Home Habari kuu MCHANGA WA DHAHABU UTATA MTUPU

MCHANGA WA DHAHABU UTATA MTUPU

1225
0
SHARE

*Wachumi wamwonya, wasema Rais anadanganywa


NA GABRIEL MUSHI

TAARIFA za kuwapo kwa wizi wa mchanga wa dhahabu unaosafirishwa nje zinadaiwa kujaa utata ambao unaweza kuligharimu Taifa, kama hatua za haraka hazitachukuliwa katika kuliweka sawa jambo hilo.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kukamatwa kwa zaidi ya makontena 280 yaliyosheheni mchanga wa dhahabu yanayosubiri kusafirishwa nje ya nchi.

Taarifa hizo zilianza kuibuka mwishoni mwa wiki iliyopita, pale Rais Dk. John Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza Bandarini, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini kupitia bandari hiyo, ikiwamo usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli alishuhudia makontena 20 ya mchanga wenye madini kutoka kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa ambayo yamezuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu Machi 2, mwaka huu, alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga huo.

Pamoja na kushuhudia makontena hayo, Rais Magufuli alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP – Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga wa madini (Makinikia ya dhahabu) unashikiliwa popote ulipo, mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika.

“Nataka niwaambie nchi yetu inachezewa mno, nimekuja kuyaona haya makontena kama yapo, na kweli nimeyaona, sasa utaratibu utakapokamilika nataka Watanzania na dunia nzima ione kilichomo humu ndani kama ni mchanga kweli ama dhahabu,” alisema Rais Magufuli.

Baada ya ziara hiyo ya Rais, kulifuatia ziara ya Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye pia alitembelea bandarini hapo na kujionea makontena 262 yaliyozuiwa.

Ziara hiyo ya Spika ilipokea maelezo kutoka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Profesa Justin Ntalikwa, ambaye  saa chache baadae uteuzi wake ulitenguliwa na Rais.

Kauli na mamuzi hayo ya Rais yametafsiriwa na baadhi ya wasomi kama njia ya mikakati ya watu wachache kutumia ukaribu wao na Rais kwa kumpa taarifa potofu.

Imani hiyo ya Rais kudanganywa juu ya taarifa za kuwapo wizi wa makinikia inawekwa wazi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja.

Katika mahojiano yake maalum na RAI, Profesa Semboja ambaye ni msomi wa uchumi anasema kuwa hakuna wizi wowote unaofanyika katika kusafirisha mchanga huo, badala yake lipo kundi la watu wachache kwa makusudi wameamua kumdanganya Rais.

Prof. Semboja ameweka wazi kuwa, inashangaza na kuchukiza namna baadhi ya watu wanapoamua kwa makusudi kuwaita wawekezaji wakubwa kuwa ni wezi, huku wakidai kuwa, makontena yaliyokutwa bandarini wameyakamata, kana kwamba yalikuwa yakisafirishwa kinyemela.

Sijui Watanzania ni wapumbavu wa aina gani, nadhani wazungu wametufanya kuwa wapumbavu kwa sababu kitu unaona ni dhahabu tunasema ni mchanga, kwa hiyo ni hopeless, nashindwa kuona terminology hii inatumiwa na watu ovyo. Ukitumia akili na busara hauwezi kuwa serious na kitu tunachozungumza sasa,” alisema.

Alisema haoni ajabu kwa Rais kukasirika kutokana na kudanganywa na watendaji wake kuwa kampuni ya Acacia inaiibia Serikali.

Alisema kampuni kubwa kama Acacia ni kampuni ya kimataifa ambayo inafuata taratibu za kidunia katika kutekeleza majukumu yake na si kutekeleza mambo kwa ujanjaujanja kama ilivyo kwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa hapa nchini.

