia kazini.

Ninaamini hilo kwa sababu kama waliopo ndani ya ajira wataamua kwenda Kenya maana yake Serikali italazimika kuziba pengo hilo kwa kuwachukua madaktari wapya.

Ninapenda vijana na Watanzania wenzangu wachape kazi kwa weledi. Waweze kuhudumia jamii yetu kwa kusaidia watoto wao, ndugu, jamaa na marafiki.

Ninaamini kuajiriwa madaktari hao wapya serikalini (kupitia mpango wa Kenya) utawezesha kupanua fursa kwao na wengine wanaokuja.

Ni matumaini yangu wataalamu wetu katika utabibu wataiwakilisha vema nchi yetu kwa utendaji wao. Tunao vijana wenye ari, maarifa ya kutosha. Tunao wazoefu wa kutosha!

Sasa turudi upande wa pili ambapo Serikali haijatumia ipasavyo katika kuamua kukubaliana na ombi la Kenya. Tukubaliane Serikali imetazama faida ya kuajiriwa madakatari hao na kupunguza pengo la ukosefu wa ajira, maboresho, bajeti na mengineyo. Hata hivyo, suala la usalama wa madaktari wetu halijawa wazi kwa kiasi cha kutosha.

Kama nilivyoeleza awali kuwa Kenya inakabiliwa na uchaguzi mkuu mwaka huu. Madaktari wao wameitisha mgomo wakitarajia kuwa Serikali itatimiza matakwa yao wakihofia kuvurugwa ama kukosa kura katika uchaguzi ujao.

Mimi kama mwanadamu mwingine nina hofu juu ya hulka na mwenendo wa Wakenya kwenye uchaguzi huu. Tunayo kumbukumbu mbaya ya uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2007. Uchaguzi wa mwaka 2013 ulikuwa na utulivu wa wastani kwani bado Wakenya hawana ile hulka ya uvumilivu kama wa Watanzania.

Mwaka 2007 kulizuka machafuko mabaya na yalisababisha hasara ndani ya jamii. Tuna kumbukumbu ya ubaguzi mkongwe wa kikabila uliowatawala Wakenya. Hapo ndipo ninapopata hofu juu ya madaktari wetu, kwamba watakuwa salama kiasi gani katikati ya uchaguzi mkuu?

Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) anakubaliana na wasiwasi huu juu ya usalama wa madaktari wetu wanaokwenda nchini Kenya. Yeye anasema: “Kenya ni wabaguzi kabisaa. They are xenophobic. Na mbaya zaidi hili linakuja wakati madaktari wao wana mgogoro na Serikali yao. Ingekuwa wana upungufu wa kawaida, ingekuwa walau kuna uhakika wa usalama. Kwa sasa ndugu zetu hawana wa kuwalinda wakienda huko. Hata huyo anayewaalika hawezi kuwahakikishia usalama.”

Sote tunakubaliana kutafuta masilahi zaidi katika taalamu zetu ni jambo la kawaida. Lakini tunahitaji kufanya kazi kwenye mazingira yenye uhakika wa usalama wa maisha yetu.

Bila usalama katika nchi yoyote hata kazi za kitaaluma kama hizo hazifanyiki kwa uhakika. Endapo Wakenya waliweza kuumizana wenyewe kwa wenyewe haitashangaza wakawadhuru madaktari wetu.

Mimi ninayo hofu juu ya hali ya Wakenya. Ninazitazama hulka zao kama ndugu zetu wa Afrika Kusini, ambao kila mawio na machweo wanafukuza Waafrika wenzetu kwa madai ya kuchukua ajira zao.

Tamko la chama cha madaktari wa Kenya lilibainisha kugomea mpango wa Serikali. Hii ni ishara tosha ya kuweza kusambaza propaganda hasi dhidi ya matabibu wetu. Je, tumejiridhisha kuwa watakuwa na usalama wa kutosha wakiwa kazini huko Kenya? Je, tunajifunza chochote kwenye nyendo zao za uchaguzi kila unapowadia?

Nimalize kwa kukumbusha hili kuwa madaktari wetu watafanya mitihani ya kupimwa kwa muda wa miezi mitatu kama inavyodaiwa taratibu za huko. Pamoja na hayo usalama wao unahitajika zaidi kuliko chochote. Tusije tukalaumiana baadaye.