Home Makala Kimataifa RAILA ODINGA, UHURU KENYATTA: NI NANI HAWA KATIKA SIASA ZA KENYA? –...

RAILA ODINGA, UHURU KENYATTA: NI NANI HAWA KATIKA SIASA ZA KENYA? – 1

1413
0
SHARE
Uhuru Kenyatta (kushoto) akipeana mkono na Raila Odinga.

NA CHRYSOSTOM RWEYEMAMU,

RAILA Odinga anatoka katika moja ya familia maarufu kisiasa nchini Kenya. Baba yake, marehemu Jaramogi Oginga Odinga, alikuwa mmojawapo wa watu muhimu katika uwanja wa siasa nchini Kenya kabla ya nchi hiyo kujipatia Uhuru na atakumbukwa siku zote katika vitabu vya historia ya nchi hiyo kama mmoja wa waasisi wa Taifa hilo.

Wasomi wengi nchini Kenya wanaamini kwamba Raila amerithi kwa kiwango kikubwa haiba na kipaji cha uongozi cha marehemu baba yake, na anaweza, katika hali ya sasa, akafanya pia yale ambayo baba yake aliweza kuyafanya wakati ule.

Ingawa sifa hizo zinaelekea kuaminika miongoni mwa Wakenya wengi, lakini zinaweka kando kitu kimoja cha kipekee kumhusu Raila ambacho si tu hakikujidhihirisha hata nyakati za marehemu baba yake, bali pia hakijionyeshi waziwazi miongoni mwa wanasiasa wengi wengine nchini Kenya kwa sasa.

Ukweli ni kwamba Raila, kwa sababu ambazo hazielezeki, ana ufuasi na mvuto mkubwa miongoni mwa watu wa kawaida nchini Kenya, na hasa vijana na watu wa kipato cha chini mijini ambao wanamwona kama mlalahoi mwenzao kwa jinsi ambavyo hana makuu maishani mwake.

Hili ukilijumlisha na ufuasi mkubwa wa karibu wa kuabudiwa alio nao miongoni mwa Wakenya wa jimbo la Luo-Nyanza, jimbo mojawapo lenye watu wengi nchini humo, linamfanya mwanasiasa huyu kuwa tishio kubwa kisiasa.

Cha kushangaza katika yote hayo ni kwamba Raila mwenyewe anatoka katika familia ya tabaka la matajiri na amesoma vizuri, hali ambayo ungetarajia imbague kutoka kwa watu masikini. Lakini kinyume chake na ukweli ulivyo, Raila kwa wananchi wa Kenya ni “mtu wa watu”.

Raila yupo karibu sana na wananchi wa kawaida, hali ambayo inampa yeye ushawishi mkubwa na nguvu ya kisiasa zaidi ya wenzake na wale wanaompinga.

Hali hii ndiyo inayoakisi kwa nini Raila alilishika na kuliweka mkononi mwake jimbo la Langata, jimbo ambalo lipo katikati ya jiji la Nairobi ambako alikuwa akishinda kila uchaguzi kwa kishindo.

Vigogo walio wengi nchini Kenya wana ufuasi mkubwa wa kidini unaowaunga mkono katika majimbo yao ya uchaguzi yaliyopo vijijini, tofauti na ilivyo kwa majimbo ya mijini ambako kuna mchanganyiko mkubwa wa watu.

Kabla Raila hajajitoa uanachama wa FORD-Kenya, chama alichokiasisi baba yake, na kujiunga na chama cha National Development Party (NDP), kulikuwapo na uvumi kuwa umaarafu wake katika jimbo la Langa’ta ulikuwa ni kwa sababu alikuwa mwanachama wa chama cha baba yake.

Minong’ono na uvumi huo uliyeyuka pale Raila alipokihama chama hicho cha FORD-Kenya baada ya kutoelewana na Mwenyekiti wake, Kijana Wamalwa (sasa marehemu), na kuamua kugombea jimbo hilo hilo la Lang’ata kwa tiketi ya NDP na kushinda kwa kura nyingi.

Hapo ndipo ilipodhihirika kuwa umaarufu wake si kwa sababu ya chama, bali ni kwa sababu yake yeye mwenyewe.

Maelewano yake makubwa na rika la vijana na walalahoi waishio mijini, inawezekana yanatokana na jinsi alivyokuwa jasiri katika kupingana waziwazi na Rais Mstaafu Daniel arap Moi wakati ilipokuwa hatari sana kwake nchini Kenya kufanya hivyo.

Hilo lilimfanya apate wapenzi wengi na kuungwa mkono na watu wengi sana, kama mwanasiasa ambaye anaamini anachokifanya na ambaye anaweza kusimama kijasiri dhidi ya udhalimu wowote wanaofanyiwa wananchi wake.

Kuwekwa kwake kizuizini mara tatu na Moi, ambako nako alikukabili kijasiri, kulisaidia sana pia kumjengea sura ya mtu jasiri kwa sababu wafungwa wengi wa kisiasa baada ya kufunguliwa na kutoka magerezani, ama walirudi wakiwa wamenywea kabisa na wasio na nguvu ya kuendelea na upinzani wao dhidi ya Serikali, au walikuwa wagonjwa kiafya kiasi kwamba hawakuweza tena kuhimili misukosuko ya kisiasa na kupambana na Serikali.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Raila tayari alikuwa maarufu miongoni mwa vijana wa mijini, ambao mara nyingi ndio huleta vurugu kubwa wanapopambana na vyombo vya dola katika kuipinga Serikali kwa maandamano.

Wapinzani wa kisiasa wa Raila walikuwa wakati huo wanalibebea bango sana jambo hilo, na kumpachika jina la kejeli la “Bwana Vurugu”.

Hata baada ya magazeti yasiyomuunga mkono kumwandika vibaya kutokana na madai hayo ya kuunga mkono vurugu nchini, umaarufu wake miongoni mwa vijana na walalahoi bado ulibaki pale pale na imara.

Raila alizaliwa Maseno katika mkoa wa Nyanza, Januari 7 mwaka 1945. Alisoma shule za msingi kijijini kwao hadi mwaka 1961 alipopata udhamini na kwenda kusoma Ujerumani Mashariki ya wakati huo. Huko, alijiunga na Chuo cha Herder na baadaye akahamia Madgeburg College of Advanced Technology (Otto Von Guericke). Alimaliza masomo yake mwaka 1970 na kutunukiwa shahada yake ya kwanza katika fani ya Uhandisi Mitambo.

Aliporudi nchini Kenya, Raila aliteuliwa kuwa Mhadhiri Msaidizi katika Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mwaka 1970, akiwa mtaalamu katika fani ya teknolojia ya uzalishaji, Raila alianzisha kampuni yake binafsi aliyoiita “Applied Engineering Services” ambayo ilijikita katika kutoa ushauri kuhusu masuala ya miradi inayohusiana na viwanda.

Maisha yake ya kisiasa, kwa kiwango kikubwa yamekuwa shwari na ya mafanikio, japo alikuwa na misuguano na migongano kadhaa na utawala wa Rais Mstaafu, Daniel arap Moi, na kumfanya atambulike (Moi) kama kielelezo cha udhalimu wa sheria ya kimabavu ya kuwaweka watu kizuizini bila ya kuwashtaki mahakamani, sheria ambayo ilitumika kuwasweka kwenye majela wapinzani wengi wa Serikali ya KANU kabla ya kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1991.

Matatizo yaliyomsibu Raila yalianza mwaka 1982 baada ya askari wa jeshi la anga la nchi hiyo kushindwa katika jaribio lao la kutaka kuiangusha Serikali ya wakati huo (ya Moi). Raila alidaiwa kuwa mmoja wa waasisi na waandaaji wa mipango ya jaribio hilo lililoshindwa, na hivyo akashtakiwa kwa kosa la uhaini.

Cha ajabu ni kwamba hata kabla ya utekelezaji wa jaribio hilo, Raila hakuwa jeshini kama ambavyo mtu angetarajia, alikuwa teknokrati (technocrat) serikalini akifanya kazi kama naibu mkurugenzi katika Shirika la Viwango (KEBS) nchini humo.

Aliwekwa kizuizini kwa muda wa miezi saba kabla ya kutupwa jela bila kufikishwa mahakamani. Aliachiwa huru Februari 6 mwaka 1988; miaka sita tangu alipokamatwa. Kuachiwa kwake huko kulikuwa kwa muda mfupi tu, kwani miezi saba tu baadaye tangu aachiwe, alikamatwa tena Septemba (1988).

Safari hii, kukamatwa kwake kulihusishwa na kikundi cha siri kilichojulikana kama “Kenya Revolutionary Movement (KRM)”, ambacho kilikuwa kikipigania kuwapo kwa siasa za vyama vingi nchini humo.

Raila aliachiwa Juni 12 mwaka 1989.  Kukamatwa kwake kwa mara ya tatu kulikuja Julai 5 mwaka 1990 wakati wa kilele cha vuguvugu na machafuko ya kudai kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini humo.

Vigogo wengine maarufu waliokamatwa pamoja na Raila na kufungwa kwenye jela maarufu na yenye ulinzi mkali ya Kamiti, walikuwa ni pamoja na Kenneth Matiba, na aliyekuwa Meya wa mji wa Nairobi, Charles Rubia.

Raila aliachiwa Juni 21 mwaka 1991, na Oktoba mwaka huo alitorokea nchini Denmark akidai kwamba Serikali ilikuwa inakusudia kumuua.

Raila alipokuwa akiikimbia Kenya, chama cha Forum for the Restoration of Democracy (FORD), kilikuwa na miezi miwili tu tangu kiundwe, lakini hata katika umri mdogo huo, tayari kikaanza kuonekana kuwa mwiba mchungu kwa Serikali ya KANU wakati huo.

Shinikizo la FORD liliulemea sana utawala wa Serikali ya Moi, ambayo mwezi Desemba mwaka 1991, ulilazimika kurekebisha kifungu Na 2 (A) cha Katiba ya nchi hiyo na kuruhusu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini Kenya.

Kutokana na marekebisho hayo, siasa nchini humo wakati ikiwa imepamba moto, Raila alishindwa kuendelea kuishi uhamishoni, na Februari mwaka 1992 alirudi nchini Kenya na kujiunga na chama cha FORD, wakati huo chama hicho kikiongozwa na baba yake, Mzee Oginga Odinga. Raila alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kawaida.

Katika miezi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1992, ilibainika kwamba si kila mtu ndani ya chama hicho alikuwa anaridhika na mwenendo wake. Tofauti kubwa za kiitikadi zilianza kujitokeza katika chama hicho, na ilipofika Agosti 1992, hatimaye kilichokuwa kikitarajiwa kutokea kilitokea.

Chama cha FORD hatimaye kilimeguka na kuzaa vyama vya FORD-Kenya, kilichokuwa kikiongozwa na Mzee Jaramogi Oginga Odinga na FORD-Asili kilichokuwa kikiongozwa na Kenneth Matiba.

Raila aliungana na chama cha baba yake na kuteuliwa kuwa naibu mkurugenzi wa uchaguzi. Lakini mambo hayakumnyookea sana Raila katika FORD-Kenya. Ingawa yeye ndiye aliyekuwa mtu wa pili katika uongozi wa chama hicho akimfuatia baba yake, Raila alikuwa akikerwa na kukoseshwa raha kwa kile alichokuwa akikitafsiri kama kutengwa na baadhi ya marafiki wa karibu wa baba yake, watu kama James Orengo, Kijana Wamalwa na Paul Muite.

Ingawa ilikuwa dhahiri kuwa Raila hakuwa na raha na jinsi mambo yalivyokuwa yakiendeshwa ndani ya chama hicho cha FORD-Kenya, alikuwa mjanja. Aligundua kuwa kukihama chama hicho wakati baba yake akiwa bado ndiye kiongozi mkuu kungekuwa kosa kubwa sana kisiasa.

Hivyo baada ya kifo cha Mzee Jaramogi Oginga Odinga Januari 1994, na Kijana Wamalwa kumrithi katika nafasi hiyo ya uongozi, haikuchukua muda mrefu kabla Raila hajaonyesha waziwazi nia yake ya kutaka kushika uongozi wa chama hicho.

Mapambano ya kuwania uenyekiti wa chama hicho yakapamba moto na kuashiria wazi wazi kwamba chama hicho kingeweza kumeguka tena.

Ingawa kwa nje chama hicho kilikuwa kikionekana kuwa chama kimoja, lakini kwa ndani kilikuwa kimegawanyika katika makundi mawili – moja lililokuwa likimtambua na kumwita Wamalwa kama Mwenyekiti na jingine la Raila.

Hatimaye Januari mwaka 1997, akiwa anawazia Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, Raila alijitoa katika chama cha FORD-Kenya na kujiunga na chama ambacho hakikujulikana kwa wengi wakati huo, cha National Development Party (NDP), kitendo ambacho kwa wengi kilionekana kama ni kujiua kisiasa.

Kitu ambacho watesi wake hawakukijua ni kiwango cha kuungwa kwake mkono na wananchi wengi wa kima cha chini na uwezo wake mkubwa wa upangaji mipango. Raila alikibadilisha kabisa chama hicho kidogo kisichojulikana cha NDP na kuwa chama chenye nguvu, chenye mvuto mkubwa na ambacho ndicho kilicholiongoza kundi la wabunge, wengi wao kutoka nyumbani kwao, Luo-Nyanza, katika kukihama chama cha FORD-Kenya na kujiunga na chama chake kipya.

Mwaka 1997, katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Lang’ata, ambao ulitokana na yeye Raila kubadilisha uanachama wake wa vyama, alishinda kwa kura nyingi, kinyume kabisa cha jinsi kura za maoni kwenye magazeti zilivyokuwa zimebashiri.

Raila alimshinda hata mgombea wa FORD-Kenya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1997, akiwa wa tatu baada ya Moi na Kibaki.

Katika uchaguzi huo wa mwaka 1997, Moi wa chama cha KANU alipata jumla ya kura 2,500,856. Mwai Kibaki (DP) alikuwa wa pili kwa kupata kura 1,911,742 akifuatiwa na Raila wa NDP aliyepata kura 667,886. Kijana Wamalwa wa FORD-Kenya alikuwa wa nne kwa kupata kura 505,704.

Raila alijikuta akilazimika wakati huo kushirikiana katika baadhi ya mambo na viongozi wa chama cha KANU ambao kwa muda mrefu ndio waliokuwa mahasimu wake wakubwa kisiasa. Raila alitetea jambo hilo kwa kusema kuwa kufanya kwake hivyo kulikuwa ni kwa ajili ya kulinda umoja wa nchi hiyo, na kwamba ilikuwa rahisi kusafisha nyumba ukiwa ndani yake kuliko ukiwa nje.

Mwaka 1997 katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 27, Raila Odinga alitoana jasho vikali na waliokuwa wapinzani wake wakuu, Rais Kibaki na Kalonzo Musyoka.

Nyota yake iliendelea kung’aa na kungoza kwa kura hadi hatua za mwisho kabla ya kile kilichoelezwa kuwa wizi wa kura zake zilizidaiwa kuibwa na washirika wa Rais Kibaki kupitia Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK).

Watu wengi wanaamini kuwa Raila alikuwa mlangoni kuwa mpangaji wa Ikulu lakini akapigwa kiwiko. Hali hii ilisabaisha rabsha na ghasia kubwa karibu nchi nzima ya Kenya na kusababisha vifo vya watu wanaosadikiwa kufikia zaidi ya 1,500 na maelfu kuwa wakimbizi nchini Uganda.

Kwa muda wa zaidi ya miezi miwili, Kibaki na Raila walitunishiana misuli wakigombea nani awe mmiliki wa Ikulu hadi juhudi za usuluhishi wa kimataifa ziliposaidia kuepusha shari zaidi.

Raila hatimaye alikubali kugawana madaraka na Rais Kibaki hadi uchaguzi mwingine ulipofanyika mwaka 2012. Wakati wote huo Raila alikuwa Waziri Mkuu mwenye madaraka makubwa nchini Kenya. Akiwa na Musyoka kama mgombea mwenza kwa upande mmoja, Uhuru Kenyatta akiwa na Ruto kama mgombea mwenza kwa upande mwingine, Kenyatta alichaguliwa kuwa Rais wa Kenya hadi Oktoba mwaka huu (2017) uchaguzi mwingine utakapofanyika. Raila alipigwa kete mwaka 2013 na Kenyatta ambaye aliingia kwenye siasa miaka kadhaa baada yake.

(Itaendelea wiki ijayo)

Mwandishi ameandaa makala haya kwa msaada wa taarifa za AfricanTribute.com Inc. 2002. Aliishi nchini Kenya mwishoni mwa miaka ya 80 na mwanzoni mwa mwaka 90. Tangu wakati huo, amekuwa akifuatilia kwa karibu sana siasa za nchi hiyo.