Home Makala GHARAMA KUBWA ZA KINYOZI WA RAIS HOLLANDE ZAIBUA GUMZO

GHARAMA KUBWA ZA KINYOZI WA RAIS HOLLANDE ZAIBUA GUMZO

240
0
SHARE
Rais Francois Hollande

Gharama za unyozi za Rais wa Ufaransa Francois Hollande zimestusha wananchi wa nchi hiyo, huku wengi wakihoji inakuwaje gharama kubwa wakati nywele za rais huyo zinazidi kunyoyoka na upara unamuingia kwa kasi?

Wananchi walikuja kufahamu habari hii baada ya msemaji mmoja wa serikali kuthibitisha kuwepo kwa kinyozi rasmi wa Rais huyo anayelipwa na serikali. Kinyozi huyo hulipwa Dola za Kimarekani 10,994 kwa mwezi (euro 9895) na kwamba huwa anasafiri naye popote anapokuwa ziarani.

Kwa mwaka mzima, kinyozi huyo anayegharamiwa na walipa kodi wan chi hiyo hupokea Dola za Kimarekani 132,000, fedha ambazo ni mara tano ya mapato ya kinyozi wa kawaida nchini humo.

Katika mahojiano na runinga moja nchini humo, Rais Hollande alilalamika kwamba mapokezi ya wananchi baada ya kujua habari hiyo yamepitiliza kiwango.

Alisema: “Wananchi wanaweza kunishutumu kwa mambo yote mengine lakini si kwa hili,” na hapo hapo kukumbusha kwamba hivi karibuni tu alikubali punguzo loa asilimia 30 kutoka mshahara wake.

Msemaji huyo wa serikali, Stéphane Le Foll alithibitisha kwamba gharama za kinyozi wa rais zilikuwa zimeingizwa katika bajeti ya Ikulu ya nchi hiyo (Elysée Palace) ambayo ni makazi rasmi ya rais huyo. Aidha alisema kwa ujumla gharama za uendeshaji wa Ikulu hiyo zimepunguzwa kati ya asilimia 15 na 20.

Fll alisema wakati akiwa katika safari na Rais, ndani au nje ya nchi, kinyozi huyo huwa karibu yake wakati wote.

Habari kuhusu gharama kubwa za kinyozi wa Rais Hollande kwa mara ya kwanza ziliibuka Agosti mwaka jana katika kitabu kilichoitwa

“L’Elysée Off” kilichotungwa na wanahabari wawili — Stéphanie Marteau na Aziz Zemouri.

Kitabu hicho kilimtambua kinyozi huyo kwa jina la Olivier Benhamou na kwamba awali alikuwa anatoa huduma za unyozi bure kwa Hollande na swahiba wake wakati wa kampeni za kugombea urais mwaka 2012.

Kuibuka kwa habari hizi za sasa za ukubwa wa gharama za unyozi wa Rais Hollande zimekuja wakati mgumu kwa Ufaransa.

Kuanzia mapema mwaka jana serikali ya nchi hiyo ilikuwa katika jitihada kabambe za kukuza uchumi ulionasa na unaotegemewa kukua kwa asilimia 1.1 tu mwaka huu.

Isitoshe migomo ya wafanyakazi kupinga sheria mpya zinazohusu sekta ya wafanyakazi zilisababisha upungufu mkubwa wa gesi ya kupikia nchini kote.

Na isitoshe sekta ya utalii imekuwa ikiathiriwa na matukio ya mashambulizi ya kigaidi katika mji wa Paris na sehemu nyingine.

Hivyo wananchi wanaona habari za Rais wao kutumia fedha nyingi za walipa kodi kama gharama za kinyozi si jambo muafaka kwa wakati huu.