Home Habari kuu LOWASSA AMGUSA NDESAMBURO

LOWASSA AMGUSA NDESAMBURO

362
0
SHARE

NA SAFINA SARWATT, KILIMANJARO


MWENENDO  wa sasa wa siasa za kimya kimya zinazoendeshwa na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umeonekana kumgusa mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Phillemon Ndesamburo. RAI linaripoti.

Tangu kumalizika kwa harakati za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, uliomwingiza Rais Dk. John Magufuli Madarakani,  Lowassa ambaye pia alipeperusha bendera ya Chadema kwenye mbio za Urais, amekuwa akitajwa kuendesha siasa za chini kwa chini ambazo lengo lake ni kukiimarisha chama hicho kwa kukipeleka kwa wananchi waliopo katika maeneo mbalimbali ya nchi mjini na kijijini.

Katika mahojiano yake maalum na RAI, Ndesamburo ambaye anatajwa kuwa mwanasiasa anayekubalika sana mkoani Kilimanjaro,   alisema moja ya mambo muhimu ambayo Chadema imefanikiwa ni kumkaribisha Lowassa ambaye mwenendo wa siasa zake za kabla na baada ya uchaguzi zinatishia uhai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Lowassa amefanya maegeuzi makubwa kwenye sikasa za upinzani ndani na hata nje ya Chadema, ujio wake kwenye upinzani umeleta mvuto na hamasa kubwa kwa vyama vya upinzani, alitikisa nchi na sisi ujio wake kwetu ilikuwa neema kubwa kwani hata CCM walikosa usingizi na hata leo wanaendelea kuhaha juu ya Lowassa. Sisi kwa lugha nyingine tunasema Lowassa ni mali isiyoisha thamani.”

Akizungumzia uimara wa Chadema katika Ukanda wa Kaskazini, Ndesamburo alisema uthubutu na ujasiri mkubwa walio nao wananchi wa Moshi Mjini na mikoa inayopakana na Kilimanjaro, ndiyo siri kubwa ya mafanikio yao kisiasa.

Ndesamburo alisema pamoja na siri hiyo, lakini pia ipo siri kubwa zaidi ambayo hayuko tayari kuifichua sasa kwa sababu wanatarajia kuitumia kumaliza CCM kwenye chaguzi zijazo.

Kuhusu uwezekano wa Chadema kuingia Ikulu kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, Ndesamburo alisema, uwezekano huo ni mkubwa sana kwa sababu tayari wanayo mikakati mingi binafsi nay a chama itakayowasaidia kushinda chaguzi zijazo na kuingia Ikulu kwa kishindo.

CHADEMA YA SASA

Akizungumzia Chadema ya sasa na ile ya miaka ya nyuma, Ndesamburo amesema kwa sasa chama chao kipo imara zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“… tuna timu bora, chama kina mvuto wa hali ya juu. Kinafanya siasa bora licha ya kuzuiwa kwa mikutano, lakini chama kimekuwa cha tofauti sana, kimejikita zaidi kwa wananchi wa kawaida kabisa, ambao awali walikuwa hawafikiwi.”

Alisema mwenendo wa sasa wa siasa hapa nchini unakifanya Chadema kuwa chama mbadala wa CCM  hali inayowapa matumaini ya kufanya vizuri kwenye chaguzi zijazo kwa sababu chama chao kinakubalika.

Chadema bado inapendwa na Watanzania, tatizo kubwa ilikuwa ni uthubutu na ujasiri kutokana na uelewa mdogo wa wapiga kura, lakini sasa tumejipanga hatutaibiwa kura, tuna timu  kila kona ya nchi, ziko imara.  Chadema ni chama makini siku zote, kimeweka mikakati mingi kulingana na utandawazi hivyo vitu vingine siwezi kuvisema nitaharibu mikakati,”alisema Ndesamburo.

HALI YA KISIASA NCHINI

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini kwa sasa, Ndesamburo amesema ni mbaya kwa sababu wanasiasa hasa wa upinzani hawajui wanakokwenda.

“Hatujui tunakwenda mbele ama tunarudi nyuma, tupo katikati ya giza nene. hatujui ni chama gani kinachotawala kwani CCM haionyeshi kama ni chama kinachotawala.

“Mikutano ya vyama vya upinzani imezuliwa. Nchi hii sasa ni kama haiongozwi kwa Katiba, yaani unaweza kusema inaongozwa kwa maamuzi ya mtu. Ukweli ni kwamba nchi inatakiwa ukombozi mkubwa bado wananchi wako utumwani,”alisema.

SERIKALI YA AWAMU YA TANO

Akizungumzia mwenendo wa kiuongozi wa Serikali ya awamu ya Tano, Ndesamburo alisema anaona ni uongozi wa ajabu sana na kwamba kamwe hakuna kiongozi anayeweza kuongoza nchi pekee yake bila kusikiliza wananchi hasa ukizingatia kuwa wananchi wanalalamika kila siku.

“Kuna malalamiko mengi sana. Rais anachokifanya si sahihi, kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani, pili amekuwa hasikilizi kero za wananchi na hayuko tayari kushirikiana na upinzani ambao anatakiwa kukaa nao na kusikiliza mawazo yao ambayo yangeweza kumsaidia katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi hasa kwa kipindi hiki cha Tanzania ya viwanda.”

BUNGE

Wakati vikao vya Bunge vikiwa vimeshaanza mjini Dodoma, Ndesamburo alisema mwenendo wa Bunge hilo si mzuri kwa sababu kuna dalili zoite za wapinzani kubanwa sana na kwamba anaona hakuna haki katika kuchangia mijadala wala hoja zenye mashiko kwa maendeleo ya jamii.

VITI MAALUM VIFUTWE

Ndesamburo ameweka wazi kuwa ipo haja ya kuzifuta nafasi za wabunge wa viti Maalum kwa sababu havina maana yoyote kwa nchi.

“ Tunahitaji kukomaa kisiasa kwani bado hatujakomaa kisiasa, pili hivi viti vinatakiwa vifutwe kabisa kwanza vimekuwa vikileta migogoro ndani ya vyama vya siasa kwani vina ubaguzi mkubwa sana. Tatu sioni sababu za kuwepo kwa viti hivyo.”

TANZANIA YA VIWANDA

Kuhusu dhamira ya Rais Magufuli ya kutaka Tanzania ya viwanda, Ndesamburo ambaye pia ni mfanyabiashara mwenye mafanikio makubwa nchini, alisema haoni kama dhamira hiyo itafanikiwa.

“Kipindi chote cha ubunge wangu nilikuwa nikipambana na Serikali kuhusu kufufuliwa kwa viwanda, lakini Serikali haikupenda maendeleo kwenye majimbo yanayongozwa na upinzani hasa kanda ya Kaskazini. Hoja ya kufufuliwa viwanda Moshi nilikuwa nikiwasilisha kwenye vikao vya Bunge mara kadhaa bila mafanikio.

“Ninavyoona mimi hakuna viwanda vitakavyofufuliwa wala kujengwa upya kwa sababu maendeleo ya uchumi yamedhorota, pia hali ya kisiasa ilivyo sasa haileti picha nzuri kwa maendeleo ya Taifa. Kwa sababu uchumi na siasa ni mambo ambayo hutegemeana ili kufikia mafanikio ya nchi yoyote duniani.”

HAJAACHA SIASA

Ingawa aliwahi kunukuliwa akisema kuwa anaachana na siasa ili akasimamie zaidi biashara zake, Ndesamburo ameibuka upya na kuweka wazi kuwa kamwe hajaacha siasa.

“Niwaambie kwamba bado nipo kwenye siasa wala sijaachana na siasa,pili nikiachana na siasa bila ukombozi wa Tanzania kupatikana nitakuwa nimebaki na deni kubwa kwenye moyo wangu.

“Baada ya kuliongoza jimbo la moshi mjini kwa miaka 20, niliamua mwenyewe kuwaachia na wengine wayaendeleze yale mema niliyofanya, pili sikuwa na uchu wa madaraka, lakini kamwe sijaacha siasa.”

SIASA NA BIASHARA
Kuhusu suala la kutenganisha siasa na biashara, Ndesamburo amesema jambo hilo ni gumu kwa sababu mahitaji ya kisiasa yanahitaji fedha halali ambazo sehemu pekee pa kuzipata ni kwenye biashara halali za mwanasiasa.

“ Si muda sahihi kabisa wa kutenganisha siasa na biashara, siasa huleta maendeleo na asilimia kubwa ya viongozi wa siasa katika nchi hii ni wafanyabiashara.”

Mwanasiasa huyo alisisitiza kuwa pamoja na kujitoa kwenye siasa za bungeni, bado anashiriki siasa za ukombozi na dhamira yake kuu ni kuhakikisha anaikomboa Tanzania kutoka gizani.

“Nchi hii bado ipo gizani, wananchi wake wako katika giza nene hawaoni nyuma wala mbele. Ila sasa nimerejea upya kwenye siasa ili kutafuta ufumbuzi wa ukombozi wa Tanzania.

“Nadhani wengi wanafahamu siku zote nilikuwa nikifanya siasa safi na bora. Nitaendelea kufanya siasa safi na bora bila kuingilia uhuru wa mtu yeyote wala kuvunja sheria za nchi nitaendelea kuheshimu watu wote wa kabila zote.”

Tangu kurejea kwa uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995, Ndesamburo amekuwa mmoja wa wanasiasa wachache nchini ambao waliamua kuacha kuwania ubunge kwa hiyari yake huku akijua wazi anayo nafasi kubwa ya kuhsinda.

Ndesamburo, ameliongoza jimbo la Moshi Mjini kwa vipindi vinne tangu 1995 mpaka 2015 alipoamua kung’atuka kwa hiyari yake.