“Hata mtu kama wewe ukiambiwa kuwa unaibiwa kumbe hauibiwa lazima uchukie, kwa sababu wanachosafirisha Acacia si mchanga, bali ni mabaki ya mchanganyiko wa madini ambao kwa lugha ya kigeni hujulikana kama  concetrete, si mchanga wa kawaida. Na hawa watu si wezi kama anavyoambiwa Rais, ukweli ni kwamba Rais anapewa taarifa potofu.

“Lengo la Rais ni zuri katika kutekeleza dhana yake ya kuifikia Tanzania ya viwanda, lakini tukiendelea hivi, hakika tutawafukuza wawekezaji na tutapoteza ajira na mapato kwa Serikali yetu,” alisema.

Hoja ya Profesa Semboja inaungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), ambaye anasema Rais angejifunza kujizuia kutoa matamko barabarani jambo ambalo lingesaidia sana nchi na kujisaidia yeye mwenyewe kutimiza ndoto zake kwa nchi anayoongoza.

“Mimi binafsi naunga mkono kuwa ni lazima tuchenjue dhahabu hapa hapa nchini badala ya kupeleka mchanga Japan na China. Lakini ni muhimu maamuzi hayo yawe na ushahidi wa kisayansi badala ya matamko holela ambayo madhara yake Kwa nchi ni makubwa mno.

“Wakati Rais anatoa amri kuhusu mchanga wa madini kusafirishwa kwenda nje ya nchi kulikuwa na mazungumzo yanaendelea kati ya Kampuni ya Acacia mining (yenye Assets zinazozalisha nchini Tanzania tu kwa sasa – Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara) na kampuni nyengine ya nchini Canada kuhusu Acacia kununuliwa kwa USD 4.4bn.

“Mara baada ya amri hiyo mazungumzo yalivunjika na hivyo mauzo kutofanyika. Iwapo Rais angechelewa kutoa kauli yake kwa wiki moja tu mazungumzo yale yangepelekea mkataba wa mauzo kusainiwa na hivyo Serikali ingepata asilimia 20 ya thamani ya Mauzo Kama kodi ya Ongezeko la Mtaji (capital gains tax ). Hivyo kauli ya Rais imesababisha hasara Kwa nchi yenye thamani ya USD 880m sawa sawa na shilingi 1.8 trilioni.

“Tafiti zinaonyesha kuwa gharama ya kujenga ‘ refinery ‘ ya kuchenjua dhahabu hapa nchini ni USD 800m. Hivyo mapato ambayo yangepatikana kutokana na kodi ya mauzo ya Acacia yangewezesha nchi kujenga refinery na kufikia lengo la Rais la kuwa na uchenjuaji wa mchanga ule hapa hapa nchini. Rais angetulia angeweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja,” anasema.

Mbunge wa Igunga Dk. Dalaly Kafumu (CCM), ambaye pia ni mtaalamu wa madini kwa upande wake anaungana na hoja ya Rais kutoshauriwa vizuri na kwamba maamuzi haya ya haraka yatalisababishia Taifa kupoteza mapato.

Dk. Kafumu ambaye aliwahi kuwa Kamishna wa madini nchini, anasema Rais yuko sawa kwa sababu uamuzi wake ni wa kisera.

“Sera ya Madini ya mwaka 2009 (niliyosimamia utengenezaji wake); kifungu 5.11; policy statement no. 3 inasema hivi: (iii) The Government will collaborate with the private sector, regional and international organisations to strategically invest in smelting and refining.

“Kwahiyo mchakato wa kuchenjua mchanga hapa nchini ni matakwa ya kisera, lakini shida inakuja tu pale ambapo shughuli hii inaanzishwa kwa haraka na dharura kubwa. Hali hiyo inaweza kuleta uhusiano usio sawa na makampuni ya kimataifa.

“Pia maamuzi haya ya haraka yatatupotezea mapato kama wengine walivyosema. Nia njema na nzuri ya Rais ni lazima iendelezwe kwa kumshauri aangalie namna bora zaidi ya kufikia malengo haya mazuri ya Sera ya Madini ya mwaka 2009.

“Washauri wa Rais – wizara yenye dhamana, tafadhali ni wajibu wenu na jukumu lenu kumsaidia Rais juu ya hili jambo jema lenye manufa kwa Taifa letu,” anasema Kafumu ambaye pia Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Viwanda na Biashara.”

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu katika andiko lake alilolitoa wiki hii alibainisha mambo kadhaa ikiwamo kuitahadharisha serikali kuwa makini katika kushughulikia suala hilo.

“Acacia wanasafirisha makinikia ya dhahabu nje kwa taratibu zote za kisheria. Badala ya kuwa na smart president tuna JPM anayeaminii kwamba ametumwa na Mungu kuinyoosha nchi hii na neno lake ndio sheria. Matokeo yake atagombana na wawekezaji na serikali zao na mabwana wakubwa wakifedha duniani ambao ndio wamiliki halisi wa rasilimali zetu.

“Watampeleka kwenye arbitral tribunal za kimataifa ambazo Mkapa na Kikwete walizikubali kuwa ndio mahakama za migogoro kati yetu na hao tuliowapa rasilimali zetu na tukipelekwa huko hatuponi,” alisema.

Profesa Ntalikwa, ambaye ameondolewa kwenye kiti chake cha Ukatibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, hakuwa mbali na wasomi na wanasiasa wanaopingana na hatua ya Serikali ya kuzuia mchanga huo kwa kudai kuwa hapa nchini hakuna kiwanda cha kuchenjua mchanga huo.

Alisisitiza kuwa lengo la wizara ni kuwa na kiwanda cha kuchenjua mchanga huo nchini, lakini uwekezaji wake ni gharama na hawajampata mwekezaji.

Aliongeza kuwa wizara yake itafanya uchunguzi tena wa kutambua ukweli wa kilichomo ndani ya makontena hayo kutokana na kuwepo ubishi kati ya TPA na TMAA.

ACACIA YAFAFANUA

Katika kuonesha kuwa wanachokifanya ni halali kampuni ya Acacia ambayo ndiyo mchimbaji mkubwa wa madini nchini kwa kupitia makampuni yake mbalimbali, ilitoa taarifa kwa umma kuhusu sakata hilo la kusafirisha makinikia ya dhahabu /shaba nje ya nchi.

Katika taarifa yake hiyo, Acacia inapinga kuhusika na madai ya kufanya njama za kutorosha makontena yenye makinikia ya dhahabu / shaba nje ya nchi na kueleza kuwa hawakuwahi kujaribu kufanya hivyo.

Kampuni hiyo imeeleza kuwa kabla ya kutangazwa kwa zuia hilo tayari walikuwa na makontena 256 ambayo sasa yamehifadhiwa Zam cargo zamani Mofed- ambaye ni wakala wa usafirishaji wa forodha (CFSI).

Taarifa hiyo iliweka wazi kuwa makontena hayo yalikuwa yamesafirishwa kutoka migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi na makontena mengine 21 yaliyokuwa katika bandari ya Dar es Salaam yakiwa  tayari yameidhinishwa na idara ya forodha na mamlaka ya mapato Tanzania TRA na yalikuwa tayari kusafirishwa na kwamba zoezi hilo linajumuisha TRA pamoja na wizara ya  nishati na madini ambao kwa pamoja wanahusika na mchakato wa kusafirisha makinikia nje ya nchi kwa utaratibu maalumu.

SPIKA AUNDA KAMATI

Katika kudhihirisha kuwa suala hilo limegubikwa na utata, Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye anaamini ni kweli kuna harufu ya wizi kwenye biashara hiyo ya kusafirisha mchanga huo, alitangaza kuunda kamati teule itakayokuwa na jukumu la kufanya uchunguzi wa kina.

Ndugai alisema wamelazimika kuunda kamati hiyo kutokana na utata uliopo katika biashara hiyo ya makinikia ya shaba maarufu kama mchanga wa dhahabu.

Alisema Watanzania wanahitaji kujua biashara hiyo ya mchanga wa dhahabu inafanywa vipi, nani wanafaidika na biashara hiyo ambayo usafirishaji wake nje ya nchi ulianza tangu mwaka 1998.

Alisema kuita mchanga wa dhahabu ni kupotosha, kwani mchanga huo una madini ya dhahabu, shaba na fedha.

“Tunachojiuliza kama kweli dhahabu ni asilimia 0.02, mwekezaji anayeangalia dhahabu kwa nini akazanie kusafirisha makontena haya nje ya nchi kwa miaka 20 sasa? Alihoji Ndugai na kueleza kuwa, lazima kuna wizi fulani unafanyika.

PROF. SEMBOJA AMPINGA

Kauli hiyo ya Spika ilipingwa na Profesa Semboja ambaye anasema kuundwa kwa Kamati hiyo ni  sawa na kupoteza fedha, kwa sababu kinachochunguzwa kwa kudhaniwa kuwa ni wizi hakipo.

Hata hivyo, alisema si jambo baya kama Kamati iliyoundwa itaitumia nafasi hiyo kujifunza zaidi biashara hiyo kwani elimu watakayoipata itawasaidia katika mijadala yao.

“Kama hela ipo ya kufanya uchunguzi, wacha waende wakafanye utafiti wao ili wajifunze, si mbaya sana kupata elimu kwa watu wote, hata CCM, majaji, vyuo vikuu,  wanaweza kuanzisha kamati wakachunguza.

“Ila hili jambo ni la kiufundi zaidi. Si jambo rahisi, kwa sababu hata mimi ni mchunguzi, naona raha kupata mawazo mbalimbali, lakini  msingi ni namna ya kukaa na hawa wawekezaji tuone jinsi gani tunaweza kuchenjua dhahabu hii hapa nchini, badala ya kusimamisha uzalishaji,” alisema Profesa Semboja.

HISTORIA YA MAKUBALIANO

Profesa Semboja anasema kinachofanywa na wawekezaji wa migodi si wizi wala uhuni, bali kipo kwa mujibu wa makubaliano katika biashara hiyo.

Alifafanua kuwa, Tanzania ilipoanza kuwa na migodi mwaka 1998, kulikuwa na uhaba wa umeme wakati huo ambao usingetosheleza kuendesha kinu cha kuchenjulia madini hayo hapa nchini.

Alisema nchi ilikubaliana na wawekezaji kuwa migodi iliyopo Kahama na Buzwagi wapeleke ‘concentrate’ China na Japan kufanya process ya pili ya kutenganisha madini na uchafu.

“Hii ni mikataba ya kisheria, tumekubaliana nao, ile concentrate maana yake ni kupembua uchafuchafu na madini, si kama hakuna madini yapo, wakishachenjua unabaki uchafu, dhahabu, shaba na kopa. Yapo madini mengine mengi hata hivyo thamani yake si kubwa, hauwezi kusema unapeleka kwenye soko kuuza hivyo ilivyo.”

Prof. Semboja alisema asilimia 50 ya mapato ya Kampuni hizi za kuchimba madini yanatokana na uuzaji wa dhahabu ambayo inasafishwa hapahapa nyumbani kwetu, hivyo wakati wa kuchambua na kuiuza,  taasisi za Serikali kama Mamlaka ya Mapato (TRA), TMAA na taasisi nyingine wanakagua kama ni kweli dhahabu imepatikana,  kwa kutumia sheria wanatozwa kodi inayopaswa.

“Ile inayopelekwa nje inakwenda kwa makubaliano rasmi, kwa sababu tulijua hatuna umeme, wala uwezo wa teknolojia ya kuisafisha. Hata hivyo, kumekuwa na mpango kuwa tukipata umeme wa kutosheleza tutaweza kufanya hilo jambo hapa nchini.

“Tayari Serikali kwa kupitia TMAA ilishafanya utafiti kujua kwa sasa ni vinu vya aina gani tunaweza kukubaliana kuvitumia. Lakini hata hii concentrate inayopelekwa nje TRA na TMAA wanakuwapo na nyingine inafanyiwa majaribio na taasisi hizi na makampuni kutoka nje kujua kwamba mwamba ni uleule au ni tofauti, kwa hiyo tujue kuwa haya makampuni si wahuni, kampuni hizi haziwezi kufanya uhuni wa kipumbavu, kusema wafichefiche halafu wapeleke nje, si kama baadhi ya wafanyabaishara wa hapa nchini, haya ni makampuni ya kimataifa, wanajua wanachokifanya, wanafuata sheria za kimataifa.

“Kitu ambacho lazima tuelewe kuwa hoja ya kutaka kuprocess hapa nchini ambayo Rais Magufuli ametaka kulitekeleza, ni hakika kuwa tulitaka kulifanya tangu zamani, tatizo serikali zote zilisuasua, sasa Rais wetu mzuri ametaka tufanye process wenyewe, na tayari ameanza kwenye baadhi ya vitu kama vile pamba na korosho, tayari amesema hakuna haja ya kupeleka India zikaongezewe thamani. Hii inamaanisha hakuna sababu ya kutaka Tanzania yenye viwanda huku ukiwa unaendelea kuuza malighafi nje, haitakuwa na maana.”

Alisema lengo la Rais ni zuri, kwani lengo na dhamira yake ni kukomesha utaratibu wa kusafirisha malighafi nje ya nchi.

HASIRA ZA RAIS

Profesa Semboja anafafanua kuwa, ni haki kwa Rais kuwa na hasira na kuamua baadhi ya kazi kuzitekeleza mwenyewe kwa sababu wapo baadhi ya watendaji wanamkwamisha kwa kutotekeleza kwa vitendo maagizo yake.

“Baada ya Rais kuzuia usafirishaji watendaji walitakiwa ku-legalize na ku-formalize statement ya Rais kwa kuwaandikia barua wawekezaji kuwa Rais kasema kuanzia sasa tusipeleke nje, badala yake tukae pamoja tujadiliane tutatekelezaje haya mambo. Jambo hili halijafanyika hivyo.

“Matokeo yake haya makampuni makubwa hayakuweza kuchukua hatua kwa taarifa za kwenye magazeti. Kwa sababu hata Serikali ya Tanzania haifanyi kazi kwa maneno ya kwenye magazeti. Na wale walikuwa wanasubiri maandishi ili waangalie namna ya kufanya, ndiyo maana wakawa wanaendelea na uzalishaji kama kawaida kwa sababu  hawakuambiwa chochote na TRA nao wanaangalia na wanapitisha makontena bila kikwazo.”

DALILI ZA KUKIMBIZA WAWEKEZAJI

Aidha, Profesa Semboja alisema mwekezaji mwenye akili timamu kwanza lazima akwazike na matamko haya.

“Lakini pia tukumbuke hili si tamko la kwanza, yamekuwapo matamko mengi ambayo yamewasumbua sana wawekezaji. Nikiri kuwa kweli wamesumbuliwa na kampuni zinaweza kupoteza asilimia 50 ya mapato yao iwapo tutaendelea hivi. Nchi tunaweza kupoteza mapato yetu, wale ni wataalaamu, tungeweza kuwa na makubaliano ndipo wakakaa na kuanza kulifanyia kazi suala hilo, ni vitu vya kawaida, kwa sababu wanaweza kusema hatutaki, lakini watu wanazungumza mezani, hawakai kwenye magazeti kwa sababu wengi wanabaki kudandia hoja ndogo za Bashite, Nape na kina Gwajima, bandarini watu wamezoea vituko.

UPATIKANAJI WA DHAHABU

Katika kufafanua namna uzalishaji wa dhahabu unavyofanyika, Profesa Semboja alisema inategemea na aina ya mwamba ambao unatumika kuzalisha hiyo dhahabu.

Tanzania tuna uchimbaji wa aina mbili za madini, kuna madini ya mwamba ambao upo juujuu, mwepesi, mzuri na una dhahabu tupu, hauna vitu vingi sana, mfano wa migodi hiyo ni Nzega, Nyamongo na Geita.

“Kwa hiyo kuchimba mpaka kuprocess hakuna tatizo lolote, wanachukua yale mawe na kukatakata kwa kutumia mashine maalumu hadi madini hayo yanatoka kama vikokoto vidogovidogo, vile vikokoto vinagongwa kwenye mashine nyingine na kusagwa hadi yanatoka mawe mepesi kuliko unga wa ngano.

“Sasa katika unga huo inachanganywa liquids (vimiminika) vya aina mbalimbali ambazo zinasaidia wao kutofautisha aina mbalimbali za shaba na madini mengine.

“Aina ya pili hii ipo katika miamba ya Kahama ambako dhahabu inatoka chini sana, kule uchambuaji unakuwa katika process mbili kubwa, moja ni hiyo ya kufikia mwamba, kupiga mawe hayo na kuyaponda ponda, lakini sasa wakati wa kuseparate inatumika teknolojia nyingine ili kuweza kupata dhahabu, lakini pia wanatumia teknolojia nyingine ya kuchoma- smelting process ili pia kutenganisha madini hayo ambayo hapa nchini haipo na ndipo wanalazimika kusafirisha Japan.”

UWEZO WA KUNUNUA KINU

Profesa Semboja anasema uwezo wa Serikali kununua mitambo ya kuchenjua madini hayo upo, kwani Rais akiamua ni jambo ambalo haliwezi kushindikana.

“Kama Rais amekuwa na uwezo wa kuwekeza kwenye shirika la ndege akatumia pesa chungu nzima, siamini kwamba kwenye madini anashindwa. Kama angepewa taarifa sahihi kitaalamu tusingekuwa tunazungumza haya, tatizo ni kwamba, Rais hapewi taarifa sahihi, kama angeelezwa kitaalamu kuwa labda tunahitaji mashine hii yenye thamani ya trilioni kadhaa, haya yote yangekuwa yamekwisha. Lakini anapewa taarifa potofu, badala ya kuambiwa unapelekwa concentrate si mchanga, pia si kwamba ni wezi wale.

“Kwanza tunampa taarifa si nzuri, si technical, tunamwambia hawajalipa kodi kumbe uongo, badala ya madini tunamwambia mchanga, lazima achukie, yeye ni binadamu. Hata wewe ukipewa taarifa hizo lazima uchukie. Na haya madini kuyaita mchanga ni ubwege.”

MITAMBO IPO

Licha ya baadhi ya wadau kusema kuwa mitambo ya kuchenjua madini hayo ni ghali na haiwezi kuwekezwa hapa nchini kwa kuwa huhitaji kiwango kikubwa cha umeme wa kuchenjua, Profesa Semboja anapingana na hoja hiyo na kubainisha kuwa ni hoja iliyopitwa na wakati.

“Mitambo hiyo wanayozungumzia ni ile ya study za mwaka 2011, ndizo zilizosema hivyo, lakini sasa miaka mitano imepita teknolojia imebadilika, ipo mitambo inayoweza kutufaa hapa kwetu, hata Rais anaweza kuzungumza na Rais wa China kumwomba tutengenezewe mashine inayokidhi mahitaji yetu, ni jambo linalowezekana kwa sababu pia sasa Rais ameisukuma Tanesco kutengeneza umeme wa kutosha na hawana sababu ya kushindwa kutengeneza umeme huo.” Alisema